Adhabu ya Mzinifu Aliye Katika Ndoa [Muhsan Zani] Katika Uislamu

بسم الله الرحمن الرحيم

Swali:

Assalamu alaikum Warahmatullah Wabarakatuh naam Sheikh na Amiri wetu. Ningependa kuuliza swali, natarajia utalijibu.

Kuhusiana na adhabu ya kifo kwa mzinifu aliye katika ndoa (muhsan), je, hii imeorodheshwa katika Fiqhi ya Uislamu? Kuna baadhi ya wanavyuoni kama vile Sheikh Abu Zahrah ambao hawaiorodheshi kama adhabu ya Hudud. Vilevile pia imeungwa mkono na Sheikh Mustafa Zarqa anaye eleza kuwa huorodheshwa katika hukmu ya Taazir. Wewe waonaje kuhusu kadhia hii?

Mwenyezi Mungu akulipe kheri, kwa wasaa wako lijibu swali langu.

Jibu:

Wa Alaikum Assalam wa Rahmatullahi wa Barakatuh,

Unauliza kuhusu adhabu ya mzinifu aliye katika ndoa (muhsan zani), je, ni ya kukatikiwa (qat’i) katika fiqh ya Kiislamu? Je, ni katika adhabu za Hudud, au si katika adhabu za Hudud bali ni katika Taazir (adhabu za chaguo la mtawala) kama baadhi ya wanavyuoni wanavyo sema katika zama hizi?

Jibu la swali lako ni kama lifuatavyo:

1- Adhabu ya mzinifu aliye katika ndoa (muhsan zani) ya kupigwa mawe hadi kufa inatoka katika hukmu za sheria na ni katika mambo ya itikadi (Aqa’id). Ni kama hukmu za sheria zote nyinginezo, ambapo dalili yake haihitaji kuwa dalili ya kukatikiwa ili kuitabanni bali yatosheleza kuwa na uwezekano mkubwa wa kuindisha dhanni (ghalabat Al-Dhann) kama inavyo julikana katika misingi ya fiqh. Hivyo basi, hakuna athari katika kuitabanni dalili hii ima iwe ya kukatikiwa au isiyo ya kukatikiwa, lakini lile lililo muhimu ni kuwa inapaswa kuthibitishwa kuwa ni dalili ya sheria kwa ajili yake, na kuna dalili nyingi sahihi katika sheria zinazo ashiria pasi na shaka kuwa adhabu ya mzinifu aliye katika ndoa ni kupigwa mawe hadi kufa kama ilivyo tajwa chini.

2- Imeonekana kuwa baadhi ya wasomi wa zama hizi hawafuati njia sahihi katika kuchukua hukmu za Kiislamu kutoka katika dalili zake, ili wawe makini wakati wa kutafuta hukmu ya Kiislamu ili kwenda sambamba na zama na kufikia rai zinazo afikiana na hukmu na rai zilizoko ulimwenguni zilizo lazimishwa na hadhara ya Kimagharibi juu ya watu kwa jina la kanuni za kimataifa na makongamano ya haki za kibinadamu na nyinginezo … Hii sio sahihi, kwa sababu linalo hitajika ni hukmu ya Mwenyezi Mungu, sio hukmu yoyote tu, wala sio hukmu inayo kubaliana na vifungu, kanuni, mikataba na rai zinazo tawala leo ulimwenguni … Jukumu lililoko ni kutabanni hukmu ya sheria kama ilivyo katika dalili zake na kuifanya kuwa mada ya utekelezaji na utabikishaji wake na kuilingania na kuipigia debe ulimwengu mzima. Ndio hukmu halali kwa wanadamu wote kwa sababu inatoka kwa Muumba wa wanadamu Mjuzi wa hali zao,

(أَلَا يَعْلَمُ مَنْ خَلَقَ وَهُوَ اللَّطِيفُ الْخَبِيرُ) “Asijue aliye umba, naye ndiye Mjua siri, Mwenye khabari?” [Al-Mulk: 14].

(أَلَا لَهُ الْخَلْقُ وَالْأَمْرُ تَبَارَكَ اللَّهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ)  “Fahamuni! Kuumba na amri ni zake. Ametukuka kabisa Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote” [Al- A’raf: 54].

Hivyo basi, hatupaswi kuyapuuza maneno ya wale walio makini katika maamuzi yao ya kwenda sambamba na wakati na kuafikiana na hadhara ya Kimagharibi, ima wakifanya hivyo chini ya shinikizo la uhalisia au kuwaridhisha Wamagharibi makafiri…

3 – Adhabu ya zina kwa mzinifu aliye katika ndoa (muhsan), ambayo ni kupigwa mawe mpaka afe, na kwa ambaye hajawahi kuwa katika ndoa, ambayo ni kupigwa mboko 100, ni adhabu ndani ya Uislamu chini ya Hudud. Tumetoa ufafanuzi wa kina na wa kutosha wa vipengee vya Hadd ya zinaa katika kitabu cha Nidhamu ya Kuadhibu, na nanukuu kutoka katika kitabu cha Nidhamu ya Kuadhibu baadhi ya yale yaliyo elezwa katika mlango “Hadd ya Zinaa”:

[Baadhi wanasema kuwa hadd ya mzinifu mwanamume na mwanamke ni mboko 100 kwa mtu aliye katika ndoa (muhsan) sawa na ambaye hajawahi kuwa katika ndoa, pasi na tofauti baina yao kutokana na maneno yake Ta’ala:

 (الزانية والزاني فاجلدوا كل واحد منهما مائة جلدة ولا تأخذكم بهما رأفة في دين الله)

“Mzinifu mwanamke na mzinifu mwanamume, mtandikeni kila mmoja katika wao bakora mia. Wala isikushikeni huruma kwa ajili yao katika hukmu ya Mwenyezi Mungu”           [An-Nur:2]

Wanasema, hairuhusiwi kuachana na Kitabu cha Mwenyezi Mungu kupitia njia ya kukatikiwa (qat’i) na yakini na kwenda katika habari zilizo pokewa na mtu mmoja mmoja (akhbar al-ahad), ambazo kuna uwezekano wa urongo ndani yake, na kwa sababu hili hupelekea kukifuta Kitabu kwa Sunnah ambapo hairuhusiwi.

Wengi wa watu wenye ilimu katika Maswahaba, Tabi’ina na wale baada yao katika wasomi wa miji tofauti tofauti katika zama zote wanasema kuwa mtu ambaye hajawahi kuwa katika ndoa hupigwa mboko 100 na aliye katika ndoa hupigwa mawe hadi afe. Hii ni kwa sababu Mtume (saw), “alimpiga mawe Ma’iz”, na kutokana na yale yaliyo simuliwa na Jabir bin Abdullah, “kuwa mtu mmoja alizini na mwanamke, hivyo Mtume (saw) aliamuru kuhusiana naye apigwe mboko. Kisha akaambiwa alikuwa ni mtu aliye katika ndoa (muhsan), hivyo akaamuru kuhusiana naye apigwe mawe.”

Yeyote anaye chunguza dalili hizi ataona kuwa maneno yake Ta’ala,

 (الزانية والزاني فاجلدوا كل واحد منهما مائة جلدة ولا تأخذكم بهما رأفة في دين الله)

“Mzinifu mwanamke na mzinifu mwanamume, mtandikeni kila mmoja katika wao bakora mia. Wala isikushikeni huruma kwa ajili yao katika hukmu ya Mwenyezi Mungu”[An-Nur:2], ni jumla. Hii ni kwa sababu neno ‘zani’ (mwanamume) na ‘zaniya’ (mwanamke) ni katika maneno yenye ujumla, hivyo yanajumuisha muhsan na asiye muhsan. Pindi Hadith ilipokuja ambayo maneno yake (saw), واغد يا أُنيْس إلى امرأة هذا فإن اعترفت فارجمها” “Ewe Unays, kesho nenda kwa mke wa huyu. Endapo ataungama, mpige mawe”, na imethibitishwa kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alimpiga mawe Ma’iz baada ya kuuliza hali yake ya ndoa (ihsan), na akampiga mawe Al-Ghamidiyyah mbali na hadith nyinginezo sahih. Hivyo basi, hadith hii imeifafanua aya hiyo. Kwa hivyo, hadith hizi zimefafanua maana jumla ya aya hiyo kwa mwengine asiyekuwa muhsan na kumtenga muhsan kutokana nayo. Kutokana na hayo, hadith hizi zilizoifafanua maana hii jumla hazikuifuta Qur’an. Inaruhusiwa kuifafanua Qur’an kupitia Sunnah na imetokea katika aya nyingi zilizo kuja kwa njia ya jumla na hadith ikazifafanua.

Hukmu ya kisheria ambayo dalili za kisheria yaani Kitabu na Sunnah zimeiashiria ni kuwa adhabu ya zinaa ni kupigwa mboko 100 kwa ambaye hajawahi kuwa katika ndoa, ikitekelezwa kwa mujibu wa Kitabu cha Mwenyezi Mungu, na kupelekwa uhamishoni kwa muda wa mwaka mmoja ikitekelezwa kwa mujibu wa Sunnah ya Mtume wa Mwenyezi Mungu.

Lakini, uhamishaji ni mubah na sio wajib, na huachiwa Imamu, hivyo endapo atataka, atampiga mboko na kumpeleka uhamishoni mwaka mmoja; na endapo atataka, atampiga mboko lakini hatamuhamisha. Lakini, hairuhusiwi kumfukuza bila ya kumpiga mboko, kwa sababu adhabu ni kupigwa mboko. Ama adhabu ya muhsan, ni kumpiga mawe hadi afe, ikitekelezwa kwa mujibu wa Sunnah ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw), ambayo imekuja kama ufafanuzi wa Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Inaruhusiwa kuhusiana na muhsan, kujumuisha upigwaji mboko na mawe juu yake hivyo atapigwa mboko kwanza kisha mawe. Pia inaruhusiwa kumpiga mawe pekee, bila ya mboko. Lakini, hairuhusiwi kumpiga mboko pekee kwa sababu adhabu ya wajib juu yake ni kupigwa mawe.

……….

Ama kuhusu dalili ya adhabu ya muhsan, kuna hadith nyingi. Imesimuliwa na Abu Hurayrah na Zayd bin Khalid aliyesema kuwa mtu mmoja katika Mabedui alikuja kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) na kusema, “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, nakusihi kwa Mwenyezi Mungu kuwa usihukumu isipokuwa kwa Kitabu cha Mwenyezi Mungu’ na mlalamishi mwengine aliyekuwa na ilimu zaidi yake akasema, ‘Ndio, tuhukumu baina yetu kwa Kitabu cha Mwenyezi Mungu.’ Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akasema, ‘Zungumza.’ Akasema, ‘Mwanangu alikuwa mwajiriwa wa huyu na akazini na mkewe. Nimeambiwa kuwa mwanangu anastahili kupigwa mawe, hivyo namkomboa kutokana nayo kwa kondoo elfu moja na ndama. Kisha nikawauliza wenye ilimu na wakanijuza kuwa juu ya mtoto wangu ni mboko mia moja na uhamisho wa mwaka mmoja, na juu ya mke wa huyu ni kupigwa mawe.’ Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akajibu,

“والذي نفسي بيده لأقضين بينكما بكتاب الله، الوليدة والغنم ردّ، وعلى ابنك جلد مائة، وتغريب عام، واغدُ يا أنيس – لرجل من أسلم – إلى امرأة هذا فإن اعترفت فارجمها، قال: فغدا عليها فاعترفت فأمر بها رسول الله صلى الله عليه وسلم فرجمت”

‘Naapa kwa yule ambaye nafsi yangu iko mkononi mwake, nitahukumu baina yenu kwa Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Ndama na kondoo hawa warudishwe, na juu ya mtoto wako ni mboko mia moja, na uhamisho wa mwaka mmoja. Ewe Unays – alimwambia mtu kutoka katika kabila la Aslam – kesho nenda kwa mke wa huyu, endapo ataungama basi mpige mawe.’ Akasema: akenda kwake akaungama basi Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akaamuru kuhusiana naye, na akapigwa mawe.” Hivyo, Mtume aliamuru kupigwa mawe muhsan na hakumpiga mboko. Imesimuliwa kutoka kwa Ash-Sh’abi ‘kuwa Ali (ra) alimpiga mawe mwanamke, alimpiga mboko mnamo alhamisi na kumpiga mawe mnamo Ijumaa, na kusema, nilimpiga mboko kwa mujibu wa Kitabu cha Mwenyezi Mungu na nilimpiga mawe kwa mujibu wa Sunnah ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw).’ Imesimuliwa kutoka kwa Ubadah bin As-Samit aliye sema, Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema,  

“خذوا عني، خذوا عني، قد جعل الله لهن سبيلاً البكر بالبكر جلد مائة ونفي سنة، والثيب بالثيب جلد مائة والرجم”

“Chukueni kutoka kwangu, chukueni kutoka kwangu. Hakika Mwenyezi Mungu amejaalia njia kwao. Bikra kwa bikra kupigwa mboko mia na uhamisho wa mwaka mmoja, na aliye katika ndoa (thayyib) kwa aliye katika ndoa kupigwa mboko mia na mawe.” Hivyo, Mtume (saw) anasema, adhabu ya muhsan ni kupigwa mboko na mawe, na Ali (ra) alimpiga mboko na mawe muhsan. Imesimuliwa kutoka kwa Jabir bin Samara kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alimpiga mawe Ma’iz bin Malik na hakutaja kupigwa mboko. Al-Bukhari amesimulia kutoka kwa Sulaiman bin Buraydah kuwa Mtume (saw) alimpiga mawe Al-Ghamidiyah na hakutaja kupigwa mboko. Muslim ameripoti kuwa Mtume (saw) alikuwa ameamuru kuhusiana na mwanamke mmoja kutoka Juhaina, hivyo nguo zake zikakazanishwa na mwili wake, kisha akapigwa mawe, na haikutajwa kupigwa mboko. Hii yaashiria kuwa Mtume (saw) alimpiga mawe muhsan na hakumpiga mboko, na akasema,

“الثيب بالثيب جلد مائة والرجم” “Aliye katika ndoa/muhsan (thayyib) kwa aliye katika ndoa/muhsan (thayyib), kupigwa mboko mia na mawe.” Hii yaashiria kuwa kupiga mawe ni wajib, huku kupiga mboko ikiwa ni mubah, na imeachiwa rai ya Khalifah. Hadd ya muhsan imefanywa kuwa ni kupigwa mboko na mawe, kupitia kuunganisha baina ya hadith hizo. Mtu hapaswi kusema kuhusiana na hadith ya Samara, kuwa yeye (saw) hakumpiga mboko Ma’iz, bali alijifunga na kumpiga mawe tu, hivyo hiyo ni kifutio cha hadith ya Ubadah bin As-Samit inayo sema, “الثيب بالثيب جلد مائة والرجم” “Aliye katika ndoa/muhsan (thayyib) kwa aliye katika ndoa/muhsan (thayyib), kupigwa mboko mia na mawe.” Mtu hapaswi kusema hivyo, kwa sababu hakuna lililo thibitishwa kuashiria kuwa hadith ya Ma’iz ilikuja baada ya hadith ya Ubadah. Bila ya ithbati kama hiyo kuhusiana na hadith hizo mbili, kutotajwa kwa mboko haimaanishi kuachana nazo, wala kufuta hukmu yake. Kukosekana kwa ithbati kuhusiana na ipi katika hizo ilikuja baada ya nyingine hupinga ufutaji huo, na hakuna jambo lenye kutilia nguvu (murajjih) moja juu ya nyingine. Lililo kuja katika hadith la ziada juu ya upigaji mawe, hukadiriwa kuwa jambo la mubah sio wajib, kwani wajib ni kupiga mawe na linalo ongezeka juu yake ni khiyari kwa Imamu, kutokana na kuziunganisha hadith hizo]. Mwisho wa nukuu kutoka kwa kitabu cha Nidhamu ya Kuadhibu.

Kwa mukhtasari: Adhabu ya mzinifu aliye katika ndoa (muhsan zani) ni kupigwa mawe hadi kifo kama ilivyo patikana katika dalili sahihi kutoka katika Sunnah ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) katika Sahih mbili na katika vitabu vinginevyo vya Hadith, ni adhabu kutoka katika Hudud na sio katika jambo la Taazir.

Na Mwenyezi Mungu ni mjuzi zaidi na Yeye ni Mwingi wa hekima.

Ndugu yenu,

Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah

12 Muharram 1441 H

11/09/2019 M

Maoni hayajaruhusiwa.