‘Mwaka Mpya’ Mbinu ya Wanademokrasia Kusahaulisha Malengo ya Umri
Mwaka 325 AD Kanisa Katoliki lilifanya mkutano mkuu wa kwanza huko Nicea. Mkutano huu uliitishwa na Mfalme Constantine (mpagani) ili kutuliza hali ya machafuko iliyosababishwa na wakristo waliokuwa wakipinga falsafa ya uungu iliyoasisiwa mwanzoni na Justin Martx, (Yusto). Huu pia ndio mkutano ulioanzisha misingi ya aqeeda ya ukristo wa leo iliyohusisha ‘utatu mtakatifu’, ‘dhambi ya asili’ na kufufuka kwa Yesu. Aidha, ndilo Baraza hili la Nicea lililoweka msingi wa Kalenda iliyokuja kuitwa Kalenda ya Greogarian kwa kulazimisha Wakiristo wote washerehekee Pasaka siku moja. Misimamo ya Baraza la Nicea ilipingwa vikali na baadhi ya Wakiristo ikabidi kanisa kuomba msaada kwa serikali (ya kipagani) isaidie kurejesha amani na utulivu. Katika upinzani huu waliteswa maelfu kama si malaki ya Wakiristo na wengi kuuwawa. Mabaki ya vifaa vya kutesea bado vinapatikana katika jumba la makumbusho huko Rhine, Ujerumani.
Kuanzishwa kwa kalenda ya Miladi ya Papa Gregory XIII lilikuwa ni jaribio la kufanya marekebisho kalenda ya Julian (iliyoanza mwaka 45BC) iliyokuwa ikitumiwa awali. Papa Gregory alisimamia mabadiliko haya, na rasmi katika tarehe 24 Februari 1582 akasaini waraka maalumu unaojulikana kwa jina la “Papal bull’ ili kuimakinisha kalenda hii : http://en.wikipedia.org/wiki/Gregorian_calendar.
Wakatoliki waliikubali kalenda hii kwa kuwa waliamini kwamba dhamira ya Mkutano wa Baraza la Nicea ulioanzisha muundo mpya wa siku ya Pasaka ilikuwa pia kuanzisha kalenda mpya. Japo kwamba lengo la Mkutano lilikuwa ni kupata tarehe maalumu ya kusherehekea Pasaka kwa Wakiristo wote kwa pamoja. Kabla ya hapo Pasaka ilikuwa ikisherehekewa mwezi wa habib ( unavyojulikana katika Bibilia )uliokuwa ukiisabiwa kwa kalenda ya mwezi. Lakini kwa kuwa muandamo wa mwezi hubadilika badilika ndipo Kanisa Katoliki likafanya mabadiliko makubwa ndani ya mwaka 325. Mabadiliko ambayo yalitoa viashiria vya kubadilisha muundo mzima wa kalenda ambao baadae ulikuja kumakinishwa na Papa Greogry wa kumi na tatu.
Hata hivyo baadhi ya makanisa yasiyokubaliana na upapa wa Kikatoliki yalikataa kalenda hii. Miongoni mwao ni Waporestanti na Kanisa la Orthodox. Mataifa mengine yalianza kuikubali kalenda hii kidogo kidogo, hata Khilafah Uthmaniya ilikubali kuitumia kalenda hii katika miaka ya 1890 wakati wa zama zake za uzorotefu, na kuibakisha kalenda ya Hijiria katika mambo ya kiroho na ibadat tu.Kama vile katika hesabu ya Ramadhani na Hijja. Hii ni baada ya kudorora kwa kiasi kikubwa kwa dola ya Kiislamu, kiasi cha baadhi ya Waislamu hususan wasomi walioathiriwa na fikra za kimagharibi kama vile mhasibu Morali Othman (Msomi wa Kiislamu aliyeathiriwa na umagharibi ) kupendekeza kutupilia mbali kalenda ya Hijiria kwa kudai ina usumbufu katika masuala ya hesabu za kifedha.
Suala la kalenda au kuhesabu siku ni jambo tu la kumuwezesha mwanaadamu kuweka kumbukumbu na malengo yake ya kiutendaji na haliingia katika masuala la kiutawala. Ndio maana, japo kuwa kalenda hii asili ni ya Kanisa katoliki , lakini inafuatwa/adopted na sehemu kubwa ya dunia kama si yote. Pamoja na ukweli kwamba si Ukatoliki unaotawala dunia leo. Na badala yake dunia inatawaliwa na mfumo wa kibepari/kidemokrasia. Kwa kuwa ukiristo kamwe sio mfumo wa kimaisha wenye sifa na uwezo wa kumtawalia mwanaadamu na wala hauna masuluhisho ya mambo ya kimaisha. Bali ni kijidini kinachojumuisha baadhi ya fikra za masuala ya kiroho tu.
Mfumo wa kibepari unazitumia sherehe za mwaka mpya kukuza na kuimarisha fikra zake za ‘uhuru’ kwa kiasi kikubwa na masoko ya kibiashara. Huhamasisha kusherehekea kwa namna tofauti kama kulewa, kuzini, kucheza miziki, kamari, kuleta vurugu nk. Aidha, wanaipotosha na kuidogosha hazina muhimu na yenye thamani ya umri wa mwanaadamu na kupongezana kwa kumaliza mwaka salama usalimini bila ya kuwaonesha watu dira na malengo ya umri huo.
Uislamu ni kinyume na Ubepari/Udemokrasia ambao huwafanya watu kutokujua lengo la kuwepo duniani. Wao huona kila kitu kinaishia hapahapa na hakuna hisabu ya matendo kwa Muumba. Na ndio maana itikadi ya Ubepari/Udemokrasia wao huona kwamba kama Muumba yupo basi baada ya kuumba na kumpa mtu akili amemuachia ajipangie mfumo wake anaoutaka maishani kwa faida na hasara ya mwanaadamu mwenyewe. Wala Muumba hana tena nafasi ya kumhisabu mtu huyu. Aidha, Uislamu kamwe haudandii sherehe zisizokuwa za Kiislamu kwa kuwa tayari una sherehe zake zilizowekwa na sheria.
Badala yake Uislamu umeweka wazi lengo la mwanaadamu katika maisha haya kwamba ni kumtumikia Muumba. Na kila dakika mtu ajihesabu kabla ya kuhesabiwa, sio kwa faida ya kimada bali katika kushikamana na maamrisho ya Muumba. Tathmini hiyo sio baada ya kumalizika mwaka. Bali ni kila dakika na kila siku. Yaani Muislamu ajihesabu kabla ya kuhesabiwa.
Waislamu lazima tukumbuke katika umri huu tuna jukumu la kuongoza ulimwengu:
وَكَذَلِكَ جَعَلْنَاكُمْ أُمَّةً وَسَطًا لِتَكُونُوا شُهَدَاءَ عَلَى النَّاسِ وَيَكُونَ الرَّسُولُ عَلَيْكُمْ شَهِيدًا
(TMQ 2:143)
Kwa bahati mbaya leo tunaishi chini ya mfumo wa kikafiri ulimwenguni kote. Licha ya kuwa ni faradhi kwetu kuishi chini ya dola ya Kiislamu ya Khilafah, na ni dhambi kubwa kuishi zaidi ya siku tatu nje ya dola hiyo. Leo ni mwaka wa 88, bado tupo chini ya utwaghuti wa kirasilimali na demokrasia ilhali baadhi bado hawajatanabahi wala kuamka. Kila siku inayopita inakatika sehemu ya umri wetu, tunasonga hatua mbele kuelekea mauti na kuhisabiwa na Allah Taala. Aidha, ni hatua moja nyuma ya muda wa kutekeleza majukumu tuliyofaradhishiwa na Allah SW. Basi jee wakati haujafika wa sisi Waislamu kuamka na kujizatiti katika majukumu yetu?
#UislamuNiHadharaMbadala
Na Hamza S. Sheshe
Maoni hayajaruhusiwa.