Uhalisia wa Tabarruj (Mapambo) kwa Ufafanuzi

بسم الله الرحمن الرحيم

Swali la Pipit Meidawati:

Assalamu’alaikum wa rahmatullahi wa baarakaatuh

Namuomba Mwenyezi Mungu daima akulinde na akusaidie. La’ala Allahu yusahhil umuuraka

Ningependa kuuliza kuhusu tabarruj. Tunaifafanua vipi na tunaitumia vipi? Ninavyojua ni kuwa tabarruj yamaanisha kuonyesha mapambo mbele ya mwanamume wa kando kisha kumvutia kutazama hayo mapambo au hata kututazama sisi. Pia inategemea tabia/mila/desturi.

Mimi naishi nchini Indonesia, tunabishana juu ya utekelezaji wa tabbaruj. Hakika, mtindo wa kimaisha wa Kimagharibi umetuathiri namna tunavyo vaa na kujipamba. Wanawake hujitia vipodozi kama poda ya uso, rangi ya mdomo, rangi ya macho nk. Baadhi ya wakati ni vipodozi vya kimaumbile au vipodozi vya kila siku. Wanafanya kazi, kusoma vyuoni, kuhudhuria vikao vya elimu, kutembeleana, nk huku wakiwa na vipodozi kama hivi. Wakati mwengine huonyesha mapambo haya zaidi ya kawaida katika matukio fulani kama siku ya harusi, au kuhudhuria sherehe ya harusi, hawajitii tu vipodozi vya kila siku, bali hujitia vipodozi vya kuvutia zaidi. Baadhi ya wanawake hufanya kazi kama waburudishaji, wasanii, waimbaji, kisha wanavaa na kujitia vipodozi vya kuvutia kweli kweli.

Je, tunapaswa kuachana na vipodozi hivyo kwa sababu vimetengezwa kwa mtindo wa kimaisha wa kimagharibi? Je, haturuhusiwi kupaka chochote katika nyuso zetu? Au ni sawa ikiwa tutajipaka vipodozi vya kila siku/kimaumbile?

Wakati huo huo, baadhi ya wanawake hujipaka itsmid (rangi ya macho ya Kifursi) machoni mwao, kwa sababu Mtume (saw) ameagiza hilo na pia kulifanya. Lakini ni wachache tu na hata wakati mwengine huwavutia wanaowazunguka.

Nadhani, Sheikh Ata Abu al-Rashta, hutajali kunipa ufafanuzi wa utekelezaji tabarruj.

Natanguliza shukran zangu nyingi, jazakallahu khairan kathiran

Wassalamu’alaikum wa rahmatullahi wa baarakaatuh

Pipit Meidawati

Samahani… mimi ni Pipit kutoka Indonesia

Swali: Фатиме Сулиманова‎‏

Assalamu alaykum wa rahmatullah. Sheikh Mpendwa, nina swali kwako, wanawake wanapotoka nje na kujitia vipodozi katika nyuso zao, je wataingia ndani ya kigawanyo cha tabarruj? Je, uke ni nini katika Shari’ah?

Jibu:

Wa Alaikum Assalam Wa Rahmatullah Wa Barakatuhu,

Maswali yote mawili yako chini ya mada moja, hivyo tutayajibu kwa pamoja:

Nyuma tumewahi kuchapisha Jibu la Swali katika mada ya tabarruj… Lifuatayo chini ni moja ya majibu yaliyo chapishwa mnamo 9/10/2016, na yanatosheleza InshaAllah:

Jibu lililotajwa:

(Kabla ya kujadili maelezo ya maswali yako, nakueleza mambo kadhaa katika mada hii ambayo yameorodheshwa katika nidhamu wa kijamii katika swala la kuwatazama wanawake, na nakueleza baadhi ya mipaka mipana

1. Mwanamke anapotoka nje katika maisha ya umma, anapaswa kuvaa vazi la Kisheria, ambalo ni: Jilbaab, kuziba uchi (‘awrah) wake, na kutoonyesha mapambo yake (tabarruj).

2. ‘Awrah (uchi) ni mwili mzima wa mwanamke isipokuwa uso na viganja vya mkono, ni haramu kwa mwanamke kuonyesha ‘awrah yake, na “kuleta mvuto” hapa haizingatiwi, yaani ima alete mvuto au asilete, kuonyesha ‘awrah (uchi) wake ni haramu…

3. Tabarruj katika lugha ni: pindi mwanamke anapo onyesha mapambo yake na urembo wake kwa wanaume, katika “Lisan Al Arab” inaeleza: “Na Tabarruj: Ni kuonyesha mapambo watu wa kando, ambapo imekemewa, lakini inaruhusiwa kumuonyesha mumewe”. Katika “Qamous Al Muheet” inaeleza: “Na alionyesha Tabarruj: Alionyesha mapambo yake kwa wanaume”.

Katika “Mukhtar As-Sahah” inaeleza: “na Tabarruj” ni pale mwanamke anapo onyesha mapambo yake na urembo wake kwa wanaume.”… Na katika “Maqayees Al –Lugha”: “Baraja’ herufi: Ba, Ra, na Jim zina machimbuko mawili asili: La kwanza lamaanisha kudhihirika, na kuonekana (Al-thuhoor and Al-Borooz), na kutokana nayo ndio Tabarruj, ambapo ni pale mwanamke anapo onyesha urembo wake).” Lile linalofahamika kutokana na neno “Idh-har” na “Al-dhuhoor na Al-Borooz” ni kuwa pambo hilo ni lenye kuvutia na kudhihirika kwa wanaume; na maana ya Kisheria sio tofauti na hiyo, Mwenyezi Mungu (swt) asema:

 [وَلَا يَضْرِبْنَ بِأَرْجُلِهِنَّ لِيُعْلَمَ مَا يُخْفِينَ مِنْ زِينَتِهِنَّ]

“Wala wasipige chini miguu yao ili yajuulikane mapambo waliyo yaficha” [An-Nur: 31]

Hivyo basi mwanamke ni lazima asitembee huku akigongesha gongesha miguu yake ardhini ili kuruhusu vikuku vyake vitoe sauti itakayomfanya mwanamume kujua kwamba wanamke huyo amevaa vito miguuni mwake chini ya nguo zake. Yote haya yamaanisha kuwa Tabarruj ina maana sawa kilugha na Kisheria, ni mapambo yanayoleta mvuto, na sio mapambo tu.

Hivyo basi, tabarruj ni mapambo/vipodozi yanayoleta mvuto pasi na kuonyesha ‘awrah, ama kuonyesha ‘awrah, ni haramu ima iwe inaleta mvuto au la… tabarruj sio zeenah )mapambo), kwani kuna mapambo ya kawaida ambayo hayaleti mvuto na yanaruhusiwa kwa mwanamke, na kuna mapambo yanayoleta mvuto yanayojulika kama tabarruj, na tabarruj ni haramu. Tabarruj inaingia ndani ya vigawanyo viwili:

Mapambo yanayovaliwa na wanawake katika sehemu za mubah za mwili wake, yaani mikononi mwake na usoni, na katika nguo zake ikiwa yanaleta mvuto

– Mapambo yanayovaliwa na wanawake katika sehemu zengine zisizo za mubah bila ya kuonyesha ‘awrah, kama kurembesha mguu wake kwa vikuku, au kurembesha mkono wake kwa bangili, huku mguu au mkono wake ukiwa umefinikwa, hivyo endapo mwanamke atauenua mguu au mkono wake kwa njia fulani, wanaume watajua kuwa kuna mapambo mguuni au mkononi mwake, basi hili linachukuliwa kuwa ni tabarruj hata kama mguu au mkono huo umefinikwa.

1. Ama zeenah (mapambo) yanayovaliwa katika sehemu za mubah za mwili wa mwanamke, au katika nguo zake, basi ikiwa yanaleta mvuto, itakuwa ni tabarruj na hivyo basi ni haramu. Maana ya kuleta mvuto ni pale mapambo hayo katika sehemu hii (ya mwili au nguo) si ya kawaida, yaani anapotembea akipishana na wanaume na mapambo haya, huvutika na uke wa mwanamke huyu, na maana ya kutoleta mvuto ni kuwa pale mwanamke anapopishana na wanaume, basi ule upande wa uke wake hauwapitikii akili mwao… jambo hili linaangukia ndani ya ufahamu wa uhalisia (tahqeeq al-manat), na si dhani ni gumu, kwani uke na uume upo ndani ya wanaume na wanawake, na ni rahisi kwao kutambua ikiwa mapambo haya yanaleta mvuto au la, hususan wanawake, kwa sababu wanajua iwapo mapambo yao ni ya kawaida au yanaleta mvuto kwa wanaume…

2. Ama mapambo yanayovaliwa katika maeneo yasiyo mubah huku ‘awrah ikiwa imefinikwa, kama vile mwanamke kuvaa kikuku katika mguu wake, kisha akagongesha gongesha miguu yake kwa nguvu ardhini ili kuifanya miguu yake itoe sauti itakayomfanya mwanamume kujua kwamba mwanamke huyu amevaa kito mguuni mwake, basi hili ni tabarruj na ni haramu… au ikiwa amevaa bangili mikononi mwake kisha kuitembeza mikono yake ili wanaume wajue kwamba kuna mapambo mkononi mwake… basi hili pia ni tabarruj, na hukadiriwa kuwa haramu hata kama miguu na mikono hiyo imefinikwa.

3. Sasa nitaanza na maelezo katika maswali yenu na kuwajibu ipasavyo:

Kuhusu, zeenah (mapambo) ya wanawake ya pete vidoleni mwake, ikiwa watavaa pete za kawaida, hawataleta mvuto… lakini ikiwa kwa mfano atavaa pete yenye kutoa mng’aro au kelele, au ukubwa wa kuvutia, nk, basi haya yote huleta mvuto na ni tabarruj… na hivyo hivyo inatekelezeka kwa viatu venye kung’ara nk…

Ama kuvaa mkufu nje ya jilbab, iwe inaleta mvuto au la hairuhusiwi kwa sababu asili ya jilbab ni kuziba mapambo yote ya ndani yaliyo valiwa katika ‘awrah yake, na mkufu ni pambo la shingo na shingo ni sehemu ya ‘awrah (uchi) hivyo ni lazima uzibwe ndani ya jilbab, hivyo basi ikiwa anataka kuvaa mkufu, ni lazima aufiche ndani ya jilbab.

Ama bangili zilizo mikononi, ikiwa akiinua mkono wake bangili zitatoa kelele, itadhahirika kuwa amevaa mapambo, na hii ni tabarruj na hairuhusiwi.

1. Jilbab ni nguo inayofinika mapambo na nguo za ndani, yaani sio mahali pa mapambo, hivyo basi, mapambo na urembo juu yake hairuhusiwi…

2. Ikiwa wanamke atatia wanja mwachoni mwake, hautaleta mvuto kwa sababu uko ndani ya macho, lakini ikiwa ataweka katika mapigo ya jicho au kope rangi fulani, basi italeta mvuto…

3. Vivyo hivyo, ikiwa atatakasa ngozi ya uso wake kuondoa baadhi ya madoa au chunusi usoni, na uso ukaonekana mrembo zaidi kuliko ulivyo kuwa awali, lakini ukawa ni uso ule ule wa kawaida, basi haitaleta mvuto, na bila shaka eneo analoishi mwanamke linacheza dori katika yale yanayoleta mvuto, kama vile kuishi kijijini au kuishi mjini… Kitu muhimu katika swala hili ni kuwa mapambo ambayo si ya kawaida eneo hilo na yanaleta mvuto yanachukuliwa kuwa tabarruj.) Jibu la Swali lililotangulia linaishia hapa.

Kwa kuhitimisha, mwanamke kwa kawaida anajua iwapo mapambo aliyovaa yanaleta mvutio kwa wanaume au la, yaani, sio vigumu kujua tofauti kati ya mapambo yanayoleta mvuto na mapambo yasiyoleta, na wanawake wanajua hili kupitia hisia / kuhisi kwao… Kwa hali yoyote ile, mwanamke mchaMungu wa Kiislamu hujiweka mbali na sio tu haramu pekee, bali pia kutokana na mambo yenye shaka (shubahaat), kama ambavyo baadhi ya Maswahaba walikuwa wakijiweka mbali na baadhi ya mambo ya mubah (yanayoruhusiwa) kwa sababu ya kukaribiana kwake na haramu… imesimuliwa kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema:

«لَا يَبْلُغُ العَبْدُ أَنْ يَكُونَ مِنَ المُتَّقِينَ حَتَّى يَدَعَ مَا لَا بَأْسَ بِهِ حَذَراً لِمَا بِهِ البَأْسُ»

“Mja hatafikia kuwa miongoni mwa wachaMungu mpaka awache lile ambalo si la makosa kwa kujitahadharisha na lile la makosa,” imepokewa na Tirmidhi aliyesema kwamba hii ni Hadith Hasan.

Nataraji kuwa jibu hili limetosheleza, na Mwenyezi Mungu (swt) ni Mjuzi Zaidi na Mwingi wa Hekima.

Ndugu yenu,
Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah

30 Shawwal 1441 H
Sawia na 21/06/2020 M

Link ya jibu hili katika ukurasa wa Amiri (Mwenyezi Mungu amhifadhi) wa Facebook:

Maoni hayajaruhusiwa.