Tunataka Mahabusu Waachiwe Huru

بسم الله الرحمن الرحيم

Habari:
Mnamo tarehe 09 Julai 2020 familia tatu za mahabusu jijini Dar es Salaam walifanya Mkutano na wanahabari kutoa mwito wa kutaka kuachiwa huru ndugu zao ambao wamekua wakishikiliwa kwa tuhuma za ugaidi bila ya kesi zao kusikilizwa kwa karibu miaka mitatu sasa !
Maoni:
Familia hizo za mahabusu hawa: Ustadh Ramadhan Moshi Kakoso, Wazir Suleiman Mkaliaganda na Omar Salum Bumbo, wote wakiwa wanachama wa Hizb ut Tahrir zilionesha masikitiko yao na kuhoji taasisi za kimahkama Tanzania, kwanini kwa karibu miaka mitatu sasa ndugu zao hao hawapewi mchakato unaostahiki kisheria kuwezesha kesi zao kusikilizwa, kupewa dhamana au kuachiwa huru
Mbali na wanaharakati wa Hizb ut Tahrir, kuna mahabusu wengi Waislamu wakiwemo masheikh na wanaharakati wa Jumuiya ya Uamsho (na wengine) wakiendelea kusibiwa na hali kama hiyo, bali ngumu zaidi, wao wamekuwa wakishikiliwa kwa zaidi ya miaka saba sasa, wakikabiliana na hali ya madhila kizuizini katika maeneo duni yenye mrundikano mkubwa wa mahabusu.
Japo dhulma kama hizi huwadhili watu wengine, lakini wanaosibiwa na kulengwa zaidi ni Waislamu. Kwa kudandia propaganda ya kigeni ya kikoloni ya kupambana na ugaidi, vyombo vya dola kila mahala ikiwemo ndani ya Tanzania hutumia kuwa ndio kisingizio cha kuua, kutesa, kuteka na kuwaweka kizuizini Waislamu wengi wakiwemo wanaharakati na masheikh bila ya hata kesi zao kusikilizwa kwa miaka.
Qadhia hii inafedhehi wazi wazi hali ya kutokuwepo usawa na uadilifu katika mchakato wa utoaji haki, kwa kuwaweka mahabusu kizuizini bila ya kesi kusikilizwa kwa miaka kwa kisingizio cha ‘bado uchunguzi unaendelea’ kwa ajili ya kukusanya ushahidi. Jambo hili linaashiria uwepo wa dhana ya dhulma ya ‘kamata kwanza, kisha uchunguzi baadae’ Kinachoitwa kamatakamata ya kupambana na magaidi ni jambo maarufu hususan katika maeneo yenye Waislamu wengi, ambapo wengi wasio na hatia wamedhikishwa na kuathirika kwa ajili tu ya kuifanyia kazi ajenda ya kibepari na ya kikoloni (kupambana na ugaidi)
Vyama vya upinzani Tanzania viliwahi kutamka kuwa karibu watu 380 wametekwa na kutoweka katika harakati za serikali za kupambana wanaodaiwa kuwa magaidi katika ukanda wa Pwani Kusini. Baadhi ya wabunge hata walidiriki kulitaka Bunge kuunda tume maalumu ya uchunguzi kuliangazia suala hili kwa undani, wakasisitiza wabunge hao kwamba harakati za serikali kupambana na watuhumiwa wa ugaidi hazikutendwa kuzingatia mipaka ya kisheria, kiasi cha kugubikwa na wimbi kubwa la uvunjaji wa haki za binadanmu ikiwemo mateso na mauaji holela (The East African, 05/05/2018).
Hali hii inazua shaka ya kiwango cha juu kwa mtu yoyote makini, kwa namna kesi nyingi za ugaidi zinavyoamiliwa nchini Tanzania na penginepo, kukiibuka maswala mengi ya msingi, ikiwemo kwanini ushahidi (wa kesi hizo) hauwasilishwi mbele ya mahkama? kwanini mahabusu (wa kesi hizo) hawapewi haki yao ya kisheria ya kusikilizwa kesi zao kwa muda muwafaka? kwanini mahabusu hao hawapewi dhamana? kwanini kuna hali ya khofu khofu na fichaficha katika kesi hizi? na mengi mengineyo. Hapana shaka yoyote, hitimisho la maswala hayo ni hali ya uwepo wa ajenda ya kidhulma kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi.
Tunatoa mwito kwa Umma wa Kiislamu na wale wote wenye hisia za kibinadamu katika nyoyo zao, kusimama kidete dhidi ya dhulma hii ya kunajisi uadilifu. Lazima tusimame bila ya kuchoka kupaza sauti katika qadhia ya mahabusu kushikiliwa bila ya kesi zao kusikilizwa, kunyimwa haki yao ya dhamana, kutokuwepo kikomo katika muda wa kukusanya ushahidi, pia tusimame dhidi ya utekaji na kanuni ya kikoloni na kibaguzi ya Sheria ya Ugaidi.
Tunawakumbusha Waislamu na wasiokuwa Waislamu kwamba madhila yanayowasibu wanadamu ulimwenguni leo ni matokeo ya uovu wa mfumo wa kibepari ambao haujali chochote hata sheria zilizotungwa kwa mikono yao wenyewe.
Ni katika dola ya Kiislamu ya Khilafah pekee ndipo uadilifu utatamalaki, sambamba na hilo heshima, damu, mali nk. vyote vitalindwa ipasavyo.
Na Said Bitomwa
Mjumbe wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Tanzania
Imeandikwa kwa ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

Maoni hayajaruhusiwa.