Karibuni Ndugu Zetu Mahujaji

Karibuni Mahujaji watukufu,

Kwanza pokeeni pole na pongezi. Poleni kutokana na uzito na mashaka ya kimaumbile ya safari na pia poleni kwa uzito na vikwazo vilivyowekwa na watawala wa Saudia ambao haukupaswa kuwepo. Amma, pongezi kwa kuwa mmeitikia amri na wajibu wa Muumba wa kutekeleza nguzo adhimu miongoni mwa nguzo za Kiislamu. Basi twataraji kwa Allah Taala Amekubali Hijja yenu na kufuta madhambi yenu.

Karibuni Mahujaji watukufu,

Kwa hakika mmeizuru nyumba takatifu ambayo wamezuru manabii na watu wema. Pia mmeyashuhudia mengi zikiwemo dalili za wazi wazi za Allah SW, ikiwa pamoja na sehemu ya kisimamo cha Nabii Ibrahim As.
Allah (S.W) Anasema:

فِيهِ آيَاتٌ بَيِّنَاتٌ مَقَامُ إِبْرَاهِيمَ وَمَنْ دَخَلَهُ كَانَ آمِنًا

‘Humo mna Ishara zilizo wazi, mahali aliposimama Ibrahim, na atakayeingia atakuwa salama….. ’’

(3:98)

Karibuni Mahujaji watukufu,

Tukitaraji kutoka kwenu zawadi mliyokabidhiwa kuja nayo kwa Umma. Tareekh inaonesha wazi mahujaji hukabidhiwa risala maalum ya muongozo kufikisha kwa walimwengu waliokosa kuhudhuria ibada hiyo muhimu.
Rasulullah (S.A.W) katika Hijja yake ya Mwisho aliwakabidhi mahujaji risala maalum, kuwataka wasikilize kwa makini na kuwapa jukumu la kuwafikishia wale wasiokuwepo.
Mtume (S.A.W) akasema: ‘‘ Hakika damu zenu na mali zenu ni haramu juu yenu, kama utukufu wa siku yenu hii, katika mwezi wenu huu na katika mji wenu huu’’.

Karibuni Mahujaji watukufu,

Tukipaswa kuwakumbusha kuwa wakati Hijja ya mwaka jana (2017) ikiendelea maelfu kwa malaki ya Waislamu wa Myanmar/Burma walikuwa wakichomwa moto, kuuwawa kinyama na kikatili na Mabudha huku jamii ya Kimataifa ikitoa baraka kwa kukaa kimya. Basi mahujaji waliokuwa wamekusanyika Makkatul Mukarram walipewa risala juu ya unyama na uharamia ule dhidi ya sehemu ya Umma wetu? Aidha, Aidha, walipewa risala yoyote juu ya dhulma, mateso, idhilali na mauwaji ya ndugu zetu wa Syria, Kashmir, Iraq, Palestina, Libya, Afghanistan, Yemen, Somalia nk.

Karibuni Mahujaji watukufu,

Pia mnajua kuwa wakati Hijja ya mwaka huu ikiendelea mwaka kulikuwa na kunaendelea mpaka leo mauwaji makubwa ya Waislamu wa Yemen wakiwemo watoto wadogo wasio na hatia, yakifanywa na Serikali ya Saudia kwa maslahi ya Wamagharibi.

Karibuni Mahujaji watukufu,

Huku tukiamini kwa dhati kuwa hamkupewa risala maalum ya kutibu dharba iliyoikumba Umma wa Kiislamu. Kwa kuwa wanaosimamaia Hijja, watawala wa Saudia ni miongoni mwa wanaofanya kazi kuupa dharba Umma wetu. Hamkupewa risala hiyo licha ya kuwa mna haki ya kuelezwa, lakini hawamkuelezwa chochote wala kupewa risala yoyote juu ya mustakbal wa Umma wetu. Basi tambueni kwa kutopewa risala hiyo, watawala hao na wasimamizi hao wa Hijja wamekufanyieni khiyana kubwa nyinyi na sisi, kwa kuwa risala hiyo ni zawadi bora kwetu.

Karibuni Mahujaji watukufu

Na tambueni kuwa watawala kwa makusudi wanaufanya mjumuiko wa Hijja usilete faida timilifu kwa Umma wetu, wanatamani tu kuwaona Waislamu wamekusanyika pamoja – mwekundu na mweupe bali wawe wamebebeshwa dhana potofu ya utaifa ndani ya mkusanyiko huo. Wanatamani watawala hao mlale fofofo wakati Marekani na washirika wake katika ardhi za Waislamu wakiendeleza uporaji wa rasilimali pamoja na mateso na unyakuzi wa Waislamu duniani kote kwa kisingizio cha ugaidi. Huku wakifanya kazi usiku na mchana kuzuiya Sheria za Allah (S.W) na badala yake watabikishe mfumo thakili wa kibepari na siasa yake batil ya demokrasia.

Karibuni Mahujaji watukufu

Hapana shaka hali hii inatuonyesha uhitaji wa dola ya Kiislamu ya Khilafah kuisimamia ibada ya Hijja kama vile Mtume S.A.W pamoja na Makhulafau Rashidah walivyosimamia Ibada hii. Chini ya watawala wa Kiislamu waliotangulia mkusanyiko wa ibada ya Hijja ulikuwa ni nukta muhimu ya kuangazia mafungamano ya kiibada, kuazia upelekaji wa daawa katika ulimwengu kupitia daawa na jihadi, kuunganisha Umma na kuangazia mustakbali wa Umma wa Kiislamu katika vipengee vyote.

Karibuni Mahujaji watukufu

Huku tunamuomba Allah (S.W) Awatakabalie Hijja zenu na Awalipe malipo ya wale waliotekeleza sawa katika Hijja zao, vilevile Aturuzuku nasi ili tuende kutimiza nguzo hiyo ya tano mwakani tukiongozwa na Khalifah na kurudi na furaha na zawadi bora kwa Ummah wetu na huzuni na hasara kwa makafiri

Ali Amour
Mjumbe wa Afisi ya Habari

Hizb ut Tahrir Tanzania

Maoni hayajaruhusiwa.