‘Arafah’ Inatukumbusha Kukamilika Kwa Uislamu

بسم الله الرحمن الرحيم

Allah Taala anasema:

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمْ الإِسْلاَمَ دِينًا…. (المائدة: 3)

“Leo nimekukamilishieni dini yenu, na kukutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni Uislamu uwe dini yenu” (Al-Maidah: 3)

Moja kati ya jambo la kukumbukwa lililotokea katika hijja ya kuaga ya Mtume SAAW ni kuteremka kwa ayah hii siku ya Arafah. Ayah ambayo imebeba ujumbe mzito kwa Waislamu wa zama zote na hasa kwa wakati huu ambao tunaishi bila ya usimamizi wa Kiislamu kikamilifu chinI ya serikali yake ijulikanayo kama Khilafah.

Ama tukichambua ujumbe uliomo ndani ya ayah hii ni lazima tuzingatie nukta zifuatazo:
1) Ayah imeelezea ‘Ikmal’ yaani kutimia kwa dini yetu. Jambo hili linamlazimu kila Muislamu kukinai kwa umakinifu ya kuwa dini ya Uislamu imetimia na ina uwezo wa kumtatulia mwanadamu kila tatizo analokutana nalo liwe la kiibada, siasa, jamii, uchumi nk. Bila shaka Uislamu umemlazimisha mwenye kutaka kuingia ndani yake ni lazima akiri aqeedah yake yenye kukinaisha akili ambayo ni kukiri kuwa hakuna anayepaswa kuabudiwa na kumpangia mwanadamu taratibu za kimaisha ila Allah tu! Na kwamba Mtume SAAW ni Mjumbe wake na aliyetumwa ili awafahamishe watu jinsi ya kumuabudu Allah Taala na kufuata taratibu zake. Kwa hivyo, Muislamu ni faradhi kila anachokifanya kiwe amekuja nacho Mtume SAAW Kinyume chake atakuwa fasiq au kafiri akipinga.

Sasa tujiulize jee Uislamu umeshindwa kumtatulia mwanaadamu nidhamu ya kisiasa na kiutawala hata Waislamu leo wawe ndio wa mbele katika kufuata siasa na tawala za ubepari? Bila shaka kila Muislamu atajibu kuwa haukushindwa. Basi ni jambo gani linawafanya wafanye hivyo? Hapa ni lazima kila Muislamu kadiri atakavyolijibu swali hilo ajue dini imetimia, hivyo wachukue njia ya Mtume SAAW ya kutawala na kuongoza kwa dini ya Allah Taala na sio dini ya kikafiri. Na ni lazima Waislamu wajue itikadi ya Kiislamu kwa hoja na jinsi inavyotatua matatizo na sio bila ya ufafanuzi. Aidha, Waislamu waijue nidhamu ya kibepari na jinsi ili tuiwache na kujiepusha, kwani tukiifuata itakuwa kama tumekinai kuwa Uislamu hauna suluhisho la matatizo ya mwanaadamu yote ila kusali, kufunga, kuhiji tu.

2.) Ama nukta nyengine ambayo yapasa kuzingatia ni ‘Itmam’ yaani kutimiza Allah SW neema yake kwetu sisi. Basi tunatakiwa tujiulize ni neema ipi hiyo?

Bila shaka kwetu sisi waislamu hakuna neema kubwa zaidi kuliko Uislamu. Kama hivyo ndivyo ilivyo basi kwanini leo Waislamu tunaiwacha neema hii na kushika laana? Kwa masikitiko kuna baadhi ya Waislamu hudiriki kusema kivitendo wacha tuuweke Uislamu kando kisha tushirikiane na makafiri katika kuandaa katiba, kutawala na kufanya siasa nao ili tupate haki sawa sisi na wao kwani tukifuata Uislamu neema yetu, wao watanyanyasika?

Je upo ujinga zaidi ya huu wa kukataa neema alivyotuneemesha nayo Allah SW? kwanini leo baadhi waone kuwa utukufu wetu utakuwa kwa kufuata mfumo wa kikafiri wa kidemokrasia na ndio ukombozi?
Kwa hakika inatupasa Waislamu aina hiyo watubu na turudi na tujue ya kuwa kwa kufuata na kuishika neema yetu ndio pekee tutapata utukufu na si venginevyo.

3. Ayah imemalizia kwa kuonesha kuwa Allah SW ameridhia ya kuwa Uislamu iwe ndio dini (mfumo) yetu na si venginevyo. Basi ni lazima kwa kila Muislamu aridhike na Uislamu kama anataka kupata radhi za Allah hapa duniani na kesho akhera.

Je sisi hatusomi au hatuoni jinsi gani Bani Israel walipoacha mfumo alioridhia Allah walifanywa nini? Au ndio sisi tuliobeba mzigo tusioujua thamani yake? Allah atuepushe tusiwe miongoni mwao.

Enyi Waislamu tunawataka kupitia Hijjah ya mwaka huu kuikumbuka Ayah hii tukufu iliyoshuka siku ya Arafah katika Hijja ya Kuaga. Aya hii imeondosha dharura za kushika mifumo mengine kinyume na Uislamu kwa kuonesha ukamilifu na utimilifu wa Uislamu. Hivyo tuushike Uislamu wetu kwa magego ili tupate kuridhiwa na Allah SW

Maoni hayajaruhusiwa.