Nuru Fauka Nuru

1. Yailahi Yaa Manani, Mola Mmiliki enzi
Twashukuru Ihsani, kwa kutujalia pumzi
Tuna furaha moyoni, kwa nuruyo Yaa Azizi
Ni Nuru fauka Nuru, Ummah imetujilia

2. Umemleta Rasuli, ujiowe twauenzi
Twapaza zetu kauli, kuenzi yake mazazi
Kauleta usahali, nuruye kama kurunzi
Ni Nuru fauka Nuru, Ummah imetujilia

3. Ameletwa makusudi , atuondoe gizani
Atupe yenye suudi, atufikishe nuruni
Mengi tukastafidi, akhera na duniani
Ni Nuru fauka Nuru, Ummah imetujilia

4. Alipolikuta giza, kila kona limetanda
Utu watu walibeza, mali ndiyo walipenda
Heshima walipuuza, unyama wakautenda
Ni Nuru fauka Nuru, Ummah imetujilia

5. Jamii aloikuta, inamithilika leo
Kila kona ni matata, kila mahala vilio
Nafuu lililopita, kulikoni tarajio
Ni Nuru fauka Nuru, Ummah imetujilia

6. Ni jamii ya vipofu, mambo yao ravuravu
Jamii lokosa hofu, ulimwengu wa maguvu
Akinyanyaswa dhaifu, kisibiwa kila ovu
Ni Nuru fauka Nuru, Ummah imetujilia

7. Ghariza zilishibishwa, wanyama afadhalia
Na ndoa zilipotoshwa, ushoga kifagilia
Uchumi ulishachushwa, ano nguvu jiporea
Ni Nuru fauka Nuru, Ummah imetujilia

8. Ulimleta kamili, nyenzo mbili sozidia
Uongofu kiakili, na dini ilo sawia
Akazibeba kikweli, jamii kuiongoa
Ni Nuru fauka Nuru, Ummah imetujilia

9. Alitenda kiutume, mfano kutuwekea
Ili nasi tujitume ,neema kurejelea
Watu wakashika shime, juhudini wakangia
Ni Nuru fauka Nuru, Ummah imetujilia

10. Alijenga ufahamu, kuonesha kila ovu
Kiwajuza binadamu, wauwate upotovu
Heshima yao adhimu, kwa Muumba Ano nguvu
Ni Nuru fauka Nuru, Ummah imetujilia

11. Ikaangazia nuru, jamii ikaongoka
Wanyonge wakawa huru, Wababe kanyong’onyeka
Akaieneza sururu, kila mahala kufika
Ni Nuru fauka Nuru, Ummah imetujilia

12. Nakhitimisha kauli, ila nuru tuishike
Njia yake tuinali, mchezo mbali tueke
Ubepari uwe chali, Nuru kila mahala iwike
Ni Nuru fauka Nuru, Ummah imetujilia


HAMZA SHESHE
#MuhammadNiNuruKwaUlimwengu

Maoni hayajaruhusiwa.