Kile Ambacho Mabenki ya Kiislamu Yanakiita Murabaha na Hukmu Yake ya Kisheria!

بسم الله الرحمن الرحيم

Kwa: Ashraf Abdul Halim Teiti

Swali:

Assalam Aleykum, Hakika sisi tunajua kuwa murabaha kama fahamu inaruhusiwa kisheria, lakini naamini uhalisia wa sasa wa murabaha katika mabenki ya Kiislamu ni kinyume na Sheria, haswa kwa watu wetu huko Palestina, ambapo mteja anaainisha bidhaa kwa mfanyabiashara na anakubaliana naye bei na anafanya mkataba wa makubaliano pamoja na benki na benki inanunua bidhaa hiyo na kuisalimisha kwa mteja huyo na benki inaiweka rehani bidhaa hiyo iwe ni nyumba, gari au kitu kingine chochote, kisha umiliki wake huhamishwa baada ya kulipa kiwango ambacho ni sawa na thamani ya bidhaa hiyo pamoja na kiasi au asilimia yenye kuamuliwa kulingana na kipindi cha malipo, na benki huzingatia kiasi kilichoongezwa kuwa ni badali ya gharama za kufanya muamala huo… Tafadhali toeni ufafanuzi wa hukmu ya kisheria juu ya mfano wa miamala kama hii? Mwenyezi Mungu awabariki.

Jibu:

Waaleykum salaam wa rahmatullah wa barakatuh,

Swali lako linajumuisha mambo matatu:

La kwanza: Murabaha na hukmu yake…

La pili: Kile ambacho mabenki ya Kiislamu yanakiita Murabaha…

La tatu: Maudhui ya rehani ya bidhaa iliyonunuliwa…

Huu hapa ufafanuzi kwako:

  • Kuhusu uhalisia wa murabaha na hukmu yake, tumeelezea hili katika jibu la swali la tarehe 19 Rajab 1434 Hijria – Mei 29, 2013 M, na kilichokuja katika jibu hilo linaloashiriwa ni haya yafuatayo:

[… Murabaha kilugha inamaanisha kuhakikisha faida, husemwa: Niliuza mzigo kwa faida, au nilinunua kwa faida.

Na kisheria: ni kwa muuzaji kuiweka bidhaa yake kwa ajili ya mauzo kulingana na gharama yake na faida maalum, nayo ni kutoka katika mauzo ya uaminifu kwa sababu inategemea uaminifu wa muuzaji kumjulisha juu ya gharama ya bidhaa kwake.

Nayo inaruhusiwa kisheria kwa sababu ni kutokana na faida iliyo juu ya bei aliyoinunulia kwayo muuzaji, basi ikiwa muuzaji atasema nakuuzia bidhaa hii kwa faida kadha juu ya bei niliyoinunulia kwayo, na mnunuzi akajulishwa bei hii, na akakubali, hii basi itakuwa inaruhusiwa kwa sababu huu ni uuzaji ambao taarifa yake inajulikana.] Mwisho.

  • Ama yale yaliyokuja katika swali lako kuhusu kile kinachoitwa murabaha katika mabenki ya Kiislamu swala hali tulishalijibu kwa ufafanuzi mnamo 24 Rajab 1434 H – 03 Juni 2013 M, na nayarudia tena kwako yale yaliyokuja katika jibu hilo linaloashiriwa:  

[… muamala wa mabenki ya Kiislamu ambao unaitwa murabaha ni muamala unaohalifu sheria, ni hilo ni kati ya mambo maarufu zaidi:

La kwanza: kwamba hufanya mkataba wa kuuza na mnunuzi kabla benki haijanunua gari au jokofu … na Mtume (saw( alikataza kuuza kile ambacho hukimiliki, kutoka kwa Hakim Ibn Hizam, ambaye alisema: Nilisema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, mtu ananijia, na kutaka nimuuzie kitu ambacho sina, kisha nikamuuzia kutoka sokoni; akasema: «لَا تَبِعْ مَا لَيْسَ عِنْدَكَ»  “Usiuze kile usicho nacho.” Imepokewa na Ahmad. Huyu ilimuuliza Mtume (saw) juu ya mnunuzi anayekuja kununua bidhaa kutoka kwake ambayo hana, hivyo akaenda sokoni na kuinunua na kisha kumuuzia, basi Mtume (saw) akakataza kuhusu hilo isipokuwa ikiwa bidhaa iko pamoja naye na kisha kuiwasilisha kwa mnunuzi akitaka atainunua na akiwa hataki hainunui.

Na ili kufafanua hilo tunasema: mtu ambaye anakwenda benki kutaka mkopo wa kifedha… benki ikamuuliza mkopo au pesa hizi wazitaka kwa ajili gani, mtu huyo akasema ili nunue jokofu au gari au mashini ya kufulia nguo… kisha benki ikafanya makubaliano na mtu huyu kwamba itamnunulia jokofu na kisha kumuuzia kwa malipo ya awamu kwa bei kadhaa, na makubaliano haya yanakuwa ni ya lazima kabla ya benki kununua jokofu hilo, halafu benki inakwenda kumnunulia jokofu mtu huyo, na mtu huyo hawezi kukataa kununua jokofu hilo kutoka kwa benki, kwa sababu makubaliano na benki yalifanywa kabla ya jokofu kuwa mali ya benki, kwa hivyo mkataba huu ulifanywa kabla ya benki kumiliki jokofu.

Na wala haisemwi kwamba benki inamuuzia mnunuzi baada ya benki kulinunua. Hii haisemwi hivyo kwa sababu makubaliano ya benki na mnunuzi uwajibu wake ulifanywa kabla ya benki kununua bidhaa hiyo kwa maana kuwa mnunuzi hawezi kukataa kuinunua baada ya benki kumnunulia, kwa hivyo mkataba ulikamilika kwa umbo la ulazima kabla ya benki kuinunua.

Lau kama benki ingekuwa na duka la majokofu na ikampa ofa kwa mtu huyo, akitaka anunue na akiwa hataki asinunue, kama muuzaji mwingine yeyote wa majokofu, basi ingekuwa ni halali kwake kuuza kwa pesa taslimu na kwa malipo ya awamu.

Pili: Hairuhusiwi ikiwa mnunuzi atachelewa kulipa mgao wa malipo deni kuongezwa juu ya mnunuzi kwa sababu hii ni riba na ndio inayoitwa riba ya kuchelewa (Riba al-Nasi’a), na ilitumika katika zama za Ujahiliya, kwa hivyo ilikuwa wakati wa kulipa deni ukifika, na mdaiwa hakuweza kulipa katika muda ulioahidiwa, deni huongezwa. Uislamu ukaja na kuiharamisha kabisa, na ukampa mdaiwa muda zaidi bila kuongezeka kwa deni,

﴾وَإِنْ كَانَ ذُو عُسْرَةٍ فَنَظِرَةٌ إِلَى مَيْسَرَةٍ وَأَنْ تَصَدَّقُوا خَيْرٌ لَكُمْ إِنْ كُنْتُمْ تَعْلَمُونَ﴿.

“Na akiwa (mdaiwa) ana shida, basi (mdai) angoje mpaka afarijike. Na mkiifanya deni kuwa ni sadaka, basi ni bora kwenu, ikiwa mnajua.” [al-Baqara: 280]. Kwa hivyo muamala kama huu uliotajwa juu hairuhusiwi kufanya pamoja na benki.] Mwisho.

  • Ama maudhui kuhusu kuweka rehani bidhaa iliyonunuliwa hadi awamu zote zilipwe, tumejibu hilo mnamo 06 ya Sha’ban 1436 H – 05/24/2015 M, jibu la kina, ambapo yaliyomo:

[… Suala hili linajulikana kifiqh chini ya neno “rehani ya kitu kilichouzwa kwa bei yake”, ikimaanisha kuwa kitu kilichouzwa kinabaki rehani na muuzaji mpaka mnunuzi alipe thamani yake. Suala hili halijitokezi ikiwa muuzaji na mnunuzi ni kama vile Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alivyosema katika hadith iliyopokewa na Al-Bukhari kutoka kwa Jabir bin Abdullah, radhi za Mwenyezi Mungu ziwe pamoja nao:

«رَحِمَ اللَّهُ رَجُلاً سَمْحاً إِذَا بَاعَ، وَإِذَا اشْتَرَى، وَإِذَا اقْتَضَى»

“Mungu amrehemu mtu ambaye ni mwema anapouza, na anaponunua, na anapoitisha kitu.” Lakini mambo haya mawili wakati mwengine yanatofautiana kuhusiana na usalimishaji bidhaa kwanza au kulipa thamani yake kwanza, Baada ya mkataba wa uuzaji, muuzaji anaweza kuizuia bidhaa, yaani kuiweka rehani kwake, hadi thamani yake ilipwe, na hapo ndipo suala hili linatokea, na suala hili wametofautiana kwalo wanachuoni wa kifiqhi, wengine wao wanaruhusu kwa masharti, na wengine wao hawaruhusu, na kuna wengine wanaoruhusu kwa hali moja na hawaruhusu kwa hali nyengine…. Na kadhalika.

Na lile ninalolipa nguvu baada ya kulisoma suala hili ni kama lifuatavyo:

Kwanza: aina kinachouzwa:

  • Kwamba kile kinachouzwa kiwe ni chenye kupimwa kwa mafungu, kupimwa kwa uzani, au kuchumwa … nk, kama kuuza mchele, kuuza pamba, kuuza vitambaa, n.k.
  • Kwamba kile kinachouzwa kiwe si chenye kupimwa kwa mafungu au kupimwa kwa uzani … nk, kama kuuza gari, kuuza nyumba, kuuza mnyama, n.k.

Pili: Bei ya kinachouzwa

  • Kwamba iwe ni taslimu, yaani pesa, kama vile kununua bidhaa kwa pesa elfu kumi iliyolipwa papo hapo.
  • Kwamba iwe ni yenye kuakhirishwa kwa muda, kama vile kununua bidhaa kwa elfu kumi na kuilipa baada ya mwaka
  • Kwamba sehemu ya bei hiyo ilipwe kwanza, na sehemu yake nyengine ilipwe baadaye, kama vile kununua bidhaa na ulipe malipo ya kwanza ya elfu tano, na hizo tano zingine zilipwe baada ya mwaka mmoja kwa mfano, au kwa mafungu ya kila mwezi ..

Tatu: Hukmu ya Kisheria inatofautiana kwa kutofautiana mambo hayo yaliyotajwa juu:

Hali ya kwanza: Kinachouzwa hakipimwi kwa mafungu wala kwa uzani… yaani kwa mfano kuuza nyumba au gari au mnyama…

Bei ni pesa, yaani ananunua gari kwa elfu moja pesa taslim, ni hili liwe limethubutu katika mkataba huo.

Katika hali hii inaruhusiwa kwa muuzaji kuizuia bidhaa, yaani ibakie rehani kwake mpaka bei ya kulipwa hapo kwa hapo ilipwe kwa mujibu wa mkataba. Na dalili ya hilo ni Hadith Tukufu iliyopokewa na At-Tirmidhi na akasema ni “Hadith Hasan” kutoka kwa Abi Umamah amesema: Nimemsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akisema katika hotuba ya mwaka wa Hijja ya kuaga (Hijjah al-Wadaa):

«العَارِيَةُ مُؤَدَّاةٌ، وَالزَّعِيمُ غَارِمٌ، وَالدَّيْنُ مَقْضِيٌّ»

Al-Zaim (kiongozi): Al-Kafil (mfadhili), Al-Gharim (mdaiwa): Dhamin (mdhamini), na hoja katika hadith hii iko katika maneno yake (saw) «وَالدَّيْنُ مَقْضِيٌّ» “Deni lapaswa kulipwa” Ikiwa mnunuzi atapokea bidhaa kabla ya kulipa bei, basi atakuwa ameinunua kwa deni, na “Deni lapaswa kulipwa”, yaani ulipaji wa deni ni aula maadamu ununuzi ulikuwa kwa pesa taslimu, na kwa ibara nyengine ni alipe bei kwanza maadamu bei hiyo iliyoko katika mkataba ni pesa taslimu… Al-Kaasani asema katika Badaai’ Al-Swanaai’ kusherehesha hadith hii (Maneno yake (saw) – “Deni lapaswa kulipwa”, yamesifia (saw) – umbo la deni kwamba lapaswa kulipwa – kwa sifa ya kijumla, hivyo endapo atachelewa kulipa bei kwa kupokea chenye kuuzwa deni hili halitakuwa limelipwa, na hii ni kinyume na andiko hilo.).

Hivyo basi inaruhusiwa kwa muuzaji kukizuia kwake chenye kuuzwa hadi mnunuzi alipe bei, na kwa hilo hapo hakutakuwa na deni, na hili linakubaliana na mkataba huo kwa sababu chenye kuuzwa hakikuwa chauzwa kwa deni bali kilikuwa chuzwa kwa pesa taslimu.

  • Kwamba bei italipwa baadaye, kama kununua gari kwa malipo ya elfu kumi zitakazolipwa baada ya mwaka, katika hali hii hairuhusiwi kuizuia bidhaa hadi malipo yakamilishwe kwa sababu bei italipwa baadaye kwa mujibu wa mkataba na itifaki ya muuzaji, basi hairuhusiwi kwake kuizuia bidhaa kama rehani ya bei yake maadamu yeye ameiuza kwa malipo ya baadaye ya bei, hivyo hana haki ya kuizuia bidhaa hiyo, na kwa hilo hairuhusiwi kwake kuizuia bidhaa hiyo bali anapaswa kuisalimisha kwa mnunuzi.
  • Kwamba sehemu ya bei italipwa sasa na nyengine italipwa baadaye, kama kununua gari kwa malipo ya kwanza ya elfu tano yaliyolipwa kwa pesa taslimu, na elfu tano nyengine zitalipwa zote mara moja baada ya mwaka, au zitalipwa kwa mafungu katika nyakati zajazo.

Katika hali hii yaruhusiwa kwa muuzaji kuizuia bidhaa hadi malipo ya sasa yalipwe, na baada ya hapo hairuhusiwi kwake kuizuia bidhaa hiyo kutimiza malipo ya baadaye, na hilo ni kwa yale tuliyoyataja katika nukta 1 na 2.

Na mukhtasari ni kuwa inaruhusiwa kwa muuzaji kuiweka rehani bidhaa juu ya malipo ya sasa kwa sasa ya bei yake, yaani endapo mkataba wa uuzaji ni kwa malipo ya hivi sasa ya bei yanayolipwa kwa pesa taslimu, basi muuzaji anaruhusiwa kuizuia bidhaa kwake hadi mnunuzi alipe bei yake ya hivi sasa kwa mujibu wa mkataba wa uuzaji.

Na vilevile inaruhusiwa kwa muuzaji kuizuia bidhaa kwake hadi mnunuzi alipe sehemu ya malipo ya hivi sasa ya bei kwa mujibu wa mkataba wa uuzaji.

Wala hapa haisemwi kuwa vipi mnunuzi ataiweka rehani bidhaa yake kabla hajaipokea, yaani kabla hajaimiliki? Na hilo ni kwa sababu rehani hairuhusiwi isipokuwa kwa kile kitu ambacho charuhusiwa kuuzwa, na ambapo bidhaa zilizonunuliwa haziruhusiwi kuuzwa isipokuwa baada ya kuzipokea kwa kuzingatia Hadith ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) ambayo imepokewa na Al-Bayhaqi, kutoka kwa Ibn Abbas amesema: amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) kumwambia Utab bin Asyad:

«إني قد بعثتك إلى أهل الله، وأهل مكة، فانههم عن بيع ما لم يقبضوا»

“Hakika nimekutuma kwa watu wa Mwenyezi Mungu (swt), na watu wa Makkah, basi wakataze kuuza kile ambacho hawajakipokea” Na Hadith ambayo imepokewa na Tabarani kutoka kwa Hakim bin Hizam amesema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, hakika mimi nauza biashara nyingi, ni yapi ambayo ni halali kwangu na yapi ambayo ni haramu? Akasema:

«لَا تَبِيعَنَّ مَا لَمْ تَقْبِضْ»

“Usiuze kitu ambacho hujakipokea”, hadith hizi ziko wazi katika katazo la kuuza kitu ambacho hamjakipokea, vipi basi kukiweka rehani chenye kuuzwa kabla ya kukipokea?

Haisemwi hivyo kwa sababu hadith hizi mbili zinahusiana na chenye kuuzwa ambacho hupimwa kwa mafungu au kwa uzani… ama ikiwa chenye kuuzwa si katika hivyo kama nyumba na gari na mnyama… basi inaruhusiwa kukiuza kabla ya kukipokea kwa kuzingatia hadith ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) ambayo imepokewa na Bukhari kutoka kwa Ibn Umar (ra), amesema: tulikuwa pamoja na Mtume (saw) katika safari, na nilikuwa juu ya ngamia mkaidi wa Umar, na alikuwa yuanishinda, alikuwa akienda mbele ya watu, kisha Umar anamkemea na kumrudisha nyuma, anakwenda mbele tena, kisha Umar anamkemea na kumrudisha nyuma, Mtume (saw) akamwambia Umar:  «بِعْنِيهِ» “niuzie”, akasema: huyo ni wako ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, akasema: «بِعْنِيهِ» “niuzie” akamuuza kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw), Mtume (saw) akasema:

«هُوَ لَكَ يَا عَبْدَ اللَّهِ بْنَ عُمَرَ، تَصْنَعُ بِهِ مَا شِئْتَ»

“Huyo ni wako ewe Abdullah bin Umar, mfanye unavyotaka”, Haya ni malipo ya kile kinachouzwa kwa zawadi kabla ya kupokelewa, ambayo inaonyesha kumilikiwa kikamilifu kwa mali ya kitu kilichouzwa kabla ya kupokewa, na inaonyesha kuruhusiwa kuiuza kwa sababu umeshakamilika umiliki wa muuzaji kwake.

Na kwa hayo inaruhusiwa kukiweka rehani kitu kilichouzwa kabla ya kukipokea maadamu inaruhusiwa kukiuza kabla ya kukipokea, lakini hii ni ikiwa chenye kuuzwa si katika vitu vinavyopimwa kwa mafungu au kwa mizani… kama nyumba, gari na mnyama na mfano wake, na katika hali ya kufunga mkataba wa uuzaji kwa bei ya hapo kwa hapo, au katika hali ya kupatikana kwa sehemu ya malipo ya bei ya hapo kwa hapo katika mkataba wa uuzaji, basi inaruhusiwa kukiweka rehani kilichouzwa kabla ya kukipokea hadi bei ya hapo kwa hapo itakapolipwa au sehemu ya bei ya hapo kwa hapo itakapolipwa.

Hali ya pili: chenye kuuzwa ni katika vinavyopimwa kwa mafungu au uzani… kama kununua kiwango kingi cha mchele, pamba au kiwango kingi cha vitambaa… katika hali hii basi hairuhusiwi kukizuia kilichouzwa kwa bei namna itakavyo kuwa uhalisi wa bei: pesa taslimu hapo kwa hapo, au malipo ya baadaye kwa mara moja au kwa mafungu:

Ikiwa bei italipwa baadaye hairuhusiwi kwake kuizuia bidhaa kama tulivyo bainisha juu.

Na ikiwa bei italipwa hapo kwa hapo hairuhusiwi kwake kuizuia bidhaa, yaani kuiweka rehani, kwa sababu hairuhusiwi kuweka rehani kitu chenye kupimwa kwa mafungu na uzani kabla ya kukipokea kuambatana na Hadith ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) ambayo tumeitaja juu. Na muuzaji hapa katika hali ya chenye kuuzwa kwa bei ya hapo kwa hapo yuko baina ya mambo mawili:

Ima aiuze bidhaa kwa bei ya hapo kwa hapo na aisalimishe kwake (mnunuzi) na anamsubiri sawa ikiwa atalipa be hapo kwa hapo au baada ya muda bila ya kuiweka rehani bidhaa hiyo… au asiiuze bidhaa hiyo, yaani bila ya kuweko uwekaji rehani bidhaa hiyo.

Kwa havyo, pindi unapofungwa mkataba wa uuzaji kwa bei ya hapo kwa hapo au ya baadaye katika hali ambapo aina ya kichouzwa ni miongoni mwa vyenye kupimwa kwa mafungu au uzani, hairuhusiwi kwa muuzaji kuiweka rehani bidhaa kwake hadi bei itakapolipwa.

Na hili ndilo ninaloliona kuwa na nguvu zaidi, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Zaidi na Mwingi wa Hekima.]

Na kwa haya yote jibu la swali lako linakuwa limekamilika.

Ndugu yenu,

Ata bin Khalil Abu Rashtah

12 Muharram Al-Haram 1442 H

Sawia na 31/08/2020 M 

Link ya jibu hili la swali kutoka ukurasa wa Amiri (Mwenyezi Mungu amhifadhi) wa Facebook

Link ya jibu hili katika ukurasa wa wa Amiri (Mwenyezi Mungu amhifadhi) wa wavuti

“Bofya Hapa uDownload Pdf”

Maoni hayajaruhusiwa.