Maonesho Ya ‘Nane Nane’ Tu Hayatoinua Sekta Ya Kilimo
بسم الله الرحمن الرحيم
Kila tarehe 8 Agosti ya kila mwaka ni siku ya Sikukuu ya Wakulima nchini Tanzania ambayo hujulikana zaidi kama Nane Nane. Katika sherehe hizi wakulima, taasisi na wadau mbalimbali wa kilimo, mifugo na uvuvi kote nchini huonesha bidhaa zao.
Kihistoria sikukuu hii ilianzishwa mwaka 1977, awali ilikuwa ‘Saba Saba’ ikiadhimishwa kila tarehe 7 Julai. Baadae mwaka 1990 ilihamishiwa kuwa Agosti, 8 na kufahamika zaidi kwa maonesho ya wafanyabiashara na hivyo imeendelea kuadhimishwa kila mwaka.
Licha ya maonesho haya ambayo hugharimu pesa nyingi kuyafanikisha kila mwaka tangu mwaka yalipoanzishwa 1977, bado sekta hii ya kilimo, mifugo na uvuvi havijaweza kutumika ipasavyo kumkomboa maskini ikiwa ni uti wa mgongo wa maisha yake ya kiuchumi.
Hali hii inatokana na ukweli wa uduni wa kifikra / kimfumo hali inayopelekea kukosekana utayari thabiti katika kusaidia wananchi licha ya uwepo wa rasilimali nyingi ambazo zinaweza kutumika kuboresha sekta hizo zinazogusa wengi katika kuendesha maisha yao.
Tanzania ina ardhi pana na yenye rutba kwa kustawisha mazao mbalimbali ya chakula na biashara lakini bado sekta hii haijatumika ipasavyo.
Kwa upande wa mifugo na uvuvi ambavyo huchangia katika pato la taifa, ambapo mifugo huchangia 7.4% na uvuvi 1.71% (Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Hotuba ya Bajeti, 2020/21), Tanzania ina idadi kubwa ya mifugo, ikiwa ni ya pili barani Afrika baada ya Ethiopia.
Kwa mujibu wa sensa ya wanyama ya mwaka 2017, Tanzania inakadiriwa kuwa na takribani ng’ombe milioni 30.5, mbuzi takribani milioni 18.8, kondoo takribani milioni 5.3, mifugo mingine iliyopo ni pamoja na kuku wa kienyeji takriban milioni 38.2, na kuku wa kisasa takribani millioni 36.6 Bila ya kusahau uwepo wa maziwa mawili makubwa, ziwa Victoria na ziwa Tanganyika na zaidi ya kilomita 1,500 za bahari ya Hindi. Zote zikisheheni samaki, rasilmali bahari nk.
Sekta ya kilimo inakabiliwa na changamoto nyingi sana ikiwemo ukosefu wa mitaji au rasilimali fedha kwa ajili ya kilimo chenye tija, upatikanaji wa pembejeo bora na huduma za ugani kwa wananchi hasa wa vijijini, upatikanaji wa miundombinu bora ya kilimo cha umwagiliaji, upatikanaji wa masoko ya uhakika ya bidhaa za kilimo, ukosefu wa miundombinu ya barabara za kusafirishia mazao, elimu ya kilimo, mbinu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kuhifadhi mazingira nk.
Pia katika sekta ya elimu kuna ukosefu wa upatikanaji wa elimu ya ujasiriamali na biashara katika mazao ya kilimo, mahusiano mema kati ya wakulima ambao ni wananchi masikini na wadau wa sekta ya kilimo katika kupata fursa mbalimbali za kilimo, kuhamasisha shughuli za kilimo zenye mvuto ili kuwavutia watu wengi zaidi hususan vijana kuwekeza kwenye kilimo nk.
Licha ya mipango na tafiti nyingi ambazo serikali imefanya katika sekta ya kilimo bado hazijaleta tija stahiki kwa sababu imekuwa ni mipango inayoishia kwenye makaratasi bila ya kufanyiwa kazi.
Kwa mfano kumewahi kuasisiwa sera nyingi kama vile “Kilimo Kwanza” au mpango wa hivi karibuni unaoitwa “Mkakati wa Taifa wa Ushirikishwaji Vijana kwenye Kilimo 2016-2021” ambao ulilenga kuleta maendeleo ya uchumi wa Taifa kupitia shughuli mbalimbali kwa kufuata mnyororo wa thamani katika sekta ya kilimo ambazo ndiyo msingi mkuu wa uchumi wa Taifa ili kupunguza tatizo la ajira kwa vijana, kuainisha fursa zilizopo katika sekta ya kilimo; kupunguza tatizo la umaskini na kuinua uchumi kiujumla.
Lakini mpaka Mkakati huu utaisha mwaka huu hakuna kilichofanikiwa katika malengo yake kama ilivyokuwa mikakati, mipango, na sera zilizopita kabla yake na zitakazokuja baada yake.
Tunaona badala ya serikali kukabiliana na changamoto za kilimo ambacho inakiri kuwa kinaajiri takribani 75% wa watu, kinyume chake ilihamisha sera na kupeleka kwenye viwanda ambayo imefeli kabla haijaanza, kwani ni ndoto viwanda kuendelea bila ya kilimo.
Msingi mkuu wa matatizo yote haya ni mfumo fisidifu wa kibepari ambao unatumika kuendesha serikali na usimamizi wa mambo iwe sera au mikakati. Mfumo huu ambao msingi wake ni Umaslahi yanayozaa ubinafsi huwafanya viongozi, watawala na watumishi wake kutokujali matatizo na masuala nyeti yanayogusa wananchi maskini walio wengi.
Viongozi hufuja pesa nyingi za Ummah kwa tafiti zisizoisha na maonesho ambayo hawayafanyii kazi baada yake. Hata mafanikio makubwa yakipatikana basi yatakuja kwa wachache matajiri na wengi watabakia na changamoto bila ya msaada wowote.
Ili kutatua changamoto za kilimo hulazimu kutatua tatizo la kimfumo kwanza, kwa kuondokana na mfumo wa kibepari kwenda katika mfumo wa uadilifu wa Uislamu ambao umetandika sera thabiti juu ya ardhi, kilimo na vyanzo vikubwa vya maji ambavyo umevifanya kuwa ni mali ya Ummah isiyofaa kumilikishwa wachache.
Aidha, serikali ya Kiislamu ya Khilafah itawekeza katika kilimo kwa nafasi yake kama msimamizi wa Ummah ili kunufaisha jamii na ustawi wa watu, itawezesha utambuzi wa fursa zilizopo kwenye sekta ya kilimo na kuzifanyia kazi. Hii ikiwemo kusambaza pembejeo, taaluma ya kilimo na kuwakwamua kwa mikopo isiyo na riba wakulima masikini walio wengi ili waweze kujiajiri kwenye sekta ya kilimo na kuchangia ustawi wa maisha yao.
Said Bitomwa
Risala ya Wiki No. 111
04 Muharram1443 Hijri / 12 Agosti 2021 Miladi
Maoni hayajaruhusiwa.