Ufafanuzi kutoka kwa Amiri wa Hizb ut Tahrir, Mwanachuoni Mkubwa, Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Kuhusu Kuthubutu Kuonekana kwa Mwandamo wa Mwezi (Hilal) wa Shawwal Mwaka Huu, 1441 H, 2020 M
بسم الله الرحمن الرحيم
(Imetafsiriwa)
Kwanza: Jana saa nne usiku (Jumamosi usiku) kwa saa za mji wa Madina, nilikuwa nimewatumia kwamba mwezi mwandamo (Hilal) haukuwa umeonekana usiku huu, kwa mujibu wa ripoti kuhusu kuthibitisha mwandamo huo, ambazo tulizipokea. Kwa kawaida huwa hatucheleweshi jambo hili la kuonekana mwezi zaidi ya saa nne au saa nne unusu usiku kwa saa za Madina, ili tusichelewe katika kuwatangazia ndugu zetu walioko mashariki. Hii ni ili tangazo liwafikie kabla ya Adhana ya Alfajiri, katika sehemu kama Indonesia. Kutokana na haya, tangazo lilitolewa kuwa Jumamosi 23/5/2020 ni ukamilisho wa mwezi ulio barikiwa wa Ramadhan, na kwamba Idd ni mnamo Jumapili 24/5/2020.
Pili: Kisha tukapokea habari kwamba mwezi mwandamo umeonekana na Waislamu watatu nchini Tanzania, ikiongezewa na mashahidi wengine wawili barani Afrika … hivyo tulituma risala kwa mjumbe wetu huko, ili awatume watu wawili kwa wale waliouona, ili kuthibitisha jambo hili. Alifanya hivyo na akatutumia jibu, ambalo ni kama ifuatavyo:
“5. Mashahidi 3 waliuona mwezi mwandamo mwembamba mno * huku ncha zake mbili zikielekea juu na upinde wake ukielekea jua ambalo lilikuwa lishazama.
6. Wamekula viapo na kutamka shahada mbele ya mashabab wetu watatu.”
Tatu: Tumepokea jibu la mjumbe takriban saa saba kamili mchana, kwa saa za mji wa Madina. Hii yamaanisha kwamba kuonekana kwa mwezi mwandamo kulikuwa ni sahihi, na upinde wa mwezi mwandamo huo ulikuwa umeelekea jua linalo zama: “yaani, upinde ulikuwa unalielekea jua ambalo tayari lilikuwa lishazama,” ikimaanisha kuwa kile kilicho onekana ni mwezi mwandamo wa Shawwal, kwa ushahidi wa Waislamu watatu.
Nne: Baada ya kujadili juu ya jambo hili, kwa msingi wa hadith ya Mtume (saw), ambayo imehadithiwa na Imam Ahmad kutoka kwa Abi Umair bin Anas (ra),
غُمَّ عَلَيْنَا هِلَالُ شَوَّالٍ فَأَصْبَحْنَا صِيَامًا فَجَاءَ رَكْبٌ مِنْ آخِرِ النَّهَارِ فَشَهِدُوا عِنْدَ رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَنَّهُمْ رَأَوْا الْهِلَالَ بِالْأَمْسِ فَأَمَرَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَنْ يُفْطِرُوا مِنْ يَوْمِهِمْ وَأَنْ يَخْرُجُوا لِعِيدِهِمْ مِنْ الْغَدِ
“Mawingu yalitanda juu yetu na kutuziba kutouona mwezi mwandamo wa Shawwal, tukapambauka hali ya kuwa tumefunga. Kisha akaja, mwendesha farasi mmoja mwishoni mwa mchana akashuhudia mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) kwamba yeye jana aliuona mwezi mwandamo basi Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akaamrisha watu wafungue siku yao ile na watoke kwa Idd kesho.” Na Bayhaqi amesimulia katika Sunan al-Kubra kutoka kwa Rabee bin Hirash kutoka kwa mmoja wa Maswahaba wa Mtume (saw) kuwa,
اخْتَلَفَ النَّاسُ فِى آخِرِ يَوْمٍ مِنْ رَمَضَانَ فَقَدِمَ أَعْرَابِيَّانِ فَشَهِدَا عِنْدَ النَّبِىِّ -صلى الله عليه وسلم- بِاللَّهِ لأَهَلاَّ الْهِلاَلَ أَمْسِ عَشِيَّةً فَأَمَرَ رَسُولُ اللَّهِ -صلى الله عليه وسلم- النَّاسَ أَنْ يُفْطِرُوا وَأَنْ يَغْدُوا إِلَى مُصَلاَّهُمْ
“Watu walihitilafiana juu ya siku ya mwisho ya Ramadhan, wakaja Mabedui wawili wakashuhudia kwa Mwenyezi Mungu mbele ya Mtume (saw) kwamba mwezi umeandama jana jioni, basi Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akawaamrisha watu wafungue na kesho waende katika mswala wao.”
Na juu ya hili, huku tukifuata mfano wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw), leo, Jumamosi 23/5/2020, ndio siku ya kwanza ya Idd ul-Fitr … Hivyo Waislamu nawafungue saumu zao na kwa sababu jambo hili limejiri baada ya Zawaal, wataswali swala ya Idd kesho … Na twamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu azikubali Saumu zetu na Visimamo (Qiyam) vyetu, na aujaaliye mwezi huu ulio barikiwa kuwa ni ishara ya kheri na baraka kwa Waislamu wote. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu awaharakishie Waislamu kusimama kwa Khilafah yao, na awaponye kutokana na kila janga la maambukizi, ili wapate afueni katika Dunia hii na kesho Akhera na Mwenyezi Mungu ndiye Mmiliki wa neema zote, Al-Adhim.
Mwenyezi Mungu (swt) aukubali utiifu wetu, Sifa Njema Zote ni za Mwenyezi Mungu Mola wa Viumbe vyote.
Assalamu Alaikum Wa Rahmatullah Wa Barakatuh
Siku ya Idd ul-Fir, 1 Shawwal 1441 H Ndugu yenu,
23/5/2020 M Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah
Amiri wa Hizb ut Tahrir
Maoni hayajaruhusiwa.