Rai za Kifiqhi Katika Kulipa Funga

بسم الله الرحمن الرحيم

Swali:

Asalaam Alaykum Warahmatullah Wabarakatuh,

Sheikh wetu, nataka kujua hukmu ya Allah ili moyo wangu upate utulivu. Nilikuwa katika jahiliyyah na kwa makusudi nikaacha funga ya Ramadhani bila ya udhuru, kisha, Alhamdulillah Allah akanirehemu nikatubu, vipi nilipe funga niliyoiacha? Je ni juu yangu kulipa fidia kila mwaka au inatosha kulipa tu?

Nataraji Sheikh wetu utanijibu swali.

Jawabu:

Waalaykum Salam Warahmatullah Wabarakatuh,

Ndugu yangu, umesema ulikuwa hufungi kwa muda mrefu tena kwa makusudi bila ya udhuru wa kisheria. Kisha baada ya miaka hiyo Allah akakuongoza kwenye njia iliyo nyoka ukawa unafunga huli mchana… Na kwasababu ya uchamungu unataka kulipa miezi ya Ramadhani zilizopita ambazo hukufunga … Namshukuru Allah kuwa amekuongoza kwenye utiifu mzuri kiasi ambacho hukutosheka kufunga tu baada ya Allah kukuongoa, bali una pupa la kulipa miezi ya Ramadhani ambayo hukuifunga. Allah akubariki, aifanye njema toba yako na akuenezee neema zake na rehema zake.

Ndugu mkarimu, sisi hatutabanni katika ibadati bali tunaliacha jambo kwa Muislamu mwenyewe afuate madhehebu yoyote katika funga au swala…nk. Na mimi hapa nitakutajia baadhi ya rai za kifiqhi katika kulipa funga, na linalokuwa wazi katika kifua chako na moyo wako ukatulizana kwalo unaweza ukalifuata:

1-Imeelezwa katika kitabu kiitwacho “Nihaayatul-Mutwalib fi diraayatil-Madhaahib”  cha mwandishi Abdul Malik Aljiweyni, mwenye laqab Imamul-Haramain (aliyefariki 478H), nacho ni katika fiqhi ya Shafi:

(Mwenye kupitwa na funga ya Ramadhani kwa masiku kadhaa, na akapata uwezo wa kuzilipa, basi haifai yeye kuchelewesha kuzilipa mpaka (ukaingia) katika mwaka ujao, hili tunalolitaja si Sunna  bali ni la lazima, ila awe anaweza  na nyudhuru ziwe zimeondoka. Na kama itakuwa kuchelewesha kulipa mpaka mwaka ujao bila ya udhuru basi itakuwa kulipa pamoja na kibaba cha chakula kila siku, na kama atachelewesha kulipa kwa miaka miwili au miaka kadhaa, ongezeko la fidia litakua kwa njia mbili: Moja ni kwamba haiongozeki, na wala si wajibu kuchelewesha kwa miaka kadhaa isipokuwa kwa kilichowajibu (ikabidi kuchelewesha) hata kwa mwaka mmoja…  na lililosahihi hasa katika hali hii ni kuongozeka kwa fidia na kuifanya upya, kwa hiyo ni wajibu kwa kuchelewesha kwa kila mwaka (kutolewa) kibaba. Basi akichelewesha miaka miwili, ni wajibu vibaba viwili kwa kila siku anayolipa, hivi ndivyo inavyozidi na kuendelea. Huu ndio msimamo katika fidia…). Hii ina maana kulipa funga ya Ramadhani kwa asiyefunga ailipe kabla ya Ramadhani ijayo na akichelewesha mpaka baada ya kuingia Ramadhan (nyengine) basi juu yake kulipa na kutoa fidia… Na ana rai nyengine, nayo ni kwamba kwa mfano, akichelewesha kulipa kwa miaka miwili atawajibika kulipa pamoja na fidia mbili. Hali iko hivyo.

2-Ama katika madhehebu ya Abuu Hanifa ni kuwa, kwa namna yoyote atayochelewesha kulipa hawajibiki (kutoa fidia) isipokuwa ni kulipa tu, ikiwa itafika Ramadhani nyengine… atalipa ile iliyompita na wala hawajibiki fidia kwa kuchelewesha:

3-Imeelezwa katika kitabu cha Almabsuut cha mwandishi Al-Sarkhasy aliyefariki mwaka 483H (Fiqhi ya Kihanafi)

Amesema: (Mtu ambae ana wajibu wa kulipa masiku katika mwezi wa Ramadhani na akawa hakulipa mpaka ikaingia Ramadhani ijayo… ni juu yake kulipa Ramadhani iliyopita na wala hatolipa fidia kwa mujibu wa rai yetu. Na kwa mujibu wa Shafi Allah amrehemu, analazimika kulipa pamoja na kulisha masikini kwa kila siku… Sisi tuna (tumeshika) dhahiri ya kauli ya Taala: “Basi atimize idadi yake katika masiku mengine” (Albaqara:184). Hamna humo (hapajatajwa muda maalumu wa kulipa) muda maalumu. Kuweka muda maalumu ni baina ya Ramadhani mbili huwa ziada, na hii ni ibada ya iliyoekewa wakati maalumu lakini kuilipa haijaekewa muda maalumu…)

4-Na imeelezwa katika kitabu cha Badaaiu Al-swanaaiu fii tartiibi Al-sharaai’i cha mwandishi Alau Diin Alkaasaany Alhanafi (Aliyefariki mwaka 587H):

(…madhehebu ya wenzetu – wanavyuoni wetu – ni kwamba wajibu wa kulipa hauna wakati maalumu, kutokana na kile tulichoeleza kuwa jambo hili la kulipa ni mutlq halina wakati maalumu, kwahiyo liende hivyohivyo kwa itlaaq yake. Na kwahivyo wamesema wenzetu kuwa muislamu atakapochelewesha kulipa Ramadhani mpaka ikaingia Ramadhani nyengine hatotoa fidia…)

Hii ina maana kwa mujibu wa madhehebu  ya Abu Hanifa kilichowajibu ni kulipa tu bila fidia, yaani atalipa miezi ambayo hakufunga tu.

Na kama nilivyokueleza mwanzoni, kuwa sisi hatutabanni katika ibadat, nilichokutajia ni baadhi ya rai za madhehebu ya Abu Hanifa, Shafi na Alfaqih Hambali. Linalokua wazi katika kifua chako basi lifanye… Allah akuwafikishe kwa alipendalo na kuliridhia.

Nataraji haya kuwa yametosheleza. Na Allah ni mjuzi zaidi na mwenye hekima zaidi.

08, Ramadhani 1440H

13, May 2019

Maoni hayajaruhusiwa.