Karibu Mwaka Mpya wa Kiislam.

Kalamu yangu nashika, kwa jina lake Halimu
Nawaomba kwa hakika, sikilizeni kwa hamu
Tumeshaufika mwaka, kalenda yetu adhimu
Shime daawa kuishika, dini iwe na hatamu

Mwaka mpya umefika, wa dini ya Isilamu
Kalenda ilotukuka, imeanza Muharramu
Wajibu kubadilika, tuwe mbali na haramu
Shime daawa kuishika, dini iwe na hatamu

Umri ushaongezeka, hebu fanyeni muhimu
Mwisho utamalizika, turudi kwake Rahimu
Tuiacheni dhihaka, dini kwetu ndo muhimu
Shime daawa kuishika, dini iwe na hatamu

Ni wakati kuamka, wakubwa na maghulamu
Sharia kuitandika, na zake zote nidhamu
Na sio kudanganyika, kuushika udhalimu
Shime daawa kuishika, dini iwe na hatamu

Umma unahangaika, katika kila sehemu
Umesheheni mashaka, kutoka kwa madhalimu
Suluhisho walitaka, Khilafah iwarehemu
Shime daawa kuishika, dini iwe na hatamu

Vilio vinasikika, si Burma wala si Shamu
Umma wapewa gharika, mabunduki na mabomu
Nayo hapa yashafika, kila mtu ahujumu
Shime daawa kuishika, dini iwe na hatamu

Mwisho sasa nishafika, chini naweka kalamu
Nasaha zimesikika, hebu zipeni muhimu
Msione napayuka, maneno haya adhimu
Ya Rabbi Ulotukuka, Umma wetu urehemu

Shairi hili lilisomwa na Ust. Mkiongwe Mbwana katika
Kongamano Maalumu la mwaka mpya wa Kiislamu.

Ijumaa 1437 Hijria / 06-11-2015

Masjid Karimullah
Tungi – Kigamboni

Maoni hayajaruhusiwa.