Usekula Unavyoangamiza Waislamu na Wanadamu

Hivi karibuni Mbunge mmoja Muislamu nchini Lebanon bi Rola Tabsh (Sunni) alishiriki katika ibada ya misa ya mwaka mpya katika kanisa moja nchini humo. Kitendo hicho kilipingwa vikali na Waislamu nchini humo kiasi cha Waislamu kupaza sauti zao kukilaani kwa nguvu zote.
https://www.alaraby.co.uk/english/news/2019/1/6/lebanon-muslim-lawmaker-angers-coreligionists-after-attending-christian-mass

Picha za ibada hiyo ya misa zilizosambazwa katika mitandao ya kijamii kila mahala zilimuonesha mbunge huyo akibarikiwa na Kasisi wa kinaswara.

Mbunge huyo awali alitetea kitendo chake hicho kwamba, muamala huo wa maingiliano ya kithaqafa / kitamaduni hakumaanisha kwamba amekuwa muumini wa dini hiyo, bali kitendo chake hicho ni kielelezo cha kuwapa heshima waumini wa dini hiyo ya Ukiristo.

Hatimaye mbunge huyo ametangaza kwamba tayari ameshaomba msamaha kwa Mwenyezi Mungu kwa kitendo chake hicho, na pia tayari ameshazuru jamii ya wanavyuoni wakubwa wa Kisunni nchini humo kuhusiana na qadhia hiyo.

Fikra ya usekula imeathiri sana baadhi ya Waislamu hususan wanasiasa sio Lebanon tu bali kila mahala. Kwa masikitiko baadhi ya Waislamu hao hawatambui kwamba hata ikiwa jamii ya wanasiasa wenzao wa dini nyengine hujihusisha katika ibada na miamala ya kidini na wasiokuwa dini zao, hilo kwa mujibu wa dini zao kamwe sio tatizo, kinyume na Uislamu ambao una muongozo wa kila kipengee katika miamala yote.

Kabla ya kuonesha madhara makubwa yanayotusibu Waislamu kutokana na fikra hii hatari, ni muhimu awali kuonesha chimbuko na tareekh/ historia ya fikra hii hatari kwa Umma wetu na kwa wanadamu kwa jumla.

Mapinduzi makubwa ya kifikra ndani ya Ulaya katika karne ya 17 yaliyotokamana na mapambano baina ya kambi ya Makasisi na kambi ya mufakiriina/wanafalsafa yalifikia kilele cha muwafaka wa ‘wewe upate nami nipate’ kwa kuzaliwa kwa fikra chafu, hatari na isiyowafikiana na maumbile ya binaadamu ya ilmania/usekula.

Muwafaka waliofikia kambi mbili hizi uliopelekea kuzaliwa fikra hii fisidifu na potofu ulikuwa ni muwafaka usiokinaisha akili, bali ni wa kitoto kamwe. Tunasema hivyo kwa kuwa muwafaka huu haukujengwa juu ya msingi mathubuti wa hoja. Kwa sababu, baada ya mzozano kurefuka baina ya kambi mbili hizi juu ya hatma na nafasi ya kanisa katika utawala, wakati makasisi wakitetea na kushikilia msimamo wao kuwa lazima kanisa libakie na nafasi katika utawala. Ilhali wanafalsafa/mufakirina wao wakikataa kata kata kanisa kuwa na nafasi hiyo kwa kuwa limeshadhulumu na kukandamiza vya kutosha, kwa kushirikiana na kuwatetea watawala mabwanyenye ambao wakitawala kwa mabavu, huku kanisa likihalalisha uovu wao kwa kuwatakasa kuwa ‘ni chaguo la Mungu’.

Basi hatima ya mzozano wa kambi mbili hizo ukafikia muwafaka wa ‘kati na kati’, yaani kila kambi isiondoke mikono mitupu au kwa maneno mengine, ‘pata nami nipate’ kwa kuzaliwa fikra mpya ya usekula/ ilmania ambayo ndiyo aqiida /fikra msingi ya nidhamu ya kidemokrasia.

Muwafaka huu ulisimama juu ya msingi mbovu. Kwa kuwa suala lilipaswa liwe, jee kuna Muumba au la? Na kama yupo Muumba basi apewe nafasi yake katika maisha ya kila siku. Na lau wangekinai kwamba hakuna Muumba hapo mambo yangeisha na kila mmoja atende atakavyo! Lakini nukta hii msingi katika mjadala huu ilirukwa kijanja, na badala yake kuwepo au kutokuwepo Muumba likawa si suala la kulijadili kamwe. Bali hitimisho likawa dini haikukanushwa moja kwa moja, lakini haikupewa nafasi yake inayostahili. Ikawa, Mungu yupo lakini amalizikie katika majumba ya ibada. Hii ndio fikra ya usekula, fikra kiongozi /aqeeda ya mfumo wa kidemokrasia ambayo imesambazwa na kuenezwa kila mahala na kufanywa kuwa kigezo katika ulimwengu wote. Na hii ndio fikra inayoshikiliwa na kulindwa takriban ndani ya katiba zote za nchi na katiba za vyama vyote vya kidemokrasia na kutetewa na kuhifadhiwa kwa nguvu zote.

Awali, madhara makubwa ya fikra hii ni upande wa kiimani. Ni fikra ya hatari inayogongana na aqeedah ya Kiislamu. Hivyo, ni dhambi kubwa kwa Muislamu kushikilia fikra hii. Na lau Muislamu anaikinai na kuikubali kwa udhati fikra hii, hapana shaka yoyote hutoka ndani ya Uislamu. Kwa kuwa inapingana na misingi ya aqida ya Kiislamu kwa dalili za kukata(qatwii)

Pili, fikra hii inawadhoofisha na kuwadumaza Waislamu kifikra katika upeo wa dini yao, kwa kuwakosesha kuwa na thiqa/kujiamini kwa kuipa dini yao ‘ubwana’ wake unaostahili ambao ndio lengo la kuletwa kwake, nalo ni kuzishinda dini zote. Hilo, hudhihirika wakati Waislamu wanapotatua matatizo mbalimbali yanayowakabili ndani ya jamii husika. Waislamu na wasikokuwa waislamu huketi pamoja kutafuta suluhisho kwa mujibu wa akili zao na sio kwa mujibu wa Uislamu. Hii maana yake kwa Waislamu hawa wanaiona dini yao haina suluhisho na uwezo wa kutatua matatizo yanayomkabili mwanaadamu.

Tatu, inapofikia hali ya Muislamu kuiona dini yake haina utatuzi na imekosa ubwana, hapo haitarajiwi tena kwake kuilingania dini yake kwa mwengine. Kwa kuwa, kimaumbile mtu humlingania mwengine kitu alichokikinai kuwa ni kitu bora kuliko alichonacho mwenzake.

Nne, Waislamu hususan viongozi wa kisiasa huburuzwa kushiriki katika hafla na ibada mbalimbali za kikafiri. Kama vile misa, ibada za kumakinishwa maaskofu, kutoa heshima za mwisho kwa wafu wa kikafiri nk. Jambo hilo hudhihirika kwa maaelfu ya mifano kila siku katika maeneo yetu na ulimwengu wote wa Kiislamu. Aidha, na viongozi makafiri nao hushirikishwa katika hafla mbali mbali za Kiislamu, na wakati mwengine hata katika misikiti. Haya hutendwa kwa kisingizio kwamba nchi haina dini na viongozi wapo kuwatumikia raia wa dini zote na wa makundi yote ndani ya jamii. Hata hivyo, jambo hili huwadhuru Waislamu zaidi, kwa kuwa dini yao ina muongozo wa ‘halali na haramu’, kinyume na wasiokuwa Waislamu.

Tano, kwa Waislamu hujitumbukiza katika suala la kindoto, la kujaribu kuridhisha kila kundi, kitu ambacho kiudhati hakiwezekani. Na kubwa zaidi, licha ya kujipendekeza kote kwa makafiri na ukafiri , hatima yao Waislamu hao hubwagwa chini, kwa kuwa kimsingi ukafiri na makafiri kamwe hawatokuwa radhi na Uislamu na Waislamu.

Mtume SAAW na makhalifa baada yake waliwatumikia raia wa makundi na dini mbali mbali wakiwemo mayahudi, washirikina/ waabudia masanamu na wakiristo, lakini walibakia kuenzi ubwana wa Uislamu na kuilingania dini yao. Kamwe hawakushiriki katika ibada zao kwa namna yoyote. Badala yake walifanya mgongano wa moja kwa moja baina ya Uislamu dhidi ya ukafiri, baina ya haqi dhidi ya batil. Na baina ya uongofu dhidi ya upotofu. Na viongozi hao hawakuwacha kuonesha uovu wa ukafiri, na kuwataka makafiri waache ukafiri wao na waingie katika dini ya haki ya Uislamu mara moja. Amesema Mtume SAAW:

“Naapa kwa yule ambae nafsi ya Muhammad imo mikononi mwake, hatosikia yoyote kuhusu mimi katika ummah huu, myahudi au mnasara, kisha akafa na hakuamini nilichotumwa nacho (risala ya Uislamu) ila atakuwa mtu wa motoni.”

Aidha, kiongozi wa Warumi (Caesar) baada ya kulinganiwa na Mtume SAAW alimjibu Mtume SAAW kwa kumueleza ‘Mimi ni Muislamu’ Mtume SAAW akajibu baada ya kusomewa barua hiyo kwa kusema:
“Kasema uwongo adui wa Mwenyezi Mungu, si Muislamu bado yupo katika dini ya unaswara/ukiristo.

Pia imesimuliwa na Qatadah kwamba Mtume SAAW alimkabili mnaswara/mkiristo mmoja akamueleza:
“Silimu ewe Abul Harith! nae akajibu: “Nimekwisha kusilimu”. Mtume akamueleza tena: Silimu ewe Abul Harith! akajibu tena: Tayari nimeshasilimu. Mtume akamueleza tena, Silimu ewe Abul Harith! akajibu tayari nimeshasilimu. Hapo Mtume akaghadhibika akamueleza: “Umesema uwongo. Mambo matatu yanakuweka wewe mbali na Uislamu. Unanua ulevi, unakula nguruwe na unamfanyia Allah Ta’ala kuwa ana mtoto”.

Leo Umma wa Kiislamu una ukame wa viongozi aina hii. Basi jee haujafika muda wa kufanya kazi kurejesha tena Khilafah Rashidah ili tupate viongozi wakweli, wachamungu ambao wataibeba ajenda ya Uislamu bila ya kuburuzwa katika matendo ya kuuridhisha ukafiri na makafiri. Na hao ndio viongozi wa kujifakhiri nao.

04 Jumada al-awwal 1440 Hijri | 10 -01- 2019 Miladi

Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania
https://hizb.or.tz/
https://web.facebook.com/Hizb-ut-Tahrir-Tanzania

 

Maoni hayajaruhusiwa.