Zaka ya wanyama

ﺑﺴﻢ ﷲ ﺍﻟﺮﺣﻤﻦ ﺍﻟﺮﺣﻴﻢ

Amiri wetu mtukufu, Assalamu Alaykum Warahmatullah Wabarakatuh,

Allah akupe nguvu na akuwafikishe na alete nusra na kumakinika kupitia mikono yenu.

Katika mlango wa Zaka ya wanyama, Imeelezwa katika kitabu cha Mali katika Dola ya Khilafah, maelezo yafuatayo: “Na zaka ni wajibu kwa ng’ombe wachungwa ambao wanachungwa aghlabu ya mwaka, na imeelezwa vilevile katika zaka ya kondoo na mbuzi katka ukurasa 155 maelezo yafuatayo: “ Na zaka ni wajibu katika kondoo na mbuzi wachungwa ambao wanachungwa zaidi ya mwaka pindi wakifikia nisabu mwaka kamili”

Swali hapa ni: Je hakuna zaka kwa kondoo na mbuzi na ng’ombe ambao si wachungwa ambao wanagharimiwa aghlabu ya mwaka? Na ikiwa wana zaka ni kiasi gani?

Na swali jengine kwa heshima lau unijibu, kwanini pametajwa zaka ya wanyama ni ng’ombe, kondoo na mbuzi na ngamia na hapakutajwa zaka ya ndege na hasa kuku ambao wamekuwa wanafugwa  kwa maelfu katika mabanda ya kileo au wao ni katika (zaka za) mali za biashara?

Na Allah akupe baraka katika juhudi yako, Wassalu Alaykum Warahmatullah Wabarakatuh.

Jawabu:

Waalaukum Salam Warahmatullah Wabarakatuh,

1-Ndio, hakuna zaka katika kondoo na mbuzi na ngombe wasiochungwa. Na hili ni kwasababu anaechungwa (assaum) ni sifa inayofahamisha hali ya  ila (illiyyah) na ufahamu (mafhuum) wa sifa ni kuiunganisha hukmu na sifa miongoni mwa sifa za kinafsi (dhaat), na hili lamaanisha kuiondoa hukmu kutoka nafsi  wakati wa kuitenga sifa hiyo. Na sharti yake ni kuwa iwe hiyo sifa ni sifa yenye kufahamisha, yaani yenye kumaanisha hali ya ila (illiyyah), na ikiwa si sifa yenye kufahamisha basi itakuwa haina ufahamu (mafhuum)… Na nakariri kwamba sharti ya ufahamu wa sifa (mafhuumu swifa) ni iwe na sifa yenye kufahamisha, mfano kauli yake (SAW):

«.. فِي صَدَقَةِ الغَنَمِ فِي سَائِمَتِهَا..»

“Katika zaka ya kondoo na mbuzi katika wanaochungwa…”. Ameitoa Bukhari. Kwani hakika ya kondoo na mbuzi (alghanam) ni jina la nafsi na lina sifa mbili; anaechungwa (assaum) na asiechungwa (al-‘ulf) na umeunganishwa wajibu na sifa ya anaechungwa(assaum), hiyo humaanisha kutokuwepo wajibu kwa asiechungwa (alma’aluufah).

2- Ama swali jengine kuwa kwanini zaka ni katika wanyama (kondoo, mbuzi, ng’ombe na ngamia) na sio kwa wanyama wengine kama ndege na kuku…n.k. Hii ni kwa sababu nass imeeleza wanyama hawa, kwa hivyo hufuatwa na kusimama hapo hapo… Na nusus zimeeleza kwa wanyama hawa watatu:

-Amepokea Abu Dhar kutoka kwa Mtume (SAW) kwamba amesema:

«ما من صاحب إبلٍ، ولا بقرٍ، ولا غنمٍ، لا يؤدي زكاتها، إلاّ جاءت يوم القيامة، أعظم ما كانت، وأسمن، تنطحه بقرونها، وتطؤه بأخفافها».

“Hakuna mwenye ngamia, wala ng’ombe na wala kondoo na mbuzi ambae hatoi zaka zao isipokuwa watakuja siku ya kiama wakubwa zaidi kuliko walivyokuwa, wanene zaidi, watampiga kwa pembe zao na watamkanyaga kwa kwato zao” Bukhari na Muslim

-Amepokea Abu Daud kutoka kwa Abu Bakr kutoka kwa Mtume (SAW) katika hadithi ndefu kwamba hakika yake amesema:

«… وفي سائمة الغنم إذا كانت أربعين، ففيها شاة…»

“… Na katika kondoo na mbuzi wanaochungwa wakifikia arobaini basi hutolewa mbuzi mmoja…”

-Na kutoka kwa Ali (RA) amesema:

«ليس في البقر العوامل صدقة

“Hakuna zaka katika ng’ombe wa kazi”. Ameipokea Abu Ubaida na Albayhaqy.

-Na kutoka kwa Amri bin Diinar kwamba imemfikia yeye kuwa hakika ya Mtume (SAW) amesema:

«ليس في الثور المثيرة صدقة»

 “Hakuna zaka katika ng’ombe dume anaetifua ardhi”. Ameipokea Abu Ubaid. Na amepokea vile vile kutoka Jabir bin Abdillah amesema:

«لا صدقة على مثيرة»

“Hakuna zaka katika anaetifua ardhi”.

Na neno (almuthiira) ni ambae anatifua ardhi, yaani anailima.

-Ametoa Alhakim katika kitabu cha Almustadrak ‘ala Al-Swahiihayn kutoka kwa Bahz bin Hakim, kutoka kwa baba yake kutoka kwa babu yake amesema: Nimemsikia Mtume (SAW) akisema:

«في كل إبل سائمة في كل أربعين ابن لبون…»

“Katika kila ngamia wanaochungwa katika kila arobaini (hutolewa zaka) mtoto wa ngamia alietimia miaka miwili na kuingia wa tatu (ibn labuun)…”  Hakim akasema sanad ya hadithi hii ni sahihi. “Na neno (Assaaima) ni wanyama wanaofugwa barani na kwenye malisho wala hawaachwi tuu huria”

  1. Kwa hivyo, hakika wanyama hawa watatu ni wajibu kutolewa zaka, na kama ilivyobainishwa hapo juu. Zaka ni kwa wanaochungwa (assaaima) yaani wanaochungwa aghlabu ya mwaka.

Na haikueleza nass kuhusu zaka kwa aina yoyote katika wanyama wengine au ndege, au wanyama wanaoishi majini. Basi husimamwa hapo kwenye nass inayoeleza kuhusu zaka ya wanyama kwa aina yao hasa. Ama wanyama wakiwa ni kwa ajili ya biashara huwajibika zaka katika wanyama hao kwa mujibu wa zaka ya mali za biashara kama ilivyowekwa wazi katika mlango wake katika kitabu cha Al-amwaal.

  1. Kwa ufupi hakuna zaka katika aina za wanyama isipokuwa wanyama: kondoo mbuzi, ng’ombe na ngamia. Ama katika mali za biashara hutolewa zaka kila mnyama akiwa ni kwa biashara, yaani kwa kuuza na kununua kwa kupatikana nusuus zinazoeleza zaka kwa kila mali ya biashara vyovyote itakavyokuwa aina yake, ni sawa ikiwa nafaka, vitambaa au wanyama… n.k. Na miongoni mwa nusuus zinazoeleza kuhusu zaka ya mali za biashara ni:

-Kutoka kwa Samura bin Jundub amesema;

«أما بعد، فإن رسول الله r كان يأمرنا أن نخـرج الصدقة من الذي نعد للبيع»

“ Ama baada ya hayo, hakika ya Mtume (SAW) alikuwa akituamrisha kutoa zaka katika kile tunachokihesabu kuwa ni cha biashara”. Ameipokea Abu Daud.

-Na kutoka kwa Abu Dhar kutoka kwa Mtume (SAW) amesema:

«وفي البَزِّ صدقته»

“Na katika bazzi kuna zaka yake”. Ameipokea Daru Qutny na Baihaqy. Na neno Albazz ni nguo na vitambaa vinavyofanyiwa biashara.

-Na amepokea Abu Ubaid kutoka kwa Abi Amra bin Hammaas kutoka kwa baba yake amesema:

«مرّ بي عمر بن الخطاب، فقال: يا حماس، أدّ زكاة مالك، فقلت: ما لي مال إلاّ جعاب، وأدم. فقال: قوّمها قيمة، ثمّ أدّ زكاتها»...

 “Umar bin Khatab alinipitia akasema: Ewe Hammaas tekeleza zaka ya mali yako, nikamwambia: sina mali isipokuwa mikoba ya ngozi na nguo za ngozi. Akasema vitie thamani kisha utekeleze zaka yake”…

Nataraji haya yatakuwa yametosheleza. Na Allah Ndie Mjuzi zaidi na Mbora zaidi wa hekima.

Ndugu yenu Atta bin Khalil Abu Rashta

19, Muharam 1439H

29, September 2018

Maoni hayajaruhusiwa.