Ubepari Unamtendea Kijana Dhulma Kubwa!
بسم الله الرحمن الرحيم
Mwishoni mwa mwaka 1999 Umoja wa Mataifa kupitia Azimio lake no. 54/120 uliwafiki pendekezo la Mkutano wa Kilimwengu wa Mawaziri wa Masuala ya Vijana kuifanya siku ya tarehe 12 Agosti ya kila mwaka kuwa Siku ya Vijana Kimataifa. Tangu wakati huo maadhimisho ya siku hiyo hufanyika kila mwaka ulimwenguni kote.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni : “Kufanya Mabadiliko katika Mfumo wa Masuala ya Chakula: Ubunifu wa Vijana kwa Afya ya Wanahadamu na Ulimwengu “
Kauli mbinu hii inalenga umuhimu mkubwa wa kuwa na chombo cha pamoja kitakachohakikisha vijana wanapaza sauti kibinafsi na kipamoja kuilinda sayari ya ulimwengu na kulinda maisha, kwa kutumia bio anuai ili kuweza kubadilisha mfumo wa masuala ya chakula. Hili ina maana pia ya kuhusisha kampeni ya kukabiliana na changamoto mbalimbali kama mabadiliko ya tabianchi, huduma za afya, kujenga jamii jumuishi, kulinda mazingira nk.
Vijana ni tabaka miuhimu kwa ustawi wa jamii yoyote tangu kuumbwa jamii ya wanadamu mpaka Siku ya Hisabu. Aidha, ni medani muhimu inayoshindaniwa katika kulinda, kutetea fikra amma iwe fikra ya kiroho au ya kimfumo. Kwa maneno mengine tuseme vijana ni tabaka nyeti mno kwa maendeleo ya mwanadamu kwa jumla.
Mfumo wa kibepari unaelewa unyeti wa vijana na umo katika mashindano makubwa kuwavuta vijana upande wake. Lakini kutokana na fikra batil na fisidifu za mfumo huo wamemtumbukiza kijana katika dimbwi la hatari na madhara makubwa. Kiasi cha kuteteresha muhimili wa ustawi wa binadamu kwa jumla.
Fikra za ‘uhuru’ za nidhamu ya kidemokrasia zimewafanya vijana wengi ndani ya nchi za Magharibi hadi nchi changa kujihusisha na vitendo vya kutisha kama uhuni, utumiaji wa nguvu, ulevi wa kupindukia nk. Kiasi kwamba imekuwa ni ajenda ya vijana ni miongoni mwa mambo yanayoumiza vichwa katika wapangaji wa sera za masuala ya kijamii. (Social Policy makers)
Ukweli ni kuwa hadhara/ fikra ya mfumo wa kibepari imejengwa juu ya msingi batil na wa hatari. Nayo inamuonesha kijana au mwanadamu kwa jumla kwamba upeo wa mafanikio yake katika ulimwengu huu ni kukithirisha kujikusanyia starehe za ulimwengu.
Fikra hii imemtia dhiki na mashaka makubwa kijana na jamii kwa jumla. Kwa kuwa inamuonesha na kumjenga kijana kuwa ili aweze kudiriki upeo na kilele cha udhati wa ufanisi/saada katika maisha yake ni kuutumia ujana wake kwa kujifaragua na kuogelea na kuzama katika bahari ya starehe.
Jambo hili humsababishia usumbufu mkubwa na kumkosesha utulivu kijana na mwanadamu yoyote. Na kimsingi kumfanya mwanadamu aishi katika maisha ya ndoto. Kwa kuwa, viwe viwavyo mwanadamu kamwe hawezi kushindana na starehe za kidunia.
Kwanza, ana mipaka maalumu ya kinguvu na uwezo katika kukidhi starehe hizo.
Pili, umri wake kila siku unazorota kiasi cha kumfanya kushindwa kuzama katika starehe hizo ipasavyo.
Tatu, ni kitu kisichowafikiana na uhalisia kamwe kwamba mwanadamu ana uwezo wa kuzikamilisha starehe zote za kilimwengu. Kwa mfano, katika wanazodai starehe maarufu katika mfumo wa kidemokrasia ni ulevi. Lakini ukweli mtu hunywa ulevi kwa kiwango fulani. Amma starehe za kimwili na maingiliano baina ya wanawake na wanaume pia yana kiwango maalum. Na isitoshe kadiri umri wa mwanadamu unavyosonga mbele wanadamu wapya wazuri wa sura huendelea kuzaliwa. Hii ndio kanuni ya maumbile. Waswahili husema: “wazuri haweshi”. Katika uhalisia kama huo vipi mwanadamu ataweza kukidhi matamanio yake kwa wazuri wote ? hata kama ana uwezo kiasi gani. Hapo utaona kijana chini ya mfumo wa kidemokrasia yumo katika maangamizi kwa kuona hafikii upeo wa starehe unaolinganiwa na mfumo wao.
Hatimae, ujana wake huyoyoma kama moshi, hakuchuma chochote zaidi ya kuathirika siha na afya yake kwa ulevi, madawa ya kulevya, zinaa na kumaliza fedha zake nyingi katika kumbi za starehe na si zaidi ya hayo.
Kwa hivyo, hadhara ya mfumo wa kibepari imekuja kumuangamiza kijana, kumtia wasi wasi na kumfanya aishi katika ulimwengu wa ndoto unaomkosesha raha kwa kumuahidi kitu kisichowezekana katika uhalisia kamwe! Kwa hakika Mfumo huu haufai kuwepo diuniani unatenda dhulma kubwa kwa vijana na wanadamu kwa jumla.
Uislamu umekuja kumtuliza na kumpa sakina ya nafsi kijana. Kwanza, kwa kumpatia majibu ya masuala ya msingi ya mwanadamu. Uislamu unafafanua kijana anatoka wapi, yupo duniani kwa lengo gani, na anakwenda wapi. Aidha, unaweka wazi nini fungamano la maisha ya kijana hapa duniani na kabla hajaja duniani. Pia lipi fungamno la maisha ya kijana hapa duniani na maisha yajayo baada ya kuondoka hapa duniani. Majibu ya masuala hayo huyahitaji kimaumbile kijana tena kwa ufafanuzi hususan anapofikia balegh. Na majibu hayo ni nyeti kwa kijana, licha ya kuwa kila mwanadamu ana ghariza/ hisia ya kimaumbile ya kuabudu inayompa hisia ya unyenyekevu kutokana na kuhisi kuwa kaumbwa na Mola, Mwenye nguvu na Mwenye kumiliki kila kitu.
Baada ya Uislamu kufafanua nafasi ya mwanadamu katika ulimwengu huu na mafungamano yake, ambayo hiyo ndio aqeedah. Sasa ukamtaka kijana kutumia fursa adhimu ya ujana wake kufungamanisha ufafanuzi au majibu aliyopatiwa kivitendo katika kumcha Mola wake kwa kujiandaa na maisha yajayo.
Zaidi, Uislamu ukamtaka kijana asibakie kuwa goigoi bila ya majukumu ya kijamii. Ukamtaka abebe jukumu ziada la khiyari yaani ndoa. Kuowa au kuolewa. Aidha, ukamlazimisha kubeba majukumu mengine ya wajibu ikiwemo kuwatunza wazazi na kuamiliana nao kwa ihsan hususan wakiwa wazee sana. Pia na kufungamana kwa wema na ndugu na jamaa zake.
Quran imekuja kuonesha katika aya nyingi namna uzee unavyoambatana na udhaifu na unyonge. Na namna ujana unavyoambatana na nguvu, msimamo na nishati. Hilo likiwa na maana ya kumtanabahisha kijana. Kwanza, katika kuamiliana na wazee awe ni mwenye rehma kwao. Lakini pili, kijana aitumie vyema fursa ya nishati ya ujana wake kabla haujamalizika.
Mtume SAAW anasema:
إِغْتَنِمْ خَمْسًا قَبْلَ خَمْسِحَيَاتِكَ قَبْلَ مَوْتِكَوَصِحَّتَكَ قَبْلَ سَقْمِكَوَفَرَاغَكَ قَبْلَ شُغْلِكَوَشَبَابِكَ قَبْلَ هَرَمِكَوَغِنَاكَ قَبْلَ فَقْرِكَ”
“Patiliza mambo matano kabla ya matano: Uhai wako kabla ya kifo chako, siha yako kabla ya maradhi yako, faragha yako kabla ya shughuli zako, ujana wako kabla ya uzee wako, na utajiri wako kabla ya ufukara wako.”
(Imesimuliwa na Ibn Abbas na kupokewa na Al-Hakim)
Kwa ufupi, mfumo wa Kiislamu sio mfumo wa ubabaishaji au wa kumueleza mwanadamu mambo yasiyokubalina na uhasia. Uislamu unamwambia kijana kwamba kuna Muumba, atumie ujana wake vyema kwa kwa kuwa unapita, abebe jukumu la familia ili watoto waje wamsaidie katika uzee wake kama yeye anavyowasaidia wazazi wake leo. Na la mwisho unamuonesha kwamba saada/ mafanikio ya kweli ni kupata radhi za Muumba kesho akhera kwa kuwa huwezi kufikia kilele cha saada katika dunia hii inayopita.
Majibu haya yote ni ya msingi kwa kijana yanakubalika kiakili na uhalisia, na hakuna mwanadamu mwenye akili iliyotuwama vyema (salim) atakayepinga haya. Na hii ni dalili kuwa dini hii ni ya haki inayowafikiana na maumbile ya mwanadamu na inayogusa masuala ya uhalisia.
فَأَقِمْ وَجْهَكَ لِلدِّينِ حَنِيفًا فِطْرَةَ اللَّهِ الَّتِي فَطَرَ النَّاسَ عَلَيْهَا لاَ تَبْدِيلَ لِخَلْقِ اللَّهِ ذَلِكَ الدِّينُ الْقَيِّمُ وَلَكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لاَ يَعْلَمُونَ (الروم: 30).
“Basi uelekeze uso wako sawa sawa kwenye Dini – ndilo umbile la Mwenyezi Mungu alilowaumbia watu. Hapana mabadiliko katika uumbaji wa Mwenyezi Mungu. Hiyo ndiyo Dini iliyonyooka sawa. Lakini watu wengi hawajui.” (TMQ ARRUM:30)
Maoni hayajaruhusiwa.