Kuungua Shule za ‘Kiislamu’ na Harufu ya Hujuma

بسم الله الرحمن الرحيم

Kuanzia katikati ya mwaka 2020 kumezuka kuungua moto kwa shule za Waislamu nchini Tanzania, ajali hizi za moto zimeshamiri kwa mfululizo na hivyo kuleta sintofahamu kubwa isiyo na mfano.
Matukio haya yameleta simanzi, huzuni na masikitiko kwa wamiliki wa shule, wazazi, walimu, wanafunzi, Ummah wa Kiislamu kiujumla kwa kupotea uhai, rasilmali na kusitisha masomo. Tuchukuwe fursa hii kuwafariji wahanga na kuwaombea Allah Taala awalipe pepo wote waliokufa kutokamana na ajali hizi.
Ukitizama kwa umakini bado kuna mambo yanatia shaka katika utokeaji wa majanga haya ya moto, na lililo wazi zaidi ni kutokea kwake mfululizo tena azikilenga shule za Waislamu. Hili ni jambo linatia shaka, kwanza: kwanini yalitokea mfululizo, pili kwanini yatokee katika shule za Waislamu?
Baadhi ya shule za Waislamu zilizokumbwa na ajali hizi ni pamoja na Ilala Isamic 04/07/2020, Kinondoni Muslim 17/07/2020, Mivumoni Islamic 18/07/2020, 23/07/2020, na 31/08/2020 yaani iliungua mara tatu ndani ya kipindi cha mwezi mmoja, African Muslim 26/08/2020, Istiqaama 27/09/2020 na tukio la karibuni la Uchira Islamic la 16/10/2020.
Iwapo tutasema ni khitlafu za umeme, maswali yanakuja, kwanini khitlafu hizo ijitokeze kwa shule kubwa zenye mrengo wa itikadi (dini) moja, Je ni shule wa Waislamu pekee ndiyo zina tatizo hilo?
Katika sintofahamu nyingine ni muda wa kutokea matukio haya. Tukiangalia tunaona kuwa matukio haya yanatokea muda ambao watu wamepumzika au wapo katika masomo. Ilala Islamic iliungua usiku, Istiqaama iliungua usiku, Uchira iliungua jioni, Mivumoni iliungua usiku na ikaungua tena asubuhi saa tatu na nusu, African Muslim iliungua asubuhi saa moja kasorobo, nk
Mida hii inaonesha ni aidha wanafunzi na walimu wanakuwa wamepumzika au wameshughulishwa na masomo, hivyo si rahisi kwa wao ambao ndiyo sehemu kubwa ya shule kujihusisha na mitambo inayoweza kuleta maafa kama pasi za nguo, kuchaji simu, kupika, nk. Hivyo hii inatupa hofu kuwa kuna uwezekano wa hujuma katika ajali hizi
Aidha, maeneo ambayo ajali hizi za moto unaanzia pia ni maeneo yanatia shaka sana ambayo ni mabweni na maeneo kama stoo. Kuhusu mabweni wahujumu wanaweza kabisa kukusudia kuzifanya shule hizi zifungwe kwa kukosa mabweni, au kushindwa kuyakarabati kwa haraka, au kwa kupoteza uaminifu kutoka kwa wazazi wa wanafunzi, nk. Hivyo wameona washambulie mabweni.
Amma kuhusu maeneo kama stoo amBapo moto ulianzia kwa shule kama Mivumoni inaonesha ni maeneo yasiyofikika na watu wengi hivyo wahujumu waliweza kutoonekana.
Vyombo vya usalama zimekuwa vikifuatilia matukio haya bila kuja na majibu ya kuridhishwa. Tangu matukio haya yaanze kutokea yakilenga shule za Waislamu nchini Tanzania hata kwa asiye na weledi wa masuala ya usalama anapata picha kuwa kuna uwezekano mkubwa wa hujuma.
Kama vyombo hivi vipo haraka sana kufanya uchunguzi katika baadhi ya maswala na kuyatolea tahadhari mfano uwezekano wa kutokea vurugu katika mikutano ya siasa, vipi washindwe kuchunguza na kuja na majibu sahihi kuhusiana na ajali hizi za moto katika shule za Waislamu!?
Kuna kauli zinazoweza kuwa na ukweli kwamba matukio haya ni kuungua moto shule za Waislamu ni aina ya hujuma za kudhoofisha Waislamu kimasomo kwa kuwa shule hizo zimeonekana kuwa na maendeleo mazuri katika miaka ya hivi karibuni. Kuanza kutoa matokeo ya kuridhisha katika miaka ya karibuni kunaweza kuwa kumewapelekea maadui wa Uislamu na Waislamu kufikiria kuzirudisha tena katika kukwama na hivyo kukosa soko kibiashara.
Katika matokeo ya kidato cha nne mwaka 2019 kwa mfano, shule ya Feza Boys ilikuwa ya 1 kati ya shule 237 kimkoa na 3 kati ya shule 3908 kitaifa, shule ya Feza Girls ilikuwa ya 6 kati ya shule 237 kimkoa, shule ya Al Hikma Boys ilikuwa ya 25 kati ya shule 237 kimkoa wakati Al Hikma Girls ilikuwa ya 17 kimkoa, shule ya Ilala Islamic ilikuwa ya 10 kati ya shule 237 kimkoa na 65 kati ya shule 3908 kitaifa, Uchira Girls ilikuwa ya 39 kati ya shule 276 kimkoa.
Ni wazi matokeo haya ya mwaka jana huenda yaliwachachafya wasiowapendelea kheri Uislamu na Waislamu na wakakusudia kuanza kampeni yao ya kuchoma moto shule kwa taswira ya ajali katikati ya mwaka 2020.
Dhana ya hujuma sio ya kupuuzwa kutokana na sababu za kimazingira na khistoria namna Waislamu walivyonyimwa elimu kwa njama na hujuma za kimfumo.
Kwa kumalizia Waislamu lazima tutambue kuwa chini ya ubepari hakuna dhamana ya usalama wa dini yetu, nafsi zetu, heshima yetu wala mali zetu. Ni wajibu wetu kulingania Uislamu wetu ili kurejesha tena mamlaka yake yatakayodhamini usalama wa Waislamu na wanadamu kwa jumla

 

Maoni hayajaruhusiwa.