Kumbukumbu ya Shahidi Sheikh Abdul Aziz Badr 21 Ramadhani 1389 Hijiria

1

Sheikh Abdul Aziz Badry, mwanachuoni wa Iraq na mwanachama wa Hizb ut-Tahrir alizaliwa 1929/ 1347 Hijri katika mji wa Sammara, Iraq. Alipata elimu yake ya kidini kwa masheikh mbalimbali kama Sheikh Amjad Al-Zahawy, Sheikh Muhammad Fu’ad Al-Alusy, Sheikh ‘Abdul-Qadir Al- Khatib nk. Alikuwa maarufu kwa kutoa kalma katika misikiti ya Baghdad na kwengineko na alikuwa na ufasaha wa hali ya juu, ghera ya kuuhami Uislamu na na ushujaa usio na mithali katika kusema haki.

Sheikh ‘Abdul-‘Aziz Al-Badry alisimama kidete dhidi ya dhulma za watawala na daima alikuwa akimkosoa mtawala wa Iraq Abdul-Karim Qasim, kutokana na udikteta na dhulma zake. Pia Sheikh aliwahi kutoa fatwa kwamba ukomunisti ni ukafiri, mfumo ulioshikiliwa na kundi katika watawala.

Sheikh ‘Abdul-‘Aziz Al-Badry baada ya kuona kuna watu wanapotosha kwa kujaribu kuufananisha ukomunisti na Uislamu, aliandika kitabu maalumu “Hukmu ya Uislamu kwa Ukomunisti’ (“Hukm al-islam fi al-ishtrakiyah”) kufafanua kwa uwazi juu ya ukafiri wa ukomunisti na namna usivyowafikiana na Uislamu.

Serikali ya Iraq ya wakati ule ilianza kumuandama Sheikh kwa kumuweka kwenye kizuizi cha nyumbani kwake (house arrest) kuanzia tarehe ya 21 Ramadhan, 1389 kwa kipindi cha mwaka mzima. (2/12/1959 – 2/12/1960) Baada ya kutoka kwenye kizuizi hicho, Sheikh aliendelea na msimamo wake bila ya kutetereka, na akawekwa tena katika kizuizi kama hicho ndani ya mwaka 1961.

Katika kipindi ambacho Sheikh Badry yuko kizuizini nyumbani kwake serikali iliwatumia baadhi ya masheikh vibaraka kumshawishi aache au apunguze misimamo yake dhidi ya watawala, masheikh wengine wakimueleza kuwa dini haina nafasi na siasa. Ni wakati huo ndio Sheikh aliandika kitabu cha : “Uislamu baina ya Wanavyuoni na Watawala” (“Al-islam bayn al- ‘ulama wa al-hukkam”) kutoa ufafanuzi juu ya nafasi ya wanachuoni kwa watawala, akitolea mifano ya Swalaf Swalih namna walivyokuwa wakiamiliana na watawala. Hatimae Sheikh akawa anafungwa jela mara kwa mara kiasi cha kufikia kufungwa mara 14.
https://en.wikipedia.org/wiki/Abd_al-Aziz_al-Badri

Sheikh Badry alitekwa mwaka 1968 usiku wakati akirejea nyumbani kwake na kuwekwa mahabusu ya Qasr Al-Nihaya. Wakati huo aliteswa sana ikiwemo kukatwa ulimi na kukatwakatwa baadhi ya viungo vyake hadi kuuwawa shahid ndani ya mwaka 1969. Baada ya siku 17 watesaji walikuja kuubwaga mwili wake nje ya nyumba yake wakidai kafariki kwa maradhi ya moyo.

Taarifa zilipoenea kwa Waislamu walibeba jeneza lake likapelekwa katika Msikiti wa Imamu Abu Hanifah kuswaliwa na kuzikwa. Mwili wa Sheikh ulisheheni majeraha kwa mateso, aliuwawa shahid mnamo mwezi wa Rabi’ Al-Awwal 1389 A. H /1969 A akiwa na umri chini ya miaka 40, baada ya kufanya kazi kubwa ya kuuhami Uislamu na daawa ya kutaka kurudisha tena maisha ya Kiislamu kwa kupitia dola ya Kiislamu ya Khilafah ndani ya Iraq.

Sheikh Badry atakumbukwa sana kwa juhudi zake kubwa za kuuhami Uislamu na kupinga dhulma na uonevu. Mwaka 1967 wakati kijidola cha Mayahudi kilipovamia West Bank, Milima ya Golan na Sinai alituma barua kwa watawala wote wa Kiislamu kuwawajibisha kwa usaliti na khiyana yao kwa kukubali kusitisha mapigano dhidi ya Mayahudi.

Aidha, Sheikh Al-Badry aliongoza ujumbe maalumu wa madhehebu ya Sunni kwenda mji wa Karbala na Najaf kuwataka Wanavyuoni wa madhehebu ya Shia nao waingilie kati kuzuiya kunyongwa Mwanachuoni Sayyid Qutb wa Misri. Kiongozi mkuu wa madhehebu ya shia kwa wakati ule Sayyid Muhsin Al-Hakim alikubali na kuandika barua maalumu kwa Raisi wa Misri Gamal ‘Abdul-Nasir kumtaka asimuuwe Sayyid Qutb, akimueleza kuwa ni miongoni mwa wanavyuoni na mufakirina mkubwa .
https://heroesofdawah.wordpress.com/…/abdul-aziz-al-badry-…/

Bila ya kusahau kwamba miongoni mwa sababu za kukamatwa kwa Sheikh Al-Badry ndani ya mwaka 1969 kuteswa hadi kuuwawa ilikuwa ni kitendo chake cha kulaani vikali dhulma ya serikali ya ‘Baath’ ya Iraq kumkamata mtoto wa kiume wa Mwanachuoni mkubwa wa madhehebu ya Shia Ayatollah Muhsin al-Hakim.

Masoud Msellem

27 Ramadhan 1439 / 12 Juni 2018

1 Comment
  1. Marquail says

    This post offers clear idea in favor of the new users of blogging,
    that truly how to do running a blog.

Leave A Reply

Your email address will not be published.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.