Matumizi ya Picha Zilizochorwa

 

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

Swali:

Assalamu Alaykum Warahmatullah Wabarakatuh…

Hukumu ya kuchora kwa mkono na uchoraji wa vitu vyenye uhai kama mwanadamu, wanyama, na kuviweka majumbani kuvining’iniza.

Jawabu:

Assalamu Alaykum Warahmatullah Wabarakatuh

-Kuhusu kuchora kwa mkono na kuchora vitu ambavyo vina uhai…

Kuchora picha za watu na wanyama wenye kufanana na vitu halisi…

Hakika hili linashikamana na uharamu uliopokelewa katika dalili kadhaa, ni sawa ikiwa kuchora kwa kalamu ya mkono, au ikiwa kwa kutumia panya (mouse) kwenye kompyuta, muda wa kwamba uchoraji (picha) kwa juhudi ya kibinadamu inafanana na chenye roho hapo uharamu unapatikana. Ametoa Bukhar kutoka hadithi ya Ibn Abass amesema: Kasema Mjumbe wa Allah (SAW): “Mwenye kuchora picha hakika Allah atamuadhibu mpaka aipulizie roho na hatoweza kuipuliza milele”. Na ametoa kwa njia ya Ibn Umar kwamba Mjumbe wa Alah (SAW) amesema: “Hakika wale ambao wanatengeneza picha hizi wataadhibiwa siku ya Qiyama wataambiwa vihuisheni mulivyoviumba”

Ama hukmu ya kuzikusanya na kuziweka majumbani na kuzining’iniza ni kama ifuatavyo:

a-Ikiwa kuziweka katika sehemu za ibada mfano sehemu za kuswalia, au mapazia ya msikiti, au uenezaji wa matangazo kwa ajili ya msikiti, na mfano wa hayo… Hili ni haramu na haifai. Na miongoni mwa dalili za hayo ni:

Hadithi ya Ibn Abass kwamba Mtume (SAW) alikataa kuingia Alka’aba mpaka zifutwe picha zilizomo humo, kwahiyo, kukataa kwa Mtume (SAW) kuingia Alka’aba ila baada ya kufutwa picha ni kielelezo cha kuacha kwa kukatikiwa (tark jaazim) kuweka picha kwenye sehemu za Ibada, kwahiyo, huwa ni dalili ya uharamu wa kuweka picha misikitini:

Ametoa Imam Ahmad kutoka kwa Ibn Abass “Hakika Mtume (SAW) alipoona picha katika Nyumba yaani Alka’aba hakuingia na akaamrisha zikafutwa”.

b-Ikiwa kuziweka katika sehemu si za ibada, dalili zilizopokelewa zimebainisha kuwa hili linafaa:

-Pamoja na ukaraha yaani ni karaka ikiwa kuziweka katika sehemu kwaajili ya heshima au taadhima kama mapazia ya nyumba au vyombo vya ufafanuzi vya taasisi za kithaqafa (kama mbao) au kwenye mashati yanayovaliwa au nguo…au mashuleni, maofisini, na matangazo ambayo hayana mahusiano na ibada, au kama kutundikwa mbele ya chumba au kuvaliwa kuvutia muonekano na mfano wa hayo… Yote haya ni karaha.

-Na inafaa (mubaha) ikiwa kuziweka katika sehemu zisizo za ibada na si katika sehemu tukufu kama kuwa kwenye zulia la chini la kukanyagia au kwenye magodoro ya kulalia au mito ya kuegemea au picha zinazofukiwa ardhini na mfano wake… Yote haya yanafaa (mubaha).

Na miongoni mwa dalili ya hayo:

-Hadithi ya Abi Talha kwa Muslim kwa lafudhi nimemsikia Mjumbe wa Allah (SAW) akisema: “Malaika haingii katika nyumba ndani yake muna mbwa na picha”. Na katika riwaya kwa njia aliyoipokea Muslim kwamba amesema: “Isipokuwa picha kwenye nguo”. Hii ni dalili ya kuvua (istithnaa) picha iliyochorwa kwenye nguo, na inavyofahamika (mafhuum) ni kuwa Malaika wanaingia katika nyumba yenye picha kwenye nguo, yaani picha iliyochorwa hasa.

Hii ina maana kwamba picha iliyokuwa “imechorwa kwenye nguo”  inafaa (jaaiz) kwasababu Malaika wanaingia nyumba yenye picha (zilizochorwa) sawa na chenye uhai (mustawiya). Lakini zimepokelewa hadithi nyengine zinazobainisha aina ya kufaa (jawaaz) huko:

-Hadithi ya Aisha (RA) ambayo ameitoa Bukhar amesema: “Mtume (SAW) aliingia nyumbani kwangu na mulikuwa na qiraam  lenye picha, uso wake ukapiga rangi kisha akaliendea lile pazia akaliondosha”. Na qiram ni aina ya nguo, na ilikuwa imewekwa kama pazia kwenye mlango wa nyumba. Na kubadilika rangi uso wa Mtume (SAW) na kuliondoa lile pazia ni kitendo chenye kumaanisha kuomba (talab) kuacha kuweka pazia mlangoni likiwa lina picha, kadhia hii ikiunganishwa na kufaa (jawaaz)  kuingia Malaika kwenye nyumba ambayo mna picha “zilizochorwa kwenye nguo” huwa ni dalili ya kwamba ombi (talab) la kuacha si la kukata (jaazim), yaani ni karaha (makruuh). Na kwa kuwa sehemu za picha hizi ilikuwa kwenye pazia lililowekwa mlangoni ambayo ni sehemu yenye kuheshimika, kwahiyo, kuweka picha kwenye sehemu yenye kuheshimika ni karaha (makruuh).

-Hadithi ya Abi Huraira ambayo ameitoa Ahmad katika kauli ya Jibril (AS) kwa Mtume (SAW): “Na amrisha pazia likatwe kisha lifanywe mito miwili ya kukanyagia”.Jibril amemuamuru Mtume (SAW) kuliondoa pazia kwenye sehemu yenye kuheshimika na kufanywa mito miwili kwalo ya kukanyagia.

Hii inamaanisha kwamba kutumia picha zilizochorwa na wengine (na kuziweka) katika sehemu ambazo si za heshima inafaa (mubaha).

Ndugu yenu Attah ibn Khalil Abu Rashtah

Maoni hayajaruhusiwa.