Kikokotoo Kipya cha Pensheni ni Janga kwa Wastaafu

بسم الله الرحمن الرحيم

Habari:

Hivi karibuni serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu ilitangaza kikokotoo kipya kwa ajili ya wastaafu ambacho kitaanza kutumika mwezi wa saba (Julai) mwaka huu 2022.

Maoni:

Kubuniwa kwa kikokotoo kipya ni matokeo ya makubaliano ya pamoja kati ya serikali, wadau wa sekta ya mfuko wa jamii ikiwemo Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) na Chama cha Waajiri(ATE).

Mwaka 2018 serikali ilianzisha kikokotoo kipya cha malipo ya penseni ambacho kilikataliwa. Kikokotoo kipya cha mwaka 2018 kilikataliwa kwa sababu kilijumuisha kupunguzwa kwa malipo ya mkupuo kutoka 50% hadi 25%. Katika kikokotoo kipya malipo hayo ya mkupuo ni 33% ambayo inamaanisha kuwa serikali imepunguza kutoka 50% ambayo ilikuwa ikilalamikiwa na wafanyakazi kwa muda mrefu, badala ya kuiongeza, serikali imepunguza hadi 33%

Kupata taswira halisi hapa ni kuwa, kama malipo jumla ya mfanyakazi (mstaafu) ni Tsh 100,000 kwa kikokotoo cha zamani ilikuwa analipwa Tsh 50,000 lakini kwa kikokotoo kipya atalipwa 33% ambayo ni Tsh 33,000. Kwa wafanyakazi wengi ambao mishahara yao ni midogo hutegemea haya malipo ya mkupuo ya kustaafu kwa ajili ya kuendeleza maisha yao kama kujenga nyumba, nk.

Kigawanyo cha penseni kwa sasa ni 1/580 kutoka 1/540. Serikali kwa makusudi imeongeza kigawanyo na hivyo kupunguza malipo ya mkupuo ya wastaafu. Kwa mfano, kama malipo jumla ya wastaafu ni Tsh 100,000 kwa kigawanyo cha mwanzo alikuwa akilipwa Tsh 185.18 lakini kwa kigawanyo kipya atalipwa Tsh 172.41 pekee. Hii ni mbinu nyingine ambayo serikali imeitumia na mwishowe ni mfanyakazi (mstaafu) ndiye anayeathirika zaidi au kunyonywa.

Kumekuwa na makubaliano ya pamoja juu ya umri wa wastani wa kuishi baada ya kustaafu kuwa ni miaka 12.5 na wastani wa mishahara ya miaka mitatu ndani ya miaka kumi kabla ya kustaafu katika kufanya mahesabu ya malipo ya penseni ya kustaafu. Wastani wa umri wa kuishi baada ya kustaafu ilikuwa miaka 15.5 katika kikokotoo cha awali, lakini serikali imeupunguza mpaka miaka 12.5 tu.

Katika kanuni ya mahesabu ya malipo ya penseni, jinsi idadi ya miaka ya kuishi baada ya kustaafu inavyokuwa mingi ndivyo na malipo ya penseni ya kustaafu inapokuwa kubwa. Hivyo, kwa miaka 12.5 inamaanisha malipo kidogo zaidi ya pensheni ya kustaafu ukilinganisha na ilivyokuwa miaka 15.5.

Hizi zote ni mbinu ambazo serikali imezitumia katika kucheza na kanuni ya mahesabu ya malipo ya penseni ya kustaafu ili wastaafu wabakie na pesa kidogo na serikali ibakie na pesa nyingi za wastaafu. Hii ni kwa sababu hali ya sasa ya mifuko ya hifadhi ya jamii ni mbaya sana, na mingi  imefilisika kutokana na mikopo mikubwa ya serikali na kwa matumizi ya miradi mikubwa hali iliyopelekea kuunganishwa kwa mifuko ya GEPF, LAPF, PPF na PSPF na kuwa mfuko mmoja wa PSSSF tangu mwaka 2018.

Ni jambo lisiloepukika chini ya mfumo wa Ubepari na kanuni yake ya kiuchumi ya uhuru wa kumiliki ambayo hufinyanga jamii yenye ubinafsi na unyonyaji ambapo wafanyakazi duniani kote wanakabiliwa na unyonyaji mkubwa katika nyanja zote ikiwemo mishahara duni, pensheni hafifu, ukosefu wa usalama mahala pa kazi, nk. Zaidi, Ubepari umeundwa katika msingi wa kupata maslahi zaidi kwa gharama yoyote hata kwa kudhuru na kudhulumu wengine ikiwemo wafanyakazi.

Katika jaribio la kupozapoza migogoro katika ajira, Ubepari unahamasisha kuundwa vyama vya wafanyakazi ambavyo kiuhalisia navyo ni sehemu ya tatizo.

Katika hali kama hii haishangazi kuona vyama vya wafanyakazi vikiwa kimya na kushindwa kuwasaidia wafanyakazi/wastaafu, na hivyo serikali imefanikiwa kupunguza kigawanyo cha pensheni kutoka 540 mpaka 580, malipo ya mkupuo kutoka 50% Hadi 33% na wastani wa umri wa kuishi baada ya kustaafu kutoka miaka 15.5 mpaka 12.5, na bado vyama vya wafanyakazi havikufanya chochote kusaidia wafanyakazi/ wastaafu.

Uislamu una mtazamo tofauti kuhusu masuala ya kazi na ajira kinyume na mifumo mingine yote ulimwenguni. Katika kanuni zake muhimu katika sera ya kazi na ajira ni pamoja na kuwepo uhusiano thabiti wa aina yake wenye mahusiano ya usawa kati ya muajiri na muajiriwa, kutolewa kwa malipo (ujira) muwafaka na kuwepo kwa mahakama maalumu inayoitwa ‘Maadhalim’ katika dola ya Kiislamu ambayo itahakikisha inafuatilia kwa karibu kuhakikisha watawala hawavunji sheria au au kufanya matumizi mabaya ya madaraka ikiwemo kulinda haki za wafanyakazi wa serikali.

Pia Uislamu chini ya dola yake ya Kiislamu ya kiulimwengu ya Khilafah unahamasisha na kulinda mazingira ya kazi yasiyo ya kinyonyaji kwa wafanyakazi.

Imam Bukhari amepokea kutokana na Abu Hurairah (ra) kuwa Mtume (saw) amesema; Mwenyezi Mungu (swt) anasema kuwa:

«ثَلَاثَةٌ أَنَا خَصْمُهُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ رَجُلٌ أَعْطَى بِي ثُمَّ غَدَرَ وَرَجُلٌ بَاعَ حُرًّا فَأَكَلَ ثَمَنَهُ وَرَجُلٌ اسْتَأْجَرَ أَجِيرًا فَاسْتَوْفَى مِنْهُ وَلَمْ يُعْطِ أَجْرَهُ»

“Watu aina tatu nitakuwa na husuma nao Siku ya Qiyama: mtu aliyechukua dhamana kwa jina langu kisha akafanya khiyana, na mtu aliyemuuza mtu huru kisha akala thamani yake (pato la kumuuza) na mtu aliyemuajiri mfanyakazi na mfanyakazi akamfanyia kazi yake kwa ukamilifu lakini hakumlipa ujira wake” (Sahih Bukhari, namba 430)

Pia imesimuliwa kutoka kwa Abdullah Bin Umar kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema:

«أَعْطُوا الأَجِيرَ أَجْرَهُ قَبْلَ أَنْ يَجِفَّ عَرَقُهُ»

“Mlipe mfanyakazi ujira wake kabla jasho lake halijakauka” (Sunan Ibn Majah)

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Said Bitomwa

Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Tanzania

Maoni hayajaruhusiwa.