Siku ya “Dhihaka Kwa Vijana

Leo tarehe 12 Agosti ni ya Siku ya Vijana Kimataifa. Ni siku iliyochaguliwa kimataifa ati kutathmini na kuangalia changamoto mbalimbali zinazowakabili vijana ulimwengu mzima.

Kwa bahati mbaya leo hii hali ya vijana kiulimwengu ni mbaya sana katika kila upande. Wengi wao wamekosa matumaini ya kuishi kamwe! Mfumo kandamizi wa kibepari unaowasimamia wanadamu kwa sasa umewatelekeza vijana kiasi cha baadhi kufikia kuchukua maamuzi magumu ambayo hayafai kama kujiua, kutumia madawa ya kulevya nk.

Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2015 za Shirika la Masuala ya Ajira (ILO) ni asilimia 25% tu ya waajiriwa duniani kote ndio vijana. Hii inamaanisha wengi wa vijana hawana kazi, ambao hawapungui asilimia 43%. Katika nchi zinazoendelea ambazo ni makoloni ya mataifa kibepari ya kimagharibi asilimia 31% ya vijana wake hawana hata elimu ya kujitosheleza kuweza kuajiriwa.

Matokeo ya vijana wengi kutokuwa na ajira wamekuwa wanajishughulisha na vitendo vya ajabu kama kucheza kamari kama njia ya kujipatia kipato. Gazeti la “Mtanzania” (Agosti 3 2016) lilitoa makala ya uchambuzi inayoonyesha namna gani vijana wengi wanavyojiingiza katika uchezaji kamari. Na serikali hazijali kwa kuwa huwa zinapata mapato mengi kupitia kuyatoza kodi makampuni hayo ya kamari.

Aidha, vijana leo wamekuwa madaraja mwanana ya kudandiwa na wanasiasa wa kidemokrasia kufikia malengo yao. Baada ya hapo wanatemwa na kutupiliwa mbali. Mfano mzuri ni namna vijana wanaojishughulisha na shughuli za kuendesha bodaboda walivyoahidiwa kwa hadaa nyingi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 nchini, na kisha baada ya uchaguzi hali yao imezidi kuwa mbaya. Kwa ufupi, vijana katika jamii chini ya mfumo wa ubepari wamekuwa wakiambulia masuluhisho hewa kwa matatizo yanayowakabili ambayo hayawafikishi popote.

Uislamu unawandaa vijana kubeba fikra thabiti za mfumo wa Kiislamu, kwa kuwa msingi wa mabadiliko yote ya mwanadamu ni kutokana na fikra anazobeba. Tukimuangalia Kiongozi wetu Mtume SAAW aliitumia vyema rasilmali watu ya vijana, kwa kuwabadilisha fikra na uoni wao ili kuleta ukombozi kwao.

Mtume SAAW aliwalingania Uislamu vijana wadogo ambao wengi wao awali walikuwa ni wahuni,wahalifu, wasio na ajira uhakika na waliokosa muelekeo. Mtume SAAW aliwafanya vijana hao wasilimu na kubeba ujumbe wa haki ambao ulikuja kuleta mabadiliko ya kimfumo katika ulimwengu. Na kwa kuwa vijana ndio waliokuwa wanadhulumiwa kwa kiwango kikubwa katika mujtamaa/jamii ya Makka wa wakati huo basi walijikuta wanaukubali ujumbe wake kwa wingi:

Kwa mfano waliweza kusilimu mas-haba wadogo na vijana kama Ali bin Abi Talib umri wake ni miaka 8, Zubeir bin Al-Awwam umri wake ulikuwa ni miaka 8, Twalha bin Ubeid Allah miaka 11, Al-Arqam bin Abi Al-Arqam miaka 12, Abdalla bin Masoud miaka 14, Said bin Zeid chini ya miaka 20 nk.
Pia Mtume Muhammad (SAAW) aliweza kuleta mabadiliko ya kimsingi katika nafsia/ matendo ya maisha ya vijana kutokana na fikra thabiti alizowafinyanga nazo. Kwa mfano, sahaba mkubwa Abu Dharr bin Ghiffar alikuwa anatokamana na kabila la majambazi, alisilimu na kuwa mbeba ujumbe wa haki kila mahala, kiasi cha kulifanya kabila lake lote kusilimu na kuweza kuacha tabia yao ya ujambazi ambayo ndiyo iliyokuwa nguzo ya uchumi wao.

Pia Uislamu huwandaa mapema vijana kuweza kuchukua majukumu ya kuwa walezi wa familia. Kwa mujibu wa nidhamu ya kijamii ya Kiislamu suala la familia ni jambo muhimu sana kwa ustawi wa jamii. Hivyo, huhimiza vijana kuoa au kuolewa haraka na mapema ili kuvunja mianya yote ya kutokea kwa zinaa na kumpoteza mwelekeo kijana. Hivyo, Uislamu huhamasisha mazingira rahisi na mepesi ya ndoa. Ndio maana hata tukaona katika historia ya Khalifah Umar ibn Abdulaziz aliweza kutoa fungu maalumu kwenye hazina ya dola “baytul maal” kuwawezesha vijana wanaotaka kuoa lau hawana mahari.

Aidha, Uislamu unadhamini kwa kila kijana na raia jumla kupata uhakika wa mahitaji ya msingi na hauwabagui watu kwa misingi yoyote.

Zaidi hayo Uislamu huwapa vijana hadhi maalum na sio kuwafanya ngazi ya kisiasa. Ndio maana ndani ya tarekhe yetu ya Kiislamu kumesheheni mifano mingi ya vijana waliopewa dhamana na kushika nyadhifa mbalimbali za kiutawala na kiutendaji. Kwa mfano, Sahaba Usamah bin Zaid ra. aliteuliwa na Mtume SAAW kuwa Kamanda wa kikosi katika jihadi huku umri wake ukiwa chini ya miaka 20 na kuwaongoza mashaba wakubwa kiumri kuliko yeye . Aidha, Khalifah Muhammad al Fatih alishika ukhalifah akiwa na umri wa miaka 21 tu.

Tofauti na hali ilivyo ndani ya mfumo wa kibepari unaotawala dunia leo, kutokana na kuwafanya vijana kukosa muelekeo, wengi wao hujiunga katika vikundi vya kihuni na kihalifu kama vile hapa Tanzania makundi ya “mbwa mwitu”, “panya road” nk. Ndani ya Marekani ambayo ndio kinara wa mfumo wa kibepari kuna makundi mengi ya vijana wahuni na kihalifu ambayo humiliki silaha na kuwadhuru raia. Makundi hayo yamekuwa yanahusishwa na vurugu za mara kwa mara. Takwimu za kitaifa nchini humo zinaonesha kuwa: kuna makundi zaidi ya 24,500 ya wahuni na ya kihalifu ambayo humiliki silaha, yakiwa na wanachama zaidi ya 772, 500 wengi wao ni vijana.

Enyi vijana na wanadamu kwa jumla!

Hakika mnajionea namna gani mfumo wa kibepari ulivyowadhulumu na kuwafanya ngazi kwa malengo yao. Kwa hakika mfumo huo umefeli si tu kuwasimamia na kuwapa hadhi stahiki vijana bali kuwasimamia wanadamu kwa ujumla. Mfumo mbadala wenye uadilifu katika kuwasimamia wanadamu ni Uislamu pekee chini ya dola yake ya Khilafah Rashidah. Huu ndio mfumo pekee ambao unaendana na maumbile ya wanadamu na ambao unaweza kutatua ipasavyo matatizo yote ya wanadamu.

12 Agosti 2018

#UislamuMfumoMbadala

Kaema Juma

Maoni hayajaruhusiwa.