Mtume (saaw) Kaleta Maadili, Utu na Ustawi kwa Ubinadamu

Maadili mema ni nuru na kinyume chake ni kiza. Mwanaadamu huhitaji nuru iangaze njia ya anakokwenda ili kumhakikishia kwenda njia sahihi, kuliko na hadhi na heshima ya utu wake.

Kuwepo kizani ni kama kuwa kipofu wa macho ugenini, kunaondosha sifa za utu, kiakili na kijamii kwa kuwa mtu huyu hawezi kuwa na malengo ya maendeleo kwa  kuhisi alipo ndipo sawa tu.

Alikuja Mtume SAW katika ulimwengu akianzia Mashariki ya Kati katika nchi ya Saudi Arabia ya sasa. Aliikuta jamii ikiwa katika kiza kisicho na mfano, watu kama wanyama kiufahamu na matendo yao. Ilikuwa kawaida ndoa za wazazi na watoto wao (baba na binti yake, mama na kijana wake), ndoa za jinsia moja (ushoga), ubaguzi na ubabe.

Mpaka anaondoka (kinamkuta kifo) Mtume SAW na baada yake kwa takriban miaka zaidi ya 1000 mbele hali hii ya kiza sio tu iliondoka kwa Bara Arabu bali ulimwenguni ulibadilika na kuwa na nuru. Maeneo yote yaliyopata bahati ya kuwa chini ya serikali ya Kiislamu ya Mtume SAW na kisha ya Makhalifa yalishuhudia ustawi wa hali ya juu wa utu wa binadamu.

Na hata kule ambako haikufika kama ilivyo sehemu kubwa ya Ulaya bado walinufaika, nao wakatoka kizani kwani zama Bara Arabu likiwa na ustawi katika nyanja zote za maisha, Ulaya lilikuwa bara la kiza. Historia inathibitisha kwamba maendeleo ya kiuchumi na kisayansi Ulaya yana chimbuko katika ustaarabu wa Kiislamu.

Mtume SAW alifahamu kwamba fikra alizonazo mwanaadamu ndio msingi wa namna ya maisha yake, kwa hiyo miondoko ya maisha (life style) mibaya itabadilika kwa kubadili fikra. Akaanza na kumfahamisha mwanadamu asili yake sahihi kama kiumbe, kisha nafasi ya maisha kwamba maisha haya ni ya kupita,  kuna maisha mengine baada ya kufariki dunia. Kuwepo duniani kuna malengo, ambapo katika maisha baada ya haya ya duniani kutakuwepo na tathmini ya utimizaji wa malengo ya kuwepo duniani.

Akajenga tabia/ akhlaq za watu zikawa ni za kisheria kama alivyoagiza Muumba wa wanadamu. Akhlaq/maadili ni tafsiri ya matendo ya binadamu imma yapi yafaa kufanywa au yapi yapasa kuachwa kwa msingi wa vipimo vya halali na haramu. Akhlaq za Kiislamu daima zinaendana na maumbile msingi ya binadamu. Akasisitiza Mtume SAAW nafasi ya tabia/akhlaq njema ni moja ya kigezo cha kujua ubora wa mtu.

Pia SAAW akafundisha kipimio rahisi cha kila mtu kujitathmini katika akhlaq, kwamba: Wema ni tabia nzuri, na uovu ni yale yanayopita katika nafsi yako na ukachukia watu wasiyajue.

Mfano wa tabia ambazo alisisitiza na kuzisimamia Mtume SAW kwa watu wake ni kuchunga mdomo, kuchunga tupu na kuwa na tabia ya haya.

Tupu amma sehemu za siri ni viungo ambavyo matumizi yake mazuri ni ustawi wa jamii, na matumizi mabaya ni kuharibika kwa jamii. Alisisitiza ndoa baina ya mtu mume na mtu mke na akapiga vita kujamiiana kuliko nje ya ndoa. Mtume SAAW alisistiza haki ya kwanza ya mtoto ni kupatiwa mzazi bora, jina bora na nasabu nzuri.

Baada ya ubepari na demokrasia kuchukua mahali pa Uislamu katika kutawala ulimwengu mambo yote yamekwenda juu chini, chini juu, na matokeo yake ulimwengu umerudi katika kiza kile alichokikuta Mtume SAW.

Ngono imekuwa rahisi na yakupigiwa kampeni kuliko ndoa. Likaibuka kundi la watoto wa mtaani. Ugumu wa ndoa na kukosekana usimamizi kumeleta ubaradhuli ambapo ushoga na usagaji ni katika agenda msingi za kushajihishwa katika jamii ikiwa na lengo la kupunguza uzazi, na hivyo kudhibiti ongezeko la watu duniani.

Matumizi ya mdomo, kauli na maneno ya watu hususan wenye nafasi katika jamii yanajenga yanapokuwa katika usahihi lakini hubomoa jamii yakiwa nje ya ubinadamu. Kusema na kuahidi uongo ni sifa msingi walizojivisha kwazo wanasiasa wa kidemokrasia na viongozi wa jamii ya sasa. Hujinadi katika kampeni kwa ahadi hewa na hadaa nyingi. Hatimaye ni dhiki na matatizo katika maisha kwani utendaji hufuata maslahi ya kibinafsi badala ya kujali Ummah kama kampeni zilivyo onesha.

Kuwa na haya, ambayo ni sifa ya mtu kutokuwa tayari kufanya jambo la kinyama na ovu mbele za watu kinyume na ubinadamu, mfano kutembea uchi, kufanya ngono hadharani, kujifakhiri kwa umalaya na uasherati leo haipo.

Baada ya Uislamu kutokuwepo katika kumtawalia mwanadamu maisha yake kumeshamiri ushenzi ambapo watu wazima hujifakhiri katika vyombo vya mawasiliano wakiwa kwa sifa za kinyama kama uhusiano wa kimapenzi baina ya mtu mke na mume bila ndoa, uhusiano  wa jinsia moja katika mapenzi nk. Wanawake kukosa kujihifadhi badala yake kujiremba na kujianika, matendo yanayochochea na kuimarisha uasherati.

Ili kurudi katika ustawi halisi wa jamii ya mwanadamu, hakuna budi dunia kurudi kiutawala na kiusimamizi katika mfumo wa utawala wa Kiislamu kama ulivyokuwa utawala wa Mtume SAW na kisha Makhalifah.

Na kimsingi ni hayo ni kwa kubadilisha fikra za binadamu zifahamu na kuukataa mfumo wa kibepari na demokrasia ambao hutumia akili za kibinadamu kumuongoza na badala yake kufahamu na kushikamana na mfumo wa haki wa Kiislamu unaongoza watu kwa sharia msingi za Muumba wa kila kitu, Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rahma.

#MuhammadNiNuruKwaUlimwengu

26 Rabi ul awwal 1440 Hijri    | 04 -12- 2018 Miladi

Afisi ya Habari –   Hizb ut- Tahrir Tanzania

https://hizb.or.tz/

https://www.facebook.com/Hizb-ut-Tahrir-Tanzania

Maoni hayajaruhusiwa.