Kuangazia Malengo ya Ndoa za Mtume (Saaw)

Tukiwa ndani ya mwezi wa Rabil-awwal (Mfungo Sita), mwezi ambao alizaliwa Rasulullah SAW aliyetumwa kuwa Rehma kwa walimwengu wote.

Mtume SAW akiwa katika silsila ya Mitume wengi As. waliotangulia, nae alitumwa kwa lengo maalumu kama walivyo Mitume wote As. la kuwaongoza wanadamu katika maisha anayoridhia Allah SW ili tufaulu duniani na akhera. Kufaulu huku kumejengwa katika kubeba majukumu tuliyoletewa katika kufuata maamrisho na kuacha makatazo

Katika majukumu makubwa naya wajibu aliyotuachia Mtume SAAW ni suala la ulinganizi yaani daawa. Jambo hili ni wajibu mkubwa na nyeti unaohitaji mikakati na mbinu mbalimbali tena za kibinadamu katika kuifuata njia iliyokwisha andikwa na sharia za Allah SW.

Mikakati na mbinu hizi ni za kibinadamu hutegemea weledi na uwezo wa mtu binafsi na pia mazingira inapofanyika da’awah hiyo. Ndoa ni moja ya mbinu na mikakati hiyo kama ambavyo Mtume SAW Ametuonesha kivitendo katika maisha na harakati zake za ulinganizi.

Lazima ifahamike kwamba da’awah ni mapambano ya kifikra na kisiasa baina ya pande mbili, Uislamu na ukafiri (leo ubepari na demokrasia yake). Pande zote mbili zinahusu watu (wabeba mifumo hii) ambapo ili kuwashinda makafiri na ukafiri wao yapasa Waislamu kuimarika kiumoja katika fikra na matendo chini ya aqidah yao. Kushinda fikra na nyoyo za maadui hulazimu ikiwezekana kupunguza kama sio kuondoa upinzania wao kama kikwazo kwa da’awah ya Kiislamu.

Tunaona Mtume SAW alimuoa Bi Khadija ra. mwanamke tajiri na mtumzima. Jambo hilo lilimsaidia kimkakati kutumia mali ya mkewe (kwa ridhaa na mkewe ra.) katika shughuli za da’awah ikiwemo kuwakomboa watumwa nk. Pia malezi, ushauri na hamasa za mkewe ra. zilimuimarisha katika da’awah, kwani changamoto kubwa kwa wanaharakati ni pale wanapokosa kuungwa mkono na watu wao wa karibu.

Aidha, Mtume SAAW alimuowa Bi. Aisha bint Abubakar kwa vile da’awah inahitaji hali ya kushibana na kuungana kinyoyo baina ya wanaharakati, na katika umoja huo kuwepo mapenzi na kuhurumiana. Mtume SAAW alifanya hayo ili kuimarisha ukaribu, mapenzi na mahusiano mema baina yake na rafiki yake (da’ai mwenzake) Abu Bakar ra.

Kadhalika, Mtume SAW alimuoa Ummu Habiba ra. bint wa Abu Sufiyan, bwanyenye wa Makkah na mpinzani mkubwa wa da’awah ya Rrasulullah SAW ikiwa mbinu ya kuwakabili wapinzani wake kihisia. Ummu Habiba alikuwa ni katika wanawake waliosilimu mwanzo na kuhama Habash kuinusuru dini, kwa bahati mbaya mumewe aliritadi. Ndoa hii pamoja na kuwa mbinu ya kumliwaza mama huyu, kumsitiri pia ilisaidia katika ulinganizi, kwani moja ya kisa kilichojiri kwa mama huyu ni kumkataza baba yake Abu Sufiyan kukaa katika tandiko la Mtume SAW, kwa hoja kwamba ni tandiko la Mtukufu, ilhali Abu Sufyan ni mtu duni mbele yake. Tukio hili lina sura ya kufedhehi haiba duni ya mpinzani (character assassination). Jambo ambalo ni muhimu kisiasa na hudhoofisha na kushughulisha akili ya adui kujitathmini.

Mtume SAW alimuoa Zainab ra, bint wa Jahash aliyekuwa mke wa Zayd bin Harthah aliyekuwa mfanyakazi huru, mwana wa kulea wa Mtume SAW aliyelelewa baada ya kukombolewa kutoka utumwani. Zainab ra alikuwa kutoka katika familia bora ya kiarabu. Ndoa hii Ilikuwa kwanza kuvunja tabia ya ubaguzi wa rangi na hadhi za kiuchumi ili ibaki kwamba utukufu ni kwa uchamungu tu (Surat Hujuraat:13), kisha kitendo cha Zainab kuolewa na Mtume SAW kililenga kuondoa uzito kwa Waislamu kuoa wake wa watoto wao wa kuwalea (Surat Ahzab : 37). Jambo hilo limepekea kuleta ufafanuzi wa kivitendo katika sharia za Allah SW katika kufahamika na kutekelezwa kwa usahihi wake.

Leo hii ambapo kumekuwepo na wanaharakati ‘wengi’ katika Uislamu na msisitizo wa watu kuingia katika ndoa ni mkubwa sana takriban kila siku haikosi japo maramoja msikitini kusikia kuongelewa jambo hili. Suali linakuja katika kuadhimisha mazazi ya Mtume SAW jee, ndoa zetu ni ndoa mkakati mipana ya kidini, au ndoa, ndoa tu?. Jee ndoa zetu kimalengo zinachangiaje katika kazi za ulingazi na Uislamu, upande chanya (kwamba da’awah inasonga mbele) au hasi (kwamba ni sababu mojawapo ya kurudi nyuma na kupotea kwa da’awah na da’ai).

Jambo hili yafaa tulitie katika vitendo sana katika nyaka hizi ambapo mfumo pinzani (ubepari na demokrasia) unashajiisha zinaa kuliko ndoa kiasi cha baadhi ya watu, wakiwemo Waislamu, ima kupuuza ibada ya ndoa au kuipa muelekeo tofauti na wa asili ambao ni ujenzi wa familia imara kiaqidah na chachu ya da’awah ya kimfumo.

Tutumie majukwaa na fursa za mikusanyiko ya mwezi huu katika kukumbushana ndoa kama mkakati aliyotumia SAW katika kuimarisha da’awah na Uislamu kwa jumla.

#MuhammadNuruYetuKigezoChetu

Abu Nuthutaq Hamza

Risala ya Wiki No. 63

26 Rabi’ al-awwal 1441 Hijri 23/11/2019 Miladi

Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania
https://hizb.or.tz/

https://www.facebook.com/Hizb-ut-Tahrir-Tanzania

Maoni hayajaruhusiwa.