Kanuni za kiidara kati ya hizo ni kanuni za barabarani na hukmu shar’i katika hayo

بسم الله الرحمن الرحيم

Assalamu Alaykum Warahmatullah

Namuomba Allah uwe katika afya kamili na kheri za Allah Mtukufu sheikh wetu, na atuhifadhi sisi na wewe kwa hifadhi yake, na auneemeshe ummah wa Kiislamu, wewe binafsi na sisi kwa utawala wa Kiislamu chini ya kivuli cha Khilafah kwa njia ya Utume.

Swali:

Ajali za barabarani zimekuwa nyingi katika nchi yetu, hili limepelekea vifo vingi vya waliopatwa na ajali hizi. Na tukawa tunatoa nasaha kutokiuka kanuni za barabarani ili kuhifadhi waendeshwa, madereva na wapanda vyombo… Kukawa kuna baadhi ya mirejesho kwamba kanuni hizi si kanuni za Kiislamu na wala hazina maandiko (nusuus)… Na kwamba kanuni zote ambazo zinatutawala si za Kiislamu zikiwemo hizo kanuni za barabarani… Baadhi ya mirejesho dhidi yao ikawa na kauli kwamba kanuni hizi ni kanuni za kisharia na haifai kuzikiuka. Mjadala unakua mkali…

Je ni haramu kukiuka kanuni za barabarani katika nchi hizi ambazo zinahukumu si kwa Uislamu ni sawa ikiwa hivyo katika nchi za Waislamu au katika nchi za ukafiri?

Na je kuna dalili za hayo?

Allah akupeni baraka. 

Jawabu:

Wa’alaykum Salam Warahmatullah Wabarakatuh,

Awali nakushukuru kwa dua yako nzuri na nakuombea wewe na Waislamu kijumla kheri kwa Allah na nusra na umakinifu…

Ama kuhusu swali lako, haya hapa maelezo ya suala hili katika sura zake kwa idhini ya Allah:

1-Kanuni hujulikanwa kuwa ni “Mkusanyiko wa kanuni za msingi ambazo mtawala huwalazimisha watu kuzifuata katika mahusiano yao”. Ina maana kuwa mtawala au dola huzichukua hukmu maalumu na kuzitabani na huamrisha kufanyiwa kazi, ahkam hizi baada ya kutabaniwa na mtawala au dola huwa ni kanuni za lazima kwa raia…

2-Kuweka kanuni kwa maana hiyo iliyoonyeshwa inafaa kisharia, na Khalifah ndie hufanya hivyo, kwasababu sharia imefanya haki ya kutabani ahkam na kuzilazimisha ni kwa Khalifah. Na tumetoa maelezo juu ya jambo hili katika vitabu vyetu. Na nakunukulia baadhi ya yaliyomo kuhusu hili katika kitabu cha Utangulizi wa Katiba, Juzuu ya Kwanza, kwenye uchambuzi wa kipengee “a” mada ya “136” ambayo inazungumza uwezo wa Khalifah:

(a) -Ndie ambae anatabani ahkam za kisheria za lazima kwa ajili kusimamia mambo ya ummah, ahkam zilizotoholewa (al-mustanmbata) kwa ijtihad sahihi kutoka katika Kitabu cha Allah na Sunna ya Mjumbe wake ili ziwe kanuni zilizowajibu kuzitii na haifai kuzihalifu.

Paragrafu (a) dalili yake ni ijmau sahaba, na hilo ni kwasababu kanuni ni neno la kiistilahi, na maana yake:  Ni amri ambayo hutolewa na mtawala ili watu waitekeleze. Na kanuni inajulikanwa kuwa (Mkusanyiko wa kanuni za msingi ambazo mtawala huwalazimisha watu kuzifuata katika mahusiano yao). Yaani anapoamrisha mtawala ahkam maalumu hivyo basi, ahkam hizi huwa ndio kanuni ambazo watu hulazimika nazo, na ikiwa mtawala hajaziamrisha haziwi kanuni, na watu hawalazimiki nazo. Na Waislamu wanakwenda kwa mujibu wa hukmu za kisharia, yaani wanakwenda kwa mujibu wa maamrisho na makatazo ya Allah na sio kwa amri na makatazo ya mtawala. Wanayokwenda nayo ni hukmu za kisharia na sio amri za mtawala. Isipokuwa hizi hukmu za kisharia wamekhitalifiana masahaba kwazo, kwa hiyo, wakafahamu baadhi yao maandiko ya kisharia (nusuus shar’iyyah) jambo, ambavyo sivyo walivyofahamu wengine na ikawa kila mmoja anakwenda kwa mujibu wa fahamu yake, na fahamu yake hii huwa ndio hukmu ya Allah kihaki yake. Lakini kuna hukmu za kisharia za usimamizi wa mambo ya ummah ambazo Waislamu wote waende kwazo kwa rai moja, na asiende kila mmoja kwa mujibu wa ijtihadi yake. Na hayo yametokea kivitendo hasa. Abu Bakr aliona mali aigawe kwa usawa kati ya Waislamu,

Kwa sababu ni haki yao kwa usawa. Na Umar akaona haisihi kupewa sawa aliyempiga vita Mtume wa Allah na aliepigana vita pamoja nae (Mtume), na kupewa fakiri kama tajiri. Lakini Abu Bakr alikuwa Khalifah akaamrisha kufanyiwa kazi rai yake, yaani alitabani kugawa mali kwa usawa na Waislamu wakamfuata katika hilo na makadhi na magavana wakaenda kwa mujibu wake, na Umar nae akafuata hilo akaifanyia kazi rai ya Abu Bakr na kuitekeleza. Na pindi Umar alipokuwa Khalifah akatabani rai inayopingana na rai ya Abu Bakr, yaani akaamrisha kwa rai yake igaiwe mali kwa kufadhilisha na sio kwa usawa. Apewe (mtu) kwa kutangulia na kwa haja. Waislamu wakamfuata, na makadhi na magavana wakaifanyia kazi. Kwa hiyo ikawa ni ijmau sahaba imefungika kwamba ni juu ya imamu kutabani ahkam maalumu zilizochukuliwa katika sharia kwa ijtihad iliyo sahihi na kuziamrisha zifanyiwe kazi na ni juu ya Waislamu kuzitii ijapokuwa zinapingana na ijtihadi zao, na kuacha kuzifanyia kazi rai zao na ijtihadi zao. Na huwa ahkam hizi zilizotabaniwa ndio kanuni. Na hapa ndipo unapopatikana kuwa uwekaji wa kanuni ni juu ya Khalifah pekee. Jambo hilo hamiliki mwengine kabisa). Mwisho.

3-Kanuni ambazo Khalifah huziweka ziko vigawanyo viwili:

a-Kigawanyo ambacho huwa ni hukmu za kisharia na Khalifah ndie anaezitabani na kulazimisha watu kuzifanyia kazi. Nazo ni kama vile hukmu za muamalati na adhabu na nyenginezo… Kigawanyo hiki ni wajibu kwa raia kujifunga nacho kwasababu mbili: Kua kwake ni hukmu za kisharia na wajibu wa kumtii mtawala wa kisharia.

b-Kigawanyo chengine ni taratibu za kiidara anazoziweka Khalifah kwa ajili ya maslahi ya Waislamu kulingana na uwezo wake (Khalifah) katika kusimamia mambo kama vile kanuni za barabarani… Na kigawanyo hiki ni wajibu kwa raia kujifunga nacho katika mlango wa uwajibu wa kumtii mtawala wa kisharia kwa mujibu wa yaliyobainishwa hapo juu…

4-Ama mtawala asiyekuwa wa kisharia na mtawala ambae anahukumu kwa hukmu za kuwekwa na binadamu kisharia si wajibu kumtii, na kanuni zake si zenye kuwafunga Waislamu (kuzifanyia kazi), kwasababu yeye hana haki juu ya Waislamu kumtii… Na siku hizi kanuni zenye kutolewa na mtawala ambae sie wa kisharia ziko za aina tatu:

a-Kanuni zilizochukuliwa kutoka katika hukmu za kisharia kama vile kanuni zinazoitwa “Kanuni za Hali ya Mtu Binafsi” (Personal Status Laws) ambazo hupanga ndoa, talaka, mirathi na mfano wa hizo kwa mujibu wa ahkam zilizochokuliwa kutoka katika fiqhi ya kiislamu. Kanuni hizi hufanyiwa kazi muda wa kwamba zimewafikiana na ahkam za kisharia. Kwasababu kuzifanyia kazi ni kutenda kwa mujibu wa hukmu za kisharia…

b-Kanuni ambazo zinakwenda kinyume na Sharia (ya Uislamu), nazo ni kama vile kanuni nyingi ambazo zinahalalisha riba, zina, unywaji ulevi, biashara zilizoharamishwa. Na kanuni zinazopanga umiliki na ugawaji, na kanuni ambazo zinapanga maisha ya kiuchumi na elimu… Haya yanaingia katika mlango wa kuhukumu kwa kile asichoteremsha Allah, jambo ambalo ni haramu. Na haifai kwa Waislamu katika mlango huu kuzifanyia kazi kanuni hizi, bali ni haramu kwao uharamu mkali na ni wajibu juu kufanya kazi kubadilisha kanuni hizi ili ziwe kwa mujibu wa hukmu za kisharia.

c-Kanuni zinazohusiana na taratibu za kiidara mfano kanuni za taratibu za nyendo barabarani, upangaji wa mambo ya elimu, ujenzi wa majumba na njia na mfano wa hayo ni katika mambo yanayoingia katika mlango taratibu za kiidara… Kanuni hizi si wajibu kisharia (Kiislamu) kuzifanyia kazi kwasababu zimetoka sehemu ambayo sharia (ya Kiislamu) hailazimishi kuitii. Lakini kuzifanyia kazi kanuni hizi si haramu kisharia (ya Kiislamu) bali inafaa (jaiz), kwasababu zinaingia katika taratibu za kisharia…

Lakini, ikiwa kutojifunga na kanuni hizi za kiidara kutasababisha dhara na udhia kwa nafsi au kwa watu wengine, hayo ni kama kutojifunga na kusimama kwenye alama nyekundu ambako kutasababisha kutokea ajali barabarani, na kudhuru nafsi au wengine… Hapo itakuwa kujifunga na kanuni hizi ni wajibu, lakini sio katika mlango wa kumtii mtawala aliyekuwa si wa kisharia, bali ni katika mlango wa madhara yanayopatikana kwa kutojifunga kwayo (hapa ni hizo kanuni za barabarani). Na Mtume (SAW) ameharamisha dhara. Amepokea Alhakim katika kitabu cha Almustadrak  kutoka kwa Abi Sa’id Alkhudri (RA) kwamba Mtume (SAW) amesema:

«لَا ضَرَرَ وَلَا ضِرَارَ، مَنْ ضَارَّ ضَارَّهُ اللَّهُ، وَمَنْ شَاقَّ شَاقَّ اللَّهُ عَلَيْهِ»،

“Hapana dhara wala kusababisha dhara. Mwenye kutia dhara Allah atamdhuru, na mwenye kutia dhiki Allah atampa dhiki”. Na akasema kuhusu hadithi hii: “Hadithi hii isnadi yake ni sahihi kwa sharti ya Muslim na kuwa hawakuitoa (Bukhari na Muslim). Na Al-Dhahabi akatoa maelezo kuhusu hadithi kwa kauli yake: “Kwa sharti ya Muslim”. Kwa hiyo wajibu wa kujifunga katika hali hizi haziingii katika wajibu wa kutii kanuni za kiidara ambazo anaziweka mtawala asie wa kisharia au mtawala si muislamu, bali wajibu unapatikana katika mlango wa uharamu wa dhara au kusababisha dhara na udhia.

5-Kwa hivyo, kujifunga na kanuni za barabarani katika nchi ya Waislamu ambayo haitawaliwi kwa sharia (ya Kiislamu) au katika nchi si ya Wislamu, kauli yangu ni: kujifunga na kanuni hizi na zinazofanana nazo katika kanuni na taratibu za kiidara inafaa (jaiz) kisharia, na si haramu wala si wajibu… Ila tu kwa hali moja, nayo ni pale kukosekana kujifunga na kanuni za kiidara kutakapopelekea dhara na udhia, basi huwa kujifunga nazo ni wajibu. Ispokuwa wajibu huu si kwa sababu ya kumtii mtawala asie wa kisharia au mtawala asie Muislamu bali ni katika mlango wa uharamu dhara na udhia…

Na yanaoonekanwa siku hizi ni kwamba katika hali nyingi hupatikana dhara kwa kutofuata taratibu za kiidara na hasa katika kanuni za barabarani. Kwa hiyo kujifunga na kanuni hizi ambazo zinaepusha dhara hufanyiwa kazi ili kuzuia dhara itakayopatikana kwa kuzikiuka (kanuni hizi).

Nataraji mas-ala haya yatakuwa yamekaa wazi pande zake zote.

Ndugu yenu Atta bin Khalil Abu Rashtah

7 Shawwal 1440H

10 June 2019

 

Maoni hayajaruhusiwa.