Zaka ya Mali ya Biashara

بسم الله الرحمن الرحيم

Swali:

Assalamu Alaykum Sheikh wetu, Allah akupe izza kwa Uislamu na aupe izza Uislamu kwasababu yako, na namuomba  Allah niwe katika watakao kupa bai’a ya Khilafah kwa njia ya utume, hakika yake Allah juu ya kila kitu ni mueza.

Nina swali kuhusu zaka yaani zaka ya mali ya biashara au zaka ya mali, je inafaa kuitoa au sehemu katika hiyo kabla ya kupitiwa na mwaka juu yake, na je kupitiwa na mwaka ni sharti ya kutoa kwake?

Allah akusaidie kwenye lililo la kheri katika Uislamu na Waislamu duniani na akhera. Wassalamu Alaykum Warahmatullah Wabarakatuh.

Jawabu:

Waalaykum Salam Warahmatullah Wbarakatuh,

Hakika kupitiwa na mwaka ni sharti katika sababu ya zaka iliyofikia nisabu, basi sharti likitimia, yaani mwaka ukipita juu ya sababu ambayo ni nisabu bila ya kupungua, zaka itakua imewajibika (kutolewa). Lakini hiyo zaka ikitolewa kabla ya kuwajibika kwake, utoaji huu unafaa (jaiz) kutokana na dalili za kisharia zilizopokelewa, na miongoni mwazo ni:

-Ametoa Baihaqy katika Al-Sunanul Kubra kutoka kwa Ali

«أَنَّ الْعَبَّاسَ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ سَأَلَ رَسُولَ اللهِ صلى الله عليه وسلم فِي تَعْجِيلِ صَدَقَتِهِ قَبْلَ أَنْ تَحِلَّ فَأَذِنَ لَهُ فِي ذَلِكَ».

“Hakika Al-Abass (RA) alimuuliza mjumbe wa Allah (SAW) kuhusu kuharakisha kutoa zaka yake kabla ya kupitiwa na mwaka akamruhusu jambo hilo”

-Na ametoa Al-Daruqutny katika Sunan yake kutoka kwa Hujri Al-Adawi kutoka kwa Ali amesema: Kasema mjumbe wa Allah (SAW) kumwambia Umar:

«إِنَّا قَدْ أَخَذْنَا مِنَ الْعَبَّاسِ زَكَاةَ الْعَامِ عَامِ الْأَوَّلِ».

“Hakika tumechukua kutoka kwa Al-Abass zaka ya mwaka mwanzo wa mwaka”

-Na ametoa Al-Daruqutny kutoka Musa ibn Talha kutoka kwa Talha hakika ya Mtume (SAW) amesema:

«يَا عُمَرُ أَمَا عَلِمْتَ أَنَّ عَمَّ الرَّجُلِ صِنْوُ أَبِيهِ؟ إِنَّا كُنَّا احْتَجْنَا إِلَى مَالٍ فَتَعَجَّلْنَا مِنَ الْعَبَّاسِ صَدَقَةَ مَالِهِ لِسَنَتَيْنِ».

“Ewe Umar hukujua kwamba ami yake mtu ni kama baba yake? Hakika sisi tulikuwa tunahitaji mali tukaiharakisha kutoka Al-Abass zaka ya mali yake kwa miaka miwili”.

Wametofautiana (wanavyuoni) kuhusu Al-Hakam katika sanad yake (hiyo hadithi) na sahihi ni kutoka kwa Al-Hasan bin Muslim ambayo ni mursal.

Kwahiyo basi, kuharakisha kutoa zaka kabla ya uwajibu wake ni jambo linalofaa (jaiz). Na kwa taarifa yako tu, hakika wengi wa wanavyuoni wanasema hivyo.

Ndugu yenu Atta ibn Khalil Abu Rashtah

Maoni hayajaruhusiwa.