Rajab Mwezi wa Faraja kwa Walimwengu

Tukiwa ndani ya mwezi mtukufu wa Rajab uliosheheni mambo mengi ya kheri na misiba katika tareekh ya Kiislamu. Ndio mwezi wa tukio kubwa la Mtume wetu SAAW kwenda safari ya kimiujiza ya Israi na Miiraj. Aidha, ni mwezi huu ndio Jemadari wa Kiislamu Salahudiin Ayoub alipokomboa miji ya Waislamu ukiwemo Msikiti Mtukufu wa Aqswa uliokuwa katika mikono ya maadui wa Vita vya Msalaba (Crusaders). Kubwa zaidi ni mwezi huu ndio madola ya magharibi ya kikoloni baada ya mikakati ya muda mrefu walifanikiwa kuingusha dola ya Kiislamu ya mwisho ya Khilafah Uthmania ndani ya tarehe 28 Rajab 1342 / 3 Machi1924.
Safari ya Mtume SAAW ya Israi na Miiraj ilijiri katika kipindi ambacho Mtume SAAW alikuwa na hali ngumu, baada ya Makureishi kukataa ujumbe wake na wakitenda vitendo mbalimbali vya dhulma dhidi yake na wafuasi wake. Aidha, ni kipindi hiki ndio Mtume SAAW aliondokewa na Ami yake aliyekuwa muhimili muhimu kumpa msaada kama mzazi. Hata hivyo, mara baada ya safari hii ya kimiujiza Mtume SAAW alipata nusra kwa kuungwa mkono na kupatiwa mkataba wa kukabidhiwa hatamu za utawala (ba’aya) na makabila ya Aus na Khazraj ya Madina. Huo ukawa ndio mwanzo wa kuasisi dola ya Kiislamu ndani ya Madina iliyotekeleza Uislamu kivitendo na kudumu kwa makarne. Hapana shaka yoyote tukio la Israi na Miiraj lilikuwa chanzo cha faraja na ushindi kwa Mtume SAAW, Uislamu na Ummah wake.

Halkadhalika, tukio la Jemadari Salahuddiin Ayoub kuwashinda makafiri na kuikomboa miji ya Kiislamu pamoja na Msikiti Mtukufu wa Aqswa lilijiri mnamo tarehe 27 Rajab 583/ Oktoba 1187, baada ya miaka ya 88 ya Waislamu kupigana na Makruseda. Vita vya Msalaba viliasisiwa mwaka 1095 miladi na makafiri kwa uadui wao dhidi ya Uislamu, Waislamu na miji yao. Baada ya ushindi huo, Msikiti Mtakatifu wa Aqswa ukarudi katika mikono ya Waislamu. Wakiristo katika miji ya Waislamu kama biladu Shaam/Syria hawakuwa nyuma katika vita hivi, bali waliungana bega kwa bega na Waislamu dhidi ya wakiristo wa Ulaya, kutokana na uadilifu na insafu waliyoishuhudia wakiristo hao katika zama zote chini ya utawala wa Kiislamu. Ushindi huu ulikuwa faraja kubwa kwa Umma wa Kiislamu na kwa wanadamu kwa jumla.

Amma tukio la kuangushwa Khilafah lililotokea pia kipindi hiki cha Rajab, ni msiba mkubwa kwa Ummah wetu na wanadamu kwa jumla. Limepelekea kutotawaliwa kwa Uislamu, kupotea amani, kwa Waislamu khaswa na wanadamu kwa jumla. Khilafah ilisimamia haki za makundi yote kwa uadilifu, insafu na kwa mafanikio makubwa. Wakati leo tunashuhudia Waislamu kuteswa na kuuliwa kwa ukatili usioelezeka ndani ya, Syria, Iraq, Afghanistan, Afrika ya Kati, Burma, India, China, na mauaji ya karibuni zaidi ya nchini New Zealand. Aidha, wakaazi na wakimbizi wa Kiislamu katika nchi za magharibi na sehemu nyengine wanapewa daraja duni, ilikuwa Julai 1492, wakati Waislamu na mayahudi walipofukuzwa kwa agizo maalumu la serikali ya Hispania (Spanish Inquisition) Khalifah Bayezid II alituma manuari maalumu chini ya Kamanda Kemal Reis kuwaokoa Waislamu na mayahudi, na akawapa hifadhi ya ukimbizi mayahudi zaidi ya 150,000 http://ilmfeed.com/when-the-islamic-state-saved-150000-jews/
Aidha, wakati leo nchi za magharibi na sehemu nyengine kukiwa na wimbi kubwa la uadui dhidi ya Uislamu na kuwaandama Waislamu kutokana na dini yao, itakumbukwa kuwa mwaka 28 Hijria/ 638 miladi) baada ya dola ya Khilafah kuukomboa mji wa Aelia (Palestina), na wakaazi wake kuusalaimisha mji huo kwa ridhaa ya nafsi zao chini ya Askofu wao Mkuu Bwana Sophronius, Khalifa Umar ra. aliandika waraka mtukufu wa kihistoria unaosomeka: Huu ni waraka wa mkataba kutoka kwa Umar, mtumwa wa Allah, Kiongozi wa Waislamu, kwa watu wa Aelia. Anadhamini usalama wa maisha yao, mali zao, makanisa yao na misalaba yao…Makanisa yao yasivunjwe wala yasiondoshwe, na kisiondoshwe chochote katika vitu vyao. Wasilazimishwe katika mambo ya dini, na asidhuriwe yoyote……”
https://www.islamicity.org/…/capture-of-jerusalem-the-trea…/

Dola iliyoyasimamia hayo kwa bahati mbaya ndiyo iliyoangushwa mwezi huu wa Rajab na kuwatumbukiza Waislamu na wanadamu katika dimbwi la dhulma ya mfumo wa kibepari leo. Tunawasihi Waislamu licha ya kuwa na huzuni na machungu kwa kupoteza dola yetu ya Kiislamu (Khilafah), pia mwezi huu wa Rajab utuhamasishe kuongeza juhudi zetu kuirejesha tena dola hiyo inayopaswa kuanzia katika nchi kubwa za Waislamu kwa kutumia njia (manhaj) ya Mtume SAAW ya mapambano ya kifikra na kisiasa, sambamba na hilo tukiwa na imani thabiti ya kurejea kwake, kama alivyobashiri Mtume SAAW aliposema :
“ Kisha itarudi tena Khilafah kwa manhaj ya Utume”

#RajabuFarajaKwaWalimwengu

29 Rajab 1440 Hijri / 05 Aprili 2019 Miladi
hizb.or.tz
https://web.facebook.com/HtTanzaniaa/

Maoni hayajaruhusiwa.