Bei za Mafuta, Ziara ya Erdogan Nchini Uingereza, Uchaguzi wa Malaysia, Armenia
بسم الله الرحمن الرحيم
La kwanza: Swali: Bei za mafuta zimeongezeka mnamo 24/5/2018 kwa tarakimu za juu, huku bei ya mafuta ambayo hayajasafishwa aina ya Brent ikifikia dolari 79 kwa pipa, na mafuta ambayo hayajasafishwa ya Texas ikifikia dolari 71 kwa pipa. Hii ni baada ya kushuka kwake kulikoshuhudiwa mnamo 2014. Je, hii yamaanisha kuwa ulimwengu umeingia katika zama mpya za bei za juu za mafuta? Je, tunaelekea katika mfumko sawa na huu uliotokea siku za nyuma wa dolari 150 kwa pipa? Na ni nini kilicho sababisha hili?
Jibu:
Mafuta, kama bidhaa nyengine yoyote ile, huathiriwa na usambazaji na matakwa. Lakini, tofauti na bidhaa nyenginezo, ustawi wa bei za mafuta si thabiti. Maana nyengine ni kuwa, mabadiliko yoyote yanayotokea katika usambazaji au matakwa yanaathari ya moja kwa moja juu ya bei ya mafuta. Hii ni kutokana na maumbile ya soko la mafuta. Hii ni ikiongezewa na athari ya utabiri, hususan pindi misukosuko ya kisiasa inapoathiri ustawi wa soko. Ili kufafanua hili tunaonesha yafuatayo:
1- Kuhusiana na usambazaji:
a- Shirika la Nchi Zinazosafirisha Mafuta (OPEC) na nchi zisizo za OPEC zimekubaliani kuweka kiwango cha usambazaji mafuta sokoni. Katika makubaliano baina ya Urusi na nchi za OPEC mwishoni mwa 2016, uamuzi ulitolewa wa kupunguza uzalishaji wa mafuta ardhini kwa mapipa milioni 1.8 kwa siku, ili kuondoa ongezeko la usambazaji juu ya soko na kuongeza bei ya mafuta. Utafiti wa shirika la Standards & Poor’s Global Plats la OPEC ulifichua kuwa uzalishaji wa mafuta wa OPEC mnamo Aprili ulipungua kwa mwezi wa tatu mfululizo kufikia kiwango chake cha chini mno kwa mwaka, mwezi uliopita ikizalisha mapipa milioni 32, yaani mapipa 140,000 kwa siku kiwango cha chini kuliko mwezi Machi. Na uzalishaji wa leo ni mapipa milioni 32.73, yaani chini ya kiwango cha OPEC kwa takriban mapipa 730,000 kwa siku. Makubaliano ya OPEC yatadumu kwa mwaka mmoja. Endapo hali za sasa zitaendelea, bei ya mafuta ambayo hayajasafishwa inatarajiwa kuongezeka zaidi. Kiongozi wa ushauri wa utafiti wa muda mrefu katika “Nyanja za Kawi”, Matthew Barry alisema: “Tunayoyaona yanayotokea, na yatatokea zaidi mbeleni, ni kuwa matatizo au vitisho vya usambazaji vinaanza kuleta athari zaidi na zaidi waziwazi katika bei”. (Chanzo: https://www.marketwatch.com)
b- Hali ya kisiasa na kiuchumi nchini Venezuela imekuwa na athari kubwa juu ya uwezo wa nchi wa kufikia shabaha zake za uzalishaji, ikizalisha mapipa milioni 1.41 kwa siku mnamo Aprili 2018, chini ya mapipa 80,000 kwa siku kufikia mwezi Machi 2018, na chini ya mapipa 540,000 kwa siku kwa mwaka wa 2017 M. Mojawapo ya sababu kuu za kushuka huku ni sera ya dola ya Venezuela; kampuni ya mafuta (PDVSA) ilikuwa na usimamizi mbaya, na mwezi uliopita (ConocolPhillips) ilishinda kesi dhidi ya kampuni ya mafuta (PDVSA) iliyogharimu dolari bilioni 2, kwa sababu ya kusitishwa kwa miradi miwili nchini Venezuela. Na (PDVSA) tayari imeshindwa kulipa deni lake la dolari bilioni 2.5. Yote haya yameathiri uzalishaji wa mafuta wa dola ya Venezuela na hivyo kuchangia kupungua kwa usambazaji. Hivyo basi bei zinaongezwa kutokana na upungufu wa usambazaji.
c- Tangazo la Raisi Trump la kujiondoa kutoka katika makubaliano ya nuklia na Iran iliibua matarajio ya vikwazo vipya katika sekta ya mafuta ya Iran. Vikwazo kwa serikali hii mithili ya hivi viliekwa kwa mara ya kwanza mnamo 2012 chini ya idara ya Obama. Kinadharia, uzalishaji wa Iran huenda ukapungua kwa asilimia 20% au mapipa 500,000 mpaka 400,000 kwa siku, ambayo ni sawia na takriban dolari bilioni 1 kwa mwezi kwa bei za sasa (Chanzo: http://foreignpolicy.com). Huku Amerika ikikosa kufichua ni hatua gani ambayo huenda ikachukua dhidi ya Iran, kuna fununu kuhusu aina ya vikwazo vya serikali vinavyolenga sekta ya mafuta ya Iran.
Hatua zote tatu hizi zimechangia katika kuanguka kwa usambazaji na natija yake ni kudhihirika kwa ongezeko la bei.
2- Kuhusu Matakwa:
a- Kumekuwa na ongezeko la matakwa ya mafuta, na Shirika la Kimataifa la Kawi linatarajia matakwa ya kiulimwengu ya mafuta kuongezeka kutoka mapipa milioni 98.7 kwa siku (bpd) mnamo 2017 hadi mapipa milioni 99.3 kwa siku (bpd) mwaka huu. Shirika la Kimataifa la Kawi lilisema katika ripoti yake ya kila mwezi kuwa matakwa ya mafuta yaliongezeka kwa mapipa milioni 1.6 kwa siku mnamo 2017 (Chanzo: https://www.reuters.com)
b- Eneo jengine la ongezeko la matakwa ya mafuta ni China. Mnamo Aprili 2018, ilitarajiwa kwamba China ingetumia zaidi ya mapipa milioni 9 ya mafuta ambayo hayajasafishwa kwa siku, kiwango kikubwa kuliko wakati mwengine wowote, na hii ni takriban asilimia 10% ya matumizi ya kiulimwengu na zaidi ya thuluthi moja ya matakwa jumla barani Asia. Na ikiwa mafuta ambayo hayajasafishwa yatafikia dolari 75 kwa pipa, hii yamaanisha kuwa gharama za mwezi za uagizaji mafuta kutoka ng’ambo za China ni zaidi ya dolari bilioni 20. Rekodi hii ya matakwa inajiri licha ya msimu wa ukarabati, ambapo kawaida kuanguka kwa uagizaji kutoka ng’ambo hutokea katika kipindi hichi cha mwaka, na inaonesha kuwa mahitaji ya mafuta ya China ni makubwa kuliko inavyotarajiwa. Benki ya Goldman Sachs imesema katika barua yake kwa wateja: “Matakwa ya China yanaashiria ongezeko la hali ya juu, na huenda yakaongezeka zaidi kuliko makadirio ya sasa” (Chanzo: https://www.reuters.com)
Kutokana na maelezo hayo ya juu, ni wazi kuna ongezeko la matakwa, lililopelekea ongezeko la bei hizi zinazoonekana.
3- Fununu: Fununu huchochewa katika tukio la mabadiliko ya ghafla katika usambazaji na matakwa ya mafuta, kuongezea nukta ya soko ambalo ni vigumu kulidhibiti. Hivyo basi, fununu huwa wazi zaidi kunapokuwa na ongezeko au upungufu mkubwa wa bei za mafuta. Ufichaji mkubwa wa fedha unachangia katika soko la mafuta ima kwa kununua au kuangazia mikataba mikubwa ya mafuta. Hivyo basi, fununu ni upanga wenye makali pande zote ambao huathiri ongezeko la matakwa na hivyo basi ongezeko la bei na huenda likaathiri kuporomoka kwa matakwa na upungufu wa bei. Kwa hali yoyote ile, athari ya fununu haijakuwa kubwa katika ongezeko la sasa la bei, lakini dori kubwa ilikuwa katika kadhia ya usambazaji na matakwa kama ilivyo fafanuliwa juu.
4 – Ongezeko la bei za mafuta la juu kama ilivyokuwa nyuma, kiasi cha kufikia mpaka 150 na zaidi, halitarajiwi kutokea kwa sababu hali za kiuchumi za kiulimwengu haziwezi kuhimili hili, kwa hivyo inatarajiwa kuwa bei ya mafuta itaendelea kuongezeka kidogo kidogo mpaka ifike kikomo pasi na kufikia mia moja, hususan kwa kuwa vita vya kibiashara vinavyonukia baina ya Amerika na China vitapelekea kupungua kwa matakwa na kisha bei za mafuta kushuka kwa urahisi. Zaidi ya hayo, shinikizo la Amerika juu ya OPEC kupitia Saudi Arabia haswa katika kuongeza uzalishaji litakuwa na athari sawia endapo bei zitapanda kwa kiwango kisichoiridhisha Amerika.
================
Pili: Swali: Erdogan aliwasili jijini London mnamo Jumapili 13/5/2018 kwa ziara ya siku tatu. Wakati wa ziara hii Erdogan alikutana na Malkia Elizabeth na Waziri Mkuu Theresa May. Ziara ya Erdogan inajiri wiki chache tu kabla ya uchaguzi wa mapema wa uraisi na ubunge nchini Uturuki mnamo Juni 24. Ni maarufu kuwa uhusiano wa Erdogan na Uingereza ni tete tangu kufeli kwa mapinduzi, sasa ni vipi ziara hili ilitokea na nini lengo lake? Je, imefaulu lengo lake?
Jibu: Ili kuonesha lengo la ziara hii, tunatathmini yafuatayo:
1- Inajulikana kuwa Erdogan anatafuta kumakinisha mamlaka yake kupitia mfumo wa utawala wa uraisi ambao mamlaka zote zimo mikononi mwa Raisi, huku nchi ikiwemo katika hali ya taharuki. Hali hii ya taharuki nchini Uturuki ilipelekea kukamatwa kwa watu 160,000 na wafanyikazi wa serikali takribani idadi sawa na hiyo kufutwa kazi katika kesi nyingi. Tangu kufeli kwa mapinduzi dhidi ya serikali ya Uturuki mnamo 2016, maelfu ya waasi wakiwemo maafisa, mawakili, maafisa wa polisi na wasomi wamefutwa kazi; wengi wao wakiwa watiifu kwa Uingereza.
Lakini, kabla ya kuondoka Istanbul kuelekea London, mnamo Jumapili, (Erdogan aliisifu Uingereza kama “mwenza na mshirika wa kistratejia”, na akasema atajadili kadhia za nchi zote mbili, eneo na za kimataifa pamoja na May mnamo Jumanne, na kusema itajumuisha matukio mapya yanayojiri nchini Cyprus, Uturuki na Uingereza zikiwa kama mdhamini wake, pamoja na kujadili “mpango wa pamoja wa utendakazi” eneo la Mashariki ya Kati. Erdogan pia alisisitiza kuwa ziara yake pia ingeangazia juu ya kuongeza biashara baina ya Uturuki na Uingereza. “Tunataka kuendeleza mahusiano yetu ya kiuchumi pasi na kukatizwa baada ya Uingereza kuondoka katika Muungano wa Ulaya,” alisema. (Chanzo: http://www.elfagr.com 13/05/2018)
2- Inaeleweka kutokana na taarifa zake kuwa aliyojadili pamoja na May ni kadhia za eneo na za kimataifa, matukio mapya yanayojiri nchini Cyprus na mpango wa utendakazi katika eneo la Mashariki ya Kati, na kuongeza biashara baina ya Uturuki na Uingereza. Ama kuhusu mpango wa utendakazi eneo la Mashariki ya Kati, si Erdogan atakaye jadiliana na May kadhia hizi za kimataifa. Angazo la mazungumzo baina ya pande mbili hizi juu ya kadhia za kiuchumi na kuongeza ubadilishanaji biashara kati ya nchi mbili hizi, kama alivyosema Erdogan katika mkutano wa waandishi wa habari katika uwanja wa ndege wa Ataturk jijini Istanbul kabla ya kuondoka, si kweli kwa sababu mambo ya kiuchumi na kuongeza biashara baina ya nchi mbili hizi yanahitaji mazingira ya utulivu wa kisiasa baina ya nchi mbili hizi. Na hili haliko, hususan baada ya mapinduzi yaliyofeli. Linalothibitisha hili ni kuwa hakutangaza kutia saini mradi wowote wa kihakika wa kiuchumi wakati wa ziara yake. Kadhia ya Cyprus imesalia, bado uko uwezekano wa kuijadili kwa sababu pande zote mbili ni wadhamini wa amani na usalama juu ya kisiwa hiki, lakini hili hutokea tu kunapokuwa na uhasama kisiwani humo, ambao kwa sasa hakuna. Hii yamaanisha kuwa yote aliyoyatangaza Erdogan kama malengo ya ziara hayana hoja, bali ni ubabaishaji tu kutokana na sababu halisi.
3- Sababu halisi yaweza kujulikana kupitia uchunguzi wa matukio tangu kufeli kwa mapinduzi na kuoanisha matukio hayo na ukweli kuwa ziara hii ilijiri kabla ya uchaguzi, na hatimaye kuonesha lengo halisi la ziara ya Erdogan nchini Uingereza:
– Ama kuhusu uhakika wa matukio hayo, inajulikana kuwa mapinduzi yaliyofeli yalitekelezwa barabara na vibaraka wa Uingereza nchini Uturuki. Erdogan amechukua hatua kali dhidi ya vibaraka wa Uingereza, hususan katika jeshi kama ilivyo elezwa katika swali na zaidi. Hili lilipelekea hasira kubwa za Uingereza dhidi ya Erdogan.
– Ama kuhusu ukweli kuwa ziara hii ilijiri kabla ya uchaguzi na kuoanisha matukio haya mawili, Uingereza imeviongoza vyama pinzani vya Uturuki vyenye utiifu kwa Uingereza, vinavyoongozwa na Chama cha Republican People’s Party kuunda muungano usio wa kawaida dhidi ya Erdogan ili kupata wingi wa watu bungeni, na ilifuata ujanja wake wa kawaida katika hali kama hizo, yaani kuingia katika uchaguzi wa ubunge kama muungano mmoja ili kujaribu kuupeleka uchaguzi wa uraisi angaa katika raundi ya pili, ili kuonesha kuwa Erdogan amepoteza rai jumla ya watu kama anavyodai, na kuitingisha sura yake hata endapo atafaulu baadaye. Hii, bila shaka, ndio hofu ya Erdogan.
Hivyo basi, ziara hii zaidi ni ya kujipendekeza kwa Uingereza kabla ya uchaguzi wa Uturuki wa Juni 24. Hii ndio sababu Erdogan alijaribu kuishawishi Uingereza katika ubadilishanaji wa baadhi ya biashara, kama vile kuwaachilia huru vibaraka wa Uingereza kutoka gerezani, na kuisifu Uingereza kama mshirika wa kistratejia, kama ilivyo katika taarifa yake, na kuitongoza Uingereza kupitia kusitisha kampeni kubwa ya “utakasaji” iliyofanywa na Erdogan dhidi ya vibaraka wa Uingereza kwa badali ya kurahisisha makabiliano na vibaraka wa Uingereza katika kampeni za uchaguzi huo. Huu ndio uwezekano mkubwa wa hii kuwa ndio sababu halisi nyuma ya ziara ya Erdogan nchini Uingereza.
4- Je, alifaulu kupata lengo lake? Yaonekana kama alifeli, na viashirio vyake ni:
“Hukumu ya wale waliojaribu kuipindua serikali iliyochaguliwa kidemokrasia ni sahihi”, May alisema, akisimama ubavuni mwa Erdogan katika afisi yake iliyoko barabara ya Downing baada ya mkutano. “Lakini ni muhimu pia Uturuki isipuuze maadili inayotafuta kuyatetea huku ikiilinda demokrasia” … (Chanzo: alarab.co.uk 16/05/2018) Yaani, May alimkashifu Erdogan mbele ya waandishi habari huku akiwa ni mgeni wake!!
– Makundi ya uhuru wa kuzungumza yalimlaani Erdogan: “Maandamano mbele ya makao makuu ya serikali ya barabara ya Downing yalihusisha makundi ya uhuru wa kuzungumza kama vile “PEN”, “Index to Censorship”, na “Reporters Without Borders”. (Chanzo: ukurasa wa Nafahat Al-Qalam 15/05/2018), na wanaharakati watetezi wa Wakurdi walibeba mabango yenye picha za Erdogan na neno “gaidi” (Chanzo: Al-Ain Al-Akhbariyah, 15/05/2018)
===============
Tatu: Swali: uchaguzi wa Malaysia ulifanyika mnamo 9/5/2018. Matokea yakawa ni kuanguka kwa Waziri Mkuu Najib na kurudi tena kwa Mahathir katika uraisi wa wizara, ukizingatia kuwa umri wake umegonga miaka 90, kana kwamba kulikuwa na mpango maalumu nyuma ya uchaguzi huu. Je, kulikuweko na malengo ya kinje ama kadhia ni kama isemwavyo kuwa ni mchezo wa kidemokrasia wa kindani?
Jibu:
1- Malaysia inajumuisha eneo la kusini mwa bara la Malay na maeneo ya kaskazini mwa kisiwa cha Borneo. Yametenganishwa na mkondo mpana wa bahari ya China Kusini.
Uislamu ulianza kuenea eneo hili kupitia wafanyi biashara Waislamu katika karne ya kumi na tatu Miladiya, ambapo watawala na mabwenyenye walisilimu mwanzo, kabla ya Uislamu kuenea kwa watu jumla. Ufalme wa Malacca, ulioko katika bara la Malay, ulipata umaarufu kutokana na ongezeko la biashara ya baharini ambapo biashara ya nchi kavu ilitatizwa na uvamizi wa Mongol. Ufalme huu ulipata uhuru kutokana na ushawishi wa China katika karne ya kumi na tano Miladiya, na punde tu ukaukubali Uislamu na kuenea kwa kasi katika kila pembe ya eneo hilo kutokana na nguvu na haiba ya ufalme huu. Lakini, eneo hili lilikoloniwa na Wareno kupitia ufalme huu wenyewe mnamo 1511 baada ya kumhonga mtu ndani yake kufungua lango la ngome ya mji wake mkuu kwa ndani.
Kisha walikuja Waholanzi mnamo 1641 na ukoloni wa Kiingereza kwa bara hili ukaanza mnamo 1786 kupitia biashara na ukodishaji bandari, na kupitia mkakati wa Kiingereza wa utumiaji matabaka tofauti tofauti ya “watu” ili wawe watawala halisi, na kuwabakisha wafalme walioko kuwa watawala jina tu. Muungano wa Malay wa bara hilo ulipata uhuru rasmi kutoka kwa Waingereza mnamo 1957. Dola ya Malaysia iliasisiwa mnamo 1963 baada ya kuunganishwa kwa Shirikisho la Malay na Kisiwa cha Bormeo na Singapore (licha ya kuvunjwa kwa Singapore kupitia kura katika Bunge la Malaysia mnamo 1965)
2- Ni wazi kuwa hata baada ya uhuru, Uingereza imeendelea kuwa na udhibiti wa kisiasa juu ya Malaysia, kwa mfano:
a- Malaysia imesalia kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Nchi za Madola ya Uingereza na mwanachama wa vuguvugu la Non-Aligned Movement (iliojiunga nalo mnamo 2003). Vile vile ni mwanachama muasisi wa Chama cha Mataifa ya Kusini Mashariki mwa Asia na Shirika la Kongamano la Kiislamu, na Waziri Mkuu Tonko Abdul Rahman alikuwa ndiye Katibu Mkuu wake wa kwanza.
b- Mnamo 1971, makubaliano ya ulinzi wa dola-tano yalitiwa saini baina ya Uingereza, Australia, New Zealand, Malaysia na Singapore baada ya kujiondoa kwa Uingereza eneo la Suez Mashariki. Inapaswa kuzingatiwa kuwa mnamo 1971, Australia ilikuwa ikitawaliwa na Chama cha Leba, ambayo ilibakia kuwa mtiifu kwa Uingereza katika karne ya ishirini.
c- Waziri Mkuu Mahathir Mohamad alipinga kuasisiwa kwa shirika linalounga mkono Amerika la “APEC”, mbalo lilizinduliwa na Australia chini ya uongozi wa mwenyekiti wa chama kinachounga mkono Amerika cha Leba, Bob Hawke mnamo 1989. Mrithi wa Hawke ni kiongozi wa Chama cha Leba, na Waziri Mkuu Paul Keating aliyemsifu Mahathir kama “Muasi” kwa kutohudhuria Kongamano la APEC mnamo 1993 eneo la Seattle, Amerika.
d- Kama badali ya APEC, Mahathir Mohamad mnamo 1997 alipendekeza kuundwa kwa Jumuiya ya Kiuchumi ya Asia Mashariki, isiyojumuisha Amerika na Australia, lakini wazo hili lilifeli na hatimaye lilibadilishwa kuwa mikutano ya Kongamano la Asia Mashariki, iliyojumuisha Australia lakini chini ya uanachama wa Waziri Mkuu wa Leba anayeunga mkono Uingereza, John Howard, lakini Amerika iliachwa nje. (Amerika na Urusi hazikuweza kujiunga na kundi hili hadi 2011).
3- Uingereza imegundua kwamba Amerika inamtongoza aliyekuwa Waziri Mkuu Najib Razak na inahofia huenda akaegemea upande wa Amerika, ingawa alikuwa waziri katika serikali za Malaysia zilizounga mkono Uingereza na kutokea katika chama hicho hicho, cha Vuguvugu la Kitaifa la Malaysia (MNM) kilichotawala Malaysia tangu uhuru. Miongoni mwa viashiria vya hofu hii ni:
a- Barack Obama alizuru Malaysia mnamo Aprili 2014, raisi wa kwanza wa Amerika kuzuru Malaysia kwa karibu miaka 50, ambapo aliamua “kuboresha uhusiano kati ya Malaysia na Amerika kuwa ushirikiano mpana”, ambayo ilikuwa ni sehemu ya sera ya Obama ya ushirika na Asia.
b- Najib na Obama walikuwa marafiki wakicheza gofu pamoja jijini Hawaii mnamo Disemba 2014. Obama alizuru tena Malaysia mnamo Novemba 2015.
c- Najib aliunga mkono kwa dhati Ushirika wa Nchi za Bahari ya Pasifiki, mradi wa Kiamerika, na kusisitiza juu ya kuhusishwa kwa Amerika, na kisha kufanya kazi na Japan ili kuendelea na Mpango wa Biashara baada ya Amerika kujiondoa katika enzi ya Trump. (Vietnam na Malaysia zilicheza dori muhimu katika kuziokoa nchi 11 katika Makubaliano ya Kibiashara kati ya Nchi za Bahari ya Pasifiki, ambayo yalikaribia kuporomoka baada ya Amerika kujiondoa), [Chanzo: https://asia.nikkei.com/Economy/Vietnam-and-Malaysia-play-vital-roles-in-making-TPP- 11]
4- Huku uchaguzi wa 2018 ukikaribia, inaonekana kama Uingereza kwa mara nyengine inamrudia tena mtumishi wake mtiifu (Mahathir Mohamad), aliyetumia jukwaa la upinzani kurudi mamlakani, na hivyo ndivyo ilivyokuwa. Malaysia sasa inatarajiwa kujitenga na sera za Amerika na kurudia kufanya kazi kupunguza Amerika kuingilia mambo ya eneo hilo kwa mujibu wa sera za Kiingereza.
================
Nne: Swali: Mnamo 8/5/2018, Bunge la Armenia lilipitisha uchaguzi wa kiongozi wa upinzani Nikol Pashinyan kama Waziri Mkuu, likifunga ukurasa wa maandamano ya zaidi ya wiki tatu dhidi ya serikali inayounga mkono Amerika ya Urusi nchini Armenia. Swali ni je, mabadiliko ya kisiasa nchini Armenia ni makubwa kiasi gani? Je, hii yamaanisha kuwa ushawishi wa Urusi utaondolewa nchini Armenia? Je, Wamagharibi “Ulaya na Amerika” wana dori katika hili?
Jibu: Kufafanua mambo haya tunaangazia yafuatayo:
1- Armenia ni nchi ndogo yenye “watu milioni 4”. Uhuru wake ulikuwa ni sehemu ya wimbi la kuvunjika kwa Umoja wa Kisovieti mnamo 1991. Chama cha Kijamhuri, ambacho kiongozi wake aling’olewa na waandamanaji, ametawala Armenia tangu 1999, na kiongozi wake, Serzh Sargsyan, alikamilisha mihula miwili tangu 2008. Utawala wake unasifiwa sana kwa udikteta na kuunga mkono Urusi licha ya kuweko kwa vyama vya upinzani vyenye uwakilishi bungeni. Na kwa kuwa katiba ya nchi hairuhusu zaidi ya mihula miwili kwa uraisi, na ili kuendelea kutawala, alifadhili mabadiliko ya kikatiba yaliyokigeuza cheo cha uraisi kutokuwa na mamlaka na kugurisha mamlaka halisi kwa waziri mkuu. Punde tu baada ya muhula wake wa pili kumalizika, Raisi Sargsyan aliondoka na kuwa waziri mkuu, (Bunge la Armenia lilimchagua Raisi Serzh Sargsyan kama waziri mkuu, katika hatua ambayo ingeimarisha mshiko wake wa mamlaka, licha ya maandamano ya maelfu eneo la Yerevan wakilaani kubakia kwake kama kiongozi wa serikali.
Bunge hilo lilimpitisha Sargsyan mwenye umri wa miaka 63 kuchukua kiti hicho. Alishinda kiti hicho kipya kwa kura 77 dhidi ya kura 17, baada ya muhula wake wa pili na wa mwisho wa uraisi kumalizika wiki jana… (Chanzo: Al-Nahar, Aprili 17, 2018). Maslahi jumla dhidi ya uteuzi wake yalijitokeza, hususan kwa kuwa enzi ya Sargsyan ilikumbwa na ugumu wa kiuchumi uliohisiwa na Warmenia na ukosefu wa fursa, ambayo kimsingi yalitokana na ufisadi wa serikali, ikiongezewa na ukosefu wa rasilimali asili kama mafuta, gesi na mali ghafi. Upinzani wa chama cha “Yelk” uliangazia kadhia zote hizi na kuchochea maandamano nchini Armenia, ambayo punde yaliangazia uongozi mpya “jumla” unaowakilishwa na mpinzani Nicole Pachinyan.
2- Maandamano hayo nchini Armenia kimsingi yalisukumwa na hali mbaya ya kiuchumi chini ya Raisi Sargsyan. Kama vile nchi nyenginezo za mfumo wa Kisovieti, ufisadi wa kiidara na wa kifedha unatawala serikali ya Armenia. Hongo imeenea serikalini kiasi cha kuwasonga watu. Watu hawana raha na utawala huo kwa sababu ya ugumu wa maisha yao. Walikuwa wanahesabu siku tu za kumalizika kwa muhula wa pili wa Sargsyan. Lakini akapanga kurudi tena kupitia wadhifa wa waziri mkuu! Hivyo basi watu wakaasi utawala wake, na mambo yakamalizikia kwa kujiuzulu kwake na kuteuliwa kwa Pashinyan kama waziri mkuu. Huku kadhia ya kiuchumi ikifinya na kufuatiwa na kadhia za ndani za kidemokrasia, Waziri Mkuu mpya Pashinyan, katika kuunda kwake serikali, alisisitiza haja ya kuweko kwa uchaguzi wa ubunge na kwamba ili serikali yake iweze kuanzisha “mabadiliko makubwa katika nyanja tofauti tofauti”. Pashinyan mapema aliahidi “Kuweka Demokrasia nchini Armenia”, kudumisha sheria, kutenganisha maslahi maalumu ya kiuchumi kutoka kwa serikali na kuimarisha kwa haraka mazingira ya uwekezaji. (Chanzo: Armenian 14/4/2018).
Hivyo, ni wazi kuwa mabadiliko ya kisiasa nchini Armenia kimsingi yamesukumwa kindani.
3- Majibu:
A- Wakati wa maandamano hayo, Amerika ilitangaza kuwa inafuatilia kwa karibu hali nchini Armenia na inaonekana kana kwamba inatathmini kuwepo kwa uwezekano wa fursa za kurefusha ushawishi wake huko. Baada ya Pashinyan kutawazwa kama waziri mkuu, (Msemaji wa Wizara ya Kigeni ya Amerika Heather Nauert alisema katika taarifa mwishoni mwa Jumanne: “Amerika inampongeza Nikol Pashinyan kama Waziri Mkuu mpya wa Jamhuri ya Armenia” na akasema: “Wizara ya Kigeni ya Amerika inatarajia kufanya kazi kwa karibu na serikali mpya pamoja na watu wa Armenia katika nyanja nyingi zilizo na maslahi ya pamoja baina ya nchi mbili hizi, ikiwemo kuongeza biashara, kufanya kazi ya kuunga mkono demokrasia na sheria, na kulinda usalama wa kieneo na wa kimataifa.” (Chanzo: Tovuti ya habari ya Armenian 9/5/2018)
B- Majibu ya Ulaya: mwakilishi wa Muungano wa Ulaya wa sera ya mambo ya kigeni na usalama, Federica Mugherini, alimpigia simu Waziri Mkuu Nikol Pashanyan.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Muungano wa Ulaya (MU), Mugherini alitoa wito kwa Pashinyan kuzuru Brussels katika fursa ya mapema zaidi. Taarifa hiyo ilieleza: Makamu wa Raisi wa Tume ya Ulaya Federica Mugherini jana alasiri alizungumza kwa simu na Nikol Pashinyan kumpongeza kwa uchaguzi wake kama Waziri Mkuu wa Armenia “Walikubaliana juu ya umuhimu wa ushirika kati ya Muungano wa Ulaya na Armenia na kutarajia kukutana naye ana kwa ana,” Mkuu wa sera ya kigeni wa MU, Federica Mogherini, pia alimkaribisha Pashinyan kuzuru Brussels “katika fursa ya mapema zaidi”. (Chanzo: ARMENPRESS 9/5/2018).
C- Majibu ya Urusi: baada ya uchaguzi wa Pashinyan na Bunge kuwa waziri mkuu mnamo 8/8/2015: Raisi wa Urusi Vladmir Putin alituma msururu wa pongezi kwa Pashinyan ambao alionesha matumaini yake kuwa kazi ya Pashinyan itasaidia kumakinisha mahusiano ya ushirika baina ya Urusi na Armenia na ushirikiano baina ya nchi mbili hizi ndani ya misingi ya dola huru za Jumuiya ya Madola, Jumuiya ya Kiuchumi kati ya Ulaya na Asia na Shirika la Mkataba wa Pamoja wa Amani. Pashinyan mapema alionesha kukinai kwake kuwa ushirika huu wa kimikakati na ushirikiano wa kijeshi baina ya nchi yake na Urusi ndio msingi wa usalama wa dola ya Armenia. Pashinyan alisema katika kikao maalumu bungeni kuwa ushirika huu wa kimikakati na Urusi utabakia kuwa kipaumbele kwa Armenia. Alisema kuwa nchi yake kamwe haitajiondoa kutoka katika Shirika la Mkataba wa Pamoja wa Amani, wala kutoka katika Muungano wa Kiuchumi kati ya Ulaya na Asia, unaojumuisha Urusi, Kazakhstan, Belarus, Armenia and Kyrgyzstan. (Chanzo: Russia Today 8/5/2018).
Ili kupunguza hofu ya Urusi kwa Armenia, Pashinyan alisema: “Mchakato wa kisiasa ulioanza nchini Armenia, kihakika, hauna muktadha wowote wa siasa za eneo”. Alisema: “Vuguvugu letu haliongozwi na maslahi ya Amerika wala ya Muungano wa Ulaya bali linaongozwa na maslahi ya Armenia na watu wake, aliendelea: “Maandamano yetu hayaelekezwi dhidi ya Urusi, vile vile hayana chembe chembe zozote za tukio la Ukraine”. (Chanzo: mtandao wa DARAJ 1/5/2018)
4- Hivyo basi, ni wazi kuwa fursa ya Urusi kudumisha ushawishi wake nchini Armenia bado ingalipo, kwa hivyo Raisi wa Urusi alimkaribisha Pashinyan katika mkutano eneo la Sochi-Urusi, na katika mkutano wao wa kwanza baina yao: Waziri Mkuu Nicole Pashinyan alimwambia Raisi wa Urusi Vladmir Putin mnamo Jumatatu kwamba angependa kuimarisha mahusiano ya karibu zaidi na Urusi katika uwanja wa kijeshi, na hakuna yoyote aliye na shaka juu ya umuhimu wa mahusiano haya ya kimikakati baina ya nchi mbili hizi. (Chanzo: Reuters 14/5/2018)
“Nadhani kuwa hakuna yeyote nchini Armenia aliye na shaka na kamwe atakayekuwa na shaka juu ya umuhimu wa kistratejia wa mahusiano kati ya Armenia na Urusi … Tunania ya kutoa motisha mpya kwa mahusiano haya, kisiasa, kiuchumi na kibiashara”, Pashinyan alisema. Kiongozi huyu wa Armenia aligundua kuwa watu wa nchi yake waliridhika na msimamo thabiti uliochukuliwa na Urusi wakati wa mgogoro wa kisiasa wa hivi majuzi nchini Armenia. (Chanzo: Russia Today 14/5/2018)
Na linalotilia nguvu fursa ya Urusi ya kudumisha ushawishi wake nchini Armenia ni lile ambalo twaweza kuliita “Ugumu wa Armenia”, ambao unauzuia upinzani kutoipa mgongo Urusi; Armenia imo ndani ya maeneo jirani na Waislamu, na ina hofu ya kudumu kwa mazingira yake ya Kiislamu. Ni jirani na Azerbaijan, ambako kuna mzozo juu ya eneo la Nagorno Karabakh, na Uturuki ambayo Armenia inaituhumu kutekeleza mauaji makubwa huko mwanzoni mwa karne ya ishirini, pamoja na ukaribu wake na Iran. Ingawa Armenia haina ukaribu wa moja kwa moja wa kijografia na Urusi, imetenganishwa na Georgia upande wa kusini mwa Urusi, ambayo imesheheni harakati za Kiislamu za kutaka kujitenga kama ilivyo Chechnya. Lakini Urusi, kama nguvu ya kimataifa iliyo karibu sana kwake, iliwapa Waarmenia hali ya usalama usoni mwa mazingira ya Kiislamu.
Tangu uhuru wake, Urusi imekuwa ikitoa usaidizi wa kijeshi kwa Armenia hususan dhidi ya Azerbaijan katika kadhia ya Nagorno-Karabakh. Imekuwa ikitoa mikopo na ruzuku za kawi na mafuta. Armenia ina uchumi dhaifu, inayotegemea juu ya misaada na malipo kutoka kwa Waarmenia walioko ng’ambo. Armenia ina imani kubwa kwa Urusi kuihifadhi kutokana na hatari za Kiislamu, na hivyo basi yaweza kukadiriwa kwamba kambi za kijeshi za Urusi nchini Armenia na ushirika wa kimikakati nayo ndio uti wa mgongo wa sera ya kigeni ya Armenia. Hata zile taarifa zilizoibuka wakati wa maandamano kutoka kwa baadhi ya waandamanaji kuhusu kuondolewa kwa kambi za kijeshi za Urusi nchini Armenia, ambazo ziliripotiwa katika gazeti la Russia Today mnamo 26/04/2018, ni taarifa tu za kupunguza hisia za baadhi waandamanaji waliopitiliza juu ya uhakika wa kiongozi wa upinzani Pashinyan, kama ilivyo shuhudiwa kupitia taarifa zake za kirafiki za kivitendo zenye kupendelea kubakia kwa ushawishi wa kijeshi wa Urusi.
5- Kwa kutamatisha, maumbile ya maandamano hayo ni ya kindani ili upinzani uchukue utawala, na ingawa utawala uliotangulia ulifungwa na Urusi, kwa kuwa Sargsyan alikuwa “mfupa wa shingo” kwa Urusi na kwamba Pashinyan alikuwa katika upinzani na Sargsyan alikuwa karibu na Urusi, nguvu ya kuhifadhi iliifanya Urusi kumkubali yule aliye mbali naye kuliko wa karibu yake! Ilidandia wimbi na kuukubali upinzani, kwa kuhakikishiwa tena na Wamagharibi juu ya ugumu wa kuvunjwa ushawishi kati ya Urusi na Armenia, kutokana na sababu tulizotaja juu. Lakini, haitarajiwi kuwa Wamagharibi, hususan Amerika, watauacha uwanja wa Armenia kwa Urusi peke yake, kama ilivyo desturi katika mizozo ya kikoloni ya kimataifa kwa mbinu zake nyingi ovu.
10 Ramadan 1439 H
26/5/2018 M
Inatoka: http://hizb.or.ke/sw/2018/05/26/majibu-ya-maswali-ya-kisiasa-bei-za-mafuta-ziara-ya-erdogan-nchini-uingereza-uchaguzi-wa-malaysia-armenia/
Maoni hayajaruhusiwa.