Muongozo Kwa Wazazi Na Walezi Kipindi Cha Likizo Ya Wanafunzi

بسم الله الرحمن الرحيم

Kwa wanafunzi mwezi huu wa Disemba huwa ni muda wa likizo ndefu ya mwisho wa mwaka kwa shule za msingi na sekondari.
Ni kipindi ambacho wanafunzi hupata fursa adhimu ya muda mrefu wa mapumziko kando na harakati zao za kimasomo za miezi mingine.
Kipindi hiki ni muhimu kwa wazazi na walezi kuwapa watoto wao muongozo na mwelekeo maalumu kwa ajili ya kuwajenga na kuwafinyanga watoto hao kuwa na mustakbali mwema kifamilia na jamii kwa jumla.
Jambo muhimu wanalopaswa kulifahamu wazazi na walezi ni kwamba, elimu ni mchakato endelevu kwa mtoto au kwa mwanadamu kwa jumla. Na kwa kuwa wao wazazi ni sehemu ya walimu nyeti wa watoto hao, basi hawana budi kukitumia kipindi hiki cha likizo kuendelea kuwapa watoto hao elimu, maarifa, maono thabiti japo sio kwa sura ya elimu ya shule.
Kwa bahati mbaya baadhi ya wazazi huwaachia watoto wao huria katika muda kama huu kuwaruhusu kurandaranda na kuzurura huku na kule bila ya mwelekeo maalum au mpangilio wenye muongozo kwa sababu tu wamefunga shule. Jambo hili ni hatari kwa ustawi wa watoto hao na jamii kwa ujumla, kwa sababu unapomuacha mtoto bila ya muongozo na dira thabiti katika miamala yake, kuna uwezekano wa kwenda kombo katika maisha yake.
Katika kipindi kama hiki wazazi hususan wa Kiislamu wanaweza kuchukua mazingatio yafuatayo yanayoweza kuwapa mwelekeo, muongozo na kuwasaidia katika kuamiliana na watoto wao na kuwapatia dira fulani wakati huu wa likizo:
1. Kufuatilia nyendo zao kwa umakini
Japo ukweli unabaki kwamba mzazi na mlezi huwa ana jukumu wakati wote kufuatilia mwenendo wa mtoto wake, akiona mazuri ampongeze na kumuhimiza na akigundua mapungufu amrekebishe, lakini kipindi hiki fursa hiyo ni pana zaidi kwa wazazi na walezi, kwa kuwa fursa ya kuamiliana na mtoto inakuwa kubwa zaidi. Aidha, ni muhimu mzazi kufuatilia mwenendo wa mtoto katika upande wa kiibada kama swala, kuongeza maarifa ya thaqafa ya Kiislamu kama kusoma vitabu, kufanya ulinganizi, usomaji Quran nk. Japo asili haya ni mambo ya wakati wote lakini muda huu ni muda wa kupatiliza zaidi. Na kama mzazi atagundua mtoto hayuko vizuri humlazimu kufanya marekebisho.
2. Kujadili maendeleo ya kimasomo
Wazazi na walezi hupaswa kuketi kirafiki na watoto wao kujadili maendeleo ya masomo na changamoto mbalimbali zinazowakabili watoto. Jambo hili mbali na kuwa na faida moja kwa moja katika upande wa kimasomo ya mwanafunzi, lakini pia lina maana pana zaidi ikiwemo kumjenga na kumfinyanga mtoto utamaduni wa kujifunza kutafiti tatizo, kulijadili na kutafuta suluhisho. Bila ya kutaja kukuza urafiki na kumtanua upeo wa mtoto kimawasiliano.
3. Kurekebisha fahamu/ fikra za kimakosa.
Wazazi na walezi yawapasa wajue kwamba wakati wote wana jukumu la kusahihisha fahamu za kimakosa ambazo watoto hupewa katika elimu ya kisekula.
Tukumbuke kwamba, kwa kuwa elimu hii inatokana na hadhara/ mfumo wa kimagharibi wa kibepari ndani yake imeingizwa baadhi ya fikra na nadharia nyingi kinyume na Uislamu. Fikra kama binadamu kutokana na sokwe (evolution), usawa baina ya mwanamume na mwanamke, fikra ya dini mseto’, fikra za kiuwongo kama za ‘uhuru’ haki za wanawake, haki za binadamu, na kimsingi zote zinazotokamana na demokrasia ni fikra batil zinazogongana moja kwa moja na misingi ya aqida ya Uislamu. Wazazi na walezi watakua na dhima/ mas-ulia mbele ya Muumba baada ya kuwapeleka watoto katika mashule haya bila ya kuweka sawa fahamu hizo katika mabongo yao. Muda huu wa likizo unaweza kutumika vyema kuondokana na dhima hiyo.
4. Kuchanganyika nao katika mambo ya kifamilia na kijamii
Katika muda huu wazazi na walezi pia hupaswa watenge muda wa kujumuika na watoto kwa kuketi pamoja, kuzungumza kirafiki, kujadili qadhia za kifamilia, kucheza, kula pamoja, kwenda msikitini, mazikoni, kusoma Quran pamoja, kufanya visomo vya dua na watoto wao ili kukuza mazingira ya ukuruba na mapenzi, na kuziepusha nyumba zetu kuwa kana kwamba kambi za kijeshi. Kwani hili ni haki yao na haki ya wazazi na walezi kwa watoto hawa, na pia baada ya likizo hawapati muda wa kuwa karibu zaidi na wazazi wao kutokana na mfumo wa maisha ya kibepari ambapo mzazi hupelekwa mchakamchaka na kazi, na mtoto hushughulishwa na mzigo wa manadharia katika masomo yake.
5. Kuwafundisha na kuwashirikisha katika stadi za maisha
Huu ni muda ambao wazazi na walezi pia wautumie vyema kuwafunda, kuwafundisha na kuwabidiisha watoto wao kwa stadi mbalimbali za kimaisha, kuwaonesha majukumu yao, haki, wajibu wao kwa wazazi, ndugu, jamaa, majirani marafiki na jamii nzima. Ikiwemo pia kuwaonesha lengo mama la kuwepo kwao hapa duniani. Hii huhusisha kuwapa majukumu ya kusaidia kazi za nyumbani, kukabiliana na wimbi la vijana magoigoi wasioweza hata kazi za kawaida kama kupika, kufua, kusafisha vyombo, kuweka mazingira vizuri, kusimamia bustani nk. Hali hiyo wakati mwengine hutokana na athari ya kudharau kuwajenga watoto mapema na majukumu hayo. Ni muhimu pia kama katika familia kuna wanaofanya stadi za kiufundi kama kujenga, umeme, fundi bomba, kushona kuwashirikisha watoto kivitendo walau wawe na maarifa msingi ya kivitendo juu ya stadi hizo.
6. Kuwafundisha kujenga udugu
Hili ni jambo muhimu katika kipindi hiki ambalo kwa Waislamu ni ibada kubwa. Ni wajibu kuwafundisha watoto kujenga na kuimarisha mshikamano wa udugu. Nalo linaweza kutendwa kwa namna moja katika mbili. Amma kufanya ziara na watoto kwa ndugu na jamaa ili wajuane vyema. Amma wazazi au walezi wanaweza kuwaruhusu watoto kubakia kwa ndugu kwa kufanya ziara kama mazingira yanaruhusu japo kwa siku chache ili kukuza mahusiano zaidi.
7. Kuwapa muda wa mapumziko.
Na mwisho pamoja na yote tuliyotaja, wazazi na walezi lazima wayatende kwa uzani wa hali ya juu ili kuwapatia watoto hao muda na fursa ya kutosha ya mapumziko. Watoto hawa hushughulishwa vya kutosha na masomo muda wote wawapo shuleni, hivyo ni muhimu na wajibu kupata muda wa kupumzika zaidi. Hivyo, wazazi wasiwanyime watoto haki yao hii kama binadamu.
8.Kuwandaa kwa mwanzo mpya
Na mwisho, kuwandaa wanafunzi kisaikolojia kwa kuwatia nguvu, moyo na ari mpya kwenda kukabiliana na masomo kwa kuanza madarasa mapya mara shule zinapofunguliwa ikiwemo pia kudurusu masomo yao japo kwa kiasi fulani, na kuwaandalia vifaa vitakavyowasaidia katika muhula mpya.
Risala ya Wiki No. 120
19 Jumada al-awwal 1443 Hijri /23 Disemba 2021 Miladi
Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania

Maoni hayajaruhusiwa.