Viongozi Wa Biladi za Waislam Kuna Funzo Seneta Mc Cain

Mwanasiasa mashuhuri wa Chama cha Muhafidhina (Republicans) nchini Marekani Seneta John Mc Cain amefariki dunia Jumamosi 25 Agosti akiwa na umri wa miaka 81 baada ya kuugua saratani ya ubongo.

Seneta McCain amewahi kushika nyadhifa mbalimbali Marekani ikiwemo pia kuteuliwa na chama chake cha Republicans kuwa mgombea wa kiti cha uraisi mwaka 1999, akiwa mgombea dhidi ya Barack Obama (Democrats). Mwaka 1997, Jarida la Time lilimtaja Seneta McCain kuwa mmoja miongoni mwa watu 25 wenye athari na ushawishi mkubwa nchini Marekani.

Seneta McCain ni mtu jasiri aliyebeba ghera ya kimfumo kwa kuulinda na kuutetea kwa namna yoyote mfumo wa kidemokrasia na kuilinda na kuifanya dola ya Marekani kuwa juu kwa namna yoyote.

Ghera na shauku ya Seneta McCain kuulinda mfumo ilimsukuma awali kujikita jeshini  kuisaidia nchi yake kufikia malengo ya kujitanua, kumakinisha athari na kuitawala dunia kwa mfumo wao katika kila pembe ya dunia. Utumishi wa Seneta McCain jeshini ulimuhusisha katika Vita vya Vietnam na kuwahi kumugharimu kuwa mateka wa kivita kwa miaka mitano kuanzia 1967, baada ya ndege yake katika medani ya vita kuangushwa. Hivyo, kwa kipindi chote hicho alikuwa mateka akiwa kwenye  mikono ya jeshi la Vietnam.

Seneta McCain anatokana na familia ya mapambano, si tu alikuwa jeshini yeye, bali wazazi wake, baba na babu yake pia walitumikia kikamilifu jeshi la Marekani wakishikilia vyeo vikubwa. Mwaka 1968 baba yake John S. McCain Jr. aliteuliwa kuwa Kamanda Mkuu wa Marekani wa harakati zote za kijeshi nchini Vietnam. Kwa maneno mengine, Seneta John McCain alitumikia jeshi akiwa pamoja na baba yake.

Mnamo mwaka 1982 wakati Seneta McCain alipoanza kujitosa rasmi katika siasa kwa kugombea nafasi ya uwakilishi kupitia Chama cha Muhafidhiina (Republican) kuna waliombeza hadharani na kumwita mbabaishaji.  Katika moja ya kampeni zake McCain alimjibu aliyeleta hoja hiyo:

“Sikiliza rafiki, nimetumia miaka 22 jeshini. Baba yangu alikuwa jeshini. Babu yangu ni vivo hivyo. Katika utumishi wa jeshi tukihangaika kwa safari huku na huko. Tulikuwa tukikaa sehemu mbalimbali za nchi na sehemu nyengine za nje ya nchi. Natamani ningekuwa na maisha ya anasa kama wewe, ya kukulia na kuishi na kutumia maisha yangu yote mwahala muzuri kama First District Arizona. Lakini wapi !!! nilikuwa na majukumu mengine. …….”

Seneta Mccain alikuwa muumini mkubwa kama walivyo wanasiasa wengine wa Marekani wa kupigania ubwana wa Marekani duniani, na hili huwa ndio dira katika mambo yao yote. Katika makala aliyoandika katika Gazeti la Foreign Affairs (Novemba/ Disemba 2007) Seneta McCain katika kutilia nguvu hoja ya ubwana wa Marekani ulimwenguni aliinukuu kauli ya Rais Harry Truman aliyowahi kuisema  :

“Mungu katuumba sisi (Wamarekani) na kutuinua juu katika hali ya kuwa na nguvu na mamlaka  kwa malengo makubwa…..”

http://www.foreignaffairs.org/20071101faessay86602/john-mccain/an-enduring-peace-built-on-freedom.html

Ghera hii ilimsukuma McCain kufanya kazi usiku na mchana kulinda na kutetea mfumo wa kidemokrasia sambamba na ubwana wa dola ya Marekani ikiwemo kuamini kutumia nguvu za kijeshi, iwe jeshi lao au kuwatumia wengine kufikia malengo hayo.

Mwezi Februari mwaka 2000, katika mdahalo wa uraisi ukimuhusisha Seneta McCain na wenzak,e alipoulizwa ni sera gani za nje angezibadilisha mara moja lau atachaguliwa kuwa raisi: Seneta McCain alijibu:

“Nitatumia nguvu za kijeshi, nitatoa mafunzo, nitatoa vifaa na kutumia watu wa ndani au nje, kujenga nguvu ambayo hatimae itazipindua serikali (zisizo za kidemokrasia) na kisha kuweka serikali za kidemokrasia………”

Senata McCain alikuwa mstari wa mbele sana na muhimili muhimu katika Bunge la Congress katika qadhia za usalama wa Taifa la Marekani na siasa za nje. Alikuwa mchangiaji mkubwa wa qadhia hizo bila ya kutilia maanani chama gani kinatawala. Nidhamu ya Marekani imestafidi/ imepata faida kubwa ya uwepo wa Seneta McCain kutokana na uzoefu wake wa kijeshi, na daima alikuwa maarufu katika kuhamasisha kuchora mikakati ya ushindi wa kivita.

Mwaka 2002/2003 McCain aliusaidia utawala wa Bush kutengeneza mazingira ya vita vya Iraq, licha ya kukosekana ushahidi wa silaha za maangamizi wala fungamano la Sadaam na Al-Qaida. Amekuwa akiunga mkono vita mbalimbali kama Afghanistan kwa lengo la kujenga haiba ya Marekani kimataifa na kueneza athari na nguvu zake kimataifa. Amefanya ziara zisizo na idadi nchini Iraq na Afghanistan baada ya qadhia ya Septemba 11, na amekuwa na ada ya kutumia Siku Kuu ya kila mwaka (tarehe 4 Julai) kwa kujumuika na majeshi ya Marekani ndani ya Mashariki ya Kati, ikiwa ni mbinu ya kuwaunga mkono na kuwapa moyo.

Seneta McCain ametumikia Kamati ya Masuala ya Kijeshi ndani ya Bunge la Marekani kuanzia mwaka 2006-2012, na mwaka 2015 akawa rasmi Mwenyekiti wa Kamati hiyo. Chini ya Kamati hiyo amekuwa akitumia ushawishi wake kuwataka maraisi wote akiwemo rais Trump kuandaa mikakati rasmi ya ushindi wa Marekani katika vita vinavopiganwa na Marekani.

Hiyo ndio ghera, shauku na msimamo wa Seneta McCain kwa mfumo wao na nchi yao hususan kuhakikisha ubwana wa dola yao kimataifa. Hapana shaka mwanasiasa huyu ni kafiri, kabeba mfumo batil, kadhulumu na kumwaga damu nyingi ya Waislamu na mwishoni ataingizwa motoni, lakini ametumikia nchi na mfumo wao kwa muhanga, ushujaa, ujasiri usio na mithali mpaka pumzi zake za mwisho katika kusimamia kile anachokiamini.

Msiba na aibu kubwa ipo kwa viongozi katika biladi za Waislamu. Wana mfumo wa haki wa Uislamu kutoka kwa Muumba Ambaye Ameshawaahidi kushinda, wana bishara za ushindi kutoka kwa Mtume SAAW ambae hatamki chochote kwa matamanio yake, wana Umma mkubwa  nyuma yao ambao unabeba itikadi ya Uislamu kiimani na wala sio kimaslahi wakitaraji malipo ya Muumba tu. Bila ya kutaja uwepo wa rasilmali watu, vitu na maliasili ya kutosha.

Basi iweje viongozi wa ukafiri wawe na ghera, ushujaa, ujasiri, kujituma na muhanga kwa ajili ya ukafiri na batil yao kama Senata McCain ilhali  viongozi katika Biladi za Waislamu wenye Uislamu ambao ni mfumo wa haki wamebakia kuwa magoigoi, mabazazi, watumwa na vibaraka kwa madola mengine katika kulinda maslahi ya madola hayo, tena wakati mwingi kwa gharama ya kudhuru raia wao. Aidha, iweje Marekani inatumia majeshi yake yaliyo kazini na wastaafu kama Seneta McCain kusukuma sera zao za nje, ilhali viongozi katika Biladi za Kiislamu wanayatumia majeshi hayo kulinda viti vyao vya enzi na kudhuru raia wao, wakikosa watawala hao ajenda msingi kwa Umma wao na kimataifa.

Ukweli ni kuwa viongozi hao katika biladi za Waislamu hawakuubeba Uislamu kama ndio mfumo, dira na muongozo wao katika kufikia malengo na ajenda zao, wakijazwa kasumba kuwa Uislamu ndio uliowabwaga. Bali watawala hao, wao ndio walioubwaga Uislamu, na kamwe Uislamu haumuinui aliyeuacha mkono.

Njia pekee kwa watawala hawa kurudisha nishati yao na kujikomboa na utumwa wa madola ya kibepari ya kikoloni ni kuubeba Uislamu kwa ukamilifu wake chini ya utawala wake wa Khilafah Rashidah ambao utawapa izza/nguvu na ushindi ya kweli duniani na akhera. Kinyume chake watadhalilika hapa hapa duniani kama walivyodhalilika vibaraka wenzao waliotangulia, kisha watakabiliwa na adhabu kali kesho mbele ya mahkama ya Muumba.

Amesema Khalifah Umar ibn Khattwab ra:

“Allah Ametupa izza kutokana na  Uislamu, na yoyote atakayetafuta izza pengine kando na   Uislamu , Allah Atamdhalilisha.”

#UislamNiHadharaMbadala

18 Dhul Hijjah 1439 Hijri    | 29-08- 2018 Miladi

Afisi ya Habari –   Hizb ut- Tahrir Tanzania

https://hizb.or.tz/

https://www.facebook.com/Hizb-ut-Tahrir-Tanzania

Maoni hayajaruhusiwa.