Mwelekeo wa Uislamu Juu ya Uhifadhi wa Mazingira

بسم الله الرحمن الرحيم

Tarehe 5 Juni ya kila mwaka ni Siku ya Mazingira Kimataifa. Mkutano mkubwa wa Mazingira uliofanyika tarehe 5- 16 Juni 1972 jijini Stokholm , Sweden ndio uliweka msingi wa kuweka maadhimisho hayo.
Nini mazingira?
Kwa ufupi, kwa muktadha wa wanamazingira, tamko mazingira hukusudiwa vitu, rasilmali na viumbe hai vyote vilivyomzunguka mwanadamu. Hivyo, mazingira yanahusisha ardhi, maji, udongo, jua, hewa, mimea, milima mito, tabianchi na kila kilichoko ardhini, baharini na angani vikiwemo viumbe hai.
Nini maana ya Uhifadhi wa mazingira
Ni matendo, hatua na jitihada zinazochukuliwa na watu binafsi, taasisi na serikali zinazolenga kuhifadhi na kulinda rasilmali za kimazingira, ikiwezekana pia kutibu madhara yaliyotokea kutokana na uharibifu wa kimazingira.
Vilio vya uharibifu wa mazingira vimezagaa leo ulimwenguni kutokana na sababu mbalimbali, kubwa zaidi ni sera na fikra za mfumo batil wa kibepari.
Qadhia ya Mazingira Kimataifa
Suala la kuifanya qadhia ya mazingira kuwa ya kimataifa lilianza tangu mwaka 1945 kwa kuundwa kamati za kimataifa za kiufundi juu ya masuala ya kimazingira. Ndani ya miaka 1960’s wimbi la harakati za kutetea mazingira na mashirikiano likaongezeka na mnamo tarehe 5–16 June 1972 mkutano mkubwa wa aina yake wa kujadili mazingira ukafanyika mjini Stockholm, Sweden. Miongoni mwa miafaka na makubaliano makubwa ya kimataifa kuhusiana na masuala ya mazingira ni kama Kyoto Protocol ya 1997 na Paris Agreement ya 2015.
Mnamo tarehe 8 Oktoba 2021 Umoja wa Mataifa ukapitisha azimio la kutambua rasmi kuwa mazingira mwanana na endelevu ni katika haki msingi za kibinadamu. Na katika azimio 48/13 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa likatoa mwito kwa ulimwengu kufanya kazi kwa mashirikiano na washirika na wadau mbalimbali ili kuilinda na kuhifadhi haki hiyo mpya ya binadamu (mazingira).
Moja katika suala nyeti la kimazingira lenye mjadala mkali kimataifa ni suala la Makubaliano ya Paris (Paris Agreement) ya 2015 yenye lengo la kutaka kupunguzwa gesi zenye madhara (greenhouse gases) hususan gesi ya CO2 ili kudhibiti joto la dunia chini ya nyuzi joto 2C ili kuzuiya dunia isikabiliwe na maafa yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi.
Qadhia ya Mazingira Kitaifa.
Kwa upande wa Tanzania kufuatia Sheria ya Taifa ya usimamizi wa Mazingira Tanzania 1983 kiliundwa chombo kinachoitwa Baraza la la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kikiwa na jukumu la kuishauri serikali na jumuiya ya kimataifa kuhusiana na suala mazingira. Kwa hivyo, baraza hilo hutoa ushauri wa kiufundi, miongozo, kuhakiki na kusimamia ili kuzuiya athari za kimazingira na kutoa elimu ya mazingira katika jamii.
Aidha, Tanzania ina Sera rasmi ya Mazingira chini ya sheria iliyoasisiwa mwaka 1997 inayoitwa The National Environment Policy of 1997 Acts. Tanzania ni mdau mkubwa wa masuala ya mazingira kiasi kwamba hivi sasa wawakilishi wake wanahudhuria Mkutano mkubwa wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa unaoitwa Stockholm +50 unaoendelea (2-3 Juni 2022) nchini Sweden. Pia Tanzania imeweka saini katika miafaka na makubaliano mbalimbali ya kimataifa inayohusiana na mazingira kama: Rio Declaration on Development and Environment mwaka 1992 na Convention on Biological Diversity mwaka 1996.
Mwaka 2004 Tanzania ikatunga sheria makhsusi inayojuulikana kama The Environmental Management Act, 2004, inayosimamia na kuratibu masuala ya mazingira.
Kwa upande wa Zanzibar, mnamo mwaka 2013 ilitoa Sera ya Mazingira kama mbadala wa sera ya awali ya mwaka 1992. Pia Zanzibar ina taasisi kadhaa za masuala ya mazingira kama Mamlaka ya Mazingira inayojuulikana kama The Zanzibar Environmental Management Authority (ZEMA) iliyoundwa chini ya sheria iitwayo Zanzibar Environmental Management Act, ya 2015, na pia kuna Kamati ya Ushauri wa Mazingira inayoitwa Environmental Advisory Committee. Taasisi hizo zipo kwa ajili ya uratibu wa kuhifandhi mazingira visiwani humo.
Misingi ya Uislamu katika Uhifadhi Mazingira:
Uislamu unazichukulia rasilmali ndani ya mazingira yaliyomzunguuka mwanadamu iwe mito, bahari, milima misitu nk. kuwa ni katika neema kubwa ambazo mwanadamu kapewa na Muumba wake.
Uislamu licha ya kuweka hatua mbalimbali za kivitendo za kuhifadhi mazingira pia umechora mtazamo mpana katika suala hili kinyume na ubepari kwa kuzingatia misingi mitatu mikubwa ifuatayo:
Kwanza, Muumba SWT Amemleta mwanadamu katika dunia hii na akampa fursa ya kufaidika kwa kutumia vitu mbali mbali na rasilmali (َمَتَاع) zilizomo ndani yake kwa namna bora, ili kusahilisha na kustawisha maisha yake na vizazi vyake.
وَلَكُمْ فِي الأَرْضِ مُسْتَقَرٌّ وَمَتَاعٌ إِلَى حِينٍ (البقرة: 36).
‘… Na katika ardhi yatakuwa makaazi yenu na mtakuwa na vitu vya matumizi kwa muda (maalum)’ (Al-Baqara :36)
Pili, dhana ya uhifadhi wa mazingira katika Uislamu huzingatia kitu cha mwanzo na cha thamani zaidi ya chochote ni maisha ya mwanadamu na sio kingine. Katika mchakato wa kuhifadhi mazingira kamwe Uislamu haufadhilishi kulinda na kuhifadhi viumbe bahari au viumbe pori, misitu nk. kwa muhanga wa maisha au ustawi wa mwanadamu.
Kwa mfano, Uislamu hauruhusu kuwazuilia wanadamu wenye njaa wasiwinde wanyama kupata chakula katika mapori kwa kisingizio cha kuhifadhi mazingira, au kuwazuiya wanadamu hao wasitumie mito kwa umwagiliaji wa kilimo kupata chakula na matumizi mengine kwa sababu tu ya kuhifadhi maji hayo kwa ajili ya wanyama waliopo katika mbuga ya wanyama karibu na mto nk.
Mtazamo huo hauna nafasi katika Uislamu, kwa sababu binadamu ndio kiumbe bora na kitukufu katika dunia, na viumbe vyengine vyote vimedhalilishwa kwa ajili ya faida na tasaruf ya mwanadamu.
وَلَقَدْ كَرَّمْنَا بَنِي آدَمَ وَحَمَلْنَاهُمْ فِي الْبَرِّ وَالْبَحْرِ وَرَزَقْنَاهُمْ مِنَ الطَّيِّبَاتِ وَفَضَّلْنَاهُمْ عَلَى كَثِيرٍ مِمَّنْ خَلَقْنَا تَفْضِيلاً (الإسراء:
‘Kwa hakika tumewatukuza mno wanadamu, tumewapa vya kupanda bara na baharini, tumewaruzuku vitu vizuri vizuri, na tumewafadhilisha kwa fadhila kubwa kuliko wengi miongoni mwa tuliowaumba’ (Al-Israai :70)
اللَّهُ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضَ وَأَنزَلَ مِنْ السَّمَاءِ مَاءً فَأَخْرَجَ بِهِ مِنْ الثَّمَرَاتِ رِزْقًا لَكُمْ وَسَخَّرَ لَكُمْ الْفُلْكَ لِتَجْرِيَ فِي الْبَحْرِ بِأَمْرِهِ وَسَخَّرَ لَكُمْ الأَنهَارَ (إبراهيم: 32).
‘Allah ndie Aliyeziumba mbingu na ardhi na Akateremsha maji kutoka mawinguni. Na kwa hayo akatoa matunda kuwa ni rizki kwenu. Na akafanya yakutumikieni majahazi yanayopita baharini kwa amri Yake, na akaifanya mito ikutumikieni.’
وَسَخَّرَ لَكُمْ الشَّمْسَ وَالْقَمَرَ دَائِبَيْنِ وَسَخَّرَ لَكُمْ اللَّيْلَ وَالنَّهَار (إبراهيم: 33).
‘Na akalifanya jua na mwezi kwa manufaa yenu daima dawamu, na akaufanya usiku na mchana kwa manufaa yenu’ (Ibrahim: 32-33)
Tatu, Uislamu unahimiza kuhifadhi mazingira kwa hatua mbali mbali za kivitendo kwa ‘qaida’ ya kuzuiya dhara. Tunaona kwa mfano mingi kama vile ulivyohimiza kuotesha mimea kwa kauli ya Mtume SAAW:
«مَا مِنْ مُسْلِمٍ يَغْرِسُ غَرْسًا، أَوْ يَزْرَعُ زَرْعًا، فَيَأْكُلُ مِنْهُ طَيْرٌ أَوْ إِنْسَانٌ أَوْ بَهِيمَةٌ، إِلاَّ كَانَ لَهُ بِهِ صَدَقَةٌ»
“Hakuna Muislamu yeyote atakayepanda mti, au kuotesha mbegu, kisha ndege, au mtu au mnyama akala kutkana nayo, isipokuwa hilo itakuwa ni sadaka kwake”. (Bukhar)
Pia Uislamu umekataza kuvuruga vyanzo vya maji, kuharibu njia za watu na maeneo ya vivuli vya watu, kama Mtume SAAW alipomuonya sahaba mkubwa Muadh ibn Jabal ajiepushe na vitendo vitatu venye kuleta laana za watu, kujiepusha kuharibu vyanzo vya maji, njia zao na vivuli vyao. (Abu Dawud na Ibn Majah).
Aidha, Uislamu umehimiza kuondoa udhia njiani ukitufundisha kuondoa kila lenye kuwatatiza watu katika mazingira, ukafanya maeneo makubwa ya malisho ya wanyama kuwa milki ya Umma ili kudhamini chakula kwa maisha ya wanyama hao nk.
Kubwa zaidi, Uislamu unatufundisha kuwa kutoa huduma kwa wanyama pia kuna ujira kama anavyoripoti Abu Hurayrah (ra) kwamba watu walimuuliza Mtume (saw) kuhusu ujira wa kuwahudumia wanyama, nae Mtume (saw) akajibu:
«فِي كُلِّ كَبِدٍ رَطْبَةٍ أَجْرٌ»
“Kuna ujira kwa kila kiumbe hai anayehudumiwa”. (Sahih al-Bukhari)
Kwa ufupi, Uislamu unakemea kwa ukali suala la kuathiri mimea, wanyama, maeneo nk. Kama Quran inavyosema:
[وَإِذَا تَوَلَّىٰ سَعَىٰ فِي ٱلۡأَرۡضِ لِيُفۡسِدَ فِيهَا وَيُهۡلِكَ ٱلۡحَرۡثَ وَٱلنَّسۡلَۚ وَٱللَّهُ لَا يُحِبُّ ٱلۡفَسَادَ]
‘Na anapokwenda huku na huko katika nchi hufanya uharibifu ndani yake na kuangamiza mimea na vizazi. Na Allah Hapendi uharibifu’ (Al-Baqara : 205 )
Hata hivyo, pamoja na hatua hizo, bado Uislamu umeweka bayana kuwa kuvunjwa amri na maagizo ya Muumba, na kuachwa maelekezo Yake pia ni chanzo kikubwa cha kuharibu, kuathiri na kuvuruga mazingira. Kwa ufupi, katika Uislamu mchakato wa kuhifadhi mazingira lazima wende sambamba na ufungumanishwe na suala la kiroho(utekelezaji wa amri za Muumba) yaani kwa kumtengeza mwanadamu kuwa na fikra, hisia na matendo sahihi mbele ya Mola wake. Kwa sababu maovu, madhambi na maasi mbele ya Mola wake hupelekea kuharibu, kuvuruga na kudamirisha mazingira kwa namna moja au nyengine.
Allah Taala Anasema:
ظَهَرَ الْفَسَادُ فِي الْبَرِّ وَالْبَحْرِ بِمَا كَسَبَتْ أَيْدِي النَّاسِ لِيُذِيقَهُم بَعْضَ الَّذِي عَمِلُوا لَعَلَّهُمْ يَرْجِعُونَ)
‘Ufisadi umedhihiri katika bara na baharini kutokana na iliyoyachuma mikono ya watu, ili (Mwenyezi Mungu) Awaonjeshe kutokana na baadhi ya waliyoyatenda ili waweze kurejea’ (Ar-Rum: 41)
Akasema tena Allah SWT:
وَلَقَدْ أَخَذْنَا آلَ فِرْعَوْنَ بِالسِّنِينَ وَنَقْصٍ مِنْ الثَّمَرَاتِ لَعَلَّهُمْ يَذَّكَّرُونَ (الأعراف: 130)
‘Na hakika tuliwaadhibu watu wa Fir-aun kwa miaka ya (ya ukame) na upungufu wa mazao ili waweze kukumbuka’ (Al-Aaraf :130)
Pia Mtume SAAW nae anasema:
لَمْ تَظْهَرْ الْفَاحِشَةُ فِي قَوْمٍ قَطُّ حَتَّى يُعْلِنُوا بِهَا إِلَّا فَشَا فِيهِمْ الطَّاعُونُ وَالْأَوْجَاعُ الَّتِي لَمْ تَكُنْ مَضَتْ فِي أَسْلَافِهِمْ الَّذِينَ مَضَوْا وَلَمْ يَنْقُصُوا الْمِكْيَالَ وَالْمِيزَانَ إِلَّا أُخِذُوا بِالسِّنِينَ وَشِدَّةِ الْمَئُونَةِ وَجَوْرِ السُّلْطَانِ عَلَيْهِمْ وَلَمْ يَمْنَعُوا زَكَاةَ أَمْوَالِهِمْ إِلَّا مُنِعُوا الْقَطْرَ مِنْ السَّمَاءِ وَلَوْلَا الْبَهَائِمُ لَمْ يُمْطَرُوا
‘…Hautodhihiri uchafu (zinaa) kwa watu mpaka kiwango cha kutangazwa ila watapewa watu hao (na Allah) maradhi ya twauni (maradhi ya maambukizi) na njaa ambayo haijawahi kutokea kabla kwa waliotangulia. Na wala (watu) hawatopunguza vipimo na mizani ila wataonjwa kwa miaka ya (njaa na ukame) na shida na mtawala jeuri juu yao. Na wala hawatozuiya (watu) kutoa zaka katika mali zao ila watazuiliwa mawingu ya mvua, na lau sio wanyama basi mvua isingenyesha kamwe…’ (Ibn Majah)
Hitimisho
Uislamu unalitazama suala la uhifadhi wa mazingira kwa umakini kwa kuwa linagusa ghariza/ hisia ya ndani ya kimaumbile ya wanadamu ya uwepo wake duniani (survival instinct). Na unalifungamanisha suala hilo kuwa ni ibada kwa Muumba SWT, kinyume na ubepari ambao unaleta mgongano katika kukabiliana jambo hili, kwa kuwa umejengwa juu ya dhana ya maslahi ya kiuchumi na kuhifadhi uhuru binafsi.
Risala ya Wiki No. 134
04 Dhu al-Qi’dah 1443 Hijria / 03 Juni 2022 Miladi
Afisi ya Habari – Hizb ut Tahrir Tanzania

Maoni hayajaruhusiwa.