Wanawake Wa Kiislamu, Mwezi Wa Shawwal Uwape Nguvu Zaidi

بسم الله الرحمن الرحيم

Katika mwezi kama huu wa Shawwal kuna mengi katika misimamo, muhanga na mafunzo ya subra yanayopaswa kuigizwa na akinamama wa Kiislamu katika ulimwengu wetu leo. Misimamo na mafunzo hayo ni ya lazima wajipambe nayo hususan katika kipindi hiki ambacho ulinganizi wa kurejesha tena maisha ya Kiislamu umepamba moto na unakaribia kufika kileleni, huku walinganizi wakikabiliwa na kila aina ya vitimbwi, dhulma, mateso, kuuwawa kutoka kwa makafiri na vibaraka wao.

Mwezi kama huu wa Shawwal ndio uliotokea vita kadhaa vikali vilivyowatia Waislamu misukosuko mikubwa. Hata hivyo Waislamu walivikabili vita hivyo kwa subra, msimamo na istiqama na kubwa zaidi wanawake nao pia walikuwa mstari wa mbele kwa subra na muhanga, kwa mifano mingi isiyomithilika.

Katika vita vya Uhud ndani ya mwezi huu mwaka wa 3AH, wakati wanawake wa kikafiri wakiwatumbuiza (kuwastarehesha) jeshi la makafiri katika medani ya vita kwa nyimbo za mahaba na za kuhamasisha heshi lao kuwapiga Waislamu, wanawake wa Kiislamu wao waliwahamasisha waume, kaka na baba zao na Waislamu jumla kwa nasaha za kiuchamungu kupigana na makafiri kwa kutaraji malipo makubwa kutoka kwa Mola wao na kuridhia qadhaa ya Allah Ta’ala kwa yoyote yatakayowasibu.

Aidha, baadhi ya wanawake walishiriki kikamilifu kutoa huduma ya mwanzo (first aid) kwa majeruhi. Na mara baada ya vita kumalizika wanawake wa Kiislamu walisaidia katika kutibu majeraha ya mujahidina, na wakizipokea taarifa za kuuwawa mashahidi vipenzi vyao katika ndugu, jamaa na waume zao kwa moyo mkunjufu na kwa subra ya hali ya juu.

Bi Fatma bint Rasullulah ni mmoja wa mfano bora, alikuwa msatari wa mbele kumuuguza baba yake majeraha ya vita. Bibi Safiya bint Abi Talib, shangazi yake Mtume (SAAW) na dada wa bwana wa mashahid Hamza bin Abi Talib ra. alipopata taarifa ya kuuwawa kaka yake alitaka kuiona maiti ya kaka yake.

Mtume SAAW awali alimuagiza Zubair (mtoto wa Bi Safiya) amzuiye mama yake. Bi Safiya akasema:
‘Kwa nini niondoke ilhali nimepata taarifa kwamba (kaka yangu) wamemkata kata vipande? lakini nasema Allah Anatosheleza na Insha Allah nitasubiri’.

Itakumbukwa kwamba bibi huyu (Bi Safiyya) ndie pia aliyemuuua kwa mkono wake Yahudi muovu katika Vita vya Ahzab mwaka wa 5AH mwezi kama huu wa Shawwal, wakati huo akiwa mama wa umri wa miaka 58 , alifanya hayo baada ya Mtume SAAW kutoa agizo katika vita vile kwamba wanawake wote wakusanywe katika ngome maalum chini ya ulinzi wa sahaba Hassan bin Thabit. Yahudi huyu alikuja kinyemela kufanya ujasusi.

Tusimsahau pia Bi Himanah bint Jahsh (Ra.) nae baada ya kupata taarifa ya kuuwawa ndugu yake Abdallah bin Jahsh, na pia kuuwawa mumewe Musab bin Umair katika Vita vya Uhud aliipokea misiba hiyo kwa subra ya hali ya juu na kuikubali qadhaa ya Allah Ta’ala.

Kadhalika mujahidina walipokuwa wakirejea kutoka Uhud na walipompa taarifa mwanamke mmoja wa kabila la Bani Dinar juu ya kufa shahid kaka yake na mumewe, mama yule aliuliza: Vipi hali ya Mtume SAAW yukoje? akajibiwa yuko hai na salama, mama huyo akaomba amuone Mtume SAAW kwa macho yake, na akaoneshwa. Hapo akajibu:
‘Msiba wote huu ulionisibu si lolote si chochote kwangu kwa kuwa wewe (Mtume SAAW) uko salama’.

Bila ya kumsahau Ummu Saad (Ra) alipopewa taarifa na Mtume SAAW juu ya kufa shahid mumewe Amr ibn Muadh nae alijibu kama Himnah bint Jahsh.

Mtume SAAW akawaombea dua wote waliondokewa na jamaa na ndugu zao katika vita vya Uhud, kisha akamueleza Ummu Saad:
‘Furahi ewe Ummu Saad na wape bishara wote ambao jamaa zao wamekufa katika Uhud, hao (mashahid) watakuwa nami katika Jannah’. Ummu Saad akajibu: ‘
‘Tumeridhika ewe Mjumbe wa Allah, nani tena atakayewalilia baada ya habari hizi njema’.

Enyi akinamama na dada zetu watukufu wa Kiislamu, ni wajibu kwenu kujipamba na sifa na mwenendo kama huu wa wanawake waliotangulia ambao Allah Ta’ala alianza kuwaridhia katika dunia hii na kesho akhera watakuwa miongoni mwa watu walioridhiwa na kuingizwa kwenye makaazi ya Jannah.

10 Shawwal 1441 Hijri – 01 Juni 2020
Hizb ut Tahrir Tanzania

Maoni hayajaruhusiwa.