Uvamizi wa Kenya Ndani ya Somalia

بسم الله الرحمن الرحيم

Uchambuzi huu unaofinyanga mahusiano ya Kenya na Somalia kwa msukumo wa madola ya kikoloni uliandikwa na Hizb ut Tahrir mnamo mwaka 2011, lakini bado una uhalisia fulani hususan kwa hali inavyoendelea sasa baina ya nchi mbili hizo. Tafadhali soma kwa makini:
Tarehe 16 Oktoba, 2011 Kenya ilivamia kijeshi ardhi ya Somalia kusini ikatangaza kwamba inasaka vikosi vya ‘Al-Shabab Al-Mujahideen’ kufuatia kutekwa nyara watalii…
Serikali ya Kenya inafanya bidii kwa kampeni hii inayoitwa ‘Linda Nchi’ kuanzisha ‘eneo huru’ lenye urefu wa kilomita 100 ndani ya ardhi ya Somalia linaloshikana na mipaka ya Kenya, ili liwe eneo lililojitenga na serikali ya Somalia ltakaloitwa Azania au Jubaland:
“Azania: Jina la eneo jipya linalohusisha Gedo, Juba kusini na Juba kati. Aidha eneo hili linajulikana kama Jubaland.”
Eneo hili litakuwa chini ya udhibiti wa Kenya, kwani Kenya imeteua mtawala wake mtarajiwa aliyekuwa waziri wa ulinzi wa zamani wa Somalia Mohamed Abdi Gandhi, kwa lengo la kudhibiti Al-Shabab Al-Mujahideen… pamoja na lengo la moja kwa moja la ki-stratejia, yaani kudhibiti bandari ya Kismayu ambayo ni kama mshipa wa uhai wa wapiganaji wa Al-Shabab… pamoja na yanayotajwa tajwa katika baadhi za taarifa kwamba eneo hilo lina hazina kubwa ya mafuta:
“Kuna taarifa kwamba Azania—au kwa uchache eneo lake la mwambao—lina utajiri wa mafuta.”
Kuhusu matukio mapya ya operesheni ya Kenya ndani ya Somali, amesema mkuu wa vikosi vya Kenya Julius Karangi mnamo tarehe 19 Oktoba mbele ya wanahabari hapo Nairobi: “Serikali na taifa la Kenya zitajiondoa Somali pindi zitakapoona kuna usalama” huku akifafanua kwamba “hakuna muda maalum” ulioekewa operesheni hiyo.
Ndege za vita za Kenya zilifanya uvamizi mkali wa anga dhidi ya mji wa Kismayu ulioko ufukweni hapo tarehe 23 Oktoba zikilenga ndege hizo maeneo yaliopo baina ya bandari ya kimataifa ya Kismayu na hazina za mafuta.
Uvamizi huu unazingatiwa kuwa ni wa mwanzo tangu Al-Shabab kumiliki Kismayu Agosti mwaka 2008.
Kabla ya hapo, ndege za Kenya zilifanya uvamizi mkali dhidi ya miji na vijiji vya jimbo la Juba chini zikiwemo Qoqani, Tabtu na Ras Kamboni. Mwai Kibaki, rais wa Kenya, alitangaza katika hotuba yake tarehe 20 Oktoba, 2011 Nairobi kwamba nchi yake itajihami ili kulinda “umoja na usalama” wa ardhi yake “kwa kutumia kila njia” Kibaki alisema: “Tutalinda umoja na amani ya ardhi yetu kwa kila mbinu itakayofaa ili kudhamini usalama na utulivu (stability)”. Na akaongeza: “Vikosi vyetu vya ulinzi vimeanza operesheni ndani na nje ya mipaka yetu dhidi ya wanaharakati wanaolenga kutingisha utulivu wa nchi yetu.”
Aidha, Kibaki akasema: “Lakini amani ya nchi yetu haidhaminiwi tu na vikosi vyetu vya ulinzi. Bali ni lazima kila mmoja wetu ashiriki kikamilifu kuhakikisha hakuna atakayetumika kuhatarisha amani na utulivu wetu.”
Somalia ilikuwa koloni la dola tatu:
1. Italia: ukoloni wake ulikuwa kusini na kati ya Somalia pamoja na sehemu ya kaskazini mashariki ikiwemo mji wa Mogadishu, mji mkuu wa nchi. Eneo hili lilipata uhuru kutoka Italia mnamo Julai, 1960. Lakini baada ya 1991 vilizuka vita vya wenyewe kwa wenyewe, eneo hili limegawanyika chini ya makabila na Al-Mahakim (utawala wa mahakama ya Kiislamu) kisha jimbo la Puntland na jimbo la Baidoa na mengineo…
2. Uingereza: Iliweka ukoloni wake eneo linaloitwa leo “Somaliland”. Eneo hili liko kaskazini mwa Somalia liliofungika baina ya Djibouti, Ethiopia na Ghuba ya Aden. Somaliland ilipata uhuru kutoka Uingereza mnamo tarehe 26 Juni, 1960 na ikaungana na Somalia iliyokuwa chini ya Italia kuasisi Somalia mpya iliyojiunga na Jumuiya ya Kiarabu mwaka 1974. Somaliland inakusanya sehemu tano kati ya 18 asili za Somali, na mji mkuu wake ni Hargeisa.Ilipoangushwa serikali ya Siad Barre mnamo tarehe 19 Januari, 1991 Mohamed Ibrahim Egal akatangaza uhuru wa eneo hili mnamo tarehe 18 Mei ya mwaka huo huo japo kuwa haikutambuliwa kimataifa.
Mwaka 2001 kulifanywa kura ya maoni iliomakinisha kujitenga kikamilifu kutoka Somalia na kubuniwa kwa Jamhuri ya Somaliland. Ndipo Somaliland ikabuni serikali, bunge na jeshi jipya pamoja na kutoa pasipoti kwa wakaazi wake kuanzia Septemba 2000. Berbera ni katika miji muhimu zaidi ya Somaliland, na ina bandari muhimu inayoenea ghuba ya Aden na kutumiwa na Ethiopia kupokea baadhi ya bidhaa zake kutoka nje. Somaliland inatambulika kuwa na utulivu zaidi ikilinganishwa na maeneo mengine ya Somalia.
3. Ufaransa: Ilikuwa na makoloni katika majimbo ya Afar na Issa yanayojuulikana kama Somalia ya kifaransa, na tangu ilipopata uhuru kutoka Ufaransa mwaka 1977 ikajuulikana kwa jina la Djibouti. Afar na Issa ni makabila mawili makuu ya eneo hili. Djibouti inatambulika kwa mujibu wa lugha, historia na maingiliano yake ya kijamii kama sehemu ya Somalia, na tangu uhuru wake imekuwa mwanachama wa Jumuiya ya Kiarabu, Umoja wa Mataifa na taasisi nyenginzo za kimataifa.
4. Sehemu za Somalia zilizokaliwa kimabavu: –
Jimbo la Ogaden
Jimbo hili pia linajulikana kama Somalia Magharibi nayo inakaliwa kimabavu na Ethiopia tangu mwaka 1954. Inajulikana katika mgao wa kiutawala wa Ethiopia kama jimbo la tano au jimbo la Ogadenia. Wengi wa wakaazi wa jimbo hili ni Waislamu wafugaji wa majangwani wenye asili ya ki-Somali.
Jimbo la Kusini Magharibi ya Somalia
Jimbo hili linajuulikana kwa jina la ‘Anfadi’ na leo ni sehemu ya Kenya. Mji wake mkuu ni Garissa, na Kenya ililiingiza kuwa sehemu ya ardhi yake tangu mwaka 1963 baada ya mwafaka wa Arusha.
Hali ya kisiasa ilivyo sasa: –
1. Kusini kati ya Somali kuna serikali ya rais Sheikh Sharif Ahmed inayotokamana na mwafaka wa Djibouti wa tarehe 26/10/2008. Inadhibitiwa kwa ushawishi wa Marekani, nayo haijawa na utulivu. Kuna harakati za Kiislamu zikiongozwa na ‘Al-Shabab Al-Mujahideen’ zinazopigana na serikali na vikosi vya Muungano wa Afrika vilivyo humo. Mkono wa Marekani wa kutenda katika dola hii ni Ethiopia ambayo jeshi lake huingia na hutoka humo kwa amri ya Marekani.
2. Somaliland inadhibitiwa na ushawishi wa Uingereza, nayo ndio yenye amani na utulivu zaidi.
3. Djibouti ambayo imebakia chini ya ushawishi wa Ufaransa. Na Ufaransa inaichukulia Djibouti kuwa ndio kituo chake kikuu katika eneo. Ndani ya Djibouti kuna kambi kubwa zaidi ya jeshi la kifaransa nje ya Ufaransa ambayo ina wanajeshi 2,700 wa kifaransa. Kambi hii inatumiwa kwa anga na baharini kuhami ushawishi wa Ufaransa katika eneo hili hadi Afrika ya kati. Ufaransa inaelewa vyema tamaa ya Marekani ndani ya Djibouti ndipo ikairuhusu Marekani ‘ili kujikinga na shari yake’ kutumia kambi yake ya zamani inayoitwa Le Moniere, pamoja na na kuiruhusu kuweka kikosi kidogo cha kimarekani kisichozidi wanajeshi elfu moja. Marekani inazingatia kuwemo wanajeshi wake mia nane katika kambi hiyo kama nukta kianzio na wala sio mwisho wa maneno. Na Marekani inajaribu kupanua kambi hili ili kuweza kuweka wanajeshi elfu mbili kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi…
Lengo la Kisiasa nyuma ya Matukio ya Karibuni: –
Uingereza imetumia kisingizio cha matukio ya kutetereka utulivu na amani katika Somalia kusini kwa kuweko harakati zenye silaha “Al-Shabab Al-Mujahideen” na tukio la kutekwa nyara watalii ndani ya Kenya ili kumnong’oneza rais wa Kenya, Kibaki, kuingiza jeshi lake kukabiliana na tukio la kutekwa nyara watalii na kuhami mipaka ya Kenya. Kisha ikaja kauli ya kubuni eneo la usalama (Azania) mipakani mwa Kenya lenye utawala usiojifunga na serikali kuu chini ya udhibiti wa Kenya.
Haya ndiyo yaliodhihirika katika tukio hili. Ama msukumo na malengo nyuma ya tukio hili ni kama yafuatayo: –
1. Uingereza inataka kubuni eneo kaskazini magharibi mwa Somalia linalofanana na eneo la kaskazini mwa Somalia (Somaliland) ili kuidhibiti Marekani isiweze kuitawala Somalia yote kikamilifu, kwani ikiwa kaskazini na Somaliland zitakuwa mkononi mwa Uingereza, hapo Marekani iliyoko katikati mwa Somalia itabanwa uwezo wake wa kivitendo kuwa na ushawishi Somalia nzima. Bali hesabu za Uingereza inadhania kwamba mwishowe Marekani itapoteza kamwe ushawishi wake kivitendo katikati ya Somalia, maadamu tu ipo baina ya kaskazini na kusini inayomilikiwa na mkono wa Uingereza.
Uingereza inadhania kwamba mustakbali wa Somalia hautokuwa zaidi ya kuwa na serikali ama ya kimajimbo (federal) au muungano wa vijidola (confederacy). Kwa hivyo, ikiwa Uingereza itamiliki kaskazini na kusini itakuwa na ushawishi wa kivitendo ndani ya Somalia. Na hayo ndio yaliyosemwa na waziri wa zamani (wa Somalia) ambaye Kenya inataka kumteuwa kuwa mtawala wa jimbo la Azania ambalo Kenya inajaribu kulibuni: Bw. Mohamed Abdi Gandhi alisema:
“Ingekuwa bora zaidi lau wasomali wangepewa fursa ya kupanga dola ya utawala wa kimajimbo (federal state) kwa sura ya mashauriano pole pole.”
2. Uingereza imefanya uhodari mkubwa kuingia Somalia kusini kwa kutumia matukio matatu: –
Kwanza: Tukio la utekaji nyara watalii na kuhami amani ya Kenya. Tukio hili limemtia haya hata Odinga, waziri mkuu wa Kenya anayeshikilia na kumili upande wa Marekani, kiasi cha kushindwa kupinga uvamizi wa kijeshi wa Kenya kuingia Somalia.
Pili: Ethiopia kuingia Somalia kaskazini mara kwa mara, hivi karibuni, wala sio mara ya mwisho tarehe 19/11/2011 kama ilivyoripotiwa na (vituo vya habari vya) BBC na AFP kwamba vikosi vya Ethiopia viliingia kaskazini magharibi mwa Somalia kwa kisingizio cha kulinda amani ya Ethiopia, yaani kwa kisingizio kile kile kinachotumiwa na Kenya kuingilia kati.
Tatu: Qadhiya hii imetengenezwa kana kwamba haihusu Uingereza tu, bali ni ya Ulaya nzima, ndipo Ufaransa na Norway pia zikashiriki kikamilifu kwa kisingizio cha kulinda mashirika yao ya mafuta.
Hivyo ndivyo hali ya kuingilia kati Somalia kulivyopangika kwa uhodari, kwa upande wa msukumo wake kiasi cha kuitia haya Marekani na wafuasi wake. Sawa sawa wawe wa Ethiopia au hata Kenya yenyewe yaani Waziri mkuu.
Matarajio:
Ama yanaotarajiwa kutokea katika uvamizi huu, kwa hakika haitarajiwi kuwa na utulivu mfano wa Somaliland. Yaani haitarajiwi kwamba kuingilia kati kwa Kenya na nyuma yake ushawishi wa Uingereza katika Somalia kusini kutazalisha utulivu kwa sababu zifuatazo: –
• Kwa upande wa eneo la karibu: Hisia za Waislamu humo Somalia kutokubali kwao kuingiliwa kimataifa ni hisia zenye nguvu hususan fikra za jihadi zinazowachangamsha Waislamu na zinazotokea kivitendo katika ‘harakati ya Al-Shabab Al-Mujahideen’ na wengine wasiokuwa wao, hali inayomaanisha kwamba haitarajiwi uvamizi wa Kenya kuleta utulivu.
• Kwa upande wa eneo pana zaidi: Serikali ya Kenya ina wakuu wawili. Na hata kama Kibaki anayemili upande wa Uingereza ametumia fursa hii kwa uhodari mkubwa kufuatia matukio yanaoathiri amani ya mipaka ya Kenya ili kusisitiza suala hili na kuingia kijeshi, lakini waziri mkuu Odinga yeye anamili upande wa Marekani. Na kwa hivyo siasa ya ‘muwafaka wa kati na kati’ itafanya kazi kivitendo, kiasi cha kuwa uvamizi wa Kenya hautodumu muda mrefu.
Odinga anasaidiwa katika jambo hilo na Ethiopia iliyoukana uvamizi wa Kenya katika ardhi ya Somalia kwa ulimi wa msemaji wa wizara yake ya mashauri ya nje, Dina Mufta, kama ilivyoripotiwa na vyombo vya habari vya Uingereza na Ufaransa aliposema: “Taarifa hii haina ukweli wowote ule. Hakuna vikosi (vya Ethiopia) katika Somalia kattu… bali si chochote isipokuwa majungu ya baadhi ya watu.” Hii inamaanisha kwamba vikosi vya Ethiopia havikuingilia kati kipindi kilichoingia jeshi la Kenya, na ni wazi kwamba makusudio ya kukana huku ni kujivua Ethiopia kisingizio cha kuingilia kati ambacho ndicho hicho hicho kilichotumiwa na Kenya kuhalalisha kuingilia kwake kati!
Na zaidi, Ethiopia imedhihirisha upinzani wake wa kubuniwa kijinchi cha ‘Azania’, kusini mwa Somalia au inayoitwa ‘Jubaland’ kwani wasomali wengi kutoka jimbo la Ogaden wanaishi humo. Na lau kijinchi hiki kitabuniwa basi kitakuwa nje ya udhibiti wa Ethiopia. Na kitasababisha matatizo yamapigano ya vikosi vya wanamgambo (militia) vya Ogaden vilivyoko kusini. Ethiopia inataka Somalia kusini kufuata mwelekeo wa serikali ya Mogadishu inayomilikiwa na Marekani, na kwa hivyo kuwa chini ya Ethiopia, ili wakimbizi waliokimbia Ogaden wabakie chini ya udhibiti wake pasina kugeuka kuwa jinamizi (ndoto ya kutisha) ya ki-amani dhidi yake.
• Upande wa kimataifa: Marekani imetamka dhidi ya kuingilia kati kwa Kenya kinyume na kauli ya Ulaya:
–Msemaji wa Ufaransa wa wizara ya mashauri ya Ulaya alisema tarehe 29 Oktoba: “Tunatamani kushiriki katika operesheni ya Kenya iliyoongozwa baada mawasiliano na mashauri ya kina pamoja na serikali ya mpito ya kimajimbo (TFG) dhidi ya uhalifu wa vikosi vya wanamgambo (militia) vya Al-Shabab ili kurudisha amani na utulivu kwa Somalia kwa muda mfupi uwezekanavyo.
–Baada siku nne ya kauli hii, Kenya ikafichua kwamba meli ya kivita ya Ufaransa ilipiga makombora dhidi ya maeneo ya Al-Shabab katika uvamizi wa mwanzo wa kijeshi wa kimagharibi dhidi ya Somalia tangu miongo miwili.
–Na jeshi la Kenya liliweka bayana kwamba jeshi la majini la Ufaransa limerusha makombora dhidi ya kijiji cha Quday cha Somali
–Kwa upande wa pili, wizara ya mashauri ya nje ya Marekani huko Washingtaon ilikana kwamba ilishiriki kwa namna yoyote ile kusaidia Kenya katika operesheni ya kivita inayofanywa Somalia.
Taarifa ya wizara ya mashauri ya nje ya Marekani iliyotolewa tarehe 25 Oktoba ilisema kwamba Marekani imejifunga na ushirikiano wa muda mrefu na Kenya katika “kupambana na ugaidi Afrika mashariki” nayo inatanguliza misaada kwa Nairobi “kujenga uwezo wake” wa kupambana na tishio la magaidi wenye silaha. Isipokuwa ilisisitiza waziwazi kwamba Marekani haishiriki kwa namna yoyote ile kusaidia operesheni ya kijeshi inayofanywa na jeshi la Kenya hivi sasa Somalia.
Kadhalika Ikulu ya Marekani (White House) imekana mnamo tarehe 29 Oktoba yaliotajwa katika gazeti la ‘Washington Post’ kuhusu ndege za Marekani zisizokuwa na rubani kuhusika na operesheni za kivita huko Somalia zikipaa kutoka kambi yake ilioko Ethiopia.
Msemaji wa Ikulu ya Marekani, Jay Carney, alikiri kuwepo ndege zisizokuwa na rubani huko Ethiopia lakini akasema kwamba hazina silaha na zinatenda operesheni za kijasusi kati ya mzunguuko wa ushirikiano baina Marekani na serikali ya Somalia “ili kushajiisha utulivu katika pembe ya Afrika.”
Mwisho: Mambo haya yote yanatilia uzito zaidi upande wa mizani unaotarajia kwamba ushawishi wa Uingereza hautofanikiwa kusini mwa Somalia kama ulivyofaulu kaskazini mwake. Na lengo la Kenya la kuimegasehemu ya Somalia kuasisi kijinchi cha kulazimisha huko kusini (Azania) kitakachotawaliwa na waziri wa ulinzi wa zamani wa Somalia (Mohamed Abdi Gandhi) halitarajiwi kupata utulivu wa muda mrefu. Yaani eneo la Azania la Somalia kusini halitarajiwi katika hali halisi zinazovyoonekana kudumu kwa muda mrefu kujitenga na Somalia kama eneo la Somaliland ilivyojitenga kaskazini…
15 Muharram, 1433 Hijri
11/12/2011 miladi

 

Maoni hayajaruhusiwa.