Kanuni Mpya za Mafao ya Wastaafu Tanzania : Dhihirisho la Sera za Kibepari
Habari:
Serikali ya Tanzania imepitisha Sheria ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (The Public Service Social Security Act 2018), ambayo imezuwa tafrani, mkanganyiko na vilio miongoni mwa wafanyakazi. Sheria hiyo mpya imeunganisha mifuko yote na kuwa miwili tu, yaani :Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Ummah (Public Service Social Security Fund (PSSSF) na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Sekta Binafsi(National Social Security Fund (NSSF). Aidha, sheria hiyo imeanzisha mafao mapya ya kilaghai kama fao la urithi (survivor’s benefits) na fao la kukosa ajira (unemployment benefits). Pia sheria imeweka umri wa kustaafu kuwa ni miaka 60 kwa lazima, na miaka 55 kwa khiyari.
Maoni:
Kuunganishwa kwa mifuko ya wastaafu na kuwa miwili ni maelekezo kutoka taasisi ya kikoloni ya Shirika la Kazi la Kimataifa(ILO), jambo linalodhihirisha wazi wazi uhusiano wa kikoloni kati ya mataifa masikini na taasisi za kibepari za kikoloni.
Zaidi ya hayo, mabadiliko haya (ya kuunganisha mifuko) yamekuja kwa hoja ya kushindwa kwa mifuko hiyo kutoa huduma (mafao) ya kiwango stahiki kwa wateja wake, yaani wachangiaji wake. Lakini kiuhalisia hali hiyo imesababishwa kwa kukombwa fedha hizo kutoka mifuko hiyo ya wastaafu, ambapo deni la serikali kwa mifuko hiyo limekusanyika kufikia takriban shilingi trilioni 8 (The Citizen, 20/11/2018).
Kanuni mpya zimeweka kikokotoo kipya cha 25% badala ya 50% kama malipo ya mkupuo (lump sum payment) na 75% kuwa ni malipo ya kila mwezi, jambo lililoleta kilio kikubwa cha uchungu kwa wafanyakazi kama upanga mkali mgongoni mwao, kwani wengi wao hutegemea malipo ya mkupuo na fao la kujitoa (withdraw benefit) (ambalo limeshabatilishwa) kuendeshea maisha yao baada ya kustaafu au kukosa ajira.
Idhilali yote hii ya wazi na dhiki dhidi ya wafanyakazi wanyonge inajiri hali ya kuwa kila taasisi penye wafanyakazi nchini Tanzania kuna vyama vya wafanyakazi ambavyo hughilibu wafanyakazi kwamba wanasimamia haki zao. Ilhali katika sakata hili, wakati wadau wengine na baadhi ya watu mashuhuri wakipaza sauti zao na kuonesha kutokubaliana na jambo hili, vyama hivyo vya wafanyakazi vinaonekana kutochukua hatua za kutosha katika kulinda maslahi ya wanachama wao. Hili linafedhehi uhalisia wa vyama vingi vya wafanyakazi kula njama na serikali dhidi ya wafanyakazi, na wakati mwengine vyama hivyo hutumika kuwa kitulizo kwa waajiriwa.Uwepo wa mifuko hii ya hifadhi ya jamii ni matokeo ya mfumo muovu wa kiuchumi wa kibepari ambao umejengwa juu ya (maslahi) kujiongezea maslahi zaidi hata kwa kuwanyonya masikini wazee wastaafu. Wafanyakazi chini ya ubepari hawafaidi mishahara yao kutokana na msururu wa makato.
Nchini Tanzania mfanyakazi hukatwa 2% ya mshahara wake kwa ajili ya chama cha wafanyakazi, 3% bima ya afya,kuanzia 9% (baadhi hufika 20% kodi ya mapato(PAYE), baadhi hukatwa 15% mkopo wa elimu ya juu, 5% hifadhi ya jamii nk. Makato hayo humuacha mfanyakazi na vijisenti kiduchu, akiendelea kuzingirwa na janga la umaskini licha ya juhudi yake kubwa na jasho jingi katika kazi anayoifanya.
Kanuni hizi za kisheria na kandamizi zinaweka masharti magumu kwa mfanyakazi kupata fedha zake kuwa eti ni lazima afikie miaka 55 au 60. Ilhali makato ya mifuko hii ya hifadhi ya jamii hutumika katika vitega uchumi mara nyingi katika miradi ya riba, ambayo hunufaisha zaidi matajiri na wanasiasa wachache, badala ya kuwanufaisha wafanyakazi wanyonge ambao ndio wachangiaji wakuu.
Mfumo wa uchumi wa Kiislamu umeweka wazi sheria kuhusu umiliki wa mali, matumizi na utawanyaji, ambapo mali binafsi kama mshahara ni milliki ya mfanyakazi, na hairuhusiwi serikali au taasisi yeyote kumuingilia bila ya matakwa yake. Hivyo, taasisi kando, kama za mifuko ya hifadhi ya jamii, vyama vya wafanyakazi hazina nafasi katika Uislamu, na haziruhusiwi kuingilia kipato cha mfanyakazi.
Mfumo thabiti na imara wa uchumi wa Kiislamu chini ya Serikali ya Kiislamu (Khilafah) utaimarisha na kuvilinda vyanzo vya mapato kwa wananchi kama ajira, urithi, misaada ya serikali kwa wananchi, zawadi, tunu nk. bila ya kuviingilia kwa mujibu wa mipaka ya kisheria.
Kwa kufanya hivyo, kutainua hali za maisha kwa waajiriwa na kutadhamini usalama wa maisha yao hata katika umri wa uzee. Zaidi ya hayo kutakuwa na hatua thabiti na mahkama kwa ajili ya kulinda mahusiano mema baina ya waajiri na waajiriwa, iwe katika sekta za utumishi wa Umma au sekta binafsi. Kwa msingi huo hakutokuwa na vyama vya wafanyakazi.
Hapo utajiri utatawanywa kwa upana miongoni mwa raia wote, na hakutokuwa na fursa ya kuwanyima fursa ya utawanyaji huo wa utajiri kwa walio wengi.
كَي لا يَكونَ دولَةً بَينَ الأَغنِياءِ مِنكُم ۚ
“…(mali itawanywe kwa wangine pia) Ili isiwe ikizunguuka baina ya matajiri tu miongoni mwenu’’ [Al Hashr 7].
#UislamuNiHadharaMbadala
Imeandikwa na Said Bitomwa
Mjumbe wa Afisi ya Habari ya Hizb ut-Tahrir Tanzania
Kwa ajili ya Afisi kuu ya Habari ya Hizb ut-Tahrir
Maoni hayajaruhusiwa.