Vijana Jiungeni Kwenye Mabadiliko ya Kweli ya Kiislamu

Tokea zamani nchi nyingi duniani zimekuwa zikiwawinda vijana kwa njia mbalimbali kama vile kuwatia tamaa na matarajio ya uongo pamoja na ahadi zenye matumaini wasiyotekelezewa daima.
Wakati tarehe 12 Agosti ya kila mwaka imechaguliwa kuwa Siku ya Vijana Kimataifa, hali ya vijana kiulimwengu ni mbaya, wengi wao wamekosa matumaini ya kuishi kamwe! Mfumo kandamizi wa kibepari unaowasimamia wanadamu kwa sasa umewatelekeza vijana kiasi cha kufikia wengine kuchukua maamuzi magumu kama kujiua, kutumia matumizi ya madawa ya kulevya nk.

Ujana ni hidaya na amana ajaaliwayo mwanadamu na Muumba wake. Ni katika wakati huu mwanadamu huwa na uwezo mkubwa wa nguvu za kiwiliwili na uwezo mkubwa wa kiakili na tafakuri. Ujana hufananishwa na jua la mchana ling’aapo, na uzee huchukuliwa kama jua lituapo ukihusishwa na udhaifu. Zaidi ya hayo, mambo mengi ya faida au hasara hufanyika wakati wa ujana, wanavyuoni wengi waliitafuta na kupata elimu yao katika umri wa ujana. Kwa mfano, Mwanachuoni, mwanasiasa na mujtahidi mkubwa wa zama hizi sheikh Taqiuddin An-Nabahan (Allah Amrehemu) alikuwa tayari ameshahifadhi quran yote akiwa tu kijana wa miaka 12. Nabii Ibrahim (as) akiwa ni kijana mdogo tu aliweza kujadiliana kwa hoja na Mfalme Nimrudh na kumshinda, Nabii Yusuf (as) aliteuliwa kuwa msimamizi wa mazao ya kilimo nchini Misri akiwa ni kijana mdogo.

Hata hivyo, mfumo wa kibepari umemtupa kijana licha ya kuwa ni rasilimali nyeti kwa ustawi wa mwanadamu.
Takwimu za mwaka 2015 za Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na Masuala ya Ajira (ILO) asilimia 25 tu ya waajiriwa duniani ndio vijana. Hii inamaanisha wengi wa waajiriwa ni watu waliovuka umri wa ujana, ilhali zaidi ya asilimia 43 ya vijana duniani hawana ajira. Katika nchi zinazoendelea ambazo ni makoloni ya mataifa ya kibepari ya kimagharibi asilimia 31 ya vijana wake hawana elimu ya kujitosheleza kuweza kuajiriwa.
Wimbi kubwa la kudai mabadiliko haramu ya demokrasia yaliyoitwa mapinduzi ya kiraia yaliyoanzia Tunisia na kuenea Bara Arabu na Mashariki ya Kati liliungwa mkono moja kwa moja na vijana. Ni vijana tena wa Kiislamu ndio washiriki wakubwa katika mapinduzi hayo ambapo walionesha ujasiri, ushupavu, muhanga mkubwa na moyo wa kufa na kupona katika kuona kwamba mabadiliko ya kiutawala yanatokea. Hata hivyo, kwa bahati mbaya sana mioyo yao ya mihanga yao ilisukumwa na utumwa wa fikra za kimagharibi za kidemokrasia na wakapambana kufa kupona kutaka mabadiliko haramu na hatari ya kidemokrasia. Mabadiliko yanayomfanya Allah (swt) asiwe na nafasi katika maisha yao. Ama huku ni kutumika vibaya mno kwa nishati na mihanga ya vijana wa Kiislamu.

Ni muhimu ifahamike kuwa uwezo mkubwa wa kufikiri, upeo wa udadisi na tafakuri pana ikiambatana na usimamizi mzuri wa kufinyangwa Kiislamu vipawa vya vijana wetu itapelekea uwepesi kwa vijana kuuona ukweli, kuifahamu haki na hatimaye kushikamana nayo. Historia inatudhibitishia ukweli huo. Tukiangalia wafuasi takribani wote wa mwanzo wa Mtume (saw) walikuwa ni vijana, na ndipo Mtume (saw) aliposema “walikuwa vijana ndio walionipokea na kunikubali lakini wazee walinikataa”. Kwa kawaida wazee wengi huwa ni wazito kufanya maamuzi magumu na waoga sana kukubali mabadiliko.

Tunashuhudia katika kisa cha watu wa pangoni (Aswhabu-ul Kahf), walikuwa ni vijana walioachana na dini na mila potofu za kishirikina na kuchukuwa mabadiliko sahihi kwa kumkubali na kumuamini Mwenyzi Mungu mmoja wa haki,
Allah (swt). Qur’an inatukumbusha kwa kauli yake (swt) Anaposema:

إِنَّهُمْ فِتْيَةٌ آمَنُوا بِرَبِّهِمْ وَزِدْنَاهُمْ هُدًى
”Hakika wao walikuwa ni vijana walio muamini Mola wao Mlezi. Na Sisi tukawazidishia uwongofu”.
[Al-Kahf: 13]

Wakati sasa umewadia kwa vijana wa Kiislamu kuunganisha nguvu zetu pamoja kwa kubeba fikra zitakazoleta mabadiliko halisi ya Kiislamu. Fikra zitakazo tukomboa na utumwa wa fikra na mfumo batil wa kibinadamu wa Urasilimali wa Kisekula na kutupeleka kuwa watumwa na watumishi kamili wa Allah (swt) peke yake. Ili kuutawalisha mfumo wa Kiislamu kwa walimwengu wote. Mfumo wa haki anao uridhia Muumba wetu.

Na
Mohamed Abdulla Mohamed
Mjumbe wa Kamati ya Mawasiliano Hizb ut Tahrir Tanzania

Kutoka Uqab: 20

Maoni hayajaruhusiwa.