Umisionari Unavyotumika Katika Ukoloni Wa Afrika

بسم الله الرحمن الرحيم

 

Ukoloni ni namna ya maisha ya jamii moja ya wanadamu kuwatawala wengine kwa hali ya kuwadhulumu haki na utu wao katika nyanja zote za maisha. Umekuwa ukoloni ukitazamwa vibaya na kila mwanadamu kwa sababu ni kinyume na uhuru na utu. Binadamu wote hawafurahii kukoloniwa japo wapo wanaokoloni wanaadam wenzao.
Ili kufanikiwa kukoloni ni lazima kuwepo na funguo za kuwafungulia milango migumu ya kimaada na kifikra iliyopo kimaumbile kwa watu wote kuhusu kutokuwa huru kwani kiasili binadamu tumeumbwa tukiwa huru katika mipaka ya kimaumbile aliyotuwekea Muumba wa mbingu na ardhi na vilivyomo na kazi ya msingi ya ukoloni ni kupora uhuru huu.
Miongoni mwa funguo za ukoloni kwa mataifa ni vilivyotajwa katika historia kwa jina la vitangulizi vya ukoloni, yaani; wamisionari, wapelelezi na wafanyabiashara. Wamisionari ni wafanyakazi wa kikristo, kwa makundi yao yote ambao walifika kwa wingi Afrika na kuandaa mazingira ya kukoloni.Umisionari ulikuwa ni koti la kuficha upelelezi. Kwahiyo hakuna namna ya kutofautisha wamisionari na wapelelezi kama funguo za kuingiza ukoloni Afrika.Mjerumani Johann Ludwing Krapf (11Januari 1810-26Novemba 1881)kwa mfano, alijivika kofia ya umisionari huku akifanya na kazi za upelelezi.
Ukoloni upo wa kifikra, kiuchumi na kisiasa. Katika aina zote, hii ya kifikra ndiyo ya msingi na hubeba nyingine zote. Na kimaumbile, fikra ndiyo huwa kikwazo kikuu kwa mwanadamu kukoloniwa. Wamisionari walifanya kazi kubwa ya kuondoa kizingiti hiki na kuweka mazingira mepesi kwa wakoloni na ukoloni halisi kuingia. Walitumia mbinu mbalimbali kama vile elimu, imani na huduma za kijamii kufanikisha kazi yao.
Elimu: ilitumika na inatumika kuandaa watumishi kwa ukoloni na wakoloni. Elimu ililenga kuwawezesha watu kusoma biblia na kupata maarifa machache ya kutumikia ukoloni katika kukoloni wenzao kwa niaba, yaani kuwa vibaraka. Hata leo hii katika ukoloni mamboleo ni wale walioandaliwa katika shule za kanisa ndiyo vibaraka wakuu wa kuimarisha ukoloni. Kwakuwa tayari uislam ulisha tangulia Afrika mashariki, elimu hii ilikuwa na jukumu la kuipinga na kufuta utamaduni wa kiislam na kuwatenga waislam au kuwatoa katika dini yao yaani kuwaritadisha.
Pia elimu ilitumika na inatumika kulainisha nyoyo za watu kukubali kuishi na ‘wabaya’ wao ambao ni wavamizi na waporaji wa rasilimali zao. Binadamu wote ni sawa, lakini usawa huu nipale wao wanapotaka kitu kwa waafrika lakini utabaka unakuwepo katika kuwanyima haki wakoloniwa. Mafunzo ya kimisionari yalisisitiza utengano wa dini na siasa na wakaandaliwa wanadini watumishi wasiasa na kubakiza kazi ya dini ni kuombea amani iliyo haribiwa na wanasiasa.Elimu ilitukuza uzungu na kudogosha wengine kama inavyofundishwa kwamba binadamu wote ni kizazi cha Nabii Nuhu ambaye alikuwa na watoto watatu (Hamu, Shemu na Yafethi) ambapo huyu Hamu ali laaniwa kwa kumchungulia utupu mzazi wake, na yeye ndiye kizazi cha Afrika, Mwanzo 10:20-23, yaani kizazi cha laana.
Elimu hii iliandaa pia ukoloni mamboleo ambao ulianza kufanya kazi baada ya uhuru wa bendera. Waliandaa wasomi wao na kuwakabidhi nchi waziendeshe kwa niaba kama anavyo tufahamisha Padri Dr C. Sivalon kwamba shirika la Maryknoll Fathers wamekubali kulipa tiketi ya kwenda Amerika na kurudi England kwa vile huyu (Nyerere) ni kiongozi wa kikatoliki, mtu kutoka jimbo la musoma ambaye anaheshimiwa na mapadri wetu. Kwa vile ni nia ya serikali ya Waingereza (wakoloni) kuwaandaa wenyeji kwa madaraka (tutakayowapa baada ya kuwapa ‘uhuru’).
Imani na ibada: zililenga na zinalenga kumtukuza mzungu na kudumisha ubaguzi wa madaraja. Wakagawa muda wa ibada zao kwa mujibu wa lugha hali iliyopo hadi leo hii kwamba kuna muda wa kiingereza na Kiswahili. Viongozi wa dini hizi (wamisionari) walikuwa wana washajihisha viongozi wa kiafrika kushirikiana na watawala wa kikoloni. Kwamba uongozi unatoka kwa Mungu,hata wazungu kuwa watawala (wakoloni) ni mpango wa Mungu.lakini yapasa kutii amri za viongozi kwa vyovyote kwa kuwa ya kaisari mpe kaisari. Eti kuna ya Mungu na yasiyo ya Mungu.
Huduma za kijamii: zinazotunika kuonesha kuwa Waafrika ni watu wa kusaidiwa, na Wazungu watu wenye utu. Waligawa misaada na huduma za kiutu kama mavazi afya, elimu na chakula ambavyo vilitumika kulainisha mioyo isione ubaya wa wakoloni na kukoloniwa. Wakafungua milango ya ukoloni na kuandaa kuondoka kwa wakoloni na kuachia nchi watu wao walio waandaa. Mfano kanisa katoliki lilianzisha idara ya walei mwaka 1957 ikiwa na jukumu la kuondoa watu wasio faa (waislam) katika siasa na kuweka wanao faa (wakatoliki ‘wasomi’) na akasisitiza Padri Paul Crane alipo tembelea Tanganyika kwamba, “Niwazi kuwa hakuna koloni lingine katika Afrika ambapo kanisa limekuwa katika nafasi nzuri kama lilivyo hapa Tanzanganyika” (Dr C.Sivalon, uk 22-24). Hawa walei waliunda vikundi vya kijamii kujiweka karibu na jamii. Wamisionari (kama nyenzo iliyotumiwa na mabepari) ndivyo kwa muhtasari walivyo karibisha na kuulea ukoloni duniani wakilenga hasa kuondoa athari za uislamu katika maisha ya wanaadam na kuweka maisha ya kibepari.
Tofauti na Uislamu, mafunzo na maisha yake kisiasa unapinga ukoloni na ubaguzi wa namna zote katika jamii. Uislamu unapo ingia katika eneo kwa kulifungua katu hauwafanyi wenyeji kuwa daraja la chini kuliko wageni (Waislamu). Haki mbele ya sharia ni kwa kila mwanadamu bila kujali cheo,imani au rangi. Ni sharia za Mwenyezi Mungu(swt) ndizo zipo juu ya kila jambo na juu ya kila mtu. Kwa sababu chimbuko la thaqafa ya kiislamu ni wahayi na sio utashi wa mwanadamu
Na Abuu Nuthtaqs Hamza Sheshe
Risala ya Wiki No. 126
13 Rajab 1443 Hijri /14 Februari 2022 Miladi
Afisi ya Habari – Hizb ut Tahrir Tanzania

Maoni hayajaruhusiwa.