Mapinduzi Bila ya Mfumo ni Nyumba Bila ya Msingi Wala Paa

بسم الله الرحمن الرحيم

Visiwani Zanzibar kumemalizika kwa mbwembwe kubwa shamra shamra nyingi za kuadhimisha yanayoitwa Mapinduzi yaliyofanyika tarehe 12- 1964.

Katika nchi za Kiislamu pamoja na nchi changa kwa jumla huiyangalia dhana ya ‘mapinduzi’ kwa mtazamo finyu, potofu na wa kughilibu wananchi. Ajabu! mapinduzi katika nchi zetu huoneshwa kana kwamba yanalingana na matukio makubwa ya mapinduzi yaliyowahi kutokea duniani kama vile Mapinduzi ya Ufaransa, Mapinduzi ya Marekani, Mapinduzi ya Urusi nk. Ilhali katika nchi zetu wanachoshindwa kuelewa au kujisahaulisha makusudi ni kuwa, matukio ya mapinduzi kama hayo tuliyoyataja na mengineyo yalikuwa ni mapinduzi ya kimfumo yaliyoleta mabadiliko ya kimsingi na sio mapinduzi kwa jina, nembo na kaulimbiu tu bila ya ajenda pana.

Tunapozungumzia suala la mapinduzi ya kimfumo ni kule mapinduzi kuwa juu ya fikra msingi inayoongoza muelekeo mzima na kuzaliwa kutokana na fikra hiyo masuluhisho mbali mbali kutatuwa matatizo ya dola husika. Sasa utaona kwamba Mapinduzi ya Ufaransa ya mwaka 1789 na ya Marekani ndani ya mwaka 1765 yalibeba mfumo wa kidemokrasia/kibepari chini ya fikra yao ya kutenganisha dini na maisha/ kisekula kuwa muongozo wao baada ya migongano iliyoibuka baina ya makasisi na wanafikra wao. Amma Mapinduzi ya Urusi (Bolshevik Revolution 1917) yalibeba fikra ya kukana uungu kwa kuona kwamba kila kitu ni kutokana na mabadiliko ya mada na hakuna zaidi ya mada. Hapana shaka hizi zote ni fikra batil zilizozaa mifumo hiyo miwili batil. Lakini kwa kuwa kwa udhati wake ni mifumo iliweza kuyafanya madola yao kuwa na malengo na ajenda pana katika kuyaendea waliyokusudia japo kwa muda, halafu madola hayo kuanguka. Na hilo ni jambo lenye kutarajiwa kwa kuwa si mifumo ya haki. Lakini ukweli unabakia kuwa madola haya yalikuwa au yana malengo ya mbali kinyume na nchi zetu zisizokuwa na mfumo zaidi ya kudandiadandia tu.

Katika hali kama hiyo utaona sasa takriban yote yanayoitwa mapinduzi katika nchi zetu kimsingi huwa sio mapinduzi kwa maana ya kupatikana mabadiliko ya kimfumo kama tulivyotaja sifa za mfumo. Bali huwa amma ni matukio ya mauwaji na dhulma kufuatia kuchanganyikiwa raia, au yalikuwa ni mbinu ya kumakinisha zaidi athari za madola makubwa ya kibepari kwa kuwagonganisha vichwa raia wa kundi moja dhidi ya wengine. Na hii ndio hali halisi ya yaliojiri ndani ya Zanzibar ndani ya mwaka 1964.

Ndani ya Afrika Mashariki wakati ule dola ya Uingereza ilikabiliwa na changamoto kadhaa. Kwanza, ilitaka kujizatiti zaidi kwa sura nyengine baada ya kufanya kazi na Utawala wa Sultan. Kwa kuwa kufuatia kampeni kali dhidi ya ukoloni mkongwe, dunia ilikuwa haikubali tena dhana ya Usultani. Uingereza ilibidi ibadilishe mbinu kwa kujizatiti kutoa uhuru wa bendera na kuweka vibaraka watakaolinda maslahi yake. Kwa bahati mbaya katika muktadha wa Zanzibar vyama vilivyofanikiwa baada ya uchaguzi kunyakuwa uhuru wa bendera wa mwaka 1963, japo kwamba havikuwa vyama vya Kiislamu, lakini Uingereza haikukinai kwamba vitaweza kulinda vyema maslahi yake.

Kwa hivyo, Uingereza haikuwa na namna ila kuleta machafuko kwa jina la mapinduzi ili kumakinisha chama ilichokikinani zaidi nacho ni Afro-Shirazi. Aidha, Uingereza ilibidi ije na mkakati wa yanayoitwa mapinduzi ili isije kuporwa ushawishi wake na dola la Marekani ambalo lilikuwa na shauku kubwa kuzichukuwa ngome zake hususan baada ya Marekani kuuchukuwa uongozi wa kilimwengu mara baada ya Vita vya Pili.

Kwa Waislamu ni wajibu tumuangalie kiongozi wetu Mtume SAAW namna alivyoleta mapinduzi ya kimsingi ya kimfumo kwa kubeba fikra thabiti ya Kiislamu kuwa ndio dira yake. Fikra hiyo ikiwa fikra huru kutoka kwa Muumba ambayo ilizalisha dola huru yenye masuluhisho ya matatizo yote ya wanadamu, Waislamu na wasiokuwa Waislamu

#UislamuNdioUfumbuziSahihi

Maoni hayajaruhusiwa.