Kukithiri Kwa Umachinga Na Suluhisho Lake

بسم الله الرحمن الرحيم

Karibuni tumeshuhudia kwa mara nyengine tena serikali kuanza kuchukua hatua dhidi ya wafanyabiashara ndogo ndogo nchini maarufu kama ‘wamachinga’. Hatua hizi zinajumuisha kutimuliwa, uvunjaji wa vibanda vyao na kuondoshwa katika maeneo yenye mzunguko mkubwa wa biashara katika jiji kuu la biashara la Dar es Salaam na majiji mengine.
Kabla hatujaangazia udhaifu wa hatua hiyo na suluhisho halisi la mgogoro huu ulioibuka, tuangalie chanzo cha uwepo wa mtindo huu wa biashara za kimachinga kimaumbile, kisera na kimfumo. Baadhi ya sababu zinazopelekea kuongezeka kwa aina hii ya biashara nchini na sehemu nyengine mpaka kufikia hatua kutokana na kukosa sera nzuri za kiuchumi inaonekana kama tatizo na kero. Miongoni mwa sababu ni kama hizi:
1. Kukithiri kwa umasikini na hitajio la kujinasua.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Wizara ya Fedha na Mipango kufuatia Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi kwa Tanzania Bara uliofanyika mwaka 2017-18 na kuchapishwa mwaka 2019 zinaonyesha kwamba kiwango cha umasikini uliokithiri, kwa maana ya kukosa kipato cha kutimiza mahitajio ya msingi kwa uzima na uhai wa mtu kinagusa asilimia 26.4 ya watu katika Tanzania Bara, yaani takribani watu milioni 12. Hao ni watu walio chini ya mstari wa umasikini yaani wanakosa wastani wa shilingi 416,927 kwa mwezi kuwawezesha kula, kuvaa na kulala, achilia mbali walio katika mstari wa umasikini wanaohimili kipato hicho lakini hawana cha ziada. (Rejea: Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi kwa Tnzania Bara wa Mwaka 2017-18: Matokeo ya Viashiria Muhimu)
Hali hii inapelekea suala kutafuta kipato liwe ni la kufa na kupona achilia mbali wanaoiba kupora na kufanya ujambazi hata machinga kujitoa katika hali ngumu ikiwemo kukaa juani, kukaa chini ya nguzo za umeme, kurejea vilingeni baada ya kuporwa na kupewa mkong’oto, ni hatua za kimsukumo wa kimaumbile ili kuhifadhi maisha yao, kwani kama si hivyo basi ni kutumbukia katika wizi, ujambazi na utapeli wa hali ya juu ili waweze kuishi.
2. Tatizo kubwa la ukosefu wa ajira.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Umoja wa Mataifa, mwaka 2016 zinaonyesha kwamba kati ya vijana 700,000 wa kitanzania wanaotafuta ajira rasmi kila mwaka ni fursa 40,000 tu sawa na asilimia 6 ya hitajio ndizo ambazo huwa wazi. Bila shaka hali hii hulazimisha vijana kujihusisha na ajira zisizo rasmi ikiwemo umachinga ili kukabiliana na hali ngumu ya maisha kwa lengo la kuhifadhi uhai (Rejea: https://news.un.org/…/472972-suala-la-ukosefu-wa-ajira…)
3. Ukubwa wa kodi na ongezeko la gharama za maisha.
Miongoni mwa sababu zinazopelekea kuibuka kwa wamachinga ni wao kutokuweza kujishughulisha na mfumo wa biashara rasmi kufuatia uwepo wa utitiri wa kodi na ushuru katika mfumo huo. Achilia mbali kodi za wazi za serikali (direct tax) kodi za kulipia maeneo yaliyo rasmi zipo juu. Wenye nyumba katika maeneo yaliyochangamka kibiashara hulazimika kupandisha kodi kulingana na ongezeko la gharama za maisha na gharama kubwa anazoziingia katika kuboresha na kuhudumia jengo lake. Hali hii haiwashindi wamachinga tu bali hata raia kwa ujumla, kwani tumeona pia moja ya sababu ya kushamiri biashara za kimachinga na wengi katika watu kukimbilia kununua mahitaji yao kwa wamachinga ni kufuata unafuu, hali inayoashiria vipato vyao havikidhi kuhimili bidhaa na huduma zilizomo ndani ya mfumo wa kodi.
4. Masoko kutotoa fursa kwa wafanyabiashara wadogo wadogo.
Ni wazi kuwa wamachinga hukiri changamoto wanazozileta katika maeneo yasiyo rasmi, hata hivyo maeneo wanayopangiwa kuhamia huwa na changamoto ya kutofikiwa na wateja, jambo linalowapelekea kurejea katika maeneo waliyofukuzwa ili biashara zao ziendelee. Hii inadhihirisha ya kwamba kwa sababu mbalimbali maeneo yenye soko kwa maana ya mzunguko mzuri wa fedha hayatengewi sehemu kwa ajili ya watu wenye mitaji midogo kuweza kujiegesha na kufanya biashara zao.
5. Kutupwa maeneo nje ya miji na mafuriko ya watu mijini
Kutupwa maeneo ya vijijini kimaendeleo, kukosekana uthabiti wa kiuchumi na pia kuekezwa nguvu kubwa ya kimaendeleo mijini ni sababu inayochangia wimbi la watu kuhamia mijini kutoka vijijini na kujihusisha na umachinga. Hilo pia huchangiwa zaidi na fikra msingi ya mfumo wa kibepari ambayo huonesha upeo wa ufanisi wa maisha (saada) ni kustarehesha kiwiliwili. Fikra hii ndio pia husukuma watu binafsi kutumikia matamanio ya nafsi zao ikiwemo kujitosa katika mambo ya za muziki, uasherati, pombe na zinazoitwa burudani mbalimbali. Hilo huenda sambamba na kiu ya kuchuma fedha kwa njia rahisi na za haraka. Jambo linalopelekea nguvu kubwa ya uwekezaji wa shughuli za kimaendeleo na nyenzo za starehe kuelekezwa zaidi mijini. Hivyo, wimbi kubwa la watu hasa vijana kughilibiwa na tamaa ya kuishi mjini na kujiendesha kwa shughuli za kimachinga husukumwa pia na kuwa karibu na upatikanaji zaidi wa zinazoitwa starehe. Na vijana waliopo mijini nao kwa kuwa wana mitaji midogo kubaki kujiimarisha ndani ya miji hiyo kwa umachinga, ilhali maeneo ya vijijini na nje ya miji yakiachwa bila ya kuendelezwa na kuwekezwa.
Kimsingi hizo ni baadhi tu ya sababu zinazopelekea kuongezeka na kushamiri kwa biashara ya machinga nchini Tanzania na kwengineko. Sababu hizi na nyingine nyingi ni ishara tosha ya kuonyesha kushindwa kwa mfumo wa kibepari (Capitalism) katika kutatua changamoto za maisha na kutoa masuluhisho sahihi ya matatizo ya kiuchumi, hali inayoleta taharuki mara kwa mara na hatari ya kuibuka machafuko kama yale ya vuguvugu la waarabu.
Kiasili tatizo hili ni dogo sana chini ya sera za Kiislamu, kwani Uislamu katika kutatua matatizo huyaangazia kama matatizo ya kibinadamu na si kama matatizo ya kiuchumi au ya kibiashara. Katika makala inayofuata InshaAllah tutaonesha suluhisho la tatizo hili la machinga kwa mujibu wa Uislamu.
Abdinasir Said
Risala ya Wiki No. 116
12 Rabi’ al-thani 1443 Hijri / 17 Novemba 2021 Miladi

Maoni hayajaruhusiwa.