Tunamkumbuka Papa Benedict Wa 16 Kwa Hasara Tatu

بسم الله الرحمن الرحيم
Aliyewahi kuwa kiongozi wa juu wa Kanisa Katoliki Papa Benedict wa 16 ( 95 ) alifariki dunia mnamo tarehe 28 Disemba 2022 na kuzikwa tarehe 5 Januari 2023 katika viunga vya makao makuu ya Kanisa Katoliki mjini Vatican.
Papa Benedict wa 16 alishika hatamu za Kanisa Katoliki mnamo Aprili 2005 kufuatia kifo cha mtangulizi wake Papa John Paul wa Pili, na kuendelea na wadhifa huo mpaka Februari 2013 alipojiuzulu kwa sababu alizotaja kuwa za kiafya na uzee, pamoja na ukweli wa kuwepo tetesi za kutajwa sababu nyengine za kuwepo husuma za ndani ya taasisi hiyo ya Vatican kama ilivyodokezwa katika kitabu cha “Nothing But The Truth – My Life Beside Benedict XVI” cha kasisi Georg Ganswein aliyekuwa msiri mkubwa wa Papa Benedict wa 16 na katibu wake binafsi.
Baada ya kifo cha Papa Benedict wa 16, wengi katika rambirambi zao wametoa kauli amma maandishi ya kumbukumbu zao kuhususiana nae, maisha yake, utumishi wake nk.
Katika makala hii tutagusia walau kwa mukhtasari kumbukumbu yetu kwa kiongozi huyo ambapo tukiri wazi kwamba daima tutamkumbuka kiongozi huyo kutokana na hasara tatu kubwa zilizopatikana ndani ya maisha yake.
Hasara hizo tatu kubwa, moja kaondoka nayo yeye binafsi Papa, moja kawaachia wafuasi wake, lakini bado wana namna ya kuirekebisha na kujiepusha na muelemeo wake, na hasara nyengine inawarudia Umma wa Kiislamu ambayo imekuwa endelevu tangu kuangushwa dola ya Khilafah ya mwisho mwaka 1924.
Hasara ya Kwanza
Itakumbukwa kuwa mnamo mwezi Septemba 2006, Papa Benedict wa 16 akiwa katika ziara ya nyumbani kwao Ujerumani alipata fursa ya kutoa muhadhara katika Chuo Kikuu cha Regensburg, kusini mashariki ya Ujerumani. Kwa masikitiko makubwa sana, miongoni mwa maelezo yake katika kuwasilisha muhadhara huo alitoa matamshi ya kashfa dhidi ya Uislamu na hususan kuhusiana na Mtume SAAW kwa kunukuu maandishi ya karne ya 14 yaliyosheheni chuki na uadui dhidi ya Mtume SAAW, Uislamu na Waislamu.
Baada ya Umma mzima wa Kiislamu kulaani na kuonyesha waziwazi hisia zao za kuchukizwa kufuatia kauli hizo za kashfa, Papa Benedict wa 16 alijifanya kisanii kuomba radhi Waislamu, huku bado akijihami kwamba yeye alinukuu tu maandishi ya zamani ambayo hayawakilishi mtazamo wake.
Qadhia hii imeacha hasara na majuto ya kudumu kwake Papa Benedict wa 16, kwa kuwa kumzungumzia Mtume SAAW, ina maana amepata fursa ya kupata taarifa za Mtume SAAW na kuona mafunzo yake, lakini kamwe Papa Benedict wa 16 mpaka anaondoka duniani hakuwa tayari kuyafuata mafundisho hayo, bali aliendelea tu kushikamana na ukiristo, dini ambayo iko kinyume na dini aliyokuja nayo Mtume Muhammad SAAW. Na Mtume SAAW alihadharisha matokeo mabaya kwa atakayepuuza ulingano wake kwa kusema:
، “‏ وَالَّذِي نَفْسُ مُحَمَّدٍ بِيَدِهِ لاَ يَسْمَعُ بِي أَحَدٌ مِنْ هَذِهِ الأُمَّةِ يَهُودِيٌّ وَلاَ نَصْرَانِيٌّ ثُمَّ يَمُوتُ وَلَمْ يُؤْمِنْ بِالَّذِي أُرْسِلْتُ بِهِ إِلاَّ كَانَ مِنْ أَصْحَابِ النَّارِ ‏”‏ ‏.
“Naapa kwa yule nafsi ya Muhammad imo mikononi mwake,
hatosikia yoyote kuhusu mimi katika Umma huu katika mayahudi au manasara na hakuamini kwa yale niliyotumwa nayo, ila atakuwa miongoni mwa watu wa motoni.” (Muslim)
Hii ni hasara ya kwanza kwake binafsi Papa Benedict wa 16 , tena sio tu hasara, bali ni hasara kubwa kuliko zote itakayombakisha katika majuto ya kudumu.
Hasara ya Pili
Baada ya Papa Benedict wa 16 kukashifu na kujeruhi shakhsiya tukufu ya Mtume SAAW na Uislamu kwa jumla, Waislamu mashariki na magharibi walichukizwa na wakapaza sauti kuonesha hisia zao.
Wapo Waislamu waliotaka kuonana na Papa huyo kama ujumbe maalumu ili wamrekebishe ufahamu wake wa kimakosa, wapo waliotumia kalamu zao kukosoa kashfa zake, wapo waliotumia mimbar, misikiti na majukwaa mbali mbali kuifikishia hadhira ya Waislamu na wasiokuwa Waislamu juu ya kashafa hiyo. Pia wapo waliojikusanya kama jopo kubwa likijumuisha wanavyuoni na watu mashuhuri katika Uislamu wakatoa waraka wa kukosoa mtazamo huo wa upotovu wa Papa Benedict wa 16. Aidha, wapo Waislamu waliomtaka Papa Benedict wa 16 aje katika medani ya mjadala baina ya dini ya Uislamu na Ukiristo. Hata hivyo, Papa Benedict wa 16 alilikataa mjadala huo, iwe alikataa kwa kauli au kwa kupotezea kimya kimya.
Kitendo cha Papa Benedict wa 16 kukataa mjadala ule ni jambo la kushangaza sana, kwa kuwa yeye ni msomi mkubwa wa theolojia katika kiwango cha kufikia uprofesa kutoka Chuo Kikuu cha Bonn tangu mwaka 1959 na ameshawahi pia kufundisha vyuo mbalimbali kwao Ujerumani na pengine kama Chuo Kikuu cha Münster, Chuo Kikuu cha Regensburg ambacho baadae aliwahi kuwa makamo raisi wake nk. Aidha, Papa Benedict wa 16 ameandika vitabu vingi na kutoa mihadhara mbalimbali mashuhuri, ndani ya baadhi ya mihadhara hiyo amekuwa akidai kifua mbele kuwa ukiristo ni dini ya hoja. Kama ni hivyo, qadhia ya mjadala ilikuwa fursa mwanana kwake kuthibitisha hoja za dini hiyo.
Papa Benedict wa 16 kukataa mdahalo nako ni hasara nyengine aliyowaachia wafuasi wake. Kwa kuwa, wafuasi hao wamekosa fursa ya kupata ufafanuzi wa kina juu ya mfumo wa Uislamu, lakini pia wamekosa fursa ya kuona mapungufu na udhaifu wa dini yao ambayo kwa bahati mbaya haifundishi zaidi ya masuala ya kibinafsi ya kiroho yasio na ufafanuzi, zaidi dini hiyo ikiwa imekosa nidhamu nyingine zote msingi kwa mwanadamu kama siasa, uchumi, siasa nk. Lau Papa Benedict wa 16 angeshiriki mjadala ule ungeweza kutanua upeo kwa wafuasi wake wakiristo, sio tu wakatoliki, bali hata madhehebu mengine yote. Na bila ya shaka wale wakiristo makini wangesilimu. Hata hivyo, bado wafuasi wa Papa na wakiristo jumla bado wana fursa ya kuikimbia hasara hii, kwa kufanya utafiti wa nia njema na uadilifu juu ya Uislamu na kusilimu, au walau kuutizama Uislamu kwa jicho la uadilifu lisilokuwa na chuki za madola ya kimagharibi.
Hasara ya Tatu
Hasara ya mwisho inayotufanya tumkumbuke Papa Benedict wa 16 inarudi kwa Umma wa Kiislamu, hasara ambayo Umma unaishi nayo kwa miaka isiyopungua 100 tangu mwaka 1924 kwa kukosekana dola ya Kiislamu ya Khilafah. Hasara hiyo imekuwa ikiutafuna Umma wa Kiislamu lakini bado tuna muda wa kujisahihisha.
Papa Benedict wa 16 baada ya kashfa zake za kiuadui kwa Uislamu alikataa mjadala, hilo sio geni na wala halikutushangaza, kwa kuwa hata ujumbe wa vigogo 60 wa kikiristo wa Najran uliokuja Madina kwa Mtume SAAW mwaka wa 9 Hijria chini ya kiongozi wao Abu-Masih ulikataa kata kata kuapizana na Mtume SAAW katika tukio la Mubahala, lakini ujumbe ule wa wakiristo walikubali kulipa jizya chini ya mamlaka ya dola. Katika kauli yao ujumbe huo ulisema kumwambia Mtume SAAW:
‘Ewe Abul-Qasim tumeonelea tusiapizane na wewe’. Mtume akawambia: ‘Basi silimuni’ wakakataa kusilimu kisha wakakubali kulipa jizya.
Papa Benedict wa 16 amemtusi Mtume SAAW na Uislamu, amekataa mjadala, hakuwahi kulipa jizya, wala hakuna dola ya Kiislamu kumtia adabu kwa kitendo chake kiovu cha jinai cha kumtukana kipenzi chetu Mtume SAAW.
Jambo hili ni hasara kubwa isiyo na mfano inayopaswa kuwafikirisha Umma wetu wa Kiislamu na kuwaaamsha kwa kuona unyonge na udhalili tulio nao leo. Ni wajibu sasa kubeba mas-ulia yetu ipasavyo kwa kurejesha tena dola ya Khilafah inayopaswa kuanzia katika ulimwengu wa Kiislamu na kuenea kila mahala ili kwa dola hiyo tuweze kujikinga na kujiepusha na hasara nyingi zinazotusibu na zitazoendelea kutusibu kwa kukosekana dola hiyo.
Risala ya Wiki No. 149
18 Jumada al-thani 1444 Hijri / 11 Januari 2023 Miladi
Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania

Maoni hayajaruhusiwa.