Mafunzo Kutoka Kikosi cha Usamah bin Zaid

Wakati tukiwa katika mwezi wa Rabiul Awwal aliozaliwa kiongozi wetu Mtume SAAW ni vyema tuangazie qadhia muhimu ya sahaba kipenzi cha Mtume SAAW na aliyepata ladha tamu ya malezi ya Mtume SAAW kupitia kwa baba yake sahaba adhimu Zaid bin Hartha aliyekulia ndani ya nyumba tukufu ya Mtume SAAW.

Qadhia hiyo ni ya kutumwa kikosi cha jeshi chini ya Jemadari Usama bin Zaid bin Haritha ndani ya mwezi wa Saffar, mwaka 11 Hijria kwenda kupambana na warumi mpakani mwa viunga vya Palestina.

Madhumuni makubwa ya jeshi hilo ni kwenda kuwatisha warumi ambao kipindi hicho lilikuwa miongoni mwa madola makuu kilimwengu (super power). Na pia kuwapa imani waarabu waliokuwa wamepakana na dola hilo kuu, na kuleta ujumbe kwa kila mmoja kwamba, dhulma inayofanywa na kanisa kwa watu, likishirikiana na watawala wake iko ukingoni kwa kuwa sasa kumepatikana dola nyengine yenye nguvu.
Itakumbukwa kuwa, kikosi hicho kilitumwa siku chache kabla ya kufariki Mtume (SAAW), jambo lililosababisha kikosi hicho kusitasita na kushindwa kwenda kutekeleza amri hiyo katika uhai wake. Kwani baada ya jeshi kutoka masafa kidogo, walipata taarifa ya kudorora zaidi kwa afya ya Mtume SAAW. Hivyo, ikabidi kikosi hicho kusimama ili kusikilizia taarifa ya mendeleo ya afya ya Mtume SAAAW itakavyokuwa. Baada ya muda mfupi, Mtume SAAW alifariki dunia.

Katika hali hiyo ikabidi kikosi hicho kutumwa chini ya Khalifah Abubakar Siddiq ra. kwenda kukamilisha malengo yake. Hili lilikuwa ni jeshi la mwisho kutumwa na Mtume SAAW katika uhai wake, na ndio maana baadhi ya wanazuoni wakauita “Ujumbe wa Mwisho”.

Yapo mengi ya kujifunza kupitia kikosi hiki, haya ni baadhi:
1. Uoni mpana wa Mtume SAAW mpaka dakika za mwisho
Uoni wa Mtume SAAW kwamba mfumo wa Kiislamu unapaswa kuenezwa kimataifa kwa walimwengu wote. Kwani licha ya kuwa Mtume SAAW kuwa katika hali ya ugonjwa, bado jukumu la kutanua dola na kuhakikisha walimwengu wanafikiwa na nuru na risala yake lilikuwa ni katika ghera yake kuu, bila ya kuzuilika kwa kuzorota kwa afya yake. Kwani Mtume SAAW alifahamu fika kwamba, uhai wa mfumo ni utanuzi wa dola kupitia njia ya daawa na jihadi.

2. Ulazima wa kutanua dola.
Maumbile ya mfumo wowote ni kujitanua. Katika hili Mtume SAAW anatuonesha ulazima wa kutanua dola kwa njia ya daawa/ siasa au Jihadi/Vita. Na ukiangalia kwa undani zaidi, ndani ya mfumo wa Kiislamu njia ya daawa/siasa, ndio njia khassa ya kutanua mfumo wake, bali Jihadi ipo kwa ajili ya kuondoa vizingiti vya daawa, na ndio maana Mtume SAAW alimwambia Ally bin Abi Talib ra. Wakati wa vita vya ufunguzi wa ngome za Khaybar, baadhi ya wanatareekh wanasema kwamba, Mtume SAAW alimpa bendera Ally baada ya kushindwa jitihada kadhaa za kufungua ngome hiyo, na kumwambia:
“Nenda kwa uangalifu mpaka ufike kwenye makazi yao, Kisha walinganie Uislamu…… (na katika kumshajiisha zaidi katika hilo la daawa kabla ya vita akasema Swallahu Alaihi wasalaam) Wallahi, Allah Akimuongoza mtu mmoja kutokana na Juhudi zako, malipo yake ni bora kuliko ngamia wekundu mia moja”.

3. Mbeba mfumo lazima aandamwe
Kama ambavyo Mtume SAAW aliwaandama makafiri kwa vita kama alivyotuma kikosi hiki kwa malengo hayo, leo Umma wetu lazima uelewe kuwa wasimamizi wa mfumo wa kibepari kuuandama mfumo wa Kiislamu, Waislamu na kuvamia biladi zetu ni jambo la kutarajiwa kwa kuwa ndio tabia ya uhai wa mfumo. Kinyume chake, makafiri wa kirasilmali kuacha kuuandama Ummah na kuukandamiza, maana yake mataifa hayo na mfumo wao utasambaratika, na hasa kwa vile mfumo wa kibepari hauwafikiani na maumbile ya binaadamu. Kwa hivyo, uhai wa mfumo wao ni kuendelea kuukandamiza Ummah wa Kiislamu na kila ambaye ni kikwazo kwa mfumo wao.

Kwa msingi huo, licha ya Ummah wetu kuhuzunika kwa madhila na dhulma za ubepari ikiwemo mauaji ya Waislamu, lazima tusimame kidete na kushikamana na mfumo wetu bila ya kutetereka tukielewa fiika kuwa maumbile ya mfumo lazima ulete mgongano, lakini mwisho , haki hushinda na batil kubwatika chini kwa fedheha na aibu.

4. Unyeti wa kuwashirikisha vijana katika kubeba majukumu
Usamma bin Zaid alipewa jukumu na Mtume SAAW la kuongoza kikosi cha kupambana na warumi akiwa kijana mwenye umri mdogo wa miaka 17 na akijuwa fika kwamba vita hivyo ni vikali kwa kuwa tayari Waislamu walishapambana nao katika vita vya Tabuk na Muta. Udogo wa Usamah na jukumu kubwa alilopewa ilipelekea baadhi ya mashaba kuwa na shaka nae kiasi cha baadhi kusitasita kuwa chini ya uongozi wake. Katika hali kama hiyo Mtume SAAW akahadharisha kwamba watu wote lazima wawe chini ya uongozi wa kijana huyo, Mtume SAAW hakuzingatia umri wake bali alizingatia uwezo wake baada ya kumpima kwamba angeweza. Mtume SAAW aliwaacha na hakuwapa masahaba wakubwa jukumu la kusimamia vita hii.

Tunatufundishwa na Mtume SAAW umuhimu wa kuwashirikisha vijana katika majukumu, kwa kuwa wao wana nishati kubwa, nguvu na ghera zaidi. Aidha, anatuonesha Mtume SAAW kwamba uhai wa mfumo wowote lazima uwe na ajenda ya kuandaa vijana wake kuweza kubeba majukumu, kwa sababu suala la uwepo kwa mfumo ni endelevu, na daima linahitaji nguvu na nishati mpya.

5. Mwanadamu anakosea sio malaika
Itakumbukwa kwamba Jemadari Usamah bin Zaid aliwahi kushawishiwa na baadhi ya mabwana wa kikureishI ili kutumia ushawishi wake kwa Mtume SAAW kumuombea msamaha mwanamke wa kabila la Makhzoum alipoiba, ili asipitishiwe hukmu ya kukatwa mkono (hadd) kwa sababu makureishi walihisi anatokana na kabila tukufu, Usamah akafanya jambo hilo kwa Mtume SAAW, lakini jambo hilo lilimkasirisha sana Mtume SAAW, kisha Mtume SAAW akawakhutubia Waislamu na kuwaonya na kuwahadharisha vikali Waislamu kwamba hiyo ilikuwa tabia ya waliotangulia, ya kuzifanya sheria ni kwa ajili ya wanyonge na madhaifu tu, na haziwagusi watukufu. Mtume SAAW akawaeleza hata kama angeiba bintie Fatma basi angemkata mkono.

Ni wazi Usamah alifanya kosa katika tukio hili. Lakini alitubu, kujuta na kuendelea kuwa mtiifu kwa Uislamu na kwa Mtume SAAW. Kwa hivyo, matukio ya kukosea nyuma hayakumzuiya Mtume SAAW kumuamini Usamah katika jukumu nyeti kama hili. Mtume SAAW alitambua kuwa mwanadamu sio malaika upo uwezekano wa kuteleza na kukosea. Hivyo, Usamah aliteleza na kutubu, baada ya hapo anastahiki kupewa majukumu ya Uislamu.

6. Malezi bora
Jemadari Usamah amefikia darja ya kuwa kipenzi cha Mtume SAAW kutokana na malezi mwanana aliyoyapata kutoka kwa wazazi wake. Usamah ni mtoto wa Zaid bin Harithah ambae alilelewa na Mtume SAAW, mpaka baadhi ya watu wakamwita Zaid bin Muhammad. Hivyo, ni wazi malezi aliyopata baba yake Usamah kutoka nyumba ya Mtume SAAW aliyafikisha kwa kijana wake Usamah, kiasi cha kuwa mtu muhimu katika Uislamu. Na kwa hakika kitendo cha makureishi kumtuma akamuombee msamaha mwanamke mwizi, ni kutokana na Usamaha kuwa kipenzi na mtu muhimu, na wa karibu kwa Mtume SAAW. Na hilo ni dalili ya wazi kuwa Mtume SAAW aliridhika na mienendo na msimamo wake thabiti katika Uislamu. Hapana shaka yoyote kwamba Mtume SAAW hasuhubiani na mtu kwa mapenzi na ukuruba ila mtu mwema. Hivyo, malezi bora ya nyumba ya Mtume SAAW yaliosafiri kutoka kwa Zaid bin Harthah mpaka kwa mtoto wake yamepelekea kupatikana mtu muhimu, mtukufu na wa kuaminiwa na Mtume SAAW katika majukumu makubwa ya Uislamu.

7. Mtume SAAW hakuwa na muamala wa kibaguzi
Ni wazi historia ya Usamah haikamiliki bila ya kumgusia baba yake Zaid bin Harthah ambaye asili alikuwa mtumwa wa mjomba wa Bi Khadija, na bi Khadija alipoolewa na Mtume SAAW alipatiwa mtumwa huyo ili amsaidie nyumbani. Bi Khadija akamzawadia mtumwa huyo Mtume SAAW. Kisha Mtume SAAW akamuacha huru Zaid bin Harthah, na akawa mtoto wa kulea wa Mtume SAAW. Itakumbukwa pia kwamba ndugu wa Zaid bin Harthah walikuja kwa Mtume SAAW kuwa tayari kumkomboa mtoto wao wamchukue, na Mtume SAAW akawaeleza yeye yuko tayari kwa lolote atakaloamua Zaid mwenyewe, lakini Zaid mwenyewe aliwakatalia jamma zake kuondoka nao, na akakhiyari aendelee kuishi na Mtume SAAW.

Huyo ndio baba wa Usamah ambaye alianzia kuwa mtumwa, hata hivyo Mtume SAAW hakuzingatia historia ya utumwa huko nyuma wala hakumbagua kuanzia baba wa Usamah wala Usamah mwenyewe. Na huu ni mfano mmoja katika mingi namna Mtume SAAW alivyoamiliana na Waislamu kwa Uislamu wao, sio kwa rangi, asili au kabila, au haiba zao. Na kamwe Mtume SAAW hakuonesha tembe ya ubaguzi wala dharau katika miamala yake.

Kwa kumalizia wakati tukiwa katika mwezi huu wa Rabiul Awwal wa kukumbuka mazazi ya Mtume SAAW, ni wajibu kubeba mafunzo haya katika maisha yetu kibinafsi na kwa Umma wetu kwa ujumla wake.

10 Novemba 2018

Khamis Saleh

#MuhammadNiNuruKwaUlimwengu

Maoni hayajaruhusiwa.