Ramadhani Itukumbushe Zama za Izzah na Heshma Yetu Kikweli

ﺑﺴﻢ ﷲ ﺍﻟﺮﺣﻤﻦ ﺍﻟﺮﺣﻴﻢ

Tukiwa katika kumi la mwisho la Ramadhani tukielekea ukingoni mwa mwezi huu mtukufu ambao katika tareekh uliinua izza yetu. Ni muhimu kujikumbusha zama za heshima, nguvu na izza ya Umma wetu ambazo leo zimekosekana.

Umma wa Kiislamu tangu kusimama kwa Dola ya Kiislamu katika mji wa Madina ulipata izza/nguvu na heshma na kuweza kujilinda dhidi ya maadui wa Uislamu. Waislamu walidumu na nguvu na heshima hiyo kwa karne nyingi sana. Japo kulitokea fitna za hapa na pale lakini bado Umma wa Kiislamu ulibakia na izza na heshima. Tofauti na leo Umma umekuwa duni, na kila mwenye kisu chake hukata sehemu ya mwili wa Umma wetu kwa namna apendavyo na atakavyo.

Zama tulipokuwa na izza na heshma chini ya Dola ya Kiislamu hakuna aliyeweza kuvunja heshima yetu , hata mayahudi wa Bani Qainuqa’ walipomkosea adabu mwanamke wa Kiislamu sokoni, adhabu yao ilikuwa ni Mtume SAAW kuandaa jeshi na kisha kuwafukuza kabisa katika mji wa Madina na kuwanyang’yanya mali zao zote ili wasirudie tena utovu wao wa adabu.

Zama tulipokuwa na izza na heshma yetu Jemadari Khalid alimtangazia vita Rustam, na yeye Rustam akaoamba msaada toka China. Mfalme wa China akamjibu kwamba hatoi msaada wa kupambana na watu ambao lau wakitaka kung’oa mlima wanaweza kuung’oa. Leo China inawatesa Waislamu Turkistan ya Mashariki mateso ya kishenzi ambayo hata mnyama hathubutu kumtendea mnyama mwenzake na hakuna wakumzuiya.

Zama tulipokuwa na izza na heshma yetu ulipozuka ugomvi baina ya pande mbili za Waislamu, Imam Ally (karama llahu waj-hahu) na Muawiyah bin abii Sufyan, mfalme Qaisar wa Ruum akamwandikia barua Muawiyah akimtaka amsaidie kwa jeshi litakalokwenda kumkata kichwa Imamu Ally ra. kisha apelekewe kichwa chake. Muawiyah japo alikuwa amemuasi Khalifa alimjibu Qaisar afunge mdomo wake au atamtumia jeshi mwanzo wake lipo kwake Qaisar na mwisho wake lipo kwa Muawiya. Na Muawiya atalitaka jeshi likate kichwa cha Qaisar ili ampelekee Imam Ally. Leo ugomvi kidogo ukizuka baina ya Waislamu basi makafiri hudandia na kuwa mstari wa mbele kama wasuluhishi, na hali wao ndio wachochezi. Kama tuonavyoona leo nchini Syria, Yemen, Libya nk.

Zama tulipokuwa na izza na heshma ya kweli misafara ya meli za Kiislamu ilipokuwa ikipita baharini maeneo ya Ulaya, serikali zao zilitoa agizo makanisa yote yasipige kengele ili Waislamu wasibughudhiwe wakiwa katika safari zao.

Zama tulipokuwa na izza na heshma ya kweli mwanaharakati wa ubaguzi wa kiyahudi (uzayuni) Dr. Theodor Herzl alipokwenda kwa Khalifah wa Waislamu ati auziwe kipande cha ardhi ya Palestina kwa mamilioni ya pesa za dhahabu, majibu ya Khalifah yalikuwa ni kumtandika kofi (kibao) kali sana mpaka akapepesuka, kisha akajishika shavu lake, na kumwambia Khalifa ninakuahidi Palestina tutaichukua tu. Na Khalifah akamjibu “subirini Khilafah itakapoanguka mutaichukua yote bure. Siwezi kuuza ardhi Waislamu waliyoikomboa kwa damu zao”.

Leo mayahudi wameikalia kwa mabavu ardhi tukufu wakiunajisi Msikiti mtukufu na watawala katika nchi za Kiislamu ndio walinzi wao wakubwa. Watawala hawa wa nchi za Waislamu wanawachezea akili za Waislamu ati kwa kufanya maadhimisho ya kuililia Al-Qudsi kwa maneno matupu, wengine wanaleta mahusiano ya wazi na kuwapa mayahudi kila wakitakacho kutoka katika nchi za Waislamu, wengine wanawatisha Waislamu ati mayahudi hawashindiki, wengine wanadai kwamba hawana nguvu kupambana na myahudi ilhali inapokuja ajenda ya kuwauwa Waislamu wenzao wako mstari wa mbele wanashirikiana na Marekani, Urusi na China kama kupeleka majeshi nchini Syria, Yemen nk kwa ajili ya kuuwa Waislamu.

Izza, heshma na nguvu yetu haitorudi kamwe kama hatukuacha ikhitilafu zetu ndogo ndogo za kimadhehebu na kifiqihi na kujifunga na Uislamu na kufanya kazi kurudisha Dola ya Kiislamu ya Khilafah inayopaswa kuanzia katika nchi kubwa za Waislamu. Mwezi huu utuzidishie ghera na hamu ya kuurudisha Uislamu ukiwa mfumo kamili wa maisha, na sio dini ya kiroho tu.

وَلِلَّهِ الْعِزَّةُ وَلِرَسُولِهِ وَلِلْمُؤْمِنِين (المنافقون: 8
“Hakika izza ni kwa Allah, Mtume wake na Waumini”

Tunamuomba Allah Taala Atughufurie madhambi yetu yote na atufunike kwa Rehma zake na kuupa Umma wetu nusra inayotokamana naye – Amiin

28 Ramadhan 1440 Hijri /02 Juni 2019 Miladi
Risala ya Wiki No. 43

Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania
https://hizb.or.tz/
https://www.facebook.com/Hizb-ut-Tahrir-Tanzania
#RamadhanNaMuongozoWaQuran

Maoni hayajaruhusiwa.