Risala Ya Idi Ul- Udh-Hiya

بسم الله الرحمن الرحيم

Tunamshukuru Allah (SWT) kwa kutuwezesha kudiriki masiku haya matukufu ya Dhul Hijjah, na leo tunasherehekea Sikukuu kubwa na adhimu ya Idi ul-udh-hiya.

Wakati tukiendelea kusherehekea Sikukuu hii tunakumbushana na kuhimizana kutekeleza Ibada adhimu ya kuchinja kwa mwenye uwezo, kutumia vichinjwa hivyo kwa ajili ya familia zetu na kutoa swadaka kwa maskini na mafukara.  Kwani ibada ya kuchinja ni Sunnah kubwa katika masiku haya.

Aidha, tunahadharishana kwamba masiku haya ya Sikukuu yasiwe sababu ya kujiingiza katika maasi na kusahau kuchunga mipaka ya Allah (SW). Bali tule, tunywe, kujipamba, kufanya ziara na familia, lakini tusimuasi Allah Taala.

Furaha ya Iddi isitusahaulishe madhila na mashaka makubwa wanayoyapata Waislamu wenzetu ulimwenguni kote, si Palestina, Yemen, Syria, China nk na pia hapa kwetu ambapo kuna mamia kama sio maelfu ya Waislamu wanaondelea kusota magerezani kwa mgongo wa kesi za ugaidi na kwa kisingizio cha dhulma cha ‘kutokamilika ushahidi’

Si hayo tu, Ummah wetu   na wanadamu kwa jumla dunia nzima tunapitia hali ngumu ya maisha kutokana na nidhamu ya kiuchumi kandamizi na ya kinyonyaji inayotokamana na mfumo muovu wa kibepari chini ya nidhamu yake ya kiutawala ya kidemokrasia. Leo kila pembe ya ulimwengu kumesheheni umaskini uliokithiri, njaa, ubadhirifu mkubwa wa mali za Ummah, mzigo wa makodi endelevu kwa maskini kutoka kwa serikali na khiyana ya wanasiasa kwa Ummah.

Na kwa upande wa kuharibiwa ibada zetu, watawala wa Saudia wanaojifanya wasimamizi wa Hijjah wamezuiya ibada hiyo kwa kisingizio cha maradhi ya Corona, ilhali wanaruhusu matamasha ya muziki kufanyika ndani ya ardhi tukufu ndani ya masiku matukufu bila ya kuwa na haya kwa Allah Taala, Mtume Saaw wala Waumini.

Kwa kumalizia, sisi ndugu zenu wa Hizb ut Tahrir tunaendelea kukuiteni katika wajibu wa kubeba ulinganizi wa haki ili kurudisha tena maisha kamili ya mfumo wa Kiislamu utakaondoa kila aina ya uonevu, dhulma za kiuchumi, mporomoko wa maadili, kuhifadhi ipasavyo ibada zote ikiwemo Hijja na kueneza uadilifu na furaha ya kweli kwa Waislamu na wanadamu wote.

Tunakutakieni Iddi Njema na Ibada Makbul

IDI UL-UDH-HIYA 1442 HIJRIA

http://hizb.or.tz/

Maoni hayajaruhusiwa.