Waachiwe Huru Sio Magaidi

Taarifa kwa Vyombo vya Habari

Ni mwaka mmoja sasa tangu wanachama watatu wa Hizb ut Tahrir Tanzania: Ustadh Ramadhan Moshi (39), Waziri Suleiman (31) na Omar Salum Bumbo (49 ) kunyakuliwa kisha kubambikiziwa mashtaka ya uongo ya ‘kula njama ya kutenda ugaidi’ na ‘kutenda matendo ya ugaidi’.

Kwa kipindi chote cha mwaka mzima, wakati ndugu zetu hao wakiwa mahabusu, licha ya kuwa mbali na familia zao, ndugu, marafiki na kusita kwa shughuli zao za uzalishaji, pia wamerundikwa katika mahabusu zenye mazingira duni kibinadamu, yakikosa usalama wa kiafya na huduma stahiki kwa jumla. Baya na la kusikitisha zaidi, kesi yao imekuwa ikitajwa tu kila wiki mbili, bila ya kuanza kusikilizwa, kwa kisingizio cha kutokamilika ukusanyaji wa ushahidi ati kwa mwaka mzima!

Sisi Hizb ut Tahrir Tanzania tunasisitiza kwa sauti pana kwamba wanachama wetu hao hawana tembe ya hatia, na ndio maana mpaka sasa kumekosekana hali ya kujiamini na ujasiri wa kuanza kusikilizwa kesi yao. Pia tunasisitiza kwamba tangu kuasisiwa Hizb ut Tahrir mnamo mwaka 1953 imekuwa ikilingania Uislamu kwa kushikamana kwa umakini wa hali ya juu na njia ya Mtume SAAW kwa kujifunga kikamilifu na njia ya kifikra na kisiasa ikijiepusha kwa hali zote na utumiaji nguvu wala mabavu.

Aidha, sisi Hizb ut Tahrir /Tanzania kwa mara nyengine tena tunavitaka vyombo vinavyosimamia utoaji haki na sheria Tanzania kuwaachia huru mara moja wanachama wetu hao. Pia tunatoa mwito kwa taasisi za haki za binadamu, viongozi ndani ya jamii, wanafikra, wanahabari na Ummah kwa ujumla ikiwemo jamii ya Kiislamu kupaza sauti zao juu ili waachiwe huru ndugu zetu hao, Sambamba na hilo kuipinga vikali sheria ya kibaguzi ya Kupambana na Ugaidi, iliyolazimishwa na madola makubwa, na inayotumika kudhulumu, kukhofisha, kutesa, kuteka nk.

Tunavikumbusha vyombo vya kusimamia haki Tanzania, wakati hapa Tanzania bado vinaendelea kuwashikilia kwa dhulma mamia ya Waislamu kwa kudandia sheria ya kibaguzi ya Ugaidi, nchi jirani kama Kenya, Uganda na Ethiopia zinaendelea kuwaachia huru wenye tuhuma kama hizo. Ni wakati sasa kwa Tanzania kujifunza kutoka kwa majirani zake.

KUMB: 1440 / 02
Jumatano, 22nd Safar 1440 AH 31/10/2018 CE

Masoud Msellem
Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari
Hizb ut Tahrir Tanzania

Pepe: info@hizb.or.tz

Hizb ut Tahrir Official Website
www.hizb-ut-tahrir.org
Hizb ut Tahrir Central Media Office Website
www.hizb-ut-tahrir.info

 

Maoni hayajaruhusiwa.