Safari Ya Mtume (Saaw) Kwenda Twaif

بسم الله الرحمن الرحيم

Katika mwezi kama huu wa Shawwal (mfunguo mosi) katika mwaka wa kumi wa Utume, aliondoka Mtume (SAAW) akifuatana na sahaba wake mtukufu Zaid bin Harithah kutoka Makka kuelekea mji wa Twaif kiasi cha maili 70 upande wa kusini mashariki mwa Makka.

Dhamira ya safari hiyo ni kuomba Nusra kutoka kwa viongozi wa kabila la Bani Thaqif wa mji wa Twaif. Nusra katika ulinganizi wa Mtume (SAAW) hukusudiwa uhamishaji wa hatamu na mamlaka ya kisiasa na kijeshi kwa kupitia kiapo maalum [baia] kinachotolewa na jopo la wenye nguvu au ushawishi katika jamii kwa lengo la kuondosha utawala uliopo na badala yake kuwezesha kusimamisha Dola ya Kiislamu.

Itakumbukwa kwamba baada ya ulinganizi wa Uislamu kuganda katika mujtamaa (jamii) wa Makka, na kukataa kwao maQureshi kwa inadi na kibri dini ya Uislamu na kutokuwa tayari kusalimisha mamlaka yao kwa ajili ya kusimamisha Dola ya Kiislamu, ilimbidi Mtume (SAAW) kwa kuelewa kwamba ujumbe wake si wa kikabila au kizalendo kuja na mkakati wa kuyakabili makabila mengine nje ya Makka ili kufanikisha lengo lake hilo.

Katika qadhia hii nyeti ya kutaka nusra Mtume (SAAW) alishika msimamo thabiti nao ni lazima wale anaowalingania kumpa nusra, waukubali Uislamu kwa ukamilifu wake na watoe mamlaka yao yote bila ya masharti yanayopingana na Uislamu ili Dola anayoikusudia kuisimamisha iwe Dola huru na sio tegemezi. Katika hilo alikuwa akiwaekea wazi na bayana makabila yote kwa kuyaeleza:

“وأن تؤمنوا بي وتصدقوا بي وتمنعوني حتى أبيِّن عن الله ما بعثني به”
“Ya kwamba mniamini, kunisadiki na kunilinda mpaka niweze kubainisha yale aliyonituma nayo Allah.”

Makabila yaliupokea mwito wake kwa hisia tofauti. Kabila la Amir bin Sa’sa’ah walimueleza Mtume (SAAW) bayana msimamo wao kwa kuweka sharti la kuchukua wao utawala baada ya kuondoka Mtume (SAAW) nao wakamjibu:
‘Tuinamishe shingo zetu kwa panga za waarabu na mara ushindi ukipatikana utawala wende kwa wengine?’

[Sira ya Ibn Hisham]

Kwa jibu hili ni wazi walielewa kwa kina upana na unyeti wa ajenda ya Mtume (SAAW) ya kuasisi Dola. Ama kabila la Shaiban bin Thaalabah, wao walionesha utayari kutoa mamlaka yao yote kwa Mtume (SAAW) kwa sharti tu mapambano ya Uislamu yasiwaguse Wafursi kwa sababu ya kuwepo mkataba wa amani baina yao. Mtume (SAAW) aliyakataa katakata masharti ya makabila yote hayo mawili na akaamua kuyakabili makabila mengine. Kadhalika yapo makabila yaliyomkatalia kimya kimya kama vile Bani Kinda, Bani Kalb, ilhali Bani Hanifah wao walimkatalia kwa kuonesha ubaya na uovu dhidi yake.

Kwa hivyo, safari ya Twaif ilikuwa ni sehemu ya mchakato huo wa kutafuta kuungwa mkono kivitendo kufikia lengo lake tukufu, na mara baada ya kuwasili Twaif alifanya hadhari kubwa kwa kuwakabili machifu watatu tu wa kabila la Bani Thaqif, nao ni mabwana Abd Yaliil, Masu’d na Habib wote wakiwa watoto wa Amr bin Umair At-Thaqafi ili kufikisha ajenda yake ya kuwataka wasilimu na watoe nusra yao kwake ili ahamie kwao na kusimamisha utawala wa Uislamu; na endapo hawatokubaliana na matakwa yake basi qadhia ile ibakie kuwa siri baina yao bila ya kudhihirishwa kwa yoyote.

Kwa bahati mbaya na kwa masikitiko makubwa, machifu wa kabila hili kama makabila mengine mengi hawakukubali matakwa ya Mtume (SAAW). Bali baya zaidi hawakuheshimu hata siri waliyoombwa kuihifadhi na badala yake si tu walivujisha siri ya mazungumzo yale, bali kwa kibri na inadi wakamtomeza Mtume (SAAW) kwa watu waovu na wahuni waliompiga kwa mawe na kuimwaga damu yake tukufu kwa kebehi, dhihaka, bughdha na majivuno. Lakini Mtume (SAAW) alidumu na da’wa yake japo kuwa alisibiwa na mitihani kama jibu baya la machifu wa Banu Thaqif nk.
Mtume (SAAW) alirejea na kuingia tena Makka akiwa amechoka na majeraha kwa dhamana/kinga ya Mut’im bin Addiy lakini hakuvunjika moyo, kutetereka wala kurudi nyuma katika mchakato wa kutafuta nusra mpaka makabila ya Aus na Khazraj ya Madina yalipompa kiapo cha vita (baay’atul-harb) huku wakimueleza:

فَأَخَذَ الْبَرَاءُ بْنُ مَعْرُورٍ بِيَدِهِ ثُمّ قَالَ نَعَمْ وَاَلّذِي بَعَثَك بِالْحَقّ ( نَبِيّا ) لَنَمْنَعَنّك مِمّا نَمْنَعُ مِنْهُ أُزُرَنَا فَبَايِعْنَا يَارَسُولَ اللّهِ فَنَحْنُ وَاَللّهِ أَبْنَاءُ الْحُرُوبِ وَأَهْلُ الْحَلْقَةِ..

“Al-Bara bin Ma’aroor [Answari] akachukua mkono wake [mkono wa Mtume (SAAW)] kisha akasema: ‘Naam naapa kwa Yule ambaye amekutuma kwa haki (kuwa Mtume) kwamba tutakulinda kama tunavyolinda wakaribu wetu. Basi ikubali bay’a yetu ewe Mtume wa Allah kwani sisi Wallahi ni watoto (yaani wazoefu) wa vita na watu wa kupigana kwa mzunguko.”

Kwa nusra aliyopewa na Answar, akaweza Mtume (SAAW) kusimamisha Dola ya Mwanzo ya Kiislamu katika mji wa Madina na kuweza kuutoa Uislamu kutoka kuwa kama ujumbe wa kinadharia na kuelekeza hali yake asili ya kuchukua utawala unaofanya kazi kivitendo katika hukmu na usimamizi kamili. Makabila ya Amir bin Sa’sa’ah, Shayban, Bani Kinda, Bani Kalb na mengineyo yaliitupa fursa ya kutoa nusra yao baada ya muda mfupi kutokana na nguvu na uimara wa Dola ya Kiislamu, hususan mara baada ya vita vya Tabuk yakaja amma kusilimu au kujisalimisha kwa kuwa chini ya himaya thabiti ya Dola ya Kiislamu. Bila ya shaka waliikosa fadhila ya kuwa ma-Answari kwa khiyari kwa kupuuza kwao Uislamu mpaka nguvu za Uislamu kwa himaya ya serikali yake ilipowalazimisha wote kutambua nguvu zake.

Miongoni mwa mafunzo makubwa katika tukio hili ni kwamba da’awa (ulinganizi) ya Mtume (saaw) ilikuwa na mipango, mbinu na malengo na haikuwa ni da’awa tu bila ya mwelekeo. Bali ilikuwa na malengo ya kusimamaisha utawala utakaobeba mfumo aliokuja nao.

Pia kuna funzo la kusimama kidete katika ulinganizi bila ya kutetereka ikiwemo mchakato wa kutafuta nusra, kwa kujifunga na msimamo, subra na kumtegemea vilivyo Allah Ta’ala pekee, kwani siri ya mafanikio ya ulinganizi ipo mikononi mwa Allah Ta’ala huwapa nusra waja Wake wanaolingania da’wa Yake Tukufu.

أَلاَ إِنَّ نَصْرَ اللَّهِ قَرِيبٌ

“Zindukeni! Nusra ya Allah [Taala] ipo karibu” [TMQ 2:214]

10 Shawwal 1441 Hijri – 01 Juni 2020

Hizb ut Tahrir Tanzania

Maoni hayajaruhusiwa.