Mapambano Dhidi ya Ushoga Tanzania
Vyombo vya habari vya Tanzania na nje karibuni vimeripoti juu ya qadhia ya kampeni ya kupambana na ushoga katika jiji la Dar es Salaam iliyoasisiwa na Mkuu wa Mkoa huo, iliyodumu kwa kipindi kifupi, kisha ikafa kifo cha ghafla, baada ya serikali kuu kutangaza kutohusika na harakati hizo.
Qadhia hii iliasisiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, mkoa wa jiji kuu la Tanzania ambao umeshamiri vitendo vya ushoga. Mkuu wa Mkoa wa Da es Salaam aliunda kamati maalumu kufuatilia na kumsaidia katika kupambana na vitendo vya ushoga, akitoa namba maalum za simu kwa yoyote mwenye taarifa za wenye kujihusisha na vitendo hivyo.
Hata hivyo, mpango huo wa mkuu wa mkoa wengi wameufasiri kama mbinu ya kuwatoa watu katika qadhia muhimu zinazojiri ndani ya mkoa wake, likiwemo suala la kutekwa mfanyabiashara mkubwa, bilionea Mohammed Dewji ambalo limeacha maswali mengi kuliko majibu, changamoto ya kushindwa kwa mabasi ya mwendo kasi kutoa huduma ipasavyo jijini, na qadhia nyingi kubwa za kitaifa. Hivyo, qadhia ya kukabiliana na vitendo vya ushoga ni kama jaribio la kuzichota hisia jumla za watu kutoka katika qadhia nyeti na kuzilekeza katika vita dhidi ya ushoga, kwa kuwa walio wengi hawakubaliani kabisa na vitendo hivyo vya ushoga.
Kampeni hiyo tahamaki ikapata upinzani mkubwa kimataifa, wanaharakati na watetezi wa haki za binadamu ndani na nje, na likaibuka shinikizo la kupingwa kimataifa, wakikumbusha kuwa, Tanzania rasmi imesaini na kuridhia mkataba wa kimataifa unaodhamini na kulinda haki za kiraia ndani ya jamii.
Shinikizo hilo likapelekea Wizara ya Mambo ya Nje Tanzania kuikana kampeni hiyo, na kutangaza wazi kuwa kampeni hiyo ya Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam ni suala lake kibinafsi, na kusisitiza kuwa Tanzania itaendelea kuheshimu na kushikamana na mikataba yote ya kimataifa iliyosaini na kuiridhia. Sambamba na hilo, Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia Waziri wake ikahakikisha kutoa ulinzi na usalama kwa jamii ya watu wanaochukuliwa kuwa ni mashoga. Huo ndio ukawa mwisho wa vita dhidi ya ushoga. Kampeni iliyokufa kifo cha ghafla. Hali iliyowavunja moyo raia wengi walioona vita dhidi ya ushoga kuwa ni hatua stahiki itakayosaidia kuwadhibu wahusika wa vitendo hivyo viovu ndani ya jamii.
Msimamo wa wanaharakati na watetezi wa haki za binadamu wa ndani kwa kampeni hii uligawanyika, wako ambao, licha ya utetezi wao wa haki za binadamu kamwe hawapendi uwepo wa ushoga na hawatetei vitendo hivyo, wapo ambao wanakubaliana navyo, na hawakufurahishwa na kampeni hii, lakini walikosa ujasiri kuipinga, na hivyo walinyamaza kimya kwa kuogopa nguvu ya hisia za Umma, lakini wapo waliothubutu kusimama kifua mbele kwa ujasiri kutetea ushoga hadharani, wakitangaza wazi kuwa tayari hata kuwatetea mashoga mbele ya mahkama.
Ukweli wa mambo ni kwamba sheria za Tanzania zinawachukulia wenye vitendo vya ushoga kuwa ni wahalifu wanaostahiki adhabu kali, na hilo ndilo alilokuwa akilikariri mara kwa mara Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, lakini kiukweli sheria hizo zimopoteza makali yake kimsingi, kwa kuwa tayari Tanzania imeshasaini na kuridhia mkataba wa kimataifa wa kulinda haki za raia jumla. Na hiyo ndio sababu Waziri wa Mambo ya Nje alipoona shinikizo kubwa limemuelemea, kwa ujanja aliikana hatua ya Mkuu wa mkoa.
Zaidi ya hayo, itakumbukwa kwamba Tanzania imekuwa na mawasiliano rasmi kitambo na jamii ya mashoga tangu mwaka 2009, wakati aliyekuwa Naibu Waziri wa Maendeleo, Vijana na Jinsia wa Tanzania Dr. Incy Nkya alipokutana rasmi na mashoga kupanga mikakati ya kupambana na ukimwi, ambapo alitamka kwa kusema:
‘Hatuwezi kiudhati kukabiliana na Ukimwi bila ya kuwa na maongezi na makahaba na mashoga, tutashinda vita hii tu ikiwa tutaungana, na si zaidi ya hivyo’ (The Weekend African 29-30 Sept. 2009)
Qadhia hii inaashiria mambo yafuatayo:
Hisia jumla za watu wa Tanzania, Afrika, na jamii kubwa ya walimwengu kwa ujumla haikubaliani na vitendo viovu vya ushoga, iwe kwa hoja za kidini, kibinadamu, mila, desturi na tamaduni zao. Na wanataka vitendo hivyo viangamizwe kabisa, kwa kuwa ni tishio kwa maadili ya kijamii na nakama kwa ustawi wa malezi na kizazi kijacho.
Nchi zinazoendelea kijumla hazikubaliani kabisa na ushoga, na huoenekana kuukubali kwa shingo upande kwa sababu tu ya kutenzwa nguvu na madola makubwa, mikataba ya kimataifa, misaada na shinikizo la kimataifa, pamoja na ukweli kwamba matendo hayo hayakubaliki ndani ya nchi zao.
Serikali za nchi changa baada ya kutenzwa nguvu na nchi kubwa kuunga mkono wimbi la ushoga, licha ya kuwa halikubaliki na wengi wa wananchi wao, hujaribu kulipeleka kwa wananchi wao kwa kuwaghilibu bila ya kuwawekea wazi, kwa kukosa ujasiri wa moja kwa moja kuwaeleza raia wao kwamba wanaruhusu jambo hilo, na badala yake hucheza na akili za raia kijanja mpaka pale panapoonekana kuna shinikizo la wazi wazi, hapo huwa hawana namna ila kuonesha unyenyekevu wao kwa jambo hilo. Hiyo ni dalili kuwa hawalifurahii wala kuridhishwa na suala la ushoga. Unyenyekevu ulioneshwa na Tanzania karibuni ni mfano hai kabisa.
Lakini pia kuna mifano mengine kadhaa kama nchi ya Malawi mwishoni mwa mwezi wa Disemba 2009, mwanamume aliyejigeuza mwanamke, Tiwonge Chimbalanga na Steven Monjeza (bwana) walikamatwa baada ya kufanya ‘hafla ya posa’. Tarehe 18 Mei 2010 wakaonekana kuwa na hatia ya kujihusisha na makosa ‘kinyume na maumbile’, na kufanya ‘matendo machafu yasiokubalika na jamii baina ya wanaume’. Lakini baada ya shinikizo la kimataifa mnamo tarehe 29 Mei 2010, aliyekuwa Raisi wa Malawi, Bingu wa Mutharika akatoa msamaha kwa wahalifu hao wawili. Si hivyo tu, bali mwezi wa Novemba 2012, Raisi aliyefuatia wa Malawi bi Joyce Banda akapiga marufuku sheria zote zinazolitia hatiani suala la ushoga. Na hatimae mwezi wa Julai 2014, Waziri wa Sheria wa Malawi akatangaza rasmi kwamba Malawi haitowakamata tena wanaojihusisha na ngono ya jinsia moja
Mfano mwengine ni nchi ya Uganda ilipotunga sheria ya kukabiliana na ushoga ya mwaka 2014 (The Uganda Anti-Homosexuality Act, 2014 ) ikitoa adhabu ya kifungo cha maisha jela kwa matendo yanayonasibishwa na ushoga. Sheria hiyo ikaitosa Uganda katika uwanja wa kimataifa, na kulaaniwa kimataifa, huku serikali nyingi ulimwenguni zikazuiya kuipatia misaada nchi hiyo. Hatimae mwezi Agosti 2014 Katiba ya Uganda ikaitengua sheria hiyo.
Tungependa kuwambia wanaoukataa uovu wa ushoga ambao tunaamini ni wengi zaidi, na wana haki ya kuukataa, yafaa wakumbuke mambo mawili:
Kwanza, wajionee wazi wazi uduni wa hali ya nchi zinazoendelea (nchi changa) namna ulivyo, nchi hizo zimekosa mamlaka ya kweli ya kujiamulia mambo yake, licha ya kuwa zimepata ‘uhuru wa bendera’. Maamuzi yao yote yawe ya kisiasa, kiuchumi na hata haya ya kijamii kama inavyodhihirika katika qadhia hii, ni kwa mujibu wa matakwa ya madola makubwa ya kibepari ya kikoloni, madola ambayo hayajali utu wala maadili mema.
Pili, nidhamu ya kidemokrasia ambayo ndio farasi anayetumika kwa kupitia fikra za ‘uhuru wa kibinafsi’ kuhubiri na kutetea ushoga na kila aina ya uovu, namna ilivyo nidhamu ya hatari na tishio kwa ustawi wa ubinadamu, na kimsingi ni aina ya dini mpya inayolazimishwa kwetu, ili kuacha dini zote, kwa kuleta nidhamu mpya yenye uoza wa kimaadili. Jambo hilo ni dalili tosha ya kutofaa nidhamu ya kidemokrasia katika kuuhudumia ubinadamu.
Amma kwa waumini na wakereketwa wa fikra za kidemokrasia, wanaharakati na watetezi wa haki za binadamu, tunawambia badala ya kupokea na kuhubiri kila kitu kinacholetwa kibubusa, ni muhimu waelewe mambo matatu makubwa msingi:
Kwanza, nidhamu ya kidemokrasia ya usekula inayohubiri fikra za ‘uhuru binafsi’ zinazodandiwa kutetea ushoga haikuibuka juu ya msingi wa hoja, bali imeibuka juu ya msingi wa kijanja. Kwa sababu baada ya mvutano mkali baina ya wanamageuzi dhidi ya makasisi juu ya nafasi ya dini, kilichofanyika ni kuja na suluhisho la kati na kati, kwalo kwa kila upande upate chochote, kwamba watu wa dini (makasisi) watapata kubakia na dini yao katika majumba ya ibada, ilhali wanamageuzi watafanya maamuzi yaliyo nje ya majumba ya ibada kwa mujibu wa matakwa ya kidemokrasia. Mjadala baina ya pande mbili hizo ulipaswa uwe amma dini (Mungu) ipo au hakuna. Lakini nukta hiyo msingi katika mjadala ikatupiliwa mbali, na kurukia suluhisho la kila upande kupata chochote, bila ya kuzingatia msingi wa hoja. Matokeo yake, ndio ikazalikana fikra ya usekula, fikra tete isiyoweza kujitetea kwa hoja za kidini wala kiakili, na ambayo ndio imani msingi ya nidhamu ya kidemokrasia. Kwa fikra hiyo duni ya usekula, mwanadamu ambaye ni kiumbe cha Mungu, tahamaki ndio akawa mgawaji wa mamlaka kwa Mungu, kwa kuyatambua uwepo wa mamlaka hayo katika majumba ya ibada, na mahala pengine anapotaka yeye mwanadamu kutambua uwepo wa mamlaka hayo kwa mujibu wa utashi wake (mwanadamu), kama ilivyotumika dhana ya ‘uwepo wa matakwa ya Mungu’/ act of God ambayo ni utetezi katika sheria ya Uzembe (negligence) katika sheria za kiengereza.
Pili, kupigia debe suala la ushoga kunatokana na kuegemea Tamko la Haki za Binadamu za Kilimwengu (Universal Human Right Declaration). Kusema kwamba haki hizo za binadamu katika Tamko hilo ni zenye sifa za kuwawafiki watu wote (Universal) hilo ni uwongo shahir dhahir. Kwa kuwa mwenye haki pekee ya kutamka kwamba muongozo fulani ni muwafaka kwa watu wote lazima awe Muumba wa ulimwengu na wanadamu, na hakuna yoyote katika walioandaa tamko hilo aliyewahi kujinasibu kwa sifa hiyo, bali wote walioandika Tamko hilo wameshaondoka kamwe duniani (wameshakufa). Hiyo ni dalili ya wazi kuwa Tamko hilo sio la kilimwengu, kwa kuwa walioandaa ni sehemu ya viumbe wa ulimwengu na sio Aliyeumba ulimwengu.
Tatu, kampeni za kutetea ushoga inamdhalilisha na kumdunisha mwanadamu na maumbile yake, kwa kuwa inamfanya kuwa kitu cha majaribio. Huko mwanzoni matendo ya ushoga yalikuwa hayakubaliki hata ndani ya nchi za kibepari za Ulaya, lakini baada ya kampeni kubwa, sasa yamekuwa ni jambo linalokubalika. Kimsingi maumbile ya mwanadamu hayapo kwa ajili ya kufanyia majaribio. Kitendo cha kufanya majaribio katika maumbile ya mwanadamu ni dalili wazi ya kutofaa kwa haki za binadamu, kwa kuwa kiasili maumbile ya mwanadamu hayabadiliki. Jambo hili lina natija ya hatari sana kwa ubinadamu.
Uislamu unamuangalia binadamu kuwa ni kiumbe kitukufu chenye hadhi ya juu na bora kuliko viumbe vyote, ambapo maumbile yake msingi hayabadiliki, na kamwe sio kitu cha kimajaribio. Mwanadamu huyu kwa kuwa ni kiumbe ana udhaifu wa kimaumbile ikiwemo mipaka ya elimu yake, kujipendelea maslahi yake binafsi na kuathiriwa na mazingira. Udhaifu huu unamnyima sifa msingi ya kuweza kutunga sheria muwafaka. Ni Muumba pekee kwa Rehma zake ndio akalibeba jukumu la kutunga sheria kwa ajili ya kumuongoza mwanadamu katika kila kipengee cha maisha yake.
﴿يُرِيدُ اللّهُ أَن يُخَفِّفَ عَنكُمْ وَخُلِقَ الإِنسَانُ ضَعِيفًا﴾
‘Na Mwenyezi Mungu anataka kukupunguzieni taabu, na mwanadamu ameumbwa dhaifu’(TMQ 4:28)
Imeandikwa na Masoud Msellem
Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari
Hizb ut Tahrir Tanzania
Kwa ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir
Maoni hayajaruhusiwa.