Mfunguo Sita: Tujikumbushe ‘Manhaj’ ya Mageuzi ya Mtume (Saw)

Mwezi wa Mfunguo Sita (Rabi ul awwal) ndio mwezi aliozaliwa kiongozi wetu Mtume Muhammad (SAW) aliyetumwa kuwa ni Rehma kwa walimwengu wote.

Mtume SAAW alitumwa kuja kuwakomboa wanadamu kutokana na kila aina ya minyororo ya dhulma iwe ya kijamii, kiuchumi, kisiasa nk. Na katika kutimiza jukumu hilo Mtume (SAW) alipata mafanikio makubwa ambayo hayajashuhudiwa mfano wake katika historia.

Hapana shaka yoyote mafanikio aliyoyapata Mtume (SAW) ni kutokana na muhanga wake na masahaba zake lakini kubwa ni kushikamana na kuifuata manhaj/njia thabiti ya mageuzi kutoka kwa Mola wake (SWT) toka mwanzo hadi mwisho bila ya kukengeuka hata kwa kiwango kidogo.

Manhaj ya mabadiliko ya Mtume (SAW) ilikusanya hatua zifuatazo:

Hatua ya kwanza ni kuasisi kikundi na kukifinyanga. Kikundi hiki ndicho kikundi cha masahaba wakiwa ndio wabebaji wa risala ya Kiislamu, kwa kuwa suala la ulinganizi sio jukumu la mtu mmoja mmoja katika kutendwa kwake. Hata mtu mmoja atakavyokuwa mhodari, bado kisharia litakuwa ni jukumu la kundi katika kubeba ulinganizi huu kama alivyosema Allah Ta’ala katika(Surat Al-Imran : 104)

Kikundi hicho cha Mtume (SAW) alikitayarisha na kukifinyanga kuwa na uwezo mkubwa wa kifikra, kisiasa na thaqafa jumla ya Uislamu, kuhimili misukosuko, kujikurubisha kwa Mola wao nk. Mchakato wa maandalizi hayo uliendelea kwa miaka mitatu kama vilivyotaja vitabu vikubwa na mashuhuri vya historia ya Uislamu.

Kutokana na hatua hii kisharia leo, huvuliwa hukmu ya ulazima wa kundi la ulinganizi kuusoma na kuufahamu Uislamu kama ni mfumo kamili wa maisha uliokusanya masuluhisho yote ya matatizo ya binadamu yakiwemo ya kiakida, kiibada, kiakhlaki, kimuamalati kama vile uchumi, utawala, jamii nk. Pia kusoma na kufahamu kwa upana wake ukafiri mambo leo yaani usekula uliozaa mfumo wa ubepari pamoja na nidhamu zake zote za maisha, na kila fikra,na ada zake chafu na fisidifu zinazogongana na Uislamu.

Hatua ya pili ni maingiliano ya wazi na jamii ya Makka. Hii ni hatua ya kujitosa katika jamii kufanya mgongano wa wazi wa kifikra, kwa kutangaza wazi wazi fikra ya Kiislamu na kupambana kwa hoja na dalili dhidi ya fikra, mitazamo na itikadi batili za kikafiri za Makureishi.

Katika kipindi hiki cha mgongano wa kifikra baina ya Uislamu na ukafiri na ushirikina wa Makka, Waislamu walikabiliwa na mauaji, mateso,kutengwa, propaganda nk. kutokana na msimamo na uthabiti wa fikra zao. Wahafidhina wa jamii ya Makka hususan viongozi wa makabila hawakutaka mageuzi wakihofia kutoweka ubwana wao.

Ulinganizi huu wa Uislamu katika hatua hii, ulikuwa katika upande wa kifikra na pia ulijumuisha upande wa kisiasa bila ya kujihusisha kwa namna yoyote na vitendo vyovyote vya utumiaji nguvu, ulijifunga katika kubadilisha fikra za watu kutoka fikra duni na dhalili na badala yake kuleta fikra ‘ali na adhimu, yaani fikra ya Kiislamu katika kila jambo. Kiasi kwamba wale waliosilimu hata kabla ya Uislamu kuwa na dola waliweza kuhisi namna ulivyoleta ukombozi mkubwa wa kifikra. Na ulinganizi huu ulikuwa wa sura ya kisiasa kwa namna mbili: Awali kwa kuwakosoa na kuwafedhehesha kisiasa wanasiasa wakubwa wa Makka kama akina Abu Jahl, Abu Lahb, Walid ibn Mughira nk. kuonesha Umma kwamba wamekosa sifa za kusimamia mambo ya jamii yao na badala yake wamuunge mkono Mtume (SAW) kama kiongozi mbadala kwao. Pili, ni kile kitendo cha Mtume (SAW) kilichoambatana na hatua ya kuutoa wazi ulinganizi wake, kwa kuyataka makabila makubwa yaliyokwishasilimu kumuunga mkono kisiasa na kijeshi (Nusra) ili aweze kusimamisha dola ya Kiislamu.

Katika hatua hii leo, kundi la ulinganizi lazima litangaze wazi Uislamu, fikra zake, nidhamu zake za maisha, njia zake za kukabili matatizo ya binadamu nk. kwa kutumia kila mbinu inayomkinika isiyogongana na sharia kama vile darsa za wazi, makongamano, semina, mihadhara, mitandao ya kijamii, vitabu nk. Pia ni lazima kukosoa wazi mfumo mzima wa ubepari, akida yake na fikra zake zote. Pia hujumuisha kuibua mipango michafu ya wakoloni dhidi ya Umma wa Kiislamu na Uislamu, na kwenye nchi kubwa za Waislamu hujumuisha kuwafedhehi na kuwakosoa watawala kwa dhuluma, ufisadi, khiyana wanazozifanya na kushirikiana kwao na wakoloni wa kimagharibi, sambamba na hilo kuwaomba Waislamu katika nchi hizo wenye ushawishi na uwezo wa kunusuru Uislamu watoe nusra yao.

Hatua ya tatu, ni ya kusimamisha dola ya Kiislamu na kuutabikisha/ kuutekeleza Uislamu kivitendo. Hii ni hatua iliyofikiwa kwa Makabila mawili makubwa ya Madina ya Aus na Khazraj kuafiki bila ya masharti kumkabidhi Mtume (SAW) hatamu za uongozi, na hapo Mtume (SAW) akaenda kusimamisha dola ya mwanzo ya Kiislamu ndani ya Madina kwa kuutabikisha Uislamu kivitendo kwa kutekeleza hukmu zote katika nyanja zote za maisha ya mwanadamu kama siasa,uchumi, jamii, mambo ya nje nk.

Hakika kweli kuna mazingatio makubwa na kigezo chema katika mchakato mzima wa manhaj ya ulinganizi wa Mtume (SAW). Tunaona licha ya wafuasi wake kuuwawa, kuteswa kikatili kwa mateso mabaya kama Familia ya Yassir, Bilal Ibn Rabah, Abdallah ibn Masoud, Suhaib Rumiy nk. bado Mtume (SAW) hakupoteza mwelekeo wala kuchanganyikiwa kwa kuingiza katika manhaj yake matendo ya utumiaji wa nguvu, mabavu wala silaha. Pia katika mwaka wa pili wa Utume
tayari Mtume (SAW) alikuwa na wafuasi mashuhuri kama Hamza, Umar nk. waliokuwa majemedari wakubwa, lakini kamwe Mtume (SAW) hakuanzisha vita ya msituni kama manhaj yake, bali alijifunga na njia ya kifikra na kisiasa. Kubwa zaidi hata katika makubaliano (Aqaba ya Pili) ya kupatiwa nusra na watu wa Madina, baada ya taarifa za kikao hicho cha siri kuvuja, watu wa Madina walimtaka Mtume (SAW) atoe idhini ili wachukuwe hatua za kijeshi dhidi ya Makureishi, bado Mtume (SAW) aliwazuiya, na kuwaeleza bado hajaamriwa hilo.

Mtume (SAW) alijizuilia kuchukua hatua za kijeshi katika kipindi chote cha ulinganizi wake licha ya mashaka na idhilali, sio kwa sababu ya woga au khofu bali ni kutokana na kufuata manhaj sahihi aliyotakiwa na Mola wake. Lau Mtume (SAW) angekuwa muoga, alipofika Madina asingepigana vita vya Jihadi mfululizo mpaka dakika zake za mwisho katika umri wake. Hii ni kwa sababu Mtume (SAW) alikuwa na ufahamu thabiti kuwa Jihadi ni chombo cha kusukuma siasa za nje za dola katika kuutangaza Uislamu pale diplomasia inaposhindwa, na kamwe jihadi sio manhaj ya kuleta mageuzi.

Aidha, Mtume (SAW) ametudhihirishia ufahamu thabiti juu ya dhana ya ‘Darul Kufr’/ dola isiyotawaliwa kwa Uislamu, na ‘Darul Islam’/ dola inayotawaliwa kwa Uislamu, ambapo ndani ya ‘Dar ul kufr’ huwa ni uwanja wa ulinganizi kwa kutumia manhaj ya kifikra na kisiasa, ilhali ndani ya ‘Dar ul Islam’ ni uwanja wa kutumika Jihad katika kufanikisha sera za nje za dola pale inaposhindwa diplomasia.

Pia katika manhaj hiyo ya Mtume (SAW) kunadhihirika wazi uwepo wa vigezo vya kisharia juu ya nukta kianzio cha dola ya Kiislamu. Kwa kuwa yeye Mtume (SAW) aliyakabili na kuyalenga makabila maalumu yenye nguvu tu kumkabidhi hatamu zao za mamlaka. Jambo hilo linavua hukmu ya uwepo wa sifa na vigezo maalum vya kisharia katika mahala pa kuasisi dola, na sio kila mahala, japo ukweli kuwa Mtume (SAW) alihitaji kuungwa mkono katika kuasisi dola, lakini kufanikisha hilo hakulikabili kila kabila, kwa kuwa manhaj yake ilimlazimu kulenga maeneo maalum yenye nguvu, yenye uwezo wa kuhimili kuasisiwa dola na pia yaliyojengwa vyema ‘wai amma’ (public awareness) na ‘rai amma’ (public opinion) kwa ajili ya Uislamu. Hiyo ndiyo manhaji ya Mtume (SAW) hadi kuanzisha dola ya mwanzo ya Kiislamu Madina. Kwa mazingira ya leo kwa manhaj hiyo, humaanisha sio kila mahala pana sifa ya kuwa nukta kianzio ya kurejesha dola ya Kiislamu (Khilafah), bali huzingatiwa maeneo yenye sifa na vigezo vya kisharia ikiwemo idadi kubwa ya Waislamu, nguvu nk. Sifa hizi hazipatikani kila mahala, bali ni zenye kupatikana katika nchi kubwa za Waislamu tu. Jambo hilo haliondoshi ulazima wa kwamba ulinganizi wa Kiislamu utafanyika kila mahala kuwajenga Waislamu ufahamu thabiti wa dini yao kama ni mfumo kamili wa maisha na kuwaandaa kuikubali na kuiunga mkono dola ya Khilafah mara itakaposimama kwa idhini ya Allah Ta’ala katika maeneo yenye sifa.

Hii ndio manhaji (njia) ya mageuzi aliyoitumia Mtume wetu na kipenzi chetu Muhammad (SAW) ambayo sisi Waislamu tuna wajibu kuifuata leo katika ulinganizi wa kurejesha maisha ya Kiislamu kwa kusimamisha Khilafah. Ni wajibu kumchukulia Mtume (SAW) ndio kigezo chetu katika ulinganizi kama alivyokuwa ni kigezo katika ibada nyengine zote, kwa kuwa zote hizi ni ibada. Allah Ta’ala anasema:

لَقَدْ كَانَ لَكُمْ فِي رَسُولِ اللَّهِ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ لِمَنْ كَانَ يَرْجُو اللَّهَ وَالْيَوْمَ الآخِرَ وَذَكَرَ اللَّهَ كَثِيرًا (الأحزاب: 21) )
“Bila shaka mna kigezo chema kwa Mtume wa Allah, kwa mwenye kumugopa Mungu na siku ya mwisho , na kumtaja Allah sana” (33:21)

Ummah wetu unapaswa katika mwezi huu aliozaliwa Mtume (SAW) kuizingatia sana manhaji hiyo kwa kuwa inatokana na ‘hukmu ya kisharia, ’ iliyovuliwa kwa dalili ya Kitabu na Sunna na kuacha kuandama manhaj (njia) za kimakosa zinazodhihirisha kuwa ni mikakati ya makafiri wa kimagharibi dhidi ya Uislamu na Waislamu ili makafiri hao wapate fursa ya kukashifu Uislamu, kuwa ni dini isiyo na njia thabiti ya mageuzi, kwa sababu baadhi ya Waislamu hushika njia za kimakosa kama vile demokrasia, matumizi ya silaha, ulinganizi wa akhlaq na ulinganizi wa kiroho tu (bila ya nidhamu za maisha). Baya zaidi makafiri maadui wa kimagharibi wanaongozwa na Marekani hutumia fursa ya kulazimisha uhalali wa kuwabugudhi, kuwatesa na kuwaua Waislamu kwa kisingizio cha kuubandika Uislamu na Waislamu jina la ugaidi . Allah (SWT) Anasema:

قُلْ هَذِهِ سَبِيلِي أَدْعُو إِلَى اللَّهِ عَلَى بَصِيرَةٍ أَنَا وَمَنْ اتَّبَعَنِي وَسُبْحَانَ اللَّهِ وَمَا أَنَا مِنْ الْمُشْرِكِينَ (يوسف:108)
“Sema hii ndio njia yangu ninaita (ninalingania) kwa Allah kwa ujuzi, mimi (nafanya hivi) na kila anaye nifuata…” (TMQ 12 : 108)

25 Rabi ul awwal 1441 Hijri /
22 Novemba/2019 Miladi
https://hizb.or.tz/
https://www.facebook.com/Hizb-ut-Tahrir-Tanzania

Maoni hayajaruhusiwa.