Mauaji ya Njombe : Dalili ya Udumavu wa Kifikra Barani Afrika

Habari:

Vyombo vya habari vya Tanzania na kimataifa vinaendelea kuripoti juu ya matukio ya mauaji ya watoto katika Wilaya ya Njombe, kusini magharibi mwa Tanzania, na tayari baadhi ya watuhumiwa wameshafikishwa katika Mahkama ya Wilaya wakikabiliwa na mashtaka ya kuuwa kwa kukusudia .
(The Citizen)

Maoni

Karibu watoto kumi tayari wameshauwawa katika kipindi cha mwezi mmoja, na wauwaji wamekuwa wakiwakata watoto hao sehemu zao za siri na viungo vya kuvutia pumzi katika mauaji yanayohusishwa na imani za kishirikina na uchawi

Mauaji haya ya kikatili na kishenzi yameleta mshtuko mkubwa na hali ya mkanganyiko katika jamii ikiwemo hata katika maeneo mingine nchini. Serikali ya Tanzania imejaribu kukabiliana na qadhia hii kwa kutuma kikosi maalumu katika eneo husika ili kufanya uchunguzi wa kina. Mauaji haya yamelaaniwa vikali kitaifa na kimataifa.

Katika taarifa ya karibuni ya Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa Tanzania Mr. Alvaro Rodriguez kwa vyombo vya habari, alisema uvamizi na mauwaji ya watoto ni jambo lisilokubalika. Pia Mwakilishi wa UNICEF Tanzania nae alitamka wazi kuwa, aina zote za vurugu na udhalilishaji dhidi ya mtoto hazikubaliki wala kuruhusiwa kwa namna yoyote iwayo.

Wakati tukiungana katika huzuni hii kubwa na kutoa mkono wa pole kwa familia na jamii iliyoondokewa kwa mauwaji haya ya kishenzi, lazima iwe wazi kwamba aina hii ya mauwaji inafanana na mauwaji ya albino na mauwaji ya vikongwe ambayo yapo Tanzania kwa miaka mingi, yakihusishwa moja kwa moja na vitendo vya uchawi au biashara ya viuongo vya binadamu ambayo baadhi huamini vina nguvu ya kichawi.

Mauwaji haya ya kishenzi yameshaangamiza maisha ya wengi wasio na hatia, wakati watendaji wa vitendo hivi wakiwa na malengo ya kunufaika kwa kupata nguvu za kishirikina kwa tamaa ya kupata utajiri au wadhifa wa kisiasa, hususan katika nyakati za uchaguzi. Ndani ya mwaka 2015, aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu Mr Zeid Ra’ad Al Hussein aliwahi kutamka kuwa wimbi wa mauwaji ya albino Tanzania lilikuwa na uwezekano wa fungamano na vugu vugu la kampeni za uchaguzi mkuu.

Mauwaji haya ya kikatili amma yawe yanahusishwa na kupata wadhifa wa kisiasa au maslahi ya kuchumi inadhirisha shahir dhahir kuwepo udumavu wa kifikra ndani ya Afrika, kama alivyowahi kutamka Sheikh Taqiudin Nabahan (rahimahullah) kuwa, Afrika iko nyuma kifikra, pamoja na lakini ina rasilmali nyingi katika upande wa malighafi na kiwango kikubwa mno cha utajiri wa wanyama na upande wa kilimo (The Political Concepts of Hizb ut Tahrir)

Afrika ina utajiri mkubwa mno wa rasilmali katika maadini, ardhi kubwa, mito mikubwa, maziwa na rasilmali watu, lakini badala ya kubeba mfumo utakaosukuma kunyanyuka kwake, mataifa ya Magharibi wanalinyonya, wakiwaacha watu wake mafukara wa vitu na mafukara wa kifikra.

Amma suala la wanasiasa kujihusisha na imani za uchawi kwa malengo ya kisiasa, hili ndio ushahidi mpana zaidi ya uozo mkubwa wa kijamii katika udumavu wa kifikra. Kwa kuwa ikiwa wanasiasa, watu ambao ndio tarajio la kuongoza jamii wanaegemea katika imani za kishirikina, hali itakuwaje kwa watu wa kawaida?

Kauli ya karibuni ya Naibu Spika wa Bunge la Tanzania kuwatuliza wabunge kufuatia kuonekana bundi (ndege ambae kwa tamaduni za Afrika ni dalili ya bahati mbaya) ndani ya ukumbi wa bunge, kwamba wasiwe na wasiwasi, kwa kuwa bundi anaeonekana mchana hawezi kuleta madhara kwa yoyote, ni dalili ya kuwepo hisia za kishirikina miongoni mwao.

Ripoti ya mwaka 2011 ya utafiti uliofanywa na shirika la Pew-Templeton Global Religious Futures Project la Marekani iliweka wazi kwamba katika nchi sita wanachama wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC), Watanzania walitajwa kuwa ndio watu wanaoamini zaidi imani za kishirikina, na ilipolinganishwa na nchi nyengine 19 zilizofanywa utafiti huo, Tanzania ikawa nchi ya tatu baada ya nchi za Senegal na Mali.

Afrika inasibiwa na hali ya kuhuzunisha na kusikitisha sana chini ya hatamu za kibepari,. Ubepari hausiti kunyonya rasilmali zake, huku ukiwahamasisha watu katika kila matendo yanayokwamisha ukombozi wake. Wakati umefika sasa, kwa watu wa bara hili tukufu lililobarikiwa kila aina ya utajiri kuamka na kuukumbatia ukombozi wa Uislamu.

Imeandikwa na Masoud Msellem

Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari
Hizb ut Tahrir Tanzania
Kwa ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

Maoni hayajaruhusiwa.