Dira Yetu Baada Ya Ramadhani

بسم الله الرحمن الرحيم

Tukiwa tumemaliza mwezi mtukufu wa Ramadhani ambao umetukumbusha utambulisho [shakhsia] yetu tukufu ya Kiislamu, ni muhimu sasa kukumbushana jukumu letu na dira yetu baada ya kumalizika kwake ndani ya siku chache zijazo inshaAllah.

Inapasa tuelewe kwamba ibada mbalimbali tunazozifanya kila siku kama vile Swaumu, Swala, Hijja nk. zote hizi zimeandaliwa na Allah Ta’ala kutujengea uhusiano wa moja kwa moja na Yeye. Jambo ambalo ni hitajio letu la kimaumbile kwa kila siku.

Lakini huo ni uhusiano aina moja tu. Bali tuna sehemu nyengine ya mahusiano kama vile baina yetu na nafsi zetu, mfano, matumizi ya vyakula, vinywaji, mavazi nk.

Pia tuna mahusiano aina ya tatu ambayo ni baina yetu na wanaadamu wenzetu yaani masuala ya muamalati kama siasa, uchumi, mahusiano baina wanaume na wanawake nk. Yote haya yamepangiwa utaratibu maalum na Allah Ta’ala ambao ni lazima kushikamana nao, kama vile tunavyoshikamana na utaratibu katika ibada maalum, kwa kuwa Uislamu haukuyagawa maisha baina ya ‘maisha binafsi’ (ya kidunia) na ‘maisha ya Mungu’ kama wanavyofanya mabepari (warasilimali) wanaposema ‘mpe Kaisari cha Kaisari, na mpe Mungu kilicho cha Mungu’!

Bali kila kilichoumbwa ni cha Mungu tu bila mshirika, na kwa hivyo mahusiano ya mwanadamu yote lazima yatekelezwe kwa mujibu wa maagizo Yake. Ndio maana Allah Ta’ala hata baada ya kumalizika ibada zetu mbali mbali bado anatukumbusha kwa kugogoteza katika mambo yetu yote tuendelee kushikamana naye:

فَإِذَا قَضَيْتُمْ مَنَاسِكَكُمْ فَاذْكُرُوا اللَّهَ كَذِكْرِكُمْ آبَاءَكُمْ أَوْ أَشَدَّ ذِكْرًا

“Na mnapomaliza ibada zenu za [Hijja], basi mtajeni Allah kama mlivyokuwa mkiwataja baba zenu, bali mtajeni zaidi” [TMQ 2:200]

فَإِذَا قُضِيَتْ الصَّلاَةُ فَانتَشِرُوا فِي الأَرْضِ وَابْتَغُوا مِنْ فَضْلِ اللَّهِ وَاذْكُرُوا اللَّهَ كَثِيرًا لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ

“Na itakapo kwisha swala, tawanyikeni katika ardhi mtafute fadhila za Allah na mkumbukeni Allah kwa wingi ili mpate kufaulu” [TMQ 62:10]

Kwa hivyo, dira yetu sisi Waislamu wakati wote ni watumwa mukhlisina wa Allah Ta’ala pekee. Utumwa huo ni katika maisha yetu yote, yawe katika masuala ya uchumi, siasa, jamii, sheria au ibada za kiroho, huwa ni lazima yatekelezwe kwa mujibu wa Sheria Tukufu za Allah Ta’ala. Kwa sababu Yeye ndie aliyetuumba na akatupa maisha haya na akatutaka tufungamanishe maisha haya na maisha yajayo ya Akhera kwa kujifunga kikamilifu na wakati wote na Sheria Zake tukufu.

قُلْ إِنَّ صَلاَتِي وَنُسُكِي وَمَحْيَاي وَمَمَاتِي لِلَّهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ

“Sema: Hakika swala yangu na ibada zangu (zote nyengine) na uhai wangu na kufa kwangu ni kwa ajili ya Allah, Muumba wa walimwengu” [TMQ 6:162]

09  Shawwal 1441 H – 31 Mei 2020 M

Masoud Msellem

Maoni hayajaruhusiwa.