Bajeti Ya Tanzania 2021/2022: Shere Na Maumivu Kwa Wananchi
بسم الله الرحمن الرحيم
Mwezi wa Juni wa kila mwaka mataifa mbalimbali duniani huwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya serikali kwa mwaka wa fedha wa serikali unaofuatia, yaani bajeti ya mwaka.
Katika bajeti hizi serikali huonesha utekelezaji wa bajeti ya mwaka uliopita na hutoa makadirio ya bajeti ya mwaka ujao na mikakati ya serikali kiujumla kuhusu mapato na matumizi ya nchi.
Mnamo tarehe 10/06/2021 Tanzania iliwasilisha bajeti yake bungeni kupitia Waziri wake wa fedha Mwigulu Nchemba, tungependa kusema yafuatayo kwa ufupi kuhusiana na bajeti hii:
Kwa kila mfuatiliaji wa mambo akisoma au kusikiliza bajeti hii atagundua kuwa si lolote bali ni muendelezo wa ada ya demokrasia ya kuwapa matumaini hewa wananchi ambayo hayana uhalisia huku tarakimu zikionekana kuongezeka katika ukubwa wa bajeti lakini hali halisi ya maisha ya watu yamebakia kuwa duni wakisubiri kwa hamu kila mwaka kusomewa bajeti nyengine na nyengine.
Bajeti ya Tanzania mwaka huu 2021/2022 ni trilioni 36.3 huku bajeti ya mwaka uliopita 2019/2020 ilikuwa ni trilioni 34.8. Mpaka mwezi wa Aprili 2021 jumla ya mapato ya ndani na nje ilikuwa ni trilioni 24.53 wakati matarajio yalikuwa ni kukusanya trilioni 30.1. Swali muhimu linakuja hapa kama uwezo ni kukusanya trilioni 24.53 na serikali ilitarajia ingekusanya trilioni 30.1 kwanini bajeti ilikuwa trilioni 34.8?.
Uwezo wa kukusanya ni tofauti na matarajio, na matarajio ni tofauti na bajeti. Hakuna maelezo zaidi ya ukweli kuwa lengo ni kukuza tarakimu kwa wananchi ilhali uhalisia wa uwezo wa serikali ni mdogo, na hii inatokana na ubadhirifu serikalini na kutegemea kodi zaidi kama chanzo kikuu cha serikali cha mapato
Bajeti pia imedhihirisha ukweli mchungu kuwa mfumo wa kidemokrasia na viongozi au wanasiasa wake ni warongo. Jumla ya misaada na mikopo iliyopata Tanzania imeongezeka kutoka trilioni 1.82 mwaka 2019/2020 na kufikia trilioni 1.89 mwaka 2020/2021 na hivyo kufanya deni la taifa kutoka trilioni 54.8 mwaka 2019 na kufikia Trilioni 59 mwaka 2020.
Wanasiasa wamekuwa wakitudanganya kuwa Tanzania ni nchi tajiri na kutoa matumaini hewa kwa wananchi huku wakijua kuwa licha ya rasilimali nyingi zilizopo bado tupo chini ya minyororo ya ukoloni mamboleo wa madola ya magharibi na Marekani ambapo rasilimali zilizopo hutumika kuwanufaisha wakoloni mabepari, ilhali serikali za nchi changa kama Tanzania kujikuta katika mzigo mkubwa wa madeni licha ya rasilimali hizo, mzigo ambao maumivu makubwa hurudi kwa mwananchi wa kawaida.
Aidha, bajeti hii imethibitisha kuwa serikali haina mpango na watu wake wala watumishi wa umma, kwani licha ya kutokuongeza nyongeza ya mishahara na kupandisha madaraja wafanyakazi kwa muda wa miaka mitano eti imeshusha kodi ya mapato ya mishahara (PAYE) kutoka 9% kuwa 8% yenye mchango mdogo katika kuinua ustawi wa wafanyakazi na watumishi wa umma kwa ujumla.
Kwa upande mwengine, kupitia bajeti ya mwaka huu 2021/2022 umetolewa ufafanuzi kuhusu namna serikali inavyohujumu malipo ya wafanyakazi kupitia mifuko ya hifadhi ya jamii. Wafanyakazi hukatwa makato kwa ajili ya mifuko hii lakini serikali hukwapua pesa katika mifuko hii na hivyo kuchelewesha malipo hayo kwa wafanyakazi pindi wanapostaafu au kukosa ajira.
Serikali imekiri hadharani kuwa ufanisi mdogo wa mifuko hii katika ulipaji wa mafao kwa wafanyakazi kwa kiasi kikubwa huchangiwa na uwepo wa madeni ambayo mifuko inaidai serikali.
Kwa upande wa umma kiujumla umezidi kujionea wazi wazi kama kawaida, namna viongozi na wanasiasa wa kidemokrasia wanavyofuja fedha za ummah bila kujali chochote, kwani matumizi makubwa ya bajeti zote huwa matumizi ya kawaida na posho za wanasiasa huwa ni makubwa mara dufu ya matumizi ya maendeleo.
Kwa mfano, katika bajeti ya mwaka huu 2021/2022 inaonesha katika matumizi ya kawaida na posho za wanasiasa ni trilioni 22.10 ilhali matumizi ya maendeleo ni trilioni 12.78. Ingekuwa wanasiasa wanajali watu wao kama wanavyodai na kudanganya ingepasa matumizi ya maendeleo yawe makubwa zaidi kuliko posho zao.
Kwa kumalizia, inaonesha wazi kuwa wabunge waliopitisha bajeti hii hawana uhalali wa kuwa ni wawakilishi wa ummah, kwa sababu kupitisha bajeti kama hii ni zaidi ya fedheha, aibu na kuchezea shere ummah. Lakini msingi mkubwa wa haya yote ni mfumo ambao bajeti hii inafanya kazi yaani ubepari. Katika ubepari wanasiasa hawajali isipokuwa maslahi na matumbo yao, familia zao na wapambe wao.
Risala ya Wiki No. 106
26 Dhu al-Qi’dah 1442 Hijri / 07 Julai 2019 Miladi
Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania
Maoni hayajaruhusiwa.