Ramadhani Iturejeshee Kujiamini Kwetu

بسم الله الرحمن الرحيم

Mwezi wa Ramadhani uko ukingoni. Mwezi ambao huunganisha Umma wetu mtukufu katika Ibada tukufu ya kufunga ambayo ni nguzo katika nguzo za dini yetu ya Kiislamu.

Hapana shaka yoyote kwamba Ramadhani ni mwezi wa kujipinda kwa nguvu zetu zote kwa kila aina ya Ibaadat kama kukithirisha kuisoma Qur-ani tukufu, kuswali swala ya tarawehe, kubakia itikafu miskitini, kuomba dua, kutaka maghfira, kutoa sadaka na mengi mengineyo katika yale yanayostawisha fungamano letu moja kwa moja kwa Allah (Taala). Kwa hakika mwenye kuyabeza hayo amejinyima thamani kubwa ya mwezi huu mtukufu Ramadhani.

Hata hivyo, katika mwezi huu pia ni wajibu tuutanue upeo wetu kinyume na tulivyozoea
kuichukulia haiba ya Ramadhani kwamba ni mwezi wa Ibaadat za kiroho tu. Kwa udhati ikiwa tutaichukulia Ramadhani kwa mtizamo wa upande mmoja wa Ibaadat za kiroho tu tutakua tunaufanyia dhulma mwezi huu mtukufu. Hii ni kwa sababu Qur-ani inatukumbusha kwamba mwezi huu ndio iliposhushwa kuwa muongozo kwa watu wote katika kila kipengee cha maisha yetu. Yawe mambo ya Ibaadat kama swala, dhikri, hijja, itikafu, sadaka. Pia kwa upande wa pili katika mambo ya muamalati (mjumuiko wa watu) kama kuuziana, utawala, vita, ndoa n.k. Kwa hivyo mwezi huu mtukufu utukumbushe na utuharakishe kuubeba msimamo wetu wa asili nao ni kuuchukua Uislamu kama mfumo kamili na bora kwa kila kipengee cha wanadamu wa zama zote.

Kwa bahati mbaya tangu kuibuka mfumo batil wa kibepari mwishoni mwa karne ya 18 miladia na kuangushwa Dola ya Kiislamu [Khilafah Uthmania] katika mwaka 1924 [miladi], fikra ya kuitenganisha dini na maisha (secularism) imekuwa ikipigiwa debe na kufanywa ndio kaulimbiu na makafiri, wakala wao katika vibaraka, wanafikra wao kiasi cha kuwachanganya baadhi ya Waislamu na kupelekea kuifanya dini yao kuwa ni dini ya masuala ya Ibaadat tu.

Huu ni msiba mkubwa! uliowapelekea baadhi ya Waislamu kupoteza thika/kujiamini katika dini yao na kuufanya Uislamu kama dini mithili ya dini nyengine kama ukiristo, ubudha na uhindu. Kuwa ni dini ya kulialia sana kwa kufanya Ibada za kiroho tu bila ya kuwa na masuluhisho yoyote maishani, na badala yake kutegemea ubepari kutatua matatizo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani ni wajibu Umma wa Kiislamu kuirejesha thika yao katika upande wa nafsiya (matendo) yao kwa kufanya Ibadat mbalimbali lakini pia kujenga na kuimarisha aqliya (mentality) yao kwa kuubeba Uislamu kama mfumo kamili ulioletwa kumkomboa mwanaadamu.

Hali hii ya kujiamini kwa Umma wetu tutairejesha kwa kuitupia macho tarekhe yetu tukufu ya Kiislamu namna ilivyojaa kila aina ya misimamo na mapambano katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.

Mtume (S.A.W) na masahaba zake watukufu licha ya kufunga, kuswali na kuomba maghfira katika mwezi huu pia walitoka mchakamchaka kuelekea Badri katika mwezi kama huu kupambana na makafiri na kuulinda mfumo wa Uislamu.
Pia katika mwaka wa nane wa Hijria mwezi kama huu wa Ramadhani waliizingira Makka na kuikomboa na uchafu wa masanamu na uongozi batil wa kiqureish na kuiweka chini ya Himaya ya Dola la Kiislamu.

Kadhalika Waislamu waliokuja baada yao hawakuichukulia Ramadhani kama mwezi wa kula vitamu na vya tunu tu na kumalizia kwa kutaka maghfira pekee bali walisimama kidete kivitendo kuitanua Dola ya Kiislamu kwa kufanya fat-hi mbalimbali na kuulinda ushindi walioupata kwa kusimama msimamo thabiti bila ya kutetereka.

Tukumbuke Jemadari Tariq bin Ziyad aliifungua (Fathi) Spain na Ureno (Andalusia) katika Ramadhani mwaka 93 Hijria, kadhalika shujaa Salahudin Ayoub aliwafurusha makafiri katika vita vya ‘Hittin’ katika mwaka 584 Hijria, lakini tusisahau pia mapambano makali ya jihadi dhidi ya Mongols katika Vita vya ‘Ain-Jaloot’ yaliotokea katika mwezi wa Ramadhani Mwaka 627 Hijiria.

Huu ndio msimamo uliobebwa na Mtume, Masahaba na Waislamu wema waliofuata, nasi kwa upande wetu lazima tuandame msimamo huu kwa sababu huu ndio msimamo wa Kiislamu kwa zama zote.

Basi kwa kila mwenye ikhlasi na kutaka ukombozi wa kweli wa Umma huu tuutumie mwezi huu mtukufu wa Ramadhani kurejesha ufahamu wa msimamo wetu wa kuchanganya ibadaat na mapambano dhidi ya mfumo wa ukafiri wa kileo ambao ni ubepari (urasilimali).

Kwa kufanya hivyo tutaweza kurejesha nafasi yetu ya asili kama Umma bora ulioletwa kuukomboa ulimwengu na binaadamu wote kwa jumla.

23 Ramadhan 1440 Hijri – 16 Mei 2020 M

Maoni hayajaruhusiwa.