Tarehe 03 Machi Siku ya Msiba mzito kwa Kuangushwa Dola ya Khilafah

Dola ya Kiislamu ya Khilafah iliyokuwa muendelezo wa dola aliyoiasisi Mtume SAAW iliangushwa rasmi tarehe 03/03/1924 / 27 Rajab1342. Dola ambayo ilidiriki kuzishinda tawala za Uajemi na Warumi (Byzantine) na kubakia kuwa dola kuu mpaka karne ya 18. Makafiri waliweza kuiangusha kufuatia kudhoofika kifikra, kuzongwa na maadui wa ndani na nje pia kampeni kabambe ya madola ya kibepari ndani ya Ulaya na Marekani. Khilafah ilikuwa ikisimamia hukmu za Kiislamu, kuwaunganisha Waislamu, kufunguwa miji nk.

Mara baada ya kuangushwa dola hiyo kulifuatiwa na hali isiyosita ya udhalilifu, majanga na maafa yasiyomithilika kwa Ummah wa Kiislamu kwa kuvamiwa, kuteswa, kuuwawa, kuchukuliwa nchi zao, kusambaratishwa uhai wa umoja wake, kugawanywa kimadhehebu na kitaifa taifa kiasi cha kukosa sauti moja yenye athari katika anga za kimataifa nk.
Majanga yote leo yanayotusibu kitaifa, kieneo na kimataifa ni matokeo ya kukosa kinga (dola) ya kuwanusuru Waislamu na kudhamini maisha, heshima na usalama wao. Tunashuhudia kwa macho mawili uvamizi wa makafiri katika miji yetu kama Iraq, Afghanistan, Syria, Somalia nk. Aidha, kumeshamiri dhulma kama mateso na ubaguzi wa kidini kama Afrika ya Kati, Burma, China, Marekani, Urusi nk. Vita vya kikatili na kidhulma dhidi ya Uislamu kwa jina la ugaidi ni matokeo ya kuanguka dola hiyo. Bila ya kutaja matendo ya kurundikwa Waislamu majela wakipata mateso ambayo hata mnyama hathubutu kumtendea mnyama mwenzake chini ya mikono ya mataifa ya kibepari kama Marekani, Uingereza na hata kutoka dola vibaraka za nchi changa duniani kote ikiwemo maeneo yetu. Aidha, suala la kukashifiwa na kukebehiwa dini kuanzia sheria zake kama hijabu, Quran, kumtukana Mbora wa Darja Mtume SAAW yamekuwa ni mambo ya kawaida kila mahala mara baada ya kuangushwa dola ya Kiislamu ya Khilafah iliyokuwa kinga kwa makarne.

Kuvunjwa Khilafah ni mpango kabambe wa nchi za kikafiri za ki-Magharibi kwa ajili ya kuendeleza sera zao za kigeni, kuuvuruga mfumo wa Kiislamu, kunyakuwa rasilmali zake na kumakinisha mfumo wao batil wa kibepari. Kufikia malengo hayo walitumia mikakati mbalimbali ikiwemo vibaraka kama Sharrif Hussein, Kamal Atarturk, Ibn Saud nk. Pia kuunga mkono harakati za kujitenga kwa maeneo yaliokuwa chini ya Khilafah kwa jina la ‘uhuru’ ili kuimega mamlaka ya Khilafah. Itakumbukwa pia Uingereza, Ufaransa na Urusi zilikubaliana mkataba wa siri wa Sykes-Picot Agreement ili kugawana ardhi za dola ya Khilafah.
Katika Vita Vikuu vya Kwanza malengo ya kuivunja Khilafaha yalikwenda kwa haraka zaidi. Nchi washirika baada ya kushinda zilinyakua maeneo muhimu ya Khilafah. Chini ya uongozi wa Uingereza zilimlazimisha Khalifah, kiongozi wa dola ya Kiislamu kusaini mkataba hapo tarehe 30 Oktoba 1918 ulioitwa wa amani ukiwa na lengo la kuipunguza nguvu dola hiyo.

Uingereza kwa kushirikiana na kibaraka wake Yahudi muovu na msaliti Mustafa Kamal aliyekuwa kamanda wa kijeshi wa Uturuki walianzisha uasi dhidi ya Khilafah. Mnamo tarehe 1 Machi 1924 Mustafa Kamal alitoa agizo bungeni la kuvunjwa Khilafah na asubuhi ya tarehe 3 Machi 1924 ilitangazwa rasmi kuvunjwa dola hiyo na kutenganishwa dini mbali na serikali. Mkataba wa Lausanne (Lausanne Treaty) ukasainiwa tarehe 24 Julai 1924 ukifuatiwa na kutambuliwa rasmi uhuru wa Uturuki. Uingereza ilitoa zawadi kwa makubaliano na Mustafa Kamal kujiondoa katika maeneo yote iliyoyakalia ya Uturuki na kuutambua rasmi uhuru wa dola hiyo. Mmoja wa wabunge ndani ya Bunge la Uingereza alipinga hatua ya nchi yake kutambua uhuru wa Uturuki. Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza Lord Curzon alifafanua na kumliwaza mbunge huyo kwa kumjibu bungeni :“Suala ni kwamba Uturuki imeshabomolewa na haitokuja juu tena, kwa kuwa tumevunja nguvu yake ya kiroho: Khilafah na Uislamu.”

Enyi Waislamu,
Hivi ndivyo dola yenu tukufu ya Khilafah ilivyoangushwa, na majanga ya kuangushwa kwake yapo mbele ya macho yenu waziwazi kitaifa na kimataifa. Kumbukeni Khilafah hata katika zama za ukingoni mwake bado iliwajali na iliwahurumia Waislamu kila mahala kiasi cha kutuma kikosi maalumu katika maeneo yetu ya Afrika Mashariki chini ya Kamanda Ali Bey kusaidia kuwakomboa Waislamu na wakaazi jumla na dhulma za Wareno.

Chini ya Khilafah makafiri walisafiri kwenda kusoma katika vyuo vyake vikuu, wayahudi na wengineo wakiomba hifadhi kukimbia mateso ya wakatoliki na ubaguzi uliokita ndani ya Ulaya, bila ya kutaja namna wakristo wa Syria na Jerusalem walivyopigana bega kwa bega upande wa jeshi la Khilafah kuwatimua makruseda/maswalibiyina (wakiristo wenzao) kutokana na insafu, wema, uadilifu wa dola ya Khilafah.
Hivyo, tuna wajibu mkubwa na dhima kubwa mbele ya Mola wetu nayo ni kushiriki katika mchakato wa kuirejesha tena dola hiyo ya kilimwengu kwa kutumia njia ya Mtume SAAW ya mivutano ya kifikra na kisiasa bila ya kuhusisha nguvu wala mabavu, ili dola hiyo ianzie katika nchi kubwa ya Kiislamu kisha kuziunganisha na kuzikomboa ardhi zote za Waislamu na ulimwengu mzima.
Basi shime tubebeni jukumu hili kwa ikhlasi kuikimbilia bishara ya Mtume SAAW ya kurejea tena kwa dola hiyo yenye nuru na neema.
..ﺜﻢ ﺘﻌﻭﺩ ﺧﻼﻓﺔ ﻋﻟﻰ ﻤﻨﻬﺎﺝ ﺍﻟﻨﺑﻭﺓ
….’.Kisha itarudi tena Khilafah kwa njia (manhaj) ya Utume’

Masoud Msellem

#3machisikuyahuzuni

Maoni hayajaruhusiwa.