Siku Ya Choo Duniani Ni Kejeli Kwa Wanyonge

Siku ya tarehe 19 Novemba ya kila mwaka ni ‘Siku ya Matumizi ya Choo Duniani’. (World Toilet Day). Inaaminika kuwa watu bilioni moja hawana uhakika wa matumizi ya choo rasmi. Hili humaanisha kuwa watu hao hawana makaazi ya kudumu na hakika.

Kukosa huko makaazi ya kudumu na ya hakika huwafanya kukidhi haja zao kwenye maeneo ambayo sio mahsusi. Wanadamu hawa wanaishi kwenye hatari kubwa sana ikiwemo ya kupata magonjwa mengi ya mripuko ambayo ni hatari kwa maisha yao na ya wengine. Pia kukidhi haja zao kwa namna hiyo kunaporomosha hadhi yao na murua jumla wa kibanadamu.

Aidha, Watu milioni 892 wanakwenda haja zao nje katika maeneo wazi, milioni 4.5 wakiwa hawana vyoo salama. http://www.worldtoiletday.info/wtd2018/ . Kukosekana kwa vyoo rasmi maana yake hupelekea matumizi ya maji yasiyo masafi ambayo yana madhara makubwa kiafya. Kwa mujibu wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) watu zaidi ya bilioni moja na laki 8 wanatumia maji ambayo sio salama kwa afya ya mwanadamu: http://rt.com/news/206767-water-faeces-contaminated-people/).

Hali hii ni dhihirisho la namna mfumo wa kibepari ulivyomtupa mwanadamu katika suala zima la huduma za kijamii. Na hata pale zinapopatikana huduma hizo, zimegeuzwa kuwa ni biashara inayowapa dhiki wananchi wengi kuimudu.
Ukosefu wa vyoo rasmi mara nyingi husababishwa na umaskini kutokana na watu hao kuishi maeneo duni au kushindwa kuhimili kujisimamia katika miundo mbinu rasmi ya maji taka. Bila ya kutaja hali ya uwepo mrundikano mkubwa wa watu mijini, kwa kuwa mfumo wa kibepari umekutupa nje ya miji, kiasi cha maeneo hayo kukosa vyanzo vya uhakika vya uzalishaji, hali inayofanya idadi kubwa ya watu kukimbilia na kurundikana mijini hata katika makaazi duni yaliokosa nyenzo muhimu kama vyoo rasmi.

Haitoshi mfumo huo kutenda dhulma hiyo na nyenginezo kwa raia, bali pia mfumo huo umesheheni kejeli na vituko kwa wanadamu. Kutenga siku maalumu ya matumizi ya choo ni dharau na kejeli kwa maskini na watu hali ya chini. Kwa kuwa kinachohitajika ni kuwapatia huduma hiyo na sio kuweka siku ya maadhimisho kuwafedhehi.

Maadhimisho haya yanafedhehi wanyonge na maskini kwamba wameshindwa kujipatia huduma hii, ilhali mfumo wa kibepari na nidhamu yake thaqili ya kiuchumi ndio umewapelekea kushindwa kuipata huduma hiyo. Bila ya kutaja kuwa huduma ya majitaka na nyenginezo imezifanya kuwa ni bidhaa za kuongeza maslahi kwa kujaza kipato na sio haki ya kila raia.

Mfumo wa Kiislamu aliokuja nayo Mtume SAAW ambae ni nuru kwa ulimwengu ni kinyume na ubepari. Unalichukulia huduma ya makaazi bora ikiwemo choo rasmi ni haki ya kila raia, ikiwemo pia huduma zote za kijamii, awe raia huyo Muislamu au si Muislamu, na kamwe si biashara au chanzo cha kujipatia maslahi. Ni haramu kubinafsisha mali za Ummah kama miundo mbinu ya maji taka, migodi, visima vya mafuta, mito na maziwa nk. Na badala yake Dola ya Kiislamu ya Khilafah itasimamia mali hizi za Umma kwa uaminifu na uadilifu mkubwa ili mapato yake yatumike katika huduma hizi na nyenginezo kurahisisha maisha ya kila raia.

Wakati huu tukiwa ndani ya mwezi wa Rabi ul awwal aliozaliwa Mtume SAAW, kiongozi na nuru ya ulimwengu, wanadamu hawana budi kufahamu kuwa wanahitaji mfumo wa Uislamu kusimamia mambo, kuwajali, kulinda maisha yao na usiopima mambo kwa kipimo cha maslahi katika matendo. Bali hupima kwa kipimo cha halali na haramu.

Kubwa zaidi, ni mfumo unaotokana Muumba wa ulimwengu, mwanadamu na viumbe vyote.

Kaema Juma

#MuhammadNiNuruKwaUlimwengu

Maoni hayajaruhusiwa.